Thursday, December 5, 2013

MUNGU ANAONA NINI NDANI YETU?


“Mkinipenda mtazishika amri zangu” na “azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” (Yohana 14:14,22).

“Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula? Yesu akawaambia, Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.” (Yohana 4:33,34).

Nimejiuliza sana maswali kwamba Mungu huwa anatuonaje tunapokwenda mbele zake? Je! Tunajiona angalau kwa sehemu na kujitambua kwamba tukoje mbele zake?

Umewahi kujiuliza ile nguvu tunayoweka katika MAOMBI na KUFUNGA na jitihada ya kutafuta MSAADA wa maombi kwa watumishi mbalimbali wa Mungu wakati tukiwa na mahitaji ya mambo ya MWILINI kama kufaulu mitihani tukiwa shule, kupata kazi, kupanda cheo, kupata wachumba, biashara zetu kufanikiwa, kupona magonjwa, nk.? Umewahi kujiuliza ni NGUVU KIASI GANI unaweka katika MAOMBI ili uweze: kujua WITO wako, kumpendeza Mungu, kukaa katika mapenzi yake, kuishi maisha ya utauwa, nk.? Ukiweka katika mizani uzito wa MAOMBI na NGUVU tunazotumia katika mambo ya mwilini na ya Mungu unaona TOFAUTI gani?

Je! Unafahamu pamoja na Wana wa Israel kutoka Misri na kuvuka Baharini kwa ushindi, kwamba walipomkasirisha Mungu kwa matendo yao bado walifia jangwani? [kwa nyoka za moto, kumezwa na ardhi, nk.?] Je! Tunajitahidi kwenye maombi kupata mafanikio na tukiisha kuvuka kile kipindi cha shida tumdhihaki na kumtukana Mungu aliyetuvusha kwa matendo yetu maovu? Tena tunamtenda dhambi kwa kuvitumia vile vitu alivyotubariki navyo? Umewahi kujiuliza kwamba ni kwanini Mungu asikuache katika hali NGUMU ili uzidi kumtafuta maana akikuinua tu kidogo unamsahau? Mungu ni wa REHEMA na si mwepesi wa hasira, anatupa kila siku ingine tena nafasi ya kutafakari njia zetu na kuona “kama iko njia ya kuleta majuto” ndani yetu ili tumrudie KUTUBU na kumwishia.

Haya maswali yalinipeleka kuwaza JE! TUNAMWOMBA MUNGU KAMA TUNAMPENDA AU “TUNAMTUMIA” TU KWENYE SHIDA ZETU KISHA KUMWACHA? Mungu anaona tunampenda YEYE au DUNIA zaidi?

“Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”(Torati 8:18)

NEEMA NA BARAKA ZITOKAZO KWA MUNGU BABA ZIWE NANYI TANGU SASA NA HATA MILELE. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment