Tuesday, April 30, 2013

ITAMBUE NAFASI YAKO KAMA KIJANA ILI ULETE MABADILIKO KATIKA MAISHA YAKO NA JAMII KWA UJUMLA(01)

Jesus Up!
Karibu katika safu hii ya mafundisho ya vijana yanayoitwa Nafasi ya Kijana. Tutakuwa na mambo kadha wa kadha ya kujifunza kuhusu Nafasi ya Kijana kwa ujumla wake tukimwangalia Kijana na sehemu anazotakiwa kusimama au wajibu anaotegemewa kuwa nao na kuufanyia kazi au majukumu aliyonayo katika maeneo mbali mbali yanayomuhusu.
Ni mafundisho yanayolenga kuleta ufahamu sahihi juu ujana na Kijana kama Ufalme wa Mungu unavyomtambua na kumtegemea pia. Lengo letu kuu ni kuwafanya vijana wawe wanafunzi wa Yesu kwelikweli kwa kufundishwa KWELI ya Neno la Mungu kuhusu Nafasi yao katika upana wa maisha yao.

Ni muhimu kila Kijana akafahamu mambo yafuatayo kuhusu yeye:
1. Ni lazima ujitambue, upate ufahamu sahihi juu ya maisha yako pamoja na mambo yote na jamii inayokuzunguka
2. Ni muhimu ujue wajibu ulionao kwako wewe mwenyewe kama mtu binafsi juu ya maisha yako
3. Kuna haja ya kujua kuwa wewe ni sehemu ya familia yako na lazima ujue wajibu wako kwa wazazi na familia kwa ujumla
4. Ni lazima ujifunze kuwa mzalendo wa taifa lako sawa na jinsi ambavyo Mungu anataka, fahamu kuwa umeunganishwa na ardhi ya Tanzania kwa mafanikio yako, Mungu akikwambia nenda nje ya nchi nenda lakini
 usifikiri mafanikio hayako Tanzania
5. Kijana anatakiwa ajitambue, ajielewe yeye ni nani na ana kusudi gani katika maisha yake
6. Unatakiwa kupata uelewa wa kutosha juu ya kipindi cha ujana na umuhimu wake ukiwa bado Kijana ili ujue namna ya kuzingatia na kujipanga kwa hapo baadae
7. Kuelewa changamoto zilizopo katika kipindi cha ujana na namna ya kuzishinda kuna uhusiano na namna unavyojitambua ukiwa bado kijana
8. Kujenga shauku, nia na kiu kwa kijana ili aweze kuishi maisha yenye mwelekeo na aweze kutimiza maono yake akiwasaidia na wengine kumjua Mungu na maisha yake kwa ujumla wake
9. Kuwekeza uthamani na nguvu ya kipindi cha ujana kwa mtazamo wa Ufalme wa Mungu

UELEWA JUU YA UJANA NA KIJANA;
 Ujana ni hatua ambayo mtu anaipitia baadaya utoto au ni kipindi cha kati cha makuzi ya mtu kabla ya utu uzima na hatimae uzee
 Ujana huanza mara baada ya mtu kubadilika kimaubile na huanzia miaka kumi na mbili wengine hadi kumi na tano ambapo mtu huanza kuwa na hisia za kimwili na kutamani sana kuwa na uhuru wake katika maamuzi. Mabadiliko haya huchochea au hupelekea hisia mbalimbali za kimwili na mabadiliko ya jumla ya tabia
 Ujana ni majira yanayopita katika makuzi ya mwanadu, ukifanikiwa kuwa mzee ni lazima ulipita katika kipindi hiki au daraja hili la ujana, kwa hiyo kama bado uko katika dara hili ni muhimu kujipanga ili usije ukajilaumu mbele ya safari

ZINGATIA HII;
“Huwezi kuyajali maisha yako kama hujui thamani yake, huwezi kujua thamani ya maisha yako kama hujajitambua kwa Neno la Mungu, huwezi kuwa na maisha ya mafanikio kama maamuzi yako hayatengenezi mafanikio, ufahamu sahihi juu ya maisha yako ndio msingi wa kujitambua kwako, yaani kuijua Kweli ili hiyo Kweli ikuweke huru na ndipo utakapokuwa huru kweli kweli, kumbuka hata usipoamua maisha yako yataendelea kama kawaida. Zaidi ya hayo kama hujui wewe ni nani huwezi kujua thamani yako, kama hujui thamani yako lazima utaishi chini ya kiwango cha maisha unayotakiwa kuishi”

UTAIJUAJE NAFASI YAKO KAMA KIJANA;
Nafasi yako kama Kijana ni wajibu wako, umuhimu ulionao kwako na kwa jamii kwa ujumla wake pamoja na familia yako.

Lazima ujue Nafasi yako katika maeneo yafuatayo:
• Kwako binafsi, • Kwa familia yako, • Kwa kanisa lako, • Kwa jamii yako • kwa mkoa wako, • kwa taifa lako na • kwa Ufalme wa Mungu.

Safari ya kujua Nafasi yako katika maeneo yako hayo yote inaanzia katika neno moja tu: KUJITAMBUA.

Jenga Ufahamu Hapa
1. Kujitambua ni hatua ya muhimu katika maisha ya mtu yoyote duniani kama anataka kuishi kwa Furaha na matumaini na kufikia malengo yake
2. Kujitambua ni matokeo ya kupata ufahamu sahihi juu eneo fulani utakaokusaidia kufanya maamuzi sahihi katika eneo husika ili uweze kufanikiwa
3. Ufahamu au maarifa unapatikana kwa kutafuta, kuchunguza na kudadisi taarifa mbalimbali kwani si kila namna ya kujitambua ni sahihi kwa kijana
4. Matokeo ya ufahamu ulionao yatafanana na ubora wa maisha unayoishi kwa kiwango cha kuathiri maamuzi yako ya kila siku
5. Kiwango cha matokeo ya kujitambua kitafanana na ubora wa taarifa ulizozipata
6. Udhihirisho wa maisha ya kujitambau ni hatua ya juu kabisa ya kuthibitisha kwamba kweli umejitambua

KUJITAMBUA NI NINI?
 “Kujitambua ni hali ya kuwa na ufahamu au uelewa (kujua) wa kutosha juu ya maisha yako kwa ujumla pamoja na mazingira yanayokuzunguka na hivyo kukufanya uishi maisha yanayofanana au kulingana na kusudi la Mungu kwako, uishi katika ubora wa maisha yanayolingana na kiwango cha ufahamu ulionao au kiwango cha kujitambua kwako kutegemeana na nguvu ya taarifa unazopata” ….............

.........LITAENDELEA!!!

**************************************************************************************
#Kwa mawasiliano zaidi juu ya huduma ya vijana mahali ulipo au audio cd na vitabu na ushauri:

Mwl Raphael Joachim Lyela
Youth Kingdom Ministries
Barua pepe: ykmjesusup@yahoo.com/ ykmjesusup@gmail.com
Mobile: 0767033300
Sikiliza Radio Uzima FM 94.0-Dodoma kila ijumaa saa kumi na moja jioni.
Tembelea: www.gospelcorner.wordpress.com
**************************************************************************************

No comments:

Post a Comment