Thursday, December 26, 2013

NDOA YA YUSUFU NA MARIA!!!


Nimetamani sana tujifuze jambo katika ndoa ya Yusufu na Maria. Nimechukua mfano huu kama ndoa/uhusiano wowote wa mwanaume na mwanamke ambao lengo lake ni kuishi kama mke na mume.

Kuna mambo kadhaa najifunza kwa maisha ya binafsi ya Yusufu na Maria. Yusufu alikuwa mtu wa haki, mtu mwenye heshima yake na jina jema katika jamii iliyomzunguka. Aliukuwa na kazi yake ya useremala ambayo yamkini ilimwingizia kipato. Kwa upande mwingine hatuambiwi Maria alikuwa anajishughulisha na nini ila alikuwa BIKIRA, ikimaanisha alikuwa msichana aliyejitunza na kuishi maisha masafi. Hawa wawili walikuwa wachumba na walidumu katika UHUSIANO huo katika USAFI wote. Kuna mambo manne (4) nataka tuone hapa. (Luka 1)

i. Kipindi cha Giza

Wakati maisha yanaendelea, ghafla! Malaika analeta habari kwa Maria kwamba atapata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu na atazaa mtoto wa kiume. Kwa Maria ilikuwa ni habari ngumu ila alikubali kama MTUMWA kwa Bwana wake kwa sababu alijua ni mapenzi ya Mungu. Sasa nisikilize vizuri, wakati Malaika Gabriel analeta habari kwa Maria kwamba AMEBARIKIWA, tena amebarikiwa kuliko wanawake wote, na kwamba mtoto atakayezaliwa atarithi kwenye kiti cha mfalme “Daudi”, Maria anasikai raha hadi anaenda kwa ndugu yake Elizabeth [mama yake Yohana mbatizaji], anamshangilia Mungu kwa wimbo na wanajazwa Roho Mtakatifu pale na Yohana naye anashangilia kwa kucheza akiwa huko tumboni kwa mama yake. Sasa nataka uone kitu ambacho mimi nakiona. Wakati Maria anaitwa AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote, kwa Yusufu ilikuwa sio Baraka ila ni balaa tupu. Kwa maana binti aliyemwamini kabisa sasa ni mjamzito katika mazingira ambayo hayaelewi, wala hajawahi kusikia kitu cha sampuli hii kimetokea wapi (all was new experience), hakuna mahali pa kurejea (reference) na wala hakuna mtu anaweza kumshauri kwa maana katika ELIMU ya dunia wakati huo hakuna mahali kitu kama hicho kimeandikwa/kimetokea. Watu hawajui nini kinaendelea. [Angalizo: Sio kila jambo kwenye ndoa/uhusiano wako utapata mjuzi wa kukusaidia, jifunze kujipanga na Mungu kwa mambo ya ndoa yako]

Katika hali hii ya GIZA, Yusufu akaamua KUMWACHA Maria kwa siri! Hii ni hali ya kuchanganyikiwa ambayo wengi wanafika katika mazingira magumu katika mahusiano yao. Ghafla tu unaona hiki “kitu” ni kigumu na unaona hakuna njia tena na unajiambia “basi bwana kama ndio hivi basi mimi naacha” au “mimi nimefanya sehemu yangu ila mwenzangu amenisaliti, naachia ngazi”, au “kwani mimi ndio wa kwanza kuachika”, “kwa vile ameenda kupata mimba huko basi na mimi sioni tena haja ya kujitunza”, “kwanza nina kazi yangu na simtegemei, potelea mbali maisha yataendelea”, nk. Ni hali ya kukata tamaa. Hiki ni kipindi cha giza. Na mwili unataka kuleta majibu ya haraka (instant solutions), kukimbia na kupotelea mbali. Lakini Malaika anakuja kusema na Yusufu na kuugeuza Moyo wake. Sijui kama Yusufu alikuwa mwombaji ila tunaambiwa Mungu alisema naye, akasikia na KURUDISHA moyo nyuma. Usipo jifunza kukaa katika MAOMBI ni vigumu kuvuka hii ngazi. Hapa ni kipindi cha KUNGOJA maana unajisikia huku ndani kwamba BADO hujapata/hujafika mahali unataka. Kumbuka “wamngojao Bwana watapata NGUVU mpya”. Unahitaji Nguvu mpya kila siku kuvuka hapa. Utagundua ule “upendo wa zamani umepoa”, sasa unahitaji NGUVU mpya. Muombe Mungu akupe nguvu mpya.

ii. Kutembea katika Baraka

Mara nyingi watu wamefikiria Baraka za Mungu kwa upande mmoja tu wa kuwa na hela, majumba, magari au kufanikiwa katika mambo ya mwilini na kusahau upande mwingine. Utasikia watu wanasema “count your blessings” (“hesabu Baraka zako”). Sasa unajua huwezi kuhesabu KITU ambacho hukijui na wala hukioni. Nakwambia Leo kuna Baraka nyingi sana Mungu anatubariki na hatuwezi kuziona wala kuzihesabu kwa maana ziko kwa jinsi ya ROHONI na kwa sababu huzioni hujui kwamba UMEBARIKIWA na unabaki ukilalamika na kunung’unika kwa sababu ulishamwekea Mungu vigezo na vitu fulani kwamba “hiki kisipotokea basi sijabarikiwa bado”. Kama mambo yako “hivi” basi bado hakijaeleweka, nk. Maria alichukuwa tu kama Malaika alivyosema na “akayatia moyoni mwake” huku akijua kwamba AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote. Kwanini aliweka moyoni mwake? Kwa maana hakuna mtu wa kawaida anaweza kuelewa hii lugha ya kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Akajua ni Mungu na hakuna haja ya kutoa maelezo ya ziada au kuuliza watu au kupeleka umbea. Akakaa mimya.

Hebu mfikirie Yusufu. Wakati anajua kabisa hii mimba sio yangu ila anamhudumia Maria. Wanaenda huko mbali mji mwingine kuhesabiwa na mama hajiwezi mimba ni kubwa. Yamkini huko njiani Yusufu alitembea kwa mguu wakati mkewe mjamzito yuko juu ya punda na yeye anakokota huku mbele, ila mimba sio yake! Yule mama anajifungua hapo, Yusufu anamsaidia, ila mimba sio yake! Ni mambo magumu kuelewa ila Yusufu alikaza USO kufanya MAPENZI ya Mungu kama Malaika alivyosema. Hapo hampendezi Maria, ila Mungu, kwa maana yeye alichagua kitu cha kumfanyia Maria tayari, yaani KUMWACHA kwa SIRI! Sasa huu mpango wa kubaki ni mpango mpya ambao anaambiwa na Malaika na anaamua kuutimiza mpango huu japo haelewi vizuri. Mimba sio yake! Na sio hivyo tu, hajawahi kumgusa kabisa huyu mama! Analea mimba miezi 9, akijua kabisa sio yeye!

Kumbuka sio kila kitu Mungu atafanya juu ya maisha yako UTAELEWA. Baraka nyingi sana tunapata sio BINAFSI. Mungu amelenga KUWABARIKI wengi kupitia BARAKA alizokupa. Katika kubariki wengi LAZIMA kuna UDHIA. Ndio maana Yesu alisema “hakuna mtu aliyeacha ndugu, wazazi, shamba, nk. na kumfuata asipate hivyo “vitu” mara 100 hapa duniani ila na UDHIA pia”. Watu wengi sana wanapenda BARAKA ila BINAFSI, wanasahau kwamba Mungu akishusha Baraka mara nyingi sana hulenga wengi sana kwa Baraka hiyo hiyo, na imekuwa udhia. Kwa maana sio UPENDAVYO wewe ila sasa ni kama WAPENDAVYO wengine pia kupitia Baraka hiyo hiyo. Hebu fikiri wewe ni Maria (mama wa Yesu), unaitwa MBARIKIWA kuliko wanawake wote, ila kijana hakai nyumbani, anapita mitaani KUHUBIRI vitu hata huelewi, ukimuuliza anasema anafanya MAPENZI ya Baba yake! Huku Yusufu naye haelewi pia. Ghafla! Watu wanajaa kila mahali hata hakuna muda wa kula na kuongea kama familia! Huwezi tena kusema huyu ni MWANANGU kwa maana hata yeye anasema “hawa wa hekaluni ndio mama na ndugu zangu”. Kijana anasema lugha ngumu-ngumu tu kila saa! Huku mtaani wanasema kachanganyikiwa (karukwa na akili) na wengine wanasema kijana ana pepo! Hebu fikiri hii ndio ile kitu Mungu anasema ni BARAKA!

iii. Machozi kwenye Baraka Yako

Bila shaka Maria na Yusufu walikuwa na vipindi vigumu na Yesu, japo waliitwa WABARIKIWA. Ghafla wanaambiwa wahame nchi kwa maana Herode anataka kumuua mtoto! Wanakimbilia Misri, sijui walikuwa na usafiri gani ila najua haikuwa rahisi. Hebu fikiri ghafla! unajikuta unaanza kupiga mahesabu ya kuacha kazi yako kama Yusufu kwa sababu ya hii BARAKA iliyokuja kwenye familia. Hebu fikiri wale wateja wake ambao alikuwa anawatengenezea furniture, anawaagaje? Hebu fikiri wale ndugu zake sasa hapo mtaani anawaagaje? Eti, anahama nchi! Maana sio tu hawamwelewi, ila wanamwona kachanganyikiwa pia. Hii ni BARAKA imeingia katika familia na watu wanaanza kuhangaika. Sasa ukifika mahali pa kukata tamaa jua UNAHARIBU ile Baraka ya Mungu kwa maana sasa inakuja kwa MTINDO ambao haujautarajia. Nakwambia kila mtu atakuelewa ukiamua kuitupilia mbali hiyo BARAKA isipokuwa Mungu. Lakini nakwambia ni aheri KILA mtu asikuelewe ila Mungu akuelewe inapofika kufanya MAPENZI yake.

Ndoa nyingi sana ni BARAKA katika maisha ya watu na pia Mungu amelenga hizi ndoa ziweze kuwa BARAKA kwa watu wengine. Utakuta hapo katikati kumetokea MAMBO magumu na watu wamesamabaratika na KUTOKA nje ya kusudi la Mungu. Sawa watu watakuelewe kwa maana kwa kweli “huyu jamaa” amekuwa kama kichaa kabisa, ila kusudi la Mungu ni nini? Nakwambia kuna BARAKA ambayo Mungu alitarajia watu wengine waipate kupitia NDOA yako ila sasa Ibilisi ameisambaratisha na amefuta BARAKA kubwa ambayo wengi wangeipata kupitia NDOA yako! Sio kila KUACHANA ni suluhisho hata kama mazingira yote ya KISHERIA na KIJAMII yamekaa sawasawa na kila mtu anakuunga mkono. Kumbuka Yusufu angeweza kumwacha Maria mapema tu akiwa kama mtu wa HAKI, ila alikaza uso kutimiza Mapenzi ya Mungu. Je! Unajua mapenzi ya Mungu kwa NDOA yako? Je! Kila mmoja anajua WITO wake na mlichoitiwa kufanya shambani mwa Bwana? LAZIMA kipo. Hebu fikiri hii MISUKOSUKO yote ya NDOA ya Yusufu na Maria halafu hawajui WITO wao ingekuaje? Mkijua kila mmoja alichoitiwa mtapona kwa urahisi zaidi katika VITA vya adui.

iv. Mahali pa Ushindi

Wakati Maria na Yusufu wanapita nyakati mbalimbali ngumu na BARAKA ya mtoto Yesu, inafika takriban miaka 30 ambapo sasa KIJANA anakomaa kuwa mtu mzima. Mara kijana anakuja na agenda za KUFA kwa ajili ya ULIMWENGU! Maria haelewi wakati kijana anasema “mkila mwili wangu na kunywa damu yangu mnauzima wa milele”! Pamoja na kupita hivi vipindi vizito sasa kijana anataka KUFA! Eti yeye ni kondoo wa SADAKA. Matarajio ya Maria alijua siku moja yeye atakuwa mama wa MFALME, mtu tajiri mtaani na watu wote, wakubwa kwa wadogo wanamwamkia na kumheshimu. Maria anapiga picha ya KIONGOZI mkubwa kwa jinsi ya mwili lakini KIJANA anakuja na AGENDA za kusulubiwa sasa. Yamkini nguvu ya kushinda mambo yote magumu ilikuwa kwenye matumaini kwamba SIKU MOJA huyu kijana atakuwa mfalme kwenye kiti cha Mfalme Daudi na hapa nitapumzika. Mambo yanakuja kinyume na matarajio yake japo anajua kuwa AMEBARIKIWA. Huyu mama anafuata kila hatua, anaona kijana anakamatwa, anapelekwa Golgotha kusulubiwa kama MHALIFU. Hebu fikiri hapo. Mama anamjua mwanae vizuri sana. Anajua ni mcha Mungu leo ghafla tu anasingiziwa vitu VIGUMU na sasa wamempiga vibaya damu inatiririka kila mahali na wanampeleka kumgongomelea MASALABANI. Mama analia Yesu anasema “USINILILIE mama, jililieni wenyewe!” Yesu alijua ili hii BARAKA ikamilike ni LAZIMA asulubiwe kwa maana yeye ni “Mwana-kondoo wa Mungu achukuaye dhambi za ulimwengu”. Hii ni Baraka kubwa ila haijakaa kwa namna watu wengi wataiona kama Baraka! Wengi wangelalamika na kuona ni BALAA kubwa kwenye familia! Kama unatarajia UZIMA wa Milele jifunze kusoma LUGHA za rohoni katika Baraka zako kwa maana nyingine zinakuja kwa mtindo ambao unaweza kukemea ukidhani ni Ibilisi au jaribu. (Luka 23)

Lengo la somo hili ni kutaka kukufungua macho juu ya mambo ambayo Mungu anafanya katika maisha yetu na tukumbuke kumshukuru hata kama hatuelewi kila kitu kwa maana “Mungu amekusudia mambo mema kwa ajili ya watoto wake kila siku”. Angalia usibebe roho ya KISASI kwa mambo yatakayokukuta katika MAHUSIANO kwa maana KILA uhusiano/ndoa itapita katika VIPINDI vigumu na vyepesi, vipindi vya huzuni na furaha, vicheko na vilio, nk. Angalia sana katika VIPINDI hivi usimkosee Mungu kwa sababu tu HUELEWEI mwenzako anafanya nini. Yamkini ameamua kukusaliti na wanawake/wanaume wengine na umejua. Kwa maana kama wewe ni mtu wa Mungu “hutakosa kuzijua HILA za Ibilisi na Mungu hatawaficha watu wake jambo”, na umefika mahali UMEJUA. Chunga USIMKOSEE Mungu kwa sababu mwenzako amemkosea Mungu. Uhusiano/NDOA ina mwisho ila uhusiano wako na Mungu hauna mwisho. Ukijua kwamba MATESO yako ni ya KITAMBO tu, usikubali KUPOTEZA hatma yako (mambo ya milele) kwa sababu ya mambo ya kitambo tu. Kaza uso wako kwa Mungu na kaa katika KUSUDI lake na WITO ulioitiwa ili ile BARAKA Mungu aliyoweka katika maisha yako ISIPOTELEE njiani. Tafakari yaliyo juu aliko Kristo kwa maana huku Duniani kuna ufisadi mwingi. Angalia MWISHO wa safari yako na ujitie moyo katika Bwana. Mambo yanayotokea kwenye uhusiano wako yasiujaze moyo wako hata ukakosa shukrani kwa Mungu wako.

Neema na Rehema zitokazo juu ziwahifadhi NIA zetu tangu sasa na hata milele. Bwana yu karibu.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment