Thursday, January 2, 2014

NGUVU katika MATENDO yako!!!NGUVU katika MATENDO yako
(Umri, mlango wa misaada kwako, uheri (less trouble) wa maisha, baraka na utajiri)

Kuna msemo uliozoeleka sana unaosema “malipo ni hapa hapa duniani”. Na kwa wenzetu wa Magharibi wanasema “what goes around comes around”. Lakini Bwana wetu alitufundisha kwamba “yale mambo tunayotaka watu watutendee inatupasa sisi pia kuwatendea hivyo”, ikiwezekana tuwatendee kwanza na bila masharti. Na “kipimo tunachowapimia wengine hicho hicho na sisi tutapimiwa”. Kumbuka sio KIPIMO hicho umetumia kumpimia mtu mmoja ila ndio KIPIMO umejichagulia watu WOTE au hata Mungu kukupimia wewe!

Ni rahisi sana kumtendea mtu WEMA baada ya yeye kukutendea wewe kwanza (kulipa wema kwa wema), ila pia ni NGUMU kumtendea wema ADUI yako au mtu USIYEMPENDA. Ndio maana Yesu alisema, “Haki yenu isipozidi ya Mafarisayo, hakika hamtauingia Ufalme wa Mungu”. Kumbuka hii HAKI haimaanishi IMANI tu ila na KUTIMIZA mambo ya KIJAMII yanayotuhusu! Yesu akazidi kufundisha akisema “kunatofauti gani kufanya jema wa watu uwapendao?” maana KILA mtu anaweza kufanya hivyo hivyo! Lakini Akatufundisha namna ya KUWEZA kwa maana ni NGUMU sana kutenda kwa namana hii. Akatufundisha KUWAPENDA adui zetu na KUWAOMBEA wanotuudhi! Huwezi kumtendea wema ADUI na mtu ANAYEKUUDHI kama HUJAJIPANGA kumowmbea! Jaribu uone, ni ngumu na hata ukiweza utaishia kunung’unika ndani yako. Mara nyingi tumesikia watu wanasema “ulinifanyia hivi na vile lakini mimi bado nakusaidi”! Hii kitu acha mara moja kwa sababu hailipi! Inaonyesha hukutoa kwa moyo mweupe ambayo ni kutoa kwa hasara! Omba kama unaona unapaswa kumsaidia mtu na ni ADUI au MTESI wako.

Mfalme Hezekia alipoambiwa na nabii kwamba “tengeneza mambo ya nyuma yako maana utakufa”, Hezekia aligeukia ukuta. Akaomba na KUMKUMBUSHA Mungu matendo yake MAZURI aliyofanya huko nyuma, Mungu akampa BONUS ya miaka 15 mbele ya kuishi. Unaweza ukashindwa kuhuasinisha UREFU wa MAISHA ya mtu na MATENDO yake moja kwa moja lakini ukiangalia kwenye maandiko utagundua kuna AMRI ya Mungu ina sema “waheshimu baba yako na mama yako ili siku zako zipate kua nyingi katika nchi, na uheri pia”. Sasa naamini huwezi kumheshimu mzazi wako MOYONI tu bila kufanya kitu. Heshima inaonyeshwa kwa matendo fulani na hayo matendo basi yana NGUVU ya kuongeza UMRI wako na kusababisha UGUMU au WEPESI (uheri) wa maisha yako hapa Duniani. Kumbuka hatuongelei majaribu wala kazi ya Ibilisi, ila ni WEWE na MATENDO yako ambayo mengi yamejikita katika TABIA yako nzuri au mbaya.

Doricas alikua mama mmoja ambaye alijitoa sana kusaidia wajane wakati ule wa Mitume. Akafa. Wale wanawake wakaona haiwezekani huyu mama afe hivi hivi tu jisi walimpenda na kufaidi vipwa vyake mbalimbali. Wakamlaza Ghorofani. Wakamwita Petro wakampa kazi ya KUFUFUA mtu “wa matendo mema” ili azidi kutenda KAZI njema! Mungu akamfufua Doricas, akampa siku zaidi za kuishi. Connection iko katika “matendo yake kwa ile jamii”.

Maandiko yanasema wazi sana kua Mungu hana upendeleo, lakini nakwambia sio kila mtu anapokea sawa na mwingine kutoka kwa Mungu huyo huyo. Sehemu ya sababu hii ni MAKUSIDI na WITO wako mbele za Mungu ila na KIASI cha utii wako katika mambo mengine ya Mungu na unavyo WATENDEA watu wengine. Yesu akasema “heri wenye rehema maana watapata rehema”. Rehema ni huruma kwa matendo. Kwa mfano, watu wawili wana shida sawa, mmoja kabla hajalia shida, watu managombania kuleta michango na misaada, huku mwingine anajitahidi kuomba na kutafuta misaada ila watu “hawaguswi” na hakuna anayemrehemu hadi anakufa na shida yake! Kumbuka, ukiwarehemu watu “wowote” nawe utapata rehema kutoka “kokote”!

Korinelio alikua “akiwapa watu VITU vingi” na alikua akisali daima. Hakua mlokole, ila alikua mtu wa MATENDO mema. Biblia inasema zile “SADAKA” zilifika Mbinguni na zikawa UKUMBUSHO mbele za Kiti cha Enzi! Kumbuka huwezi kutoa kwa kiwango hiki kama huna REHEMA ndani yako. Kwa MATENDO ya Kornelio, jinsi alivyo WAREHEMU watu, Mungu akamrehemu na kumpa zawadi ya WOKOVU yeye na NYUMBA yake! Kumbuka, wakati anatoa hivyo vitu na misaada alivyovitoa vyote viliitwa “vitu” na sio “sadaka”. LAKINI kwa Mungu unapotoa hata kama umempa mtu offer ya soda katika “kutoa kwema”, hiyo ni sadaka kamili na inaenda Mbinguni “kule ambako hakuna wezi, nondo, wala kutu iharibuyo”, na Mungu huachilia BARAKA juu yako na hutajua kwamba ni ile soda tu!

Kuna uhusiano mkubwa sana wa maisha ya kawaida ya mtu na mafanikio yake ya kiroho na hata uwezekano wa kuingia Mbinguni au kutokuingia. Dhambi iko upande mmoja, ila kuna upande wa pili ambao ni ngumu kuupima. Kwa mfano, yule kijana tajiri aliyemfuata Yesu na kumuuliza afanyeje ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu aliambiwa “Je! Umezishika amri?” Kijana akasema NDIO, “Yesu akampenda!” ila akamwambia “uza ulivyo navyo na uwape masikini”. Kijana akageuka na kuondoka kwa maana alikua na mali nyingi. Sasa kumbuka, ninachotaka uone hapa ni 1. Kumshika Mungu ni muhimu, 2. Je! Hao jirani zako na watu waliojaa kila kona wajane, yatima, masikini, wenye shida mbali mbali umefanyaje? Yesu akasema “ni vyepesi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko TAJIRI kuingia katika Ufalme wa Mungu”! Wengi humu watajiona ni SALAMA kwa maana wanajiita wao sio MATAJIRI. Sikiliza, Utajiri una awamu zake. Utajiri unakua au kupungua kutokana na nini UNAFANYA au HUFANYI. Kila mtu kwa awamu yake aliyo sasa ni TAJIRI kwa hivyo vitu Mungu alivyokupa, na utajiri huu UNAKUA au KUPUNGUA kwa kadri unavyojipanga na Mungu ua na JAMII inayokuzunguka. Kumbuka, ukijipanga sawasawa na Mungu na Jamii kwa pamoja utabarikiwa DUNIANI na UZIMA wa milele. Ukijipanga KIJAMII zaidi utafanikiwa pia na utakua tajiri kwa maana “KILA apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu na KILA apandaye haba atavuna haba”. Mbegu ni mbegu usidanganyike ikipandwa ITAOTA tu! Hata kama aliyepanda ni Korinelio ambaye hajaokoka wala hajajazwa Roho mtakatifu, tofauti tu ni kwamba haendi mbinguni.

Lengo la somo hili ni kukufungua macho juu ya MATENDO yako ya kila siku kwa WATU wengine katika JAMII, ili uweze kuona jinsi ambavyo matendo yako yanaweza 1. Kuathiri umri wako wa kuishi 2. Uheri wa maisha yako 3. Kufungua misaada (rehema) kutoka kwa watu mbalimbali na Mungu pia, na 4. Kubarikiwa kwa Baraka za aina nyingi.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment