Monday, December 2, 2013

PIMA HATUA ZAKO!!!



Ukitaka kujua umbali au kimo utakachofikia kiroho angalia aliko kiongozi wako wa KIROHO. Kwa maana yatosha mwanafunzi kulingana na mkufunzi wake ila hampiti.

Sasa nisikilize vizuri. Kila ajikwezaye atadhiliwa naye ajidhiliye atakwezwa. Ninazungumzia tabia ya ndani ya unyenyekevu ambayo Mungu anaipenda. Kupitia tabia hii mtu huinuliwa na kuwa MKUU kuliko wenzake kwa kukubali kuwa MDOGO kuliko wenzake. Kuna kundi dogo la watu ndani ya Kanisa ambao wao watanyenyekea chini ya Mkono wa Mungu na viongozi wao. Kama wamezingatia mambo matatu yafuatayo kati ya mengi watafika mbali: 1. watautafuta uso wa Mungu kwa BIDII, 2. wataacha uovu na kusafisha njia zao mbaya 3. watatafuta kusudi la Mungu hata kama hawapati faida kwa jinsi ya mwilini. Sasa hili kundi dogo, kwa maana ni dogo kweli, litajikuta na nguvu nyingi sana za kiroho na watafanikiwa kwa jinsi ya rohoni na mwilini kwa kadri watakavyokaa katika kusudi la Mungu.

Mambo kadhaa yatajitokeza.
1. VITA na VIPINGAMIZI kutoka kwa viongozi wao na watu wengine kwa sababu ya wivu. Hali hii ya kuinuliwa ikiibuka katika kundi hili dogo, wapo watakaovumilia na kunyenyekea na kudumu hapo chini ya viongozi wao na wengine wataondoka na kuanzisha huduma au kujiunga na viongozi wengine. Sasa hii ni hali ya kawaida sana kwa nyakati tulizo nazo kuwa na makundi ya namna hii.TAHADHARI! kwa lile kundi linalohama kwa sababu ya MADHAIFU ya walikotoka. Angalia usihame kwa KIBURI ila uhakikishe ni makusudi ya Mungu juu ya maamuzi unayofanya maana unaweza kujikuta umepoteza ile nguvu uliyodhani unayo. Katika hili twajifunza pale ambapo Yesu alipoanza huduma, na nguvu za Mungu kudhihirika sana katika maisha yake, vita iliibuka kwa wakuu wa DINI. Kumbuka, Yesu hakufanya kitu ambacho hakumwona Baba yake anafanya, ilikua ni mapenzi ya Mungu kabisa ila VITA ilikuwa kali. Kila mtu asimamaye katika mapenzi ya Mungu kwa uelekevu na kumpendeza LAZIMA Mungu atajidhihirisha kwa maana “jicho la Mungu linakimbia-kimbia duniani kote kumsaka mtu wa namna hii ili Ajionyeshe mwenye nguvu”. Usistushwe uonapo vita wakati unajua ufanyacho ni mapenzi ya Mungu. Simama katika nafasi yako kwa unyeyekevu na fanya huduma uliyoitiwa kwa uaminifu.
2. Mungu atawapa hili kundi dogo nguvu za maamuzi katika kanisa au huduma wanakotumika. Kwa kadri hili kundi dogo linavyojinyenyekesha na kumtii Mungu, Mungu atawapa hekima na maarifa hata na nguvu za kiuchumi kiasi kwamba hawa VIONGOZI watawatafuta kwa ushauri, msaada na mambo mengine ya kihuduma na mwishowe kama hawa WAKUU wanazidi “kulala”, maamuzi mengi au makubwa yatategemea hili kundi dogo la watu walioamua kumpendeza Mungu na kuutafuta uso wake kwa bidii hata kama majina yao hayapo kwenye orodha ya mashemasi, au watu wowote wenye vyeo kanisani. Kumbuka mfano wa Paulo. Japo alikuwa mfungwa kati ya wafungwa wengine na wasimamizi wao, wakati wanasafirishwa baharini yeye alikuwa ndio anasema cha kufanya na watu wanamsikiliza kwa sababau kwa wakati huo ndiye aliyekuwa amesimama na mapenzi ya Mungu peke yake na anatenda makusudi ya Mungu hata kama ni mfungwa.


Wakati VIONGOZI wengi sana wanasahu kazi ya “mchungaji wa kondoo” na wanageuza hiyo huduma kama “mchungaji wa mshahara”, hawatajua ni saa ngapi hili kundi dogo limekamata usukani na kusukuma kazi ya Mungu mbele wao wakiwa busy na miradi yao. Jipange katika nafasi yako na ni MARUFUKU kumnyooshea mtumishi wa Mungu kidole. Fanya kazi ya huduma na ONGOZWA na Mungu. Kama jinsi DAUDI alivyosimama katika nafasi yake wala hakushindana na Mfalme SAULI japo alitaka kumwangamiza, kaza macho yako katika WITO wako na acha VITA na wanadamu. ADUI yetu ni Ibilisi peke yake! Daudi hakufurahia kuanguka kwa Sauli japo kibinadamu Sauli alikuwa ADUI kwa Daudi! Alijua japo yeye amepakwa MAFUTA ila alihehimu nafasi ya SAULI hadi wakati wa Bwana ulipotimia. Na aliomboleza KIFO cha SAULI, hakufanya SHEREHE kwa sababu alijua kwamba pamoja na madhaifu ya SAULI, bado alikuwa ni MASIHI wa BWANA! Uwe makini Mungu anapokuruhusu kuona MADHAIFU ya watumishi wa Mungu!

Mara nyingi sana watu wamejisahau na kufikiri MUSA atadumu milele! Yamkini wewe ni Joshua au Kaleb na hujitambui. Na mara nyingine kuna watumishi kama Eliya ambao wanadhani wengine wote wamekwisha na wako wenyewe kwenye HUDUMA, kumbe Bwana amejisazia Elfu saba wasiopiga goti kwa Baali. Hapa nazungumza na hawa Elfu saba, Joshua na Kaleb. Wamo katika kundi kubwa la WALIOITWA na watafuata kuchukua MIKOBA ya VIONGOZI wao na kupeleka kazi ya Mungu mbele. Mara nyingi hawa watu hawaandaliwi na mtu, Mungu huwaandaa mwenyewe na atakupaka mafuta huko huko MACHUNGANI kama Daudi. Wakati unapambana na DUBU na SIMBA, jua unaandaliwa KUMSHUGHULIKIA Goliath katika KIZAZI chako. Baadhi watakulia miguuni pa Makuhani kama Eli kama ilivyokuwa kwa Nabii Samweli. Vyovyote itakavyokua, kama Mungu anakuaanda huko VICHAKANI kama Daudi au HEKALUNI kama Samweli, kaa katika kusudi la Mungu na jipange sawaswa maana kwa jinsi ya MWILINI wengi hawakuoni na yamkini wanakudharau kwa sabau wewe ni kijana wa kuchunga mbuzi tu ila siku UPAKO wa DAUDI unadhihirika juu yako ndipo watakapojua kuwa UKIMYA wako ulikuwa MBELE za Bwana ukijifunza na kukuwa kwa NDANI.

Neema na Rehema zitokazo juu ziwe nanyi tangu sasa na hata Milele. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment