Thursday, December 12, 2013

JUA NGUVU YA NIA YAKO!!!


Katika mambo ya muhimu sana kwa maisha ya IMANI, moja wapo ni kujua NIA yako katika mambo fulani ya kimwili na kiroho. Kwa lugha nyepesi ni muhimu kujua MOYO wako “unasema nini juu ya jambo fulani” (nimetumia KUSEMA kwa maana Moyo unatoa sauti ya yale uwazayo mbele za Mungu). Au kwa lugha nyingine ni vizuri kujua “MTIZAMO wako juu ya mambo fulani” (Kuna picha/kitu halisi kinajengwa ndani yako na mawazo yako na ndicho Mungu anachokiona).

Sababu ya msingi ya kujua NIA (makusudi ya Moyo) yako ni kupima kiwango cha MUNGU kuhusika na hayo mambo UWAZAYO/UNAYOHITAJI ambayo mengi yanapita MOYONI mwako kama MAWAZO tu. Majibu ya maombi yako hayaji kwa yale mambo ambayo ULIMI wako ulitamka wakati wa maombi, bali yale mambo ambayo NIA (makusudi ya moyo) yako imetamka wakati wa kuomba. Sasa unaweza ukafikiri nataka kusema nini hapa ila ukitafakari kwa makini utagundua kwamba “unaweza kuomba au kunena jambo tofauti na unavyo NIA ndani yako (unavyo sikia/ona hilo jambo NDANI yako)”. Sikia, “Kwa MOYO mtu huamini hata akapata HAKI”, ticket ya kupokea inaitwa IMANI, na hukaa moyoni. Moyo wako ukinena (NIA) kwa imani UNAPOKEA majibu ya maombi yako! “Kinywa kinapitisha tu yaujazayo moyo wako”!

NIA yako ikisema KITU tofauti na ULIMI wako unachokisema, katika kuchagua kati ya haya MAWILI, Mungu anasikiliza NIA (makusudi ya moyo) yako na sio ULIMI (mambo yatokeayo akilini mwako) wako! Ndio maana Suleiman alisema “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.” (Mithali 16:1). Haijalishi ULIMI wako umekiri sana mangapi, je! Nia yako imejipanga sawasawa na KUSUDI la Bwana? Ukitaka MAJIBU mazuri, maandalio ya MOY O ni wewe unafanya sio Mungu, JAWABU la ULIMI kwa uombapo ni kazi ya Mungu kujibu.

Kutokana na UMUHIMU wa NIA (makusudi ya moyo) ndani ya mtu ndio maana “Mungu anachunguza moyo na kujaribu viuno”. Na katika vitu 6, naam 7 achukiavyo Mungu mojawapo ni “moyo uwazao mabaya” (Mithali 6:18). Sasa sisi tunapambana na watu kwa MATENDO au MANENO yao lakini kwa MUNGU hata ULIMI usiposema, MOYO unasema na Mungu anasikia na KUONA. Yesu akasisitiza, “sio alacho mtu hunajisi ila kimtokacho”, kwa maana kinatoka ndani ya MOYO na NIA yako inasema moyo ULICHOKUSUDIA kufanya. Kabla dhambi haijafanyika kwa jinsi ya mwili, ilianza kufanyika ndani ya moyo wako kisha UNAITIMIZA kwa MAKUSUDI ya MOYO wako (NIA).

Jifunze kudhibiti NIA yako kwa sababu hapo ndipo penye NGUVU ya kushinda au kushindwa kwako. Kama unataka kufanikwa zingatia “kulinda sana moyo wako kuliko vyote ulindavyo”. Watu wengi sana wanasahau kwamba MAWAZO ya mioyo yao yanapiga KELELE kwa SAUTI japo ULIMI haujasema kitu! Kwa Mungu hayo mawazo yanapita kama PICHA/SANAMU ndio maana Mungu anasema “umechukua vinyago na kuvitia moyoni”, yaani kule ndani yako Mungu anaweza kuona OBJECTS au PICHA japo wewe UNAWAZA tu. Yesu akasema “amwangaliaye mwanamke kwa kumtamni MOYONI mwake amezini”, sasa kila mtu anajua tamaa ni kama WAZO tu ndani ya mtu ila Mungu akiangalia kama umefuga hayo mawazo, Yeye anaona KITENDO/SAUTI/PICHA/SANAMU! Ndio maana Mungu anasema “anachukia MOYO uwazayo mabaya” kwa sabubu kwake ni VITU HALISI kuliko sisi tunavyofikiri na mara nyingi tunapuuzia tu.

Mungu alipomtokea Sulemain na kumwambia aombe kitu chochote, NDANI ya Sulemani kulikuwa na MENGI ila aliomba KUSUDI la Mungu juu ya KAZI aliyoitwa kufanya ili AMPENDEZE Mungu. Jambo hili LIKAMPENDEZA Mungu. Nataka uone kitu cha tofauti hapa. Usije ukafikiri Sulemani alikuwa na AKILI sana ndio maana ALISEMA hivyo. KUMBUKA, ilikuwa ni NDOTO tu! (1 Wafalme 3:8). Kila mtu anajua kwamba tukilala hatutumii AKILI kama tukiwa macho, sasa Sulemani aliwezaje KUOMBA kitu sahihi kwenye NDOTO? Inamaana MOYO wa Suleiman ulikuwa UKITAMANI kumpendeza Mungu (alikuwa na NIA) ambayo Mungu alipomtembelea japo ULIMI wake haukunena, NIA iliyoko ndani yake ILINENA na Mungu akajibu.

Ukisoma sehemu nyingine Bwana anasema “niko pamoja nanyi katika mipango yenu, KABLA ya kuomba mimi Bwana nitajibu, na mkiwa katika KUNENA nitasikia”! Sasa watu watakubaliana na mimi kwamba kila mmoja wetu huwa ana mipango ndani ya MOYO. Ukiwa na NIA (makusudi ya moyo) safi mbele za Mungu, hiyo MIPANGO yako katika MAWAZO yako, Mungu anasema NINASIKIA! Kabla HUJAOMBA, Mungu anajibu! Ukisoma kitabu cha Ayubu utaelewa vizuri NGUVU ya mawazo yako. Tunaambiwa Ayubu “hakumwazia Mungu kwa upumbavu”. Hili ni jambo KUBWA na Ibilisi amelificha kwa watu wengi ukiangalia ndani yao ni MAWAZO machafu tu na kuwaza vitu vya AIBU na wao hawajui kwamba mambo mawili yanatokea: i. Moyo wako unakua chukizo kwa Bwana ii. Unadhoofisha kiwango cha kupokea majibu ya maombi yako kwa maana MOYO wako unanena tofauti na ULIMI wako. Umepoteza UELEKEVU! “Na macho ya Mungu yanakimbia-kimbia diniani kote, anatafuta huo uelekevu ndani yako ili ajionyeshe mwenye NGUVU”

Petro akasema “kwa hiyo VIFUNGENI VIUNO VYA NIA ZENU, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu” (1Petro1:12,13). Hapa napata picha kwamba tunaweza KUAMUA kushughulika na NIA zetu na kizidhibiti, ndio maana tunaambiwa TUZIFUNGE NIA zotu viuno na kua na kiasi!

Kuna maswali mengi huwa najiluza. Hivi Mungu akiniangalia huku ndani ANAONA nini? Watu wengi sana utawakuta wamepiga MAGOTI kwenye IBADA kanisani/sehemu mbalimbali, lakini ndani ya MIOYO yao kwa kweli WAMESIMAMA. Jiulize tu, kwamba kweli kuna UWIANO (synchronization) kati ya USEMAYO, UTENDAYO na UWAZAYO? Watu hawatuoni lakini nakwambia kuna watu MIOYO yao inavurumisha matusi kwa nguvu kama wafanyavyo wavuta bangi. Sawa, watu hawasikii lakini nakuhakikishia leo Mungu wako anasikia SAUTI! Basi AMUA leo, katika dunia hii iliyojaa UOVU na HARUFU ya UVUNDO inayopanda kwa Mungu kila siku, wewe uwe MANUKATO na KITU cha kupendeza Mungu anapo CHUNGUZA moyo wako. Jifunze KUMBARIKI MUNGU kwa MAWAZO ya MOYO wako. Ukifanikiwa hili Mungu atajibu HAJA ya MOYO wako kabla hujaomba kwa sababu NIA yako husema kwa SAUTI mbele za Mungu.

Ukitaka kujua UMEFANANAJE mbele za Mungu, angalia NAFSINI mwako, kile kitu unachokiona ndani yako NDIVYO ULIVYO mbele za Mungu, kwa maana imeandikwa "mtu aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo".

Roho Mtakatifu tusaidie. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment