Monday, December 9, 2013

MAOMBI YENYE NGUVU!!!


Kama kuna kitu unahitaji kujua kama Mkiristo ni kuomba VIZURI. Wanafunzi wa Yesu walimwomba Bwana awafundishe kuomba kwa maana waliona wanafunzi wa Yohana wanavyoomba wakajua lazima kuna namna ya kuomba na sio kufurumuka tu na maneno bila utaratibu (Luka 11).

Kama kuna swali gumu nilikuwa najiuliza ni hili la kuomba kwa muda mrefu. Yesu anasema “KESHENI mkiomba msiingie majaribuni”, sehemu nyingine anauliza “hamkuweza kukesha nami hata saa moja tu?”. Katika Agano la Kale utaona neno “WALINZI” limetumika. Bwana anasema “Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya” (Isaya 62:6). Sasa kwa WAOMBAJI watajua hii lugha ya “KUMKUMBUSHA” Bwana maana yake ni nini. Unapoomba sio kwamba Bwana hajui, unamkumbusha tu, ndio maana “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama itupasavyo”. Sio tu kwamba hatujui kuomba ila hata cha kuomba mara nyingi hatujui hadi Roho atusaidie. Kumbuka, unapoomba hutakiwi kukaa kimya hadi utakapoona majibu ya maombi yako. Hii TABIA ya KUDUMU/KUKESHA katika maombi imejirudia tena wakati Yesu anafundisha wanafunzi wake FAIDA za kuomba BILA KUKOMA. Yesu “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:1-8). Nilinachotaka uone hapa ni aina ya UOMBAJI unaotakiwa na jinsi unapaswa kujipanga na kuwa na nguvu za kuomba kwa muda mrefu. Nitakupa moja ya SIRI muhimu za kukusadia kuwa na nguvu za kukusukuma angalau muda zaidi kidogo katika maombi.

Kuna mambo mawili nataka uone. La kwanza ni BIDII na la pili ni MUDA. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa BIDII. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa BIDII mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.”(Yakobo 5:15,16). Ukiona mtu “anajifanya” eti anatamka neno “moja tu” na mambo yanatokea, anataka kuonyesha kwamba yeye yuko juu sana na karibu sana na Mungu na miujiza ni kama tu switch ya umeme, ON/OFF matatizo kwisha! Huwa najiuliza swali hili, je! Huyu jamaa huwa anakesha na kuomba sana na sasa anamalizia tu kile alichokuwa ameomba/anomba kwa muda mrefu? Na kama sio mwombaji, je! Hii nguvu ya ON/OFF na huku ameshika kiuno imetoka wapi? Naishia hapo. Usifike mahali ukaona watumishi wa Mungu wanatumika kwa mtindo ambao hujawahi kuona ukakimbilia kusema ni PEPO. Utaingia kwenye matata MAKUBWA kama ni Mungu kweli anawatumia. Lakini pia UJUE sio kila atendaye MIUJIZA anatoka kwa Mungu.


Biblia inasema Eliya aliomba kwa BIDII! Sasa wewe unasema hapa ni kuamuru tu mambo kama ON/OFF na huna TABIA ya kukesha kwenye maombi! Kumbuka Yesu aliamuru mambo kwa mtindo huu, just ON/OFF mambo yanatokea, wanafunzi wake wakajitahidi kuiga, “IKAGOMA”! Wakamwendea wakamuuliza “mbona sisi inagoma?” Yesu akasema “mambo mengine hayawezekani ila kwa KUFUNGA na KUOMBA”. Tunasoma kwenye maandiko kwamba Yesu alikesha milimani akiomba na asubuhi anaingia hekaluni kuhudumu. Anasema “sifanyi kitu ambacho sikumwona Baba yangu akifanya!” Swali je! Aliona saa ngapi? Kama Yesu ALIFUNGA na KUOMBA, halafu wewe HUTAKI kujifunza tabia hii na unataka tu usimame kama “AFANDE” na kutoa tu ishara kwa mkono mambo yanatokea, watu wanarushwa huku na kule. Jua unakaribia MAHALI pa GUMU.

Hatua SABA za maombi zitakusaidia kuomba kwa MUDA mrefu. Kumbuka siku zote MAOMBI hayaendi bila NENO. Ukitaka kufanikiwa kuomba ni LAZIMA uwe msomaji wa NENO pia. Jipe angalau milango (chapters) 2 kwa siku. Asubuhi na jioni au muda wa kusubiri (ukiwa kwenye gari, bank, nk.) Hizi hatua SABA sio ubunifu wangu ila ni SALA ya BWANA.

Hatua ya kwanza: Liitie Jina la Bwana wa Majeshi.
Yesu alisema “mkiomba neno LOLOTE kwa Jina langu nitafanya”. Pamoja na kwamba Daudi alimkabili Goliath kwa kombeo, fimbo na jiwe, alitumia “Jina la Bwana”. Hiyo ndio siri ya ushindi wake. Sehemu nyingine Daudi akasema “hawa wanataja magari na farasi lakini mimi nitalitaja jina la Bwana Mungu wangu”. NGUVU zako za kuomba na MAFANIKIO ya uombayo yapo katika Jina la Yesu.

Sasa, unaposimama na kuanza “Baba yetu/yangu uliye Mbinguni. JINA lako LITUKUZWE”. Jiulize, litukuzwe na nani? Kama ni wewe basi anza kulitukuza jina la Bwana. Usikurupuke na kuanza tu kukemea pepo bila utaratibu hapo, No! Mtukuze Mungu kwanza. Kukemea ni hatua ya 6 huko mwisho wakati umeshajaa NGUVU. Yesu akasema “huwezi kuchukua vitu vya mwenye nguvu mpaka umemfunga kwanza”. Sasa unamfungaje mwenye nguvu wakati huna NGUVU?

Watu wanajiuliza sasa nitamtukuzaje Mungu? Sikiliza. Wana wa Israel walipovuka mto Yordani na maji yakatindika mbele yao, waliambiwa waokote mawe 12 hapo mtoni wayaweke iwe ukumbusho huko mbele kwamba “Mungu alifanya matendo makuu”. Mungu anapenda hiki kitu. Taja “matendo makuu ya Mungu” yoyote unayoyajua huko kwenye Biblia, mshangilie na kumshukuru kwa sababu ya UWEZA na NGUVU zake. Unavyozidi KUZAMA katika kutafakari na KUTAJA matendo makuu ya Mungu, taratibu utagundua kuna kitu kinatokea, unaanza kujaa CHARGE! Unavyozidi kutaja na kumtukuza Mungu, NGUVU inaongezeka na unaanza kuwa mwepesi ghafla. Hii hatua ukipita vizuri, inakupa NGUVU ya kusogea hatua ya 2.

Hatua ya pili: Ita Ufalme wa Mungu.
Hakuna ufalme usio na mfalme! Ndani ya MFALME kuna MAMLAKA na NGUVU. Sasa unapoita Ufalme wa Mungu uje, kimsingi umeagiza MAMLAKA za Mbinguni zishuke kukuhudumia wewe na mambo unayoyaombea. Ndani ya ufalme wa Mungu kuna KILA kitu unachokitaka. Mahitaji yako yote yanapatikana humo. Lakini jipange na MOYO wako vizuri maana ukiomba vitu kwa tamaa yako hupati kitu (fuatilia somo kwenye “Mafundisho ya Neno la Mungu LIKE page” lenye kichwa “Jinsi ya kumwona Mungu akijidhihirisha kwako”). Jifunze kwamba NENO la Mfalme ndio NENO la MWISHO. Huwezi kumfundisha Mfalme chakufanya kama hataki. Wewe UNAMSIHI kwamba MAPENZI yake yatimizwe . Ukifika hapo unaingia hatua ya 3.

Hatua ya 3: Jua Mapenzi ya Mungu kwa unachokiombea.
Mapenzi ya Mungu yapo katika NENO la Mungu. Huwezi kupokea kama unaomba pasipo IMANI. Na tunajua kwamba “imani huja kwa kusikia, na kusikia huja kwa NENO la Kristo”. Sasa ukiwa na Neno la Mungu juu ya “hicho” unachoombea, jua una mtaji wa IMANI. Sasa kumbuka. Unapoenda mbele za Mungu uwe kama yule mama mjane ambaye alienda BILA KUCHOKA, “akirudi-rudi kudai haki yake” (Luka 18). Ukijua AHADI zako na NENO juu ya kitu unachoomba, kaa hapo usiondoke, omba na dai ahadi yako kwa UPOLE na UNYEYEKEVU mbele za Bwana, tena bila kuchoka (usipayuke kama mtu asiye na imani). Ukirudi-rudi hadi upokee kumbuka siku zote, “Mungu huliangalia Neno lake akalitimize, na Yeye hulituma Neno kama mvua ishukavyo juu ya Nchi, Litaenda (halikosi shabaha) kwa YALE mambo aliyoliagiza na halitamrudia bure”. Hakuna faida kama unajua KITU unachoomba kipo kwenye MAANDIKO. Hapo ndio nguvu na mafanikio yako yalipo. Kama una jambo “nyeti” unataka Mungu akutendee, hakikisha unachukua kalamu na karatasi na unatafuta mistari ya KUSIMAMIA. Imani ya KUPOKEA uombacho imejikita katika UFUNUO wa hilo Neno.

Hatua ya nne: Omba mahitaji yako.
Maombi ya unachokihitaji yamejengwa kwenye hatua ya 3 hapo juu. Unapoomba RIZIKI au mahitaji mbalimbali ya mwilini na rohoni, kwako au kwa mtu mwingine, yote yamejikita katika MAPENZI ya Mungu ambayo unayapata katika Neno. Neno hilo hilo linakupa imani ya kupokea majibu ya maombi yako. Sasa kumbuka siku zote kwamba majibu ya maombi yetu yako ya aina mbili tu. NDIO au HAPANA! Jifunze kwamba hata HAPANA imo katika mapenzi ya Mungu pia. Mungu anakuwazia mema siku zote, hakunyimi kitu bila SABABU. Na imetupasa kumshukuru Mungu katika Mambo yote. Kama tumepokea au hatujapokea yote ni mapenzi ya Mungu kwetu. Ukisikia mtu anakuhakikishia kwamba “LAZIMA” jambo fulani litatokea kwa MUDA anaotaka yeye, jiulize swali hili, Je! Mungu alimhakikishia hilo jambo kwa namna hiyo? Na kama hajahakikishiwa na Mungu, jiulize tena swali hili, je! Ukiri tu ushindi NJE ya MAPENZI ya Mungu ili “kumpinda” Mungu afuate matakwa yako? Ukijua majibu, jifunze UMUHIMU wa kujipanga kwenye mapenzi ya Mungu na KUMSHUKURU kwa KILA jambo.

Hatua ya tano: Toba.
Hii hatua huwa inakuwa ya tano kama tu wewe unadumu katika maombi muda wote, ila mara nyingi sana inakuwa ya kwanza pia. Mungu ni mtakatifu, “ujasiri wa kukariba Kiti cha rehema tunaupata katika Damu ya Yesu tu” mara nyingi sana ukianza kuomba unaweza KUSUKUMWA kujitakasa. Sizungumzii hii hatua ya kujitakasa ambayo inaweza kutokea mwanzo wa maombi. Nazungumzia hii hata ya 5 ambayo sasa unazama kwenye TOBA kwa UPANA wake. Hii hatua ukiifaya vizuri itakuwa ni UFUNGUO wa matatizo mengi sana na KIPOKELEO cha maombi yako. Yesu anaagiza “kila tusimamapo kusali tusamehe ili na sisi tusamehewe”. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]” (Marko11:24-26). Ili uweze KUPOKEA jifunze KUACHILIA watu waliokukosea/wadeni wako! Nakwambia jitahidi KUSAKA “huko” ndani yako KILA mtu ambaye ukimuwaza moyoni unasikia UCHUNGU na ukimpata, MSAMEHE na KUOMBA kwa ajili yake hadi upate UHURU. Kama bado una FUNDO ukimuwaza huyo mtu jua BADO hujavuka hapo hatua ya tano. Watu wengi sana wameshindwa “kupokea wanayoamini” (Marko 11) kwa sababu wameshindwa kuvuka hatua ya tano! Omba NEEMA ya KUSAMEHE kama inakuwa Ngumu na Yesu atakusaidia kumsamehe Mtu. Kama Yesu aliweza kuwasamehe WALIOMSULUBISHA katikati ya mijeledi, misumari, taji ya miba na kuangikwa msalabani huku anatukanwa na kutemewa mate, wakati yote yanaendelea ANAWASAMEHE na kumwomba Baba awasamehe! Yaani anapigwa, ila yeye yuko kwenye maombi! Huyu Yesu anaweza kukupa NEEMA hii ya KUSAMEHE mwenzako kwa faida yako WEWE mwenyewe KUVUKA hatua nyingine.

Hatua ya sita: Shughulika na ADUI.
Watu wengi sana wamejifunza njia moja tu ya kushughulika na Ibilisi. Kila mmoja yuko busy KUKEMEA kwa Jina la Yesu! Sawa, ni muhimu lakini nataka ujifunze Neno hili. Yesu alimwona Petro jinsi anakavyo mkana kabla hajamkana! Hakikumsumbua Yesu kwa sababu “huko” katika MAOMBI yake alikwisha omba kwamba “imani ya Petro isitindike wakati Ibilisi anampepeta kama ngano”. Yesu hakumkemea Ibilisi “asimpepete Petro ila aliomba Petro ASIANGUKE kwenye hilo JARIBU na akisimama awasaidie wenzake”. Majaribu ni package (kivunge/kifurushi) sio kitu kimoja. Sasa ukiwa na utaalamu wa kukemea kuna kitu kwenye hicho kifurushi kitakuwia kigumu. Kifurushi cha jaribu kina mambo makubwa matatu. Kwanza, jambo/kitu utakachojaribiwa nacho. Pili, kitakachotokea wakati unakutana na hicho “kitu” (kupepetwa kama ngano) na tatu, kusudi la jaribu. Ufanye nini baada ya jaribu (simama na imarisha wenzako). Hakuna mwanadamu atakemea MAJARIBU yasije maana majaribu yamo katika mapenzi ya Mungu. Unapaswa kutambua mambo haya matatu kwa makini sana: jaribu (kitu kinachokujaribu), namna ya kujaribiwa, na kusudi la jaribu. Sasa ukikazana tu na kukema huwezi kufanikiwa kila kitu kwa maana katika hilo jaribu, japo ni Ibilisi anakujaribu lakini ni Roho Mtakatifu katoa kibali kwa KIPIMO! Na huwezi kumkemea Roho Mtakatifu kwa maana ndani ya hilo JARIBU kuna KUSUDI la Mungu!

Kumbuka aliyempeleka Yesu Nyikani kujaribiwa hakuwa Ibilisi. Alipelekwa na Roho Mtakatifu! Sasa nataka ujifunze KUOMBA na sio KUKEMEA tu! Omba Mungu kwamba “usianguke majaribuni na uokolewe na yule Mwovu”. Jifunze kumshinda Ibilisi kwa Maombi sio kumkemea tu. Mara nyingi sana ukikuta mambo magumu na unawekwa kwenye “kona” badala ya kukemea pia unamwambia Ibilisi “imeandikwa”, halafu unamsomea msitari wa Biblia na Ibilisi anaachilia mara moja! Kumbuka “nao wakamshinda kwa Damu ya Mwana-kondoo na NENO la ushuhuda wao”, Neno lina nguvu ya kumshinda Ibilisi. Kwanini? Yesu ni Neno! Na tumehakikishiwa kwamba ni “aheri dunia iondoshwe kuliko yodi moja ya andiko kuondoshwa”. Sasa unaweza kuona kwamba hakuna UJANJA ibilisi anaweza kufanya kushindana na Neno la Mungu. Kwa mfano ni rahisi Ibilisi kuangamiza dunia ila sio Neno la Mungu! [japo dunia inalindwa na hakuna uharibifu wa kuangamiza dunia yote ambao utatokea kama Mungu hajaruhusu. Kumbuka agano la upinde wa mvua, nk. hii dunia imewekwa akiba..]

Hatua ya saba: Rudisha Utukufu kwa Mungu.
Hii hatua ni ya muhimu sana kama hatua nyingine zilizotangulia. “kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”. Ulianza na “Jina lako Litukuzwe” na kuita “Ufalme wa Mungu uje”, sasa ukishahudumiwa na Mfalme na kuamini kwamba KILA ulichoomba kimesikika kwa Mfalme sasa lazima utoe HESHIMA kwa Mfalme! Unamalizia kwa kusema “kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!” Kumbuka kumshukuru Mungu kabla ya kupokea uliyoomba kwa sababu “imani ni hakika ya mambo YATARAJIWAYO na ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana”. Mambo yatarajiwayo maana yake hujayapata ila UNAJUA yanakuja. Haya mambo yakiwa BAYANA unapata ujasiri wa KUKIRI kwa maana una UDHIHIRISHO wa NDANI kwamba umepokea ulichoomba. Usiiishie hapo, rudi-rudi kama yule mama mjane, kukumbusha hadi uhitimishe maombi yako kwa kuona sasa kwa jinsi ya mwilini jambo limetokea.

HITIMISHO

Kama utakuwa umefuata hizi hatua saba, na kujimimina utagundua kumbe saa nzima imeisha na unataka kuendelea kuomba. Fanya mazoezi halafu unipe ushuhuda. Najua hutaanza kupiga masaa tu kwa mara moja, ila angalau utavuka hatua kwa hatua.

Jambo la muhimu sana la kujifunza katika maombi ni juu ya MAHALI na MUDA. Watu wengi sana wamesindwa kuomba kwa sababu ya kufungwa na MAHALI na/au MUDA. Ukijifunza kuomba kila mahali, ukitembea, ukipika, ukifua, ukiwa darasani, ukiwa safarini, nk., utagundua unaweza kuombea mambo mengi sana kwa siku na kurudi-rudi kwa Mungu mara kadhaa “kumkumbusha jambo” kwa sababu huhitaji kujifungia mahali. Kama unaweza kuomba kwa “kunena” ni nzuri sana hasa unapokuwa katika michakato ambayo inachukua attention yako. Mtume Paulo anatufundisha kwamba tutumie mbinu zote mbili. Kuomba kwa lugha na kwa akili pia. “usikae kimya usiku wala mchana” (Isaya 62) usifungwe na muda.

Ukisikia unasukumwa KUFUNGA, fanya hivyo kwa kipimo cha mambo unayojihusisha nayo kama umetingwa na KAZI au aina ya MAJUKUMU yanahitaji sana nguvu za mwili. Ikiwezekana jipe siku malumu katikati ya wiki na kama kazi yako inahitaji nguvu nyingi za mwili jaribu kufanya maombi ya namna hii wakati wa mapumziko ya wiki, nk. Kila mtu afanye kama Roho Mtakatifu atakavyomongoza.

Neema ya Bwana wetu Yesu na izidi kwenu mnapojifunza na KUYATENDA haya. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment