Sunday, December 8, 2013

NJIA YA WOKOVU!!!


Kwenye maaandiko tunajifunza kwamba watu walioanza kumfuata Yesu wakati huo wa Mitume hawakuitwa Wakristo bali waliitwa “watu wa NJIA”. Kati ya namna mbalimbali ambazo Yesu kujitambulisha, mojawapo alijiita yeye ni NJIA. Na akasema hii NJIA inatufikisha wapi. “mimi ndimi njia ya Kweli na Uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa kupita kwangu”. Hakuna njia isiyomfikisha mtu mahali fulani. Kila mtu anachagua njia kwa makusudi ya kufika mahali fulani, awe anapenda au hapendi ila kitakachomfanya afike hapo MAHALI ni njia aliyojichagulia. Yesu anashauri na kutualika akisema “ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13, 14)

Nataka tujifunze hii njia ya Yesu. Hii njia ina sifa nyingi zisizovutia isipokuwa sifa moja kwamba itakufikisha kwa Baba. Kwanza watu watakaoiona hii njia ni wachache achilia mbali watakao pita juu yake. Sasa kusudi la njia ni kupita/kutembea na wala sio kukaa au kusimama. Unapoitwa kwa Yesu, ukakubali na “kukata shauri” KUMFUATA, jua umepata MWALIKO wa kutembea katika hii NJIA. Kupata mwaliko haina tofauti na kupata TIKETI ya kusafiria. Usipochukua hatua na kupanda basi huwezi kuona mambo yaliyoko njiani. Utajifariji na tiketi yako mkononi kwa sababu imeandikwa UNAKOKWENDA ila usipoanza safari hufiki huko japo pameandikwa kwenye tiketi yako.

Sifa moja ya muhimu sana ya NJIA “hii” ni wembamba wake. Tunaambiwa IMESONGA. Kuna tofauti ya wembamba na kusonga. Katika mawazo yangu napata picha ya njia ambayo iko katikati ya kuta ndefu kila upande. Kwa lugha ya kawaida ningeiita “uchochoro”. Yaani ni nyembamba lakini pia imesongwa na kuta huku na huku. Ukiwa na MAFURUSHI makubwa UNANASA hapo kwa sababu kumesonga sana. Hii hali ya kusonga/kubana huwezi kuiona kama HUJAANZA safari. Ukisikia mtu anasema WOKOVU ni “tambarare” jiulize kwamba anapita njia gani? Maana huku kumebana, yeye tambarare anaipata wapi? Bwana wetu mwenyewe alisema “ulimwenguni mnayo dhiki lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu”, sasa alishinda nini kama kila mahali ni tambarare na hakuna vita?

Sasa kuna mambo mengi sana ukiyaangalia utagundua yanakupasa kufanya KAMA umeanza safari ya kumfuata YESU. Kwanza NJIA inaelekeza uelekeo (direction) ambao hujachagua wewe ila mwenye njia (Yesu). Utagundua kwamba huwezi kubeba kila kitu (kiburi, tamaa mbaya, uzinzi, uchungu, kutokusamehe, etc.) ukafanikiwa kupita kwa sababu njia imesonga. Kwa sababu hii njia ni ya kufikirika (theoretical/hypothetical) japo ni dhahiri (practical/real) wakati wa kupita inakuwa ngumu kuonekana na wachache wataiona pale watakapochukua HATUA. Usipochukua hatua na kuanza safari huwezi kuelewa maana ya KUSONGA!

Kuna mambo manne MUHIMU yatakatokuwezesha kutembea katika NJIA hii. La kwanza, kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako, kutubu na kugeuka. La pili, kujazwa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu sio NGUVU ila ni NAFSI ya Mungu japo pia Ana NGUVU. Roho Atakufundisha yote, kukukumbusha pia kukufariji uwapo njiani (hutakua yatima ujapopita nyikani). La tatu, kusoma Neno kwa BIDII tena KILA siku. Kama unavyokula chakula cha mwilini, lisha na roho yako ipate nguvu. Neno lina nguvu ya kukutakasa na kutenda mapenzi ya Mungu maishani mwako. La nne, DUMU katika maombi ili usianguke MAJARIBUNI na upate mwongozo (direction) uwapo safarini. Huwezi kutenda mapenzi ya Mungu kama wewe sio muombaji.


Kama hujasikia KUBANWA/KUZONGWA anza kujiuliza swali hili, Je! Umeanza safari? Na kama umeanza, jiulize tena Je! Hujabanwa/hujanasa kwa sababu umetua kila mizigo ya dhambi, uchungu, nk.? Kama unajua bado kuna shida ndani yako na hujatengeneza vizuri mambo na “kutaka amani na watu wote na huo utakatifu”, jiulize tena swali, Je! Uko njia nyembamba au pana? Ukipata majibu ya hayo maswali chukua hatua zipasazo.

Mambo muhimu ya kukumbuka ukiwa NJIANI (safarini). Kuna vibao vingi sana vya kukupoteza (DIVERSIONS). Kuna kona nyingi (mambo magumu na mateso) na njia-panda nyingi (mahali pa kuchagua kumtii Mungu au Ibilisi) na mara nyingi njia-panda (makutano ya barabara) hayako kwenye mteremko, ila yako kwenye mwinuko. Baada ya kuchoshwa na “safari”, unafika njia-panda, kushoto (kwa Ibilisi) ni mteremko na kulia (kwa Yesu) ni mlima zaidi! Kama UMEKAZA uso wako kwa Yesu, utapita KONA zote, na ukifika NJIA-PANDA utapinda kuelekea tena kwenye NJIA nyembamba (kwa Yesu) hata kama huko mbele ni MLIMA zaidi.

Ukizidi kuendelea na safari utagundua kuna MABANGO makubwa yameandikwa jina lako. Mengi ya haya mabango yamebeba lugha ya kukebehi, matusi, kukatisha tamaa, kukera, nk. Usiangalie MABANGO, kaza uso wako kwa Yesu kama Stefano. Sio rahisi, hata Yesu amesema sio rahisi ila njia inapitika. Wakati Stefano anapigwa mawe, hakukimbia badala yake alipiga magoti. Akatazama juu USHINDI wake ulipo! Hakutizama warusha mawe (MABANGO), hakusikiliza wanayosema wakati wanarusha mawe (ujumbe kwenye mabango), aliangalia JUU. Badala ya kuwarushia maneno ya LAANA, Stefano alikua busy kuwaombe watesi/wauaji wake msamaha. Wakati watu wanaona damu inatiririka mwilini mwake, Stefano alimwona Yesu na Jeshi la malaika watakatifu. Wakati watu wanaona mauti, Stefano anaona UZIMA wa MILELE! Akakaza USO wake kwa BWANA na kumaliza SAFARI yake salama.

Jiulize ni watumishi wangapi leo wataambiwa wana BELIZEBULI wasipigane ngumi? Jiulize ni wana wa Mungu wangapi leo wakinenewa tu jambo hata kama ni la uongo wanakwazika na kuwa wakali? Eti wanachafuliwa majina na kuvunjiwa heshima! Sawa, ila mtizame yeye aliyejiita “NJIA” ambaye tunamfuata,“Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.” (Yohana 13:2-4). Yesu alipogundua ana KILA KITU (kwa lugha ya kawaida tungesema UTAJIRI wa kila namna), na yuko kwenye njia (safarini) “Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa ALITOKA KWA MUNGU NAYE ANAKWENDA kwa Mungu” akijua hayo, alivua VAZI lake (sio kukunja shati mikono au kukunja suruali), akajifunga kitambaa kiunoni, akachukua maji (hakumtuma mtu akalete kwa maana wakati huo alikuwa ni MTUMISHI anayetumika), akainama, akawanawisha na kuwafuta kwa kitambaa (nguo iliyo mwilini mwake)! Huyu ni Bwana na NJIA tunayoifuata.

Ujumbe huu umekuja kukumbusha habari ya NJIA na yatupasayo kufanya katika NJIA hii. Mungu atupe NEEMA ya kujikagua na kupata UTHIBITISHO wa ndani kwamba tuko njiani au la! Roho anashuhudia pamoja na roho zetu kama sisi ni wana wa Mungu, naye Atatupa kutambua kwamba tuko katika njia gani kwa maana haachi kushuhudia juu ya “DHAMBI, HAKI na HUKUMU”. Msikilize Roho Mtakatifu na MAELEKEZO yote atakayokupa, UTAFIKA salama kwa BABA.

NEEMA ya BWANA wetu YESU KRISTO iwe nanyi tangu sasa na hata MILELE AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment