Friday, November 29, 2013

EPUKA LAANA HII!!!


Kama kuna kitu KIMEUA (kimwili, kiakili, kimaendeleo, kiroho, nk.) WATU wengi ni kumfanya MTU mwingine kuwa TEGEMEO lake la kipato. Kuna tofauti ya KUMHITAJI mtu na kumfanya mtu TEGEMEO lako. Hakuna MWANADAMU ataishi chini ya jua bila KUHITAJI msaada kutoka kwa mwingine, ila Biblia inatukataza kuwafanya hawa watu kuwa TEGEMEO! Sikiliza, "Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.” (Yeremia 17:5) Sio mimi nimesema ila ni maandiko.

Sasa utajuaje kwamba umefikia hii hatua mbaya ya LAANA? Nitakupa mfano. Ukijikuta UNAKWAZIKA au UNAUMIA sana kama mtu fulani HAJAKUSAIDIA au hata KUKUSIKILIZA katika shida yako jua huyo mtu kwako ni TEGEMEO! Unamlaumu kwani yeye ndio Mungu? haya basi sio Mungu, kwani yeye ndio Shetani anayeleta shida na mateso kwa watu? Ndio maana unaweza ukawa na shida nyingi sana, lakini kuna watu wala hukumbuki KUWALAUMU kwa kutokukusaidia! Sababu? Wao sio TEGEMEO kwako.

Sasa, ukijifunza kumfanya Mungu kuwa TEGEMEO lako, ukiwa na shida Yeye atakua wa kwanza kujua, maana utamshirikisha yeye na KUOMBA kama hakuna mtu pembeni...sasa Mungu akimgusa MTU kukupa kitu "huku moyoni" kitakachotokea UTAJISIKIA kumshukuru Mungu na sio huyu mtu, japo utamshukuru kweli lakini kuna HATUA unatakiwa kufika na kusema "NIMEMWONA MUNGU" na unabarikiwa (amani, furaha, mafanikio, nk.) baada ya huo MSAADA! Na utagundua huyo "mtu" aliyekusaida HAWEZI kuwa kwazo wala JARIBU kwako kwa maana moyo wako UNAJIKUTA unamwelekea Mungu na sio huyu mtu aliyekusaidia! LAKINI kama mtu ni TEGEMEO lako, huwezi kuepusha moyo wako kumfuata huyu "mtu" anayekusaidia.....jaribu utagundua moyo wako una nguvu kuliko akili yako....UKITAKA kupona na dunia hii, na KUUDHIBITI moyo wako sawasawa, mfanye MUNGU kuwa TEGEMEO lako ama sivyo jiandae kabisa kutumika, kuwa mtumwa, kudhalilika, kunyanyaswa, kutukanwa, hata kufa na majanga mbalimbali....hii ndio inaitwa LAANA! "AMELAANIWA mtu yule amtegemeaye mwanadamu..."..

Ukikuta ndani yako unasema “hii shida yangu kama isingekea fulani, sijui ingekuaje”, au “kama kuna watu duniani basi fulani sitamsahau”, au “kuna watu wana roho nzuri…” halafu humalizii au unaguna hapo mwisho mhhh.. ANGALIA unakaribia LAANA kama haijakupata tayari. Utakuta mtu hawezi kutoa USHUHUDA wa maisha yake bila kumtaja MTU fulani, na anamhusisha moja kwa moja na MAFANIKIO yake fulani katika maisha. Usije ukafikiri unamsaidia huyo mtu, UNAMWANGAMIZA! Kama kuna hatari duniani, ni kuchukua UTUKUFU wa Mungu na kumpa mtu. “20 Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. 21 Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. 22 Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho. 23 Neno la Bwana likazidi na kuenea.” (Matendo 12: 20-23)

Kama hili Neno limekufikia hapo ulipo, nakusihi kwa Neema za Bwana, tafuta mahali umemfanya mwanadamu kuwa TEGEMEO lako, na nenda mbele za Mungu kwa TOBA ukiwataja hao watu na kumshukuru Mungu kwa sababu ALIWATUMIA na KUMRUDISHIA Mungu utukufu wake, na kuomba REHEMA juu yako na juu ya hao watu ili msiishie katika LAANA na mkaangamia. Katika Jina la Yesu.

Mungu atusaidie kuelewa hii SIRI kwa sababu Ibilisi hawezi KUKULAANI ila unajilaani mwenyewe kwa kutokujua mambo ya muhimu kama haya. AMANI na NEEMA ya BWANA wetu YESU iwe juu yetu sote. AMEN.

Frank Philip.

No comments:

Post a Comment