Tuesday, November 26, 2013

UMUHIMU WA MWANA MPOTEVU!!!


Mara nyingi sana kumekua na hali ya kujihesabia haki kati ya wana wa Mungu kwa sababu eti fulani kaanguka kwenye dhambi, karudi nyuma, nk., na mimi niko fit! Hii hali imelifikisha kanisa mahali ambapo “kurejezana kwa roho ya upole” kumepungua ila wengi “wanajaribiwa” nafsini mwao kwa sababu ya MWANA mpotevu na UZINZI wake.

Sikiliza, pamoja na kwamba MWANA mpotevu ni MPOTEVU lakini bado ana haki kama MWANA! Pamoja na kwamba ndugu zake wanamshangaa anavyo kengeuka na kumwasi BABA yao hadharani, BADO baba yake anampenda. Kama kuna fumbo duniani ni kujua tofauti ya WALIOITWA na WATEULE. Maandiko yanasema WALIOITWA ni wengi ila WATEULE ni wachache. Kukuweka mahali pagumu zaidi kibinadamu, maandiko yanasema MTEULE ataanguka mara saba ila atainuka! Ndo maana utasikia “usifurahi ee adui yangu, niangukapo mimi nitainuka tena” na utukufu wa mwisho utakua mkubwa kuliko wa kwanza. Wakati ADUI za Mungu wanashangilia KUANGUKA kwa mteule, ghafla! Anainuka na upako mwingine tena MKUBWA! Haleluyaa. Usikose kujua UMUHIMU wa mwana mpotevu, kwa maana Mungu anamwita CHOMBO KITEULE!

Wakati SAULI wa Tarso “anatesa na kuharibu” kanisa, watu walimuona muuaji, pepo mchafu, adui, nk. Mungu alikuwa anaona “chombo kiteule”! Sasa wako wengi sana leo ni WAHARIBIFU kanisani na nje ya kanisa. Waangalie sana maana kuna ghadhabu ya Mungu, na kikombe cha ghadabu yake kikijaa na kumiminwa juu yao hawataamini kitakachotokea, ila tunaomba ile NEEMA iliyomfundisha SAULI wa Tarso (mtume PAULO), iwatembelee hawa ndugu. Na sisi wengine humo tukikumbuka KUWAOMBEA watakatifu ili wasimame katika wito wao na kazi ya INJILI isonge mbele na MWILI wa Kristo ujengwe.

MWANA mpotevu (huyu mpendwa) alipodai sehemu ya URITHI (tunapomwomba Mungu mali huku duniani kwa sababu sisi ni WARITHI wa Baraka za Ibrahim), na kupata PESA, MALI, UMAARUFU, nk., alienda NCHI ya mbali (akakaa mbali na Baba yake na ndugu zake [dhambi inamtenga mtu na Mungu]. Mwili wa Kristo na kama ndugu katika familia moja na baba yetu ni Mungu). Huko katika NCHI ya mbali, akazini na kutapanya mali hadi AKAFILISIKA! Sasa anarudi kwa BABA yake na kutamani kuwa MTUMISHI potelea mbali hata kama sio MWANA! Anatamani tena ile kazi ya HUDUMA kule “Shambani mwa Baba”, Sasa sikiliza. BABA alimuona kwa “mbali” akapiga mbio kumlaki, kumbusu na kumvika VAZI jipya (wokovu) na PETE (mamlaka) kidoleni, na kufanya KARAMU. Ndugu zake (wapendwa) wanalalamika “sisi tuko hapa hata hatujazini, wala kumkosea BABA ila huyu MWASHERATI anakuja na kufanyiwa PARTY! Tuko busy hapa tunazaa matunda huyu jamaa alikuwa na MAKAHABA huko sasa anapata MUALIKO kama MTU wa MUHIMU!” Chunga hili eneo na UJIFUNZE kuwarejesha wenzako kwa UPOLE na UNYENYEKEVU huku ukijiangalia USIJARIBIWE na KUMKOSEA Mungu kwa sababu wengine wamemkosea! Huyu mwana mpotevu ni MUHIMU kwa BABA!

Amani, Baraka, Furaha, Upendo na Neema vizidi kwenu.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment