Monday, December 30, 2013

MAOMBI YENYE NGUVU.......SEHEMU ya III MAOMBI YENYE NGUVU
Imani ya Kupokelea Majibu ya Maombi Yako

Katika Mfululizo wa somo lenye kichwa “MAOMBI YENYE NGUVU”, nimeona nizame kidogo kwenye kipengele cha ‘iv’ cha sehemu ya II ya somo hili kinachosema “JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA”.

Mara nyingi sana watu wanachukulia SOMO la imani kwa wepesi usiostahili. Kama kuna kitu cha muhimu katika maisha ya Mkristo ni kujua FAIDA na MADHARA ya kutokuwa na IMANI. Sijui ni kwanini utasikia mara nyingi sana watumishi wa Mungu wakihusianisha imani na kushindwa kupokea majibu ya maombi lakini ni mara chache utasikia wakitia mkazo somo hili la IMANI kwa KUSUDI la KUMPENDEZA Mungu.

Kusudi la Msingi la IMANI sio kupokea majibu ya maombi yako ila KUMPENDEZA Mungu. Sababu ya msingi ni kwamba mahitaji tunayoomba kwa Mungu sio ya kila saa na kila siku, ila mambo YOTE tuyatendayo katika maisha muda wote yanahitaji IMANI ili umpendeze Mungu kwa sababu imeandikwa “haiwezekani kumpendeza pasipo imani” (Waebrania 11:6) na “kila jambo lisilofanyika katika imani ni dhambi”. Sasa jiulize kwamba unafanya mambo mangapi pasipo imani? Kutokana na mistari hii miwili najifunza kwamba LENGO la msingi la IMANI ni kumpendeza Mungu na ndipo faida zingine huja pale unapoitumia imani hiyo KUOMBA au KUPOKEA majibu ya maombi yako.

Katika sehemu hii ya III ya somo hili natamani tujifunze hiki kipengele cha IMANI ya kupokea majibu ya maombi yako. Nitatumia mfano wa NDOA ya Zakaria na Elizabeth ambao ni wazazi wa Yohana mbatizaji na Maria, mama wa Yesu.

Nitaanza na Zakaria na Elizabeti. “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana” (Luka 1: 5-7). Hawa wawili walikuwa wakiishi maisha ya KUMTUMIKIA Mungu katika usafi na utauwa. Walitamani sana kupata mtoto na walimwomba Mungu (kwa sababu walikuwa na IMANI ya KUOMBA) kwa muda mrefu bila majibu. Haikuwasumbua kwamba hawakujibiwa, walizidi kukaa katika HUDUMA na UTUMISHI Mungu aliowaitia na waliendelea na zamu zao.

Mungu akamtuma malaika Gabriel kupeleka ujumbe kwa Zakaria akiwa madhabahuni katikati ya huduma. Malaika akasema “Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.” (Lika 1:13). Alipoambiwa habari za MAJIBU ya maombia yake, “Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” (Luka 1:18-20). Sasa nataka uone kwamba hawa WATUMISHI waliomba kweli ila ilipofika mahali Mungu anasema “nimesikia MAOMBI yenu na sasa najibu” bado HAWAKUSADIKI/HAWAKUAMINI kama inawezekana! Yaani hawana imani ya kupokea MAJIBU ya maombi yao! Sasa Malaika akamfanya bubu. Kwa haraka unaweza kuona kama ni ADHABU ya kutokuamini kwake (Mungu hafurahishwi na mtu wa kusita-sita/mashaka/kutokuamini kama Anaweza) ila kuna sababu ya pili ambayo ni KUHARIBU imani ile ya KUPOKEA majibu kwa UKIRI mbaya (negative confession) basi dawa ni kumnyima kuongea hadi majibu ya maombi yatokee.

Ukija kwa upande wa Maria, mama wa Yesu. Gabriel huyo huyo alikuja na habari ya kupata mtoto ila “kwa uweza wa Roho Mtakatifu”. Utagundua kwamba Maria na yeye aliuliza swali linalofanana na la Zakaria ila hakupigwa na ububu! Ujumbe huu ulimjia Maria miezi 5 baada ya Elizabeti kuwa mjamzito. Sasa wakati Maria anamuuliza Gabriel haya mambo yatakuaje, kulikuwa na SHIDA ya IMANI ya KUPOKEA huo muujiza pia. Kabla Gabriel hajaondoka ilibidi ainue imani ya Maria kwa kumpa “Neno la Mungu lililotamkwa kwa kinywa cha malaika kwa Zakaria” (“Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu”). Baada ya Gabriel kuleta ujumbe “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” (Luka 1:34-38). Huu msitari wa 38 unatuonyesha imani ya Maria imeinukana na kuona INAWEZEKANA kisha Malaika akaondoka.


Tukiendelea kujifunza hapa utaona “basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” (Luka 1: 39-45).

Hawa wanawake wawili walimshangilia Mungu kwa pamoja ila ukitizama kwa makini utagundua baada ya Elizabeti kujazwa Roho Mtakatifu, alirudia yale “maneno ya kuimarisha imani ya Maria” na mwishowe utaona kwamba anasema “aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”. Ikimaanishwa kwamba kuna IMANI inatakiwa KUPOKEA hiyo ahadi japo kweli kabisa ni Malaika/Bwana amesema. Kumbuka siku zote, AHADI iliyoko kwenye Neno la Mungu sio yako hadi utakapokuwa na IMANI ya KUTOSHA kuimiliki/kuipata hiyo AHADI.

Tukiendelea kujifunza utaona Maria anaimba wimbo wa kumshukuru Mungu baada ya haya maneno ya Elizabeti. Maneno ya wimbo wa Maria ni marudio ya yale ambayo malaika alikwisha kusema na jinsi alikubali kusudi la Mungu kutimia kwake, huku akiona ni UPENDELEAO wa pekee kupokea BARAKA hii kubwa. Huu ni UKIRI wa kuimarisha na kulinda IMANI yake ya KUPOKEA mtoto.

Ukifuatilia zaidi utaona Maria alikaa kwa Elizabeti miezi 3. Yamkini walikuwa wakitiana moyo katika kubeba MIMBA muhimu katika maisha yao na kufikilia KUJIFUNGUA salama sawa na KUSUDI la Mungu. Sasa mara nyingi sana katika maisha yetu tumekuwa na imani nzuri tu wakati wa kuomba, ila HALI HALISI zimetufanya kuona HAIWEZEKANI KUPOKEA majibu ya maombi yetu na imekuwa kikwazo. Fikiri hii hali, binti anaambiwa atapata mimba bila kumjua mwanaume! Na upande mwingine kikongwe aliyepitiliza siku za kuzaa anaambiwa atapata mimba! Hali halisi inasema HAIWEZEKANI. Sasa kama mtu hatakuwa na IMANI, na hajui namna ya kuzimisha sauti za SAYANSI, TEKINOLOJIA na ELIMU zingine, imani ya KUPOKEA inakufa. Hata kama ni Yesu anakuja/anazaliwa, ILIBIDI Maria awe na IMANI ya KUPOKEA! Ilibidi Malaika Gabrieli ampe Maria mfano wa “jambo lisilowezekana” na jinsi ambavyo “limewezekana kwa Mungu” ili kuinua IMANI yake ya KUPOKEA.

Kitu cha kukusaidia kukuza/kupata IMANI ya kupokea majibu ya MAOMBI yako ni KUJIFUNZA matendo Makuu ya Mungu katika Biblia, na kuyatafakari usiku na mchana, na kuyataja unapotarajia MAJIBU ya maombi yako. Jifunze KUKIRI matendo makuu unayoyajua ya Mungu wetu ukiwa katika maombi kwa mfano, wakati Daudi anamkabili Goliath alisema maneno ya IMANI yake kwa Mungu, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu” (1 Samweli 17:34-37). Zungumza na HALI unayopitia na uitangazie USHINDI katika MAOMBI, itaje hiyo shida kwa jina “lake” na uiambie kwa maneno kama unazungumza na mtu, huku ukiikemea kwa Jina la Bwana wa Majeshi. Wakati huo ukitamka matendo mengine MAKUU ya Mungu ambayo yamefanyika kwa watu wengine. Kwa kufanya hivyo ghafla! Utaanza kuona Mungu ni MKUBWA kuliko hiyo shida/jambo unaloomba na IMANI yako inaongezeka wakati huo MASHAKA yakitoweka. Kumbuka Ibilisi huleta VITA katika FIKRA zetu ili kutujengea ngome, na njia mojawapo wa kumshinda ni kwa kutumia “NENO la ushuhuda na Damu ya Mwana-kondoo” (Ufunuo wa Yohana). Hii ni SIRI ya KUJAZA imani ya KUPOKELEA lakini pia kumshinda Adui azuiaye.

Mungu atusaidie kujenga IMANI zetu kwa KUJIFUNZA kwa bidii maandiko na kuomba. Hatimaye tuweze kutenda KILA jambo kwa imani kwa kusudi la kumpendeza Mungu na kuweza KUOMBA na KUPOKEA majibu ya maombi yetu kwa hiyo IMANI.

Roho Mtakatifu atufundishe NENO la Mungu na kutuwezesha kupata UFUNUO katika hilo Neno ili kujenga IMANI zetu. AMEN.

Frank Philip.

1 comment:

  1. duh asante kwa neno zuri, maana umenifungua sana kupitia neno hili

    ReplyDelete