Wednesday, December 18, 2013

(MAOMBI YENYE NGUVU).....SEHEMU ya II


Katika maisha yetu ya kila siku tumetamani MAMBO mengi mbalimbali yatokee. Mengi ya haya MAMBO yako nje ya uwezo wetu na IMETUPASA kuhitaji msaada wa Mungu au watu wengine. Mara nyingi utagundua ni vigumu sana KUTEGEMEA misaada ya watu KUTIMIZA mahitaji yetu ya kila siku. Njia rahisi ni kujua jinsi ya kujipanga vizuri na Baba yako wa Mbinguni na kwa kupitia Yeye, anaweza kuinua watu mbalimbali kuja kuingilia kati hali unazopitia na kukusaidia. Ikishindikana kabisa, Mungu anaweza kuinua kunguru, mawe au Malaika kuja kukupigania, na hii imetokea kwa wengi hata kwako pia inawezekana.

Kusudi la somo hili fupi ni kutaka kuhusianisha USHINDI wako na (i) NAFASI yako katika Kristo na KUZAA kwako MATUNDA, na (ii). KIWANGO chako cha MAOMBI na pia ujue (iii). VIKWAZO vya Majibu ya maombi yako, (iv). Kutofautisha imani ya KUOMBA na KUPOKEA, na (v). Ujue jinsi ya KUJITEGEMEA kimaombi.

i. NAFASI yako katika Kristo
Mambo kadhaa ni ya LAZIMA: (a) kukaa ndani ya Yesu, (b). Neno kukaa ndani yako, na (c). Omba lolote utapewa. Yesu alitufananisha na yeye akiwa mzabibu, akasema“ sisi ni matawi ya mzabibu na yeye ni Mzabibu. pasipo yeye sisi hatuwezi jambo lolote”. Pamoja na kwamba Yesu alikuwa anazungumzia KUZAA matunda, utagundua pia mistari iliyofuata alisema juu ya MAOMBI. Kwa upande mwingine kuna uhusianao kati ya KUZAA matunda na KUJIBIWA maombi yako. (Yohana 15:1-6).

ii. KIWANGO cha maombi
Yesu alipowatuma wanafunzi wake kwenye HUDUMA mambo mengine yalikuwa magumu, japo wametumwa na Bwana! Walipomuuliza kwanini mambo mengine yanagoma? Yesu alijibu “mambo mengine hayawezekani bila KUFUNGA na KUOMBA”. Hapa tunapata picha kwamba kuna kiwango fulani cha maombi kinaweza kukuvusha hadi hatua fulani. Ukifikia hiyo hatua inahitaji GIA nyingine ya maombi ya kiwango cha juu zaidi ili uvuke kwenda kwenye hatua ya juu zaidi.

Pamoja na BIDII (diligence) na KUDUMU (persistance), haya mambo mawili ni ya muhimu sana KUPIMA kiwango cha USHINDI wako katika yale unayoyaombea. Kuna wakati itakupasa kuongeza NGUVU/KIASI cha kuomba ili kuvuka mahali ulipo. Hata kama wewe ni TAWI na UKO ndani ya Yesu vizuri na Neno (imani) limejaa ndani. (Luka 18)

iii. VIKWAZO vya MAJIBU ya Maombi yako
Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUPOKEA majibu ya MAOMBI na HALI ya MUOMBAJI mwenyewe pamoja na KUTIMIZA viwango vingine kama (i) na (ii) hapo juu. Kila mtu anajua kwamba tukiomba sio mara zote mambo hutokea wakati huo-huo. Kuna kipindi cha KUSUBIRI na wakati mwingine kinakuwa kirefu. Ili uweze KUPOKEA majibu yako angalia usikate tamaa kwa maana “Mtavuna kwa wakati msipozimia roho.” Huhitaji IMANI kubwa kupokea MAJIBU ya Maombi yako. “Imani kidogo sana kama chembe ya haradali tu, inaweza kuhamisha milima na kufanya mambo makubwa sana maishani mwako ila usipokuwa na SHAKA juu ya yale mambo uombayo”. MASHAKA ni KIKWAZO kikubwa cha kupokea uombayo hata kama una IMANI. Kwa lugha nyepesi, mashaka ni sumu ya IMANI yako. Adui anajua ukiomba kwa imani utapokea, sasa akishindwa kukuzuia usiombe, basi ataleta MASHAKA katika yale uyaombayo ili USIPOKEE. Ukiwa makini utamsikia katika “mawazo yako” akikukukatisha tamaa na saa nyingine akikuzomea kabisa. Pambana na hayo mawazo maana ni vita inayoweza kuathiri IMANI yako na majibu ya maombi yako. (2 Wakorinto 10:1-6)

iv. JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA
Watu wengi sana wana IMANI ya KUOMBA ila wachache wana IMANI ya KUPOKEA. Ukiwauliza watu juu ya maombi kwa kweli watakuambia Mungu anajibu ila ukichunguza WANACHOONA ndani ya MIOYO yao ni KUSHINDWA zaidi kuliko KUSHINDA. Matokeo yake hawawezi KUPOKEA majibu kwa maana hawana IMANI ya KUPOKELEA.

Nitakupa mfano. Pamoja na kwamba Yesu ni mponyaji na Muumbaji wa Ulimwengu, utasikia mahali anasema “imani yako imekuponya”. Ina maana imani ya KUPOKEA ni ya MPOKEAJI na sio imani ya Yesu japo kuna mahali ALIWAHURUMIA tu watu akafanya mambo kabla hata hajaombwa na mtu (Luka 7:12,13). Kati ya maeneo ambayo Yesu hakufanya miujiza ni kule mitaa ya nyumbani kwao, SABABU sio uhaba wa IMANI ya Yesu ila IMANI ya WAPOKEAJI haikwepo. Yesu hakufanya kitu japo wengi walikuwa na shida zao nyingi na aliwahurumia! Ndipo akasema “nabii hakubaliki kwa watu wake.”

v. EPUKA MAOMBI TEGEMEZI
Kuna kundi la watu wamefanya baadhi ya watumishi kama TIKETI ya kupokelea majibu ya MAOMBI yao. Sawa, kuna kiwango cha NEEMA juu ya watumishi wa Mungu kinachoweza kukuvusha mahali, lakini nakwambia kuna wakati hata YESU “alipoitizama imani ya watu, ndipo alipotenda jambo” pengine aliacha kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao! UELEKEVU wa MOYO wako kwa Yesu utakusaidia sana katika KUPOKEA majibu ya maombi yako.


Sasa tunakumbushwa siku zote kuomba kwa imani na kuambiwa kwamba “kuomba kwake mwenye HAKI kwa faa sana akiomba kwa bidii”. Jifunze na uchukue MAZOEZI ya kutumia IMANI yako kwa maana imani ina tabia ya KUKUA au KUPUNGUA. Kumbuka KUKUZA imani ya KUPOKEA majibu ya maombi yako kwa maana hiyo ndiyo inayokwamisha wengi. Kumbuka adui mkubwa wa imani ya KUPOKEA anaitwa MASHAKA.

Dawa ya kupambana na MASHAKA ni kufanya MAZOEZI ya KUOMBA wewe mwenyewe na KUPUNGUZA utegemezi wa WATUMSHI wa Mungu. Sisemi ni vibaya kuombewa, ninachotaka kusisitiza ni wewe kujijengea UWEZO wa kusimama kwa MIGUU yako MIWILI kumwamini Mungu kwamba UNAWEZA kuomba na KUOPOKEA mwenyewe. Kumbuka wewe ni TAWI la Mzabibu na mtumishi pia ni tawi tu, anayejibu maombi ni MZABIBU (Yesu). Ukiweza kuepuka utegemezi kwa MATAWI mengine utagundua UMEVUKA hatua nyingine ya IMANI na KUMPENDEZA Mungu pia kwa sababu “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani”. Wengi sana tunaweza kumshangaa Petro jinsi alivyoweza kutembea kidogo juu ya maji na ALIPOONA upepo, akazama! Hiyo ndio kazi ya MASHAKA. Nadhani kama Petro angefanya tena mazoezi kwa mara nyingine, angekuwa hahitaji tena Mtumbwi kwenda ng’ambo! Kwanini? Alikuwa na IMANI ya kutosha KUTEMBEA juu ya maji ila MASHAKA yalikuwa kikwazo.

Nitakupa mfano. Nguvu ya DAUDI na UJASIRI aliokuwa nao wakati anamkabili Goliath, haikuwa kwa sababu tu alijuwa uweza wa Jina la Bwana wa Majeshi, ila “kama alivyofanya MAZOEZI ya kupambana na DUBU na SIMBA”, alijuwa kwa jinsi ILE ILE, BWANA atampigania kwa Goliathi. Hakubakia tu KUAMINI moyoni, DAUDI alimtangazia Goliath (adui) kwa SAUTI ya juu, mambo aliyoamini. Mara nyingi sana wakati UNAOMBA, adui akileta SAUTI ndani yako za kukutia mashaka, kumbuka KUMTANGAZIA kwa SAUTI juu ya USHINDI wako. Kwa njia hii utaweza kushinda MASHAKA. Msomee adui Neno, mwambie “imeandikwa”, kisha taja Neno (imani) katika biblia unalosimamia katika hayo maombi.

Uzoefu wa kutumia IMANI yako unakupa nguvu ya kuvuka hatua nyingine ya KUPOKEA mambo uombayo katika kiwango cha juu zaidi. Ukiwa unamtegemea MTUMISHI fulani tu, MOYO wako unaanza kuwa dhaifu na unaona PASIPO kujua unahamisha UELEKEVU wako kutoka kwa Mungu na kuuweka kwa huyu MTUMISHI. Hali hii imekuwa mtego mkubwa kwa watu wengi sana, wamehamisha MACHO yao kwa YESU na wengine wamefikia mahali pa kuona MTU mwingine anahusika na matatizo yao ndio maana wakati ule dada zake Lazaro walimlaumu Yesu (mtumishi) kwa kusema “ungekuwepo hapa kaka yetu asingekufa”!

Mungu atusaidie kuongeza IMANI ya KUPOKEA majibu ya maombi yetu.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment