Saturday, November 30, 2013

JIFUNZE KUWA KONDOO!!!


Kama kuna vitu vya kushangaza ni jinsi ambavyo Yesu amemtumia mnyama Kondoo kujifunua au kutufundisha SIRI za Mungu. Yeye mwenyewe amejiita “Mwana-kondoo” sio KONDOO DUME MKUBWA! No! yeye ni kifaranga/kitoto cha kondoo tu! Mwana-kondoo au mtoto wa kondoo! (alama ya unyeyekevu wa hali ya juu). Nataka tujifunze nini maana ya kuwa Kondoo japo sitaweza kumaliza maana yake kwa sababu ni kubwa.

Jina la Mwana-kondoo lilitumika kwa mara ya kwanza Mbinguni (Ufunuo 5:1-14). Pale ambapo Mungu alitafuta “wa kwenda kuokoa Ulimwengu”, WOTE wakakaa kimya! Lakini akonaekana MWANA-KONDOO kutoka kabila ya YUDA naye AMECHINJWA! (kusulubiwa) na kwa Damu ya huyu MWANA-KONDOO Ulimwengu umeokolewa! Hii ni Damu ya thamani isiyoharibika iwezayo KUKUNUNUA kutoka katika hali yoyote na BEI zako MBAYA na kukufanya kiumbe KIPYA cha thamani kwa Mungu.

Sasa hatua ya kwanza, jua Yesu ni Mwana-kondoo. Hatua ya pili jua kwamba alipodhihirika katika mwili alitufundisha kuwa YEYE ni MCHUNGAJI mkuu wa Kondoo. Na sisi watu wake akatuita kondoo wa MALISHO yake. Kazi ya mchungaji ni KULISHA, KULINDA na KUTUNZA kondoo. KAZI ya kondoo ni KULA, KUKUA, KUMSIKILIZA mchungaji, na KUZAA (kuleta faida kwa Mchungaji).

Tabia ya Mchungaji wa kondoo (Yesu) ni KUTANGULIA kondoo na sio kukaa nyuma. Amejiita MLANGO wa kondoo. Sio tu KUKUTANGULIA katika mambo yote ila HAKUNA kitu kinapita kukuangamiza kikakatiza MLANGONI kama uko ndani ya Yesu! Kwanini? Yesu ni Mlango wa kondoo! Sifa nyingine ya muhimu hapa ni ile inayomtofautisha Yesu na Wachungaji wa MSHAHARA! Anasema “maisha ya kondoo kwa hao wachungaji wa mshahara sio kitu”, akija MBWA MWITU mchungaji wa mshahara hukimbia, ILA Mchungaji wa kondoo (YESU) anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake! Sasa jua neno hili, kabla ADUI hajakuua wewe ni lazima amuue au amshinde kwanza Yesu kama wewe ni kondoo wa zizi lake! Kwanini? Sababu wewe uko NDANI yake na YESU ni Mlango! Haya maandiko NDIVYO YALIVYO kama huyaamini omba IMANI zaidi Mungu akusaidie “kutokuamini kwako”. Kama kuna mahali salama ni kwa YESU.

Sasa haisaidii sana kujiita wewe ni kondoo halafu uko nje ya ZIZI. Lazima Uwe na UHAKIKA juu ya mambo mawili. 1. WEWE ni KONDOO, na 2. WEWE ni KONDOO wa ZIZI la YESU. Ya 3 sio muhimu kwa maana Yesu anajua kazi yake kwamba YEYE ni “MCHUNGAJI wako na hutapungukiwa na kitu na anajua atakulisha majani safi, atakuchunga kwa fimbo yake atakulinda na kukufariji kwa gongo lake na ujapopita kwenye bonde la uvuli wa mauti hutaogopa mabaya..,nk” Anajua kazi yake huna haja ya KUMWOMBA wala KUMFUNDISHA maana ALIJIPA mwenyewe hii kazi na AKAAHIDI “kulitizama NENO lake na KULITIMIZA”. Kazi yako wewe ni kuwa KONDOO wa ZIZI lake, basi! Mengine ni “kukumbushana na kuhojiana na unaeleza shida zako na hoja zako na Bwana anakupa haki na haja za moyo yako”. Na kama UMEJIKUTA nje ya ZIZI kwa namna fulani MCHUNGAJI anakuambia “njoo tusemezane, dhambi zako zijapokua nyekundu kama damu, bendera, nk zitakua nyeupe kama dheluji, sufu, nk..” Anasamehe na kukukaribisha TENA.

Sikiliza, kwa kondoo aliyepotea (katika dhambi), Mchungaji wa KONDOO (Yesu) yuko RADHI aache kondoo wengine 99 zizini, akakusake huko ukilikopotelea na akikupata, sio tu anakurudisha ila ANAKUBEBA MABEGANI mwake wakati anakurudisha. Usifanye mchezo kabisa mtu ANAPORUDI NYUMA au KUANGUKA dhambini. Wakati kanisa na watu “wanaojihesabia haki kwa matendo yao mema” wanakuinukia, Ibilisi na VIBARAKA vyake wanapokuzomea, MCHUNGAJI Yesu anakuja huko speed! Anakunyanyua ghafla! Kabla hawajakaa sawa, ADUI zako wanagundua unaanza KUFANIKIWA tena kwa UPAKO mkubwa, kumbe safari hii uko JUU ya MABEGA ya Yesu na sio miguu yako inatembea ila ni miguu ya BWANA, Simba wa kabila la YUDA ananguruma na kuwasambaratisha ghafla! Anakurudisha zizini kwa AMANI! Hii ni NEEMA ya ajabu sana mbayo kama hujaijua bado hujamjua huyu MCHUNGAJI wa kondoo ninayesema habari zake.


Utajuaje kwamba wewe ni kondoo? Sikiliza, sifa chache sana nakupa kati ya nyingi na zitakusaidia. 1. Kondoo husikia SAUTI ya mchungaji. Kandoo anamjua mchungaji na mchungaji AKIITA kandoo wanasikia na kutii. Hawachanganyi sauti ya Mchungaji wao na sauti ya Mbwa mwitu hata siku moja. Je! Unaisikia sauti ya Yesu na kutii akuitapo au akuonyapo au akukatazapo kufanya mambo fulani katika maisha yako? Jijibu mwenyewe. 2. Mchungaji anaongoza kondoo anakotaka YEYE sio kondoo wanachagua cha kufanya wao wenyewe. Je! Katika maamuzi yako, mipango yako, njia zako, kazi, huduma, nk. Unamshirikisha Yesu KWANZA au unamshirikisha “mtumishi” au rafiki kwanza? Sio tu kumshirikisha, je! Ni wa KWANZA kushirikishwa? Na unafanya nini unapogundua hupaswi kwenda/kufanya/kukaa/kujihusisha na mambo fulani? Unamtii na kuongozwa na Mchungaji Yesu? 3. Kondoo huwa ANAZAA: kondoo wengine (ndama), sufi, mbolea kisha huchinjwa kama kitoweo. Sufi kuhudumia wanadamu na mbolea kuhudumia mimea. Huko mbele kuchinjwa (kufa) kwa sababu mbili kubwa 1. Karamu (uzima wa milele) au 2. Msiba (jahanam ya moto) Je! Katika maisha yako umezaa matunda gani katika Ufalme wa Mungu? Unautarajia ufalme wa Mungu au Jehanam ya moto? Jijibu mwenyewe maana MAISHA ni KUPANGA na KUCHAGUA.

Katika hayo mambo matatu kati ya mengi ya KUJIPIMA, jiangalie mwenyewe maana haijalishi jina la DHEHEBU au mahali unasali au watu WANAKUJUA vipi, maana tunasoma kuna MBWA MWITU wenye ngozi ya kondoo! Sasa sisi huku nje hatuoni ila unajijua huko ndani ukijiweka katika mizani ya hayo mambo matatu na mengine kujua kama wewe ni KONDOO au MBUZI au MBWA MWITU, nk. Kisha chukua hatua ikupasayo.

Siku Bwana anakuwa Mchungaji wako HUTAPUNGUKIWA na kitu. Na ukigundua kitu kimepungua UNAMKUMBUSHA hii ahadi KAMA una UHAKIKA kwamba wewe ni KONDOO wa ZIZI lake! Hii ni faida moja KUBWA ya kuwa KONDOO wa zizi la Mungu. Usiige maneno ya Zaburi 23 na kuyakiri kwa bidii kama BWANA sio Mchungaji wako, hufiki mbali! PATA uhakika ndani yako, jipange sawa sawa na upate ujasiri wa kusema kama mfalme DAUDI kwamba “Bwana ni Mchungaji wangu”!

Neema na Baraka zitokazo juu ziwajaze na kuwafundisha kukaa chini ya Mchungaji MKUU wa kondoo, Yesu Kristo tangu sasa na HATA Milele. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment