
Kwenye maaandiko tunajifunza kwamba watu walioanza kumfuata Yesu wakati
huo wa Mitume hawakuitwa Wakristo bali waliitwa “watu wa NJIA”. Kati ya
namna mbalimbali ambazo Yesu kujitambulisha, mojawapo alijiita yeye ni
NJIA. Na akasema hii NJIA inatufikisha wapi. “mimi ndimi njia ya Kweli
na Uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa kupita kwangu”. Hakuna njia
isiyomfikisha mtu mahali fulani. Kila
mtu anachagua njia kwa makusudi ya kufika mahali fulani, awe anapenda au
hapendi ila kitakachomfanya afike hapo MAHALI ni njia aliyojichagulia.
Yesu anashauri na kutualika akisema “ingieni kwa kupitia mlango ulio
mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao
ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia
imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13, 14)
Nataka tujifunze hii njia ya Yesu. Hii njia ina sifa nyingi zisizovutia
isipokuwa sifa moja kwamba itakufikisha kwa Baba. Kwanza watu
watakaoiona hii njia ni wachache achilia mbali watakao pita juu yake.
Sasa kusudi la njia ni kupita/kutembea na wala sio kukaa au kusimama.
Unapoitwa kwa Yesu, ukakubali na “kukata shauri” KUMFUATA, jua umepata
MWALIKO wa kutembea katika hii NJIA. Kupata mwaliko haina tofauti na
kupata TIKETI ya kusafiria. Usipochukua hatua na kupanda basi huwezi
kuona mambo yaliyoko njiani. Utajifariji na tiketi yako mkononi kwa
sababu imeandikwa UNAKOKWENDA ila usipoanza safari hufiki huko japo
pameandikwa kwenye tiketi yako.
Sifa moja ya muhimu sana ya
NJIA “hii” ni wembamba wake. Tunaambiwa IMESONGA. Kuna tofauti ya
wembamba na kusonga. Katika mawazo yangu napata picha ya njia ambayo iko
katikati ya kuta ndefu kila upande. Kwa lugha ya kawaida ningeiita
“uchochoro”. Yaani ni nyembamba lakini pia imesongwa na kuta huku na
huku. Ukiwa na MAFURUSHI makubwa UNANASA hapo kwa sababu kumesonga sana.
Hii hali ya kusonga/kubana huwezi kuiona kama HUJAANZA safari. Ukisikia
mtu anasema WOKOVU ni “tambarare” jiulize kwamba anapita njia gani?
Maana huku kumebana, yeye tambarare anaipata wapi? Bwana wetu mwenyewe
alisema “ulimwenguni mnayo dhiki lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda
ulimwengu”, sasa alishinda nini kama kila mahali ni tambarare na hakuna
vita?
Sasa kuna mambo mengi sana ukiyaangalia utagundua
yanakupasa kufanya KAMA umeanza safari ya kumfuata YESU. Kwanza NJIA
inaelekeza uelekeo (direction) ambao hujachagua wewe ila mwenye njia
(Yesu). Utagundua kwamba huwezi kubeba kila kitu (kiburi, tamaa mbaya,
uzinzi, uchungu, kutokusamehe, etc.) ukafanikiwa kupita kwa sababu njia
imesonga. Kwa sababu hii njia ni ya kufikirika
(theoretical/hypothetical) japo ni dhahiri (practical/real) wakati wa
kupita inakuwa ngumu kuonekana na wachache wataiona pale watakapochukua
HATUA. Usipochukua hatua na kuanza safari huwezi kuelewa maana ya
KUSONGA!
Kuna mambo manne MUHIMU yatakatokuwezesha kutembea
katika NJIA hii. La kwanza, kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa
maisha yako, kutubu na kugeuka. La pili, kujazwa Roho Mtakatifu. Roho
Mtakatifu sio NGUVU ila ni NAFSI ya Mungu japo pia Ana NGUVU. Roho
Atakufundisha yote, kukukumbusha pia kukufariji uwapo njiani (hutakua
yatima ujapopita nyikani). La tatu, kusoma Neno kwa BIDII tena KILA
siku. Kama unavyokula chakula cha mwilini, lisha na roho yako ipate
nguvu. Neno lina nguvu ya kukutakasa na kutenda mapenzi ya Mungu
maishani mwako. La nne, DUMU katika maombi ili usianguke MAJARIBUNI na
upate mwongozo (direction) uwapo safarini. Huwezi kutenda mapenzi ya
Mungu kama wewe sio muombaji.

Kama hujasikia KUBANWA/KUZONGWA
anza kujiuliza swali hili, Je! Umeanza safari? Na kama umeanza, jiulize
tena Je! Hujabanwa/hujanasa kwa sababu umetua kila mizigo ya dhambi,
uchungu, nk.? Kama unajua bado kuna shida ndani yako na hujatengeneza
vizuri mambo na “kutaka amani na watu wote na huo utakatifu”, jiulize
tena swali, Je! Uko njia nyembamba au pana? Ukipata majibu ya hayo
maswali chukua hatua zipasazo.
Mambo muhimu ya kukumbuka ukiwa
NJIANI (safarini). Kuna vibao vingi sana vya kukupoteza (DIVERSIONS).
Kuna kona nyingi (mambo magumu na mateso) na njia-panda nyingi (mahali
pa kuchagua kumtii Mungu au Ibilisi) na mara nyingi njia-panda (makutano
ya barabara) hayako kwenye mteremko, ila yako kwenye mwinuko. Baada ya
kuchoshwa na “safari”, unafika njia-panda, kushoto (kwa Ibilisi) ni
mteremko na kulia (kwa Yesu) ni mlima zaidi! Kama UMEKAZA uso wako kwa
Yesu, utapita KONA zote, na ukifika NJIA-PANDA utapinda kuelekea tena
kwenye NJIA nyembamba (kwa Yesu) hata kama huko mbele ni MLIMA zaidi.
Ukizidi kuendelea na safari utagundua kuna MABANGO makubwa yameandikwa
jina lako. Mengi ya haya mabango yamebeba lugha ya kukebehi, matusi,
kukatisha tamaa, kukera, nk. Usiangalie MABANGO, kaza uso wako kwa Yesu
kama Stefano. Sio rahisi, hata Yesu amesema sio rahisi ila njia
inapitika. Wakati Stefano anapigwa mawe, hakukimbia badala yake alipiga
magoti. Akatazama juu USHINDI wake ulipo! Hakutizama warusha mawe
(MABANGO), hakusikiliza wanayosema wakati wanarusha mawe (ujumbe kwenye
mabango), aliangalia JUU. Badala ya kuwarushia maneno ya LAANA, Stefano
alikua busy kuwaombe watesi/wauaji wake msamaha. Wakati watu wanaona
damu inatiririka mwilini mwake, Stefano alimwona Yesu na Jeshi la
malaika watakatifu. Wakati watu wanaona mauti, Stefano anaona UZIMA wa
MILELE! Akakaza USO wake kwa BWANA na kumaliza SAFARI yake salama.
Jiulize ni watumishi wangapi leo wataambiwa wana BELIZEBULI wasipigane
ngumi? Jiulize ni wana wa Mungu wangapi leo wakinenewa tu jambo hata
kama ni la uongo wanakwazika na kuwa wakali? Eti wanachafuliwa majina na
kuvunjiwa heshima! Sawa, ila mtizame yeye aliyejiita “NJIA” ambaye
tunamfuata,“Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake,
na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka
chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga
kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi
miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.” (Yohana 13:2-4).
Yesu alipogundua ana KILA KITU (kwa lugha ya kawaida tungesema UTAJIRI
wa kila namna), na yuko kwenye njia (safarini) “Yesu, hali akijua ya
kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa ALITOKA KWA MUNGU NAYE
ANAKWENDA kwa Mungu” akijua hayo, alivua VAZI lake (sio kukunja shati
mikono au kukunja suruali), akajifunga kitambaa kiunoni, akachukua maji
(hakumtuma mtu akalete kwa maana wakati huo alikuwa ni MTUMISHI
anayetumika), akainama, akawanawisha na kuwafuta kwa kitambaa (nguo
iliyo mwilini mwake)! Huyu ni Bwana na NJIA tunayoifuata.
Ujumbe huu umekuja kukumbusha habari ya NJIA na yatupasayo kufanya
katika NJIA hii. Mungu atupe NEEMA ya kujikagua na kupata UTHIBITISHO wa
ndani kwamba tuko njiani au la! Roho anashuhudia pamoja na roho zetu
kama sisi ni wana wa Mungu, naye Atatupa kutambua kwamba tuko katika
njia gani kwa maana haachi kushuhudia juu ya “DHAMBI, HAKI na HUKUMU”.
Msikilize Roho Mtakatifu na MAELEKEZO yote atakayokupa, UTAFIKA salama
kwa BABA.
NEEMA ya BWANA wetu YESU KRISTO iwe nanyi tangu sasa na hata MILELE AMEN.
Frank Philip.

Watumishi wa Mungu wengi sana hawaendi mahali kufanya HUDUMA hadi
wapewe mwaliko rasmi na kutimiziwa baadhi ya masharti ikiwemo KISI
fulani cha malipo au gharama. Sipingi kulipiwa gharama kwa sababu
maandiko yanasema “watahubirije kama hawakupelekwa?”
Ninachotaka kuweka wazi hapa ni aina tatu za MIALIKO. Mwaliko wa kwanza, kuna wakati hujaalikwa na mtu kwenye huduma/kanisa lake
ila Mungu amekualika kwenda kufanya kazi maalumu. Mwaliko wa pili, kuna
wakati hujaalikwa na Mungu ila watu wanataka ukahudumu kanisani/mahali
fulani. Na mwaliko wa tatu, kuna wakati utakua umealikwa na Mungu
kufanya huduma na watumishi wa mahali hapo hawajakualika. Aina zote hizi
za mialiko huwezi kukwepa kama wewe ni mtumishi wa Mungu, au Mwana wa
Mungu kwa sababu WOTE tumeitiwa KUSUDI maalimu katika mwili wa Kristo,
uwe unajua au hujui.
Umewahi kujiuliza ni mara ngapi Yesu
amealikwa hekaluni kuhubiri? Kwanza wale wakuu wa DINI walikua
wanatafuta namna ya kumfungia mahali hata asitembee licha ya kuhubiri
hekaluni kwao. Lakini Baba yake “alimwalika” kufanya huduma na alienda
MAHALI alipotakiwa na KUTIMIZA kusudi bila kusubiri “watu” kumwalika.
Angalia mitume 11 wa Yesu, walikua wanawindwa na kuonekana ni VICHAA na
wenye PEPO. Watu waliochanganyikiwa na wasifaa katika jamii. Wakuu
waliwaona kwama mahali pa kuwafaa ni jela! Lakini ilikua ikifika “saa ya
sala” utawaona wako hekaluni. Sasa usifikiri walikua wanapewa tu nafasi
kule mbele kwenye viti maalumu na kuhehimiwa! No! walikua wanafanya
kazi ya Mungu katika mazingira yoyote “wakati ufaao na wakati usiofaa”.
Sitaki nikupe ushuhuda binafsi lakini kwa sehemu tu nataka nikwambie
mimi binafsi nimeenda mahali pengi sana bila kualikwa. Mara nyingine
sikusema hata neno moja na mara nyingi hata “wenyeji” hawakujua kama
nimwo katikati yao, ila huwa nahakikisha nimeacha MBEGU na FOOT PRINTS
kwamba kuna “mtu wa Mungu alipita hapa”. Kuna idadi kubwa sana ya
Watumishi wa Mungu wako namna hii na nimeona niweke hii SIRI hadharani
ili usikae tu pale KANISANI au MAHALI popote kama boga. Wala usishawishi
watu WAKUALIKE na kukupa nafasi za Mbele, Muulize Mungu kusudi lake na
nini anataka ufanye kwa wakati huo. Matokeo ni mkubwa sana sana katika
ulimwengu waroho ukitembea namna hii.
Ukiona mtu anafugwa
kwenda mahali eti kwa sababu hela haijaingia kwenye accounti yake ya
benki, jiulize swali hili, Je! Hana nauli? Na kama nauli anayo na
amegoma kwenda kwa sabau hela haijaingia kwa account yake, juilize tena
swali, Je! Anamtumikia nani? Kama anamtumikia Mungu, tena jiulize swali,
Je! Amealikwa na Mungu au wanadamu? Na kama amealikwa na Mungu, jiulize
tena swali, Je! Anatenda MAPENZI ya nani? Haya majibu ni kwa matumizi
binafsi na ujipange sawasawa kuyajibu kama wewe unatarajia UZIMA wa
MILELE.
Namaliazia kusema kwamba, MIALIKO maalumu ni michache
sana. Mavuno yako tayari na ni MENGI. Bwana wa mavuno anasema “watenda
kazi ni wachache”. Kwa bahati mbaya, hawa watendakazi wachache pia
wanasubiri mialiko maalumu! Funguka Macho ya Rohoni kwa Jina la Yesu.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Ufunuo wa KWELI ya Mungu uwe nasi sasa na hata MILELE. AMEN.
Frank Philip.

Mara nyingi sana tumeona watu wanatamani kumwona Mungu akijidhihirisha
katika maisha yao, hata ikiwezekana kwa ngurumo na matetemeko, ila kila
mahali ni kimya kama Mungu hayupo. Nataka nikupe SIRI moja kati ya
nyingi ambazo zinaweza kukusaidia.
Umewahi kujiuliza nini kinatokea wakati Mungu anatafuta watu wa kujidhihirisha kuwa mwenye NGUVU hawaoni!
na upande mwingine watu wanatafuta UDHIIRISHO wa Mungu kwenye
maisha/huduma zao hawaoni kitu pia? Tunafahamu kwamba “Kwa maana macho
ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa
ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda
upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita.” (Mambo ya Nyakati 16: 9)
Kwa upande mwingine kila mtu anajua na kukiri kwamba Mungu yuko karibu
sana kuliko hata pumzi yake, nk. lakini kwa kweli anasema tu huku hata
akiomba inakuwa kama Mungu yuko ng’ambo ya bahari au Mbingu imepauliwa
kwa zege. Hata inafika watu wa Mungu wanaamua “kuteremkia Misri”
(kufuata njia za kidunia kama rushwa, nk.) ili kupata msaada, kwanini?
Wanaona Mungu yuko mbali na wanaona kila kitu mbele yao ni milima na
bahari tu na hawawezi kuvuka hapo. Ghafla! Wanaanza kujirahisisha na
kufanya dhambi kama vile Mungu hayupo. Huku tunaambiwa Mungu ni SHAHIDI
mwepesi! Sasa mbona inakua NGUMU kujidhihirisha na matendo yake MAKUU
akitutetea kama ni shahidi MWEPESI? “Nami nitawakaribieni ili kuhukumu;
nami nitakuwa shahidi mwepesi juu ya wachawi, na juu ya wazinzi, na juu
yao waapao kwa uongo; na juu yao wamwoneao mwenye kuajiriwa, kwa ajili
ya mshahara wake, wamwoneao mjane na yatima, na kumpotosha mgeni asipate
haki yake, wala hawaniogopi mimi, asema Bwana wa majeshi.” (Malaki 3:
5)
Sikiliza kwa makini, Mungu sio mwanadamu, Yeye anaona “NIA
iliyoko ndani yetu”. Weka moyo wako vizuri juu ya mambo uombayo ama
sivyo hupati kitu. “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu,
wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa
hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili
mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa
dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia
hujifanya kuwa adui wa Mungu.” (Yakobo 4:1-3)
Sasa utakuta wana
wa Mungu wamefika mahali wamejichanganya sana. Nusu kwa Mungu nusu
mtaani/kwa Ibilisi. Halafu unatarajia udhihirisho wa Mungu kwa radi na
matetemeko. Utakuta mtu anakiri ushindi pale tu anapotaka KITU kwa Mungu
ila akijaribiwa KUTENDA dhambi anakua mpole wala hafungui kinywa! Hadi
anazini, kula rushwa, kusema uongo, nk. halafu baadae anatubu! Ule
“UKAMILIFU wa UELEKEVU wa Moyo” (Nyakti 16:9) kama wa Ayubu wakati wa
majaribu uko wapi? Kama moyo wako ni MWELEKEVU kwa UKAMILIFU (soma hapo
juu kifungu cha pili), wakati macho ya Bwana yanakimbia-kimbia duniani
KUSAKA watu wa kujidhihirisha mwenye NGUVU, lazima yataku NASA tu na
Mungu anaanza kuwa shahidi mwepesi kwako ghafla! Ila kama bado nusu moyo
umeweka kwa boyfriend/girlfriend na mnafanya uchafu au ku-chart dirty
stories, au upande mmoja rushwa, dhuluma, na upande mwingine Mungu, hapo
sahau kuona UDHIHIRISHO wa Mungu. Utaomba na mbigu itakuwa kama chuma
juu yako, utasikia kama mkiwa jangwani kwa maana Roho Mtakatifu ni
Mtakatifu kweli, usitarajie umburute kama silaha tu ya kushambulia
wakati UNASHIDA halafu unaishi maisha ya KUMHUZUNISHA na KUMZIMISHA.
Mungu ATAWAONA na atajionyesha mwenye NGUVU sio kwa kila mtu ila
“waliokamilika moyo kuelekea kwake”, na jicho lake liko busy kutafuta,
kwa kukimbia-kimbia duniani kote kumsaka huyu mtu. Kwanini Mungu
anafanya msako? Kwasababu hawa watu ni ADIMU!
Watu wengi
wamekuwa ADUI wa Mungu bila kujijua huku wanamwita Baba! Haiwezekani
unafanya urafiki na DUNIA na mambo yake halafu unatarajia Mungu ni baba
yako! Ndio maana “Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu,
mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala
sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma. Mbona hamyafahamu
hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu. Ninyi
ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo
kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika
kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema
yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”
(Yohana 8:41-43).
Sasa chunga njia zako vizuri. Sisemi kila
mdhaifu katika dhambi ni mtoto wa Ibilisi, tunajua kuna habari ya “Mwana
lakini ni mpotevu”. Ameenda huko duniani kuishi kwa maisha ya anasa ya
UZINZI lakini ni “mwana”. Tunajua habari ya Yesu kwamba kuna “kondoo”
mmoja mahali nje ya zizi, amepotea, na Yesu yuko tayari kuacha hawa 99
ili AKAMSAKE huyu mmoja! Sasa nakupa shauri, kimbilia kwa Yesu haraka,
kama wewe ni kondoo na unajua uko nje ya zizi au kama ni mwana mpotevu
uko huko duniani, rudi kwa Baba. Weka moyo wako vizuri KUMWELEKEA yeye
peke yake kwa UTIMILIFU utaona MACHO ya Mungu yakikutembelea kwa maana
yanakutafuta siku nyingi na hayakuoni, na utashuhudia NGUVU zake
maishani mwako kwa maana HAKIKA atajidhihirisha kwako.
Neema na Baraka zitokazo juu ziwajaze mnapozidi kuyatafakari na kuyatenda mapenzi ya Mungu. AMEN.
Frank Philip.

“Mkinipenda mtazishika amri zangu” na “azipokeaye amri zangu na
kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba
yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” (Yohana 14:14,22).
“Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula? Yesu
akawaambia, Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na
kuitimiza kazi yake.” (Yohana 4:33,34).
Nimejiuliza sana maswali kwamba Mungu huwa anatuonaje tunapokwenda
mbele zake? Je! Tunajiona angalau kwa sehemu na kujitambua kwamba tukoje
mbele zake?
Umewahi kujiuliza ile nguvu tunayoweka katika
MAOMBI na KUFUNGA na jitihada ya kutafuta MSAADA wa maombi kwa watumishi
mbalimbali wa Mungu wakati tukiwa na mahitaji ya mambo ya MWILINI kama
kufaulu mitihani tukiwa shule, kupata kazi, kupanda cheo, kupata
wachumba, biashara zetu kufanikiwa, kupona magonjwa, nk.? Umewahi
kujiuliza ni NGUVU KIASI GANI unaweka katika MAOMBI ili uweze: kujua
WITO wako, kumpendeza Mungu, kukaa katika mapenzi yake, kuishi maisha ya
utauwa, nk.? Ukiweka katika mizani uzito wa MAOMBI na NGUVU tunazotumia
katika mambo ya mwilini na ya Mungu unaona TOFAUTI gani?
Je!
Unafahamu pamoja na Wana wa Israel kutoka Misri na kuvuka Baharini kwa
ushindi, kwamba walipomkasirisha Mungu kwa matendo yao bado walifia
jangwani? [kwa nyoka za moto, kumezwa na ardhi, nk.?] Je! Tunajitahidi
kwenye maombi kupata mafanikio na tukiisha kuvuka kile kipindi cha shida
tumdhihaki na kumtukana Mungu aliyetuvusha kwa matendo yetu maovu? Tena
tunamtenda dhambi kwa kuvitumia vile vitu alivyotubariki navyo? Umewahi
kujiuliza kwamba ni kwanini Mungu asikuache katika hali NGUMU ili uzidi
kumtafuta maana akikuinua tu kidogo unamsahau? Mungu ni wa REHEMA na si
mwepesi wa hasira, anatupa kila siku ingine tena nafasi ya kutafakari
njia zetu na kuona “kama iko njia ya kuleta majuto” ndani yetu ili
tumrudie KUTUBU na kumwishia.
Haya maswali yalinipeleka kuwaza
JE! TUNAMWOMBA MUNGU KAMA TUNAMPENDA AU “TUNAMTUMIA” TU KWENYE SHIDA
ZETU KISHA KUMWACHA? Mungu anaona tunampenda YEYE au DUNIA zaidi?
“Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za
kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama
hivi leo.”(Torati 8:18)
NEEMA NA BARAKA ZITOKAZO KWA MUNGU BABA ZIWE NANYI TANGU SASA NA HATA MILELE. AMEN.
Frank Philip.

(HATUA za HUDUMA na VIPAWA vyako)
1. Jua kutofautisha kati ya HUDUMA na BIASHARA. Msukumo wa HUDUMA hauko
katika kufanya FAIDA bali kutenda kile mtu anachokifanya kwa “jamii”
fulani, na hiki “kitu/shughuli” kimejikita katika Mapenzi ya Mungu.
Malengo na Madhumuni ya huduma ni KUTUMIKIA sio KUTUMIKIWA. Kumbuka
katika UFALME wa Mungu, hakuna aliyeacha ndugu, wazazi, au shughuli yake
NYINGINE na akachagua kufanya HUDUMA
katika Ufalme huu asirudishiwe mara 100! Mtihani upo katika kukaa kwa
UAMINIFU na kwa SABURI ukimtizama yeye ALIYEKUTUMA na wala sio FAIDA.
Ili UINULIWE unahitaji kufaulu mtihani wa UNYENYEKVU na ITAKUPASA
kunyeyekea CHINI ya mkono wa Mungu ulio hodari UKISUBIRI akukweze kwa
WAKATI WAKE. Huu wakati unakuja, ila ni wa kusubiri. Usidanganywe na MTU
yeyote, huu ni wakati wa MAUMIVU na KUPIMWA imani yako kama kweli UKO
KAZINI au unatafuta hela! UKIFAULU hapo, hakuna mahali hutakanyaga wala
pesa hutapata. Hakuna ALAYE ataweza kumaliza “mavuno yako” japo kwa
kweli walaji watakuwepo! Ili uweze kusimama mahali “hapa” (pa kupimwa na
kusubiri kuinuliwa), katika njia ya kufikia “MAHALI pa USHINDI” wako
utahitajika kufanya MAOMBI ya dhati kabisa huku ukichunga KINYWA chako
maana anayekupima UVUMILIVU na IMANI yako mara nyingi sana ni YULE BWANA
“unayemtumikia” ili ajue ATAKUPANDISHA cheo hadi wapi. Jinsi
utakavyoshinda huu MTIHANI (interview) ndio UTAPANDA mbali zaidi.
Kumbuka mfano wa talanta (5, 2, 1), kiwango cha KUPOKEA hakikua kwa
Bwana atoaye bali UWEZO wa mtumishi APOKEAYE. Ukitaka kupokea VINGI
jiandae kujifua vizuri katika MAOMBI na SABURI. Huku ukila Neno kwa
WINGI maana hivyo ndivyo vitendea kazi shambani mwa Bwana lakini pia
ndio CHANZO cha IMANI katika Kristo. Nyenzo na vitendea kazi vya muhimu
katika HUDUMA ni IMANI na MAMLAKA! Kumbuka Mamlaka inapatikana katika
KUMTII Mungu katika mambo YOTE. Hivi viwili vinafanyaje kazi? IMANI ni
kama FEDHA, NGUVU au UFUNGUO. Ili uweze kumiliki MAMBO fulani katika
ulimwengu huu, na wa roho unahitaji hiki kitu ambacho kinaitwa IMANI.
Kuna wakati utahitaji KUTEKA kambi ya adui ili ujitwalie MATEKA, bila
NGUVU (imani na mamlaka) huwezi maana adui ameitwa ni “mwenye nguvu”.
Kuna wakati unahitaji FUNGUO za kufunga au kufungua vitu katika
ulimwengu huu na wa roho ili HUDUMA isonge mbele bila mamlaka huwezi
kufurukuta.
HUDUMA inasema hivi “nimetenda ‘Mapenzi ya Mungu’
kiasi hiki na KUMRUDISHIA Mungu utukufu wake, na Mungu anasema “moja
mia, au moja sitini au moja thelathini”, kulingana ni KIWANGO chako cha
KUPOKEA kama MTUMISHI MWEMA na MWAMINIFU” Kwenye HUDUMA mara nyingine
hakuna ulinganifu wa ULICHOPANDA na UTAKACHOVUNA kwa jinsi ya mwili.
Huwezi Kupima mafanikio ya HUDUMA kwa kiwango cha PESA japo ukifanya
HUDUMA LAZIMA pesa ije. Kipimo ni KIASI cha kutenda MAPENZI YA MUNGU.
Ndipo huyu atapanda MBEGU ile ile katika UDONGO ule ule, huyu atavuna
100, mwingine 60 na mwingine 30!
Msukumo wa BIASHARA ni kupata
PESA. Biashara inasema “nimewekeza kiwango ‘hiki’ na FAIDA lazima iwe
‘hivi’ la sivyo ni HASARA”. Sasa kumbuka kuna WATUMISHI wengi sana
wanafanya KAZI ya MUNGU kama BIASHARA. Kipimo cha Mafanikio yao ni IDADI
ya BIDHAA walizozalisha na kiwango cha PESA iliyoingia. FURAHA yao sio
KUFANYA mapenzi ya Mungu ila ni faida wanayopata katika KAZI ya mikono
yao. Mara nyingi sana WATUMISHI wa namna hii huchanganya BARAKA za MUNGU
na MALI! Yaani mwenye ‘NAZO’ zaidi AMEBARIKIWA zaidi kuliko mwenye
VICHACHE! Ndio maana BWANA wangu aliita kuna WACHUNGAJI wa MSHAHARA na
wachungaji wa KWELI (Mchungaji mwema). Mtumishi ambaye anafanya
biashara, kitu cha kwanza sio “KONDOO” (mapenzi ya Mungu) ila MSHAHARA
(pesa). Sasa hiki ni KIPIMO kigumu sana na kimefichwa mbali na huwezi
kuona kwa macho ya nje, ILA Mungu aonaye SIRINI hujua ni nani anafanya
HUDUMA na ni yupi anafanya BIASHARA. Sasa kumbuka, haya makundi mawili
yote yataleta MATUNDA kwa Ufalme wa Mungu, tofauti yao ni kitu kinaitwa
THAWABU! Thawabu hulipwa MBINGUNI na MSHAHARA hulipwa DUNIANI. Hili
kundi la WAFANYA BIASHARA watapata MSHAHARA (PESA) wao na Yesu akasema
“wameshalipwa duniani”. Tabia yao ni kusimama MAHEKALUNI, KUPAZA SAUTI,
KUSIMAMA kwenye KONA za NJIA na kuvaa KANZU NDEFU ili watu wawaone na
sio MUNGU awaone”. KUJIONYESHA na MASHINDANO ya mwilini ndio JADI yao.
Sawa, watashinda na kupata PESA, ila thawabu yao huko Mbinguni ni sifuri
maana wamekwisha kupokea kwa WANADAMU sifa na utukufu! Wale wanaofanya
HUDUMA mara ZOTE ni wanyenyekevu wa moyo, wanatanguliza Mapenzi ya Mungu
na wanaogopa KUJISIFU na kugusa UTUKUFU wa Mungu. Maombi na kufunga ni
sehemu ya MAZOEZI yao RASMI ya huduma, tena CONSTANTLY na sio wakati wa
MATAMASHA tu. Kumbuka HUDUMA ni MAISHA sio EVENT! Hili kundi la wafanya
HUDUMA mara nyingine hudhulumiwa na kulipwa kidogo (nusu pesa kama yule
mama aliyeweka sarafu kwenye sanduku la hazina na Yesu akasema, “hiyo ni
zaidi kuliko zile matajiri walizotoa”) lakini FAIDA yao ni KUBWA kama
wametenda mapenzi ya Mungu na kurudisha UTUKUFU wake bila kuugusa hata
tone. Hili kundi ni la muhimu sana kwa maana linazaa double double.
MATUNDA hapa duniani na Uzima wa milele. Ila kundi la WAFANYA BIASHARA
linazaa matunda hapa duniani na kukosa UZIMA wa milele! Kwa maana hata
kwa MZAHA Yesu atahubiriwa na miujiza itafanyika ila wale watendao hayo
watapotea milele! Chagua kukaa katika MSTARI wa Mungu usifanye kazi ya
HASARA Mtumishi wa Mungu. Kila mtu na ajipime kazi yake mwenyewe na
AJITAMBUE na kujipanga sawasawa asije akasema HAKUJUA! Maana usishangae
Yesu anakutembelea na KIKOTO halafu usiamini, maana wale watu waliofanya
biashara hekaluni wakati “ule” hawakumjua Yesu kama “mchapaji” pia!
Chunga sana, Yesu ni yeye yule JANA, LEO na hata MILELE.
Matendo ya
Mitume 20: 33 “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. 34
Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji
yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35 Katika mambo yote
nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia
wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema
mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. 36 Alipokwisha kunena haya
akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. 37 Wakalia sana wote,
wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, 38 wakihuzunika zaidi kwa
sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena.
Wakamsindikiza hata merikebuni.”
Kuna vipawa vingine vitatumika
sio kama HUDUMA bali BIASHARA. Sasa, kama Mungu amekupa kufanya
biashara au kazi ya kukuingizia KIPATO kwa namna yoyote USIMSAHAU Mungu
katika biashara hiyo. Tafuta makusudi yake na hakikisha BISAHARA yako
INAMTUKUZA Mungu na inaheshimu na KUTII makusudi ya Mungu. Kama Mtumishi
wa Mungu katika BIASHARA yako, jifunze kutafuta kusudi la Mungu na
kukaa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu daima. Chunga sana
unavyowahudumia watu na kuweka viwango vya BEI na tozo mbalimbali.
“Mungu hapendi mizani za uongo”. Pima kazi na malipo kwa ulinganifu na
“usichukue zaidi ya ikupasavyo”. Na jua kwamba sio kila mara utafanya
kazi/biashara kwa MASLAHI ya kibinadamu (kazi au bidhaa kuuzika kwa bei
ya faida kwa namna ya kibiashara). Ukijikuta unasukumwa kufanya kitu
CHOCHOTE kwa pesa tu, jua unakaribia mahali pa gumu. Ukisikia mtu
anasema “hii kazi haina maslahi” na haangalii kama Mungu anataka nini
ila pesa tu, ni hatari. Sio kila wakati utafanya kazi kwa malipo ya
pesa, Mungu anaweza kubadili mfumo wa malipo kwa baadhi ya kazi.
Usipokua makini unaweza kujikuta unajifungia milango ya muhimu wakati
unakimbiza pesa na ukajikuta hufiki mbali. Pamoja na kufanya faida,
REHEMA iwe ndio mhimili wa maamuzi yako ya ki-PESA au kuhudumia wateja
wako.
2. Mfumo wa duniani utakulazimu kufanya mambo mabalimbali
wakati wa kufanya HUDUMA na mengine ni magumu. KUMBUKA wewe ni MTUMISHI
(mtumwa), kuna Bwana aliyekutuma. Ukibinafsisha HUDUMA ikawa yako
itakua NZITO mabegani mwako. Kwa maana kila HUDUMA ina VITA, na Maandiko
yanasema HAKUNA askari aendaye VITANI kwa GHARAMA zake! Ukifika mahali
pa kujisahau ukaanza kusema “huduma yangu” huku ukisahau kua wewe ni
MTUMWA na sio BWANA (boss) au MMILIKI wa hiyo HUDUMA unakaribia kufikia
MAHALI pa gumu. Hata siku moja USISAHAU kwamba kuna “organization
structure” ya Mungu ambayo yeye ni TOP BOSS na sisi ni vibarua tu. Sasa
hapo juu yako kunaweza kua na VIONGOZI wako wa KIROHO, chunga
usiwavunjie HESHIMA na ukakosa kuwasikiliza kwa KISINGIZIO cha HUDUMA na
UPAKO juu yako. Imempasa KILA mmoja kuitii mamlaka iliyo kuu katika
KAZI ya HUDUMA na ni vyema sana ukaitambua mamlaka “inayokuhusu” na
kukaa VIZURI nayo maana inaweza ikawa SABABU ya wewe KUKUA au KUANGUKA
kihuduma. Katika MFUMO huu wa Utawala, jua kuna wakati utakua na watu
chini yako. ANGALIA basi kwa sababu na sisi tu wa BWANA wetu ambaye
tunamtumaini KUTUBARIKI nasi tusizuie mkono wetu kuwabariki walio chini
yetu na kuwatanguliza kama BWANA wetu alivyotupa mfano wa kunawisha
miguu wafuasi wake. Ukitaka kua BOSS/MKUU sharti ujifunze “kuvua nguo
(utukufu) na kujifunga taulo kiunoni KISHA “kuinama” (kunyenyekea) na
kuwanawisha (kuwatumikia) MIGUU michafu walioko chini yako kwa
USTAHIMILIVU”.
3. Katika mfumo wa kufanya kazi ya Mungu
utahitaji VIBALI na michakato mingi ya KISHERIA na imekupasa kumpa
KAISARI kilicho chake kwa UAMINIFU wote. Huwezi kuepuka wezi, nondo na
wadudu mbalimbali (ma-promota, producer, nk.) walao maadam uko duniani.
Ila jua Bwana ni fungu lako na HUTAPATA hasara kwa maana yeye anaona
SIRINI na anajua shida yako na ATAKUJAZI. Kumbuka kuweka HAZINA yako
Mbinguni pia maana huko hakuna kutu, nondo wala wezi. Na unahitaji
ULINZI wa Mungu ili HUDUMA yako “isipukutishe majani/maua” kabla ya
KUZAA, na yeye anaweza pia KUMKEMEA yeye ALAYE (Ibilisi na watu wake),
ulinzi huu unaupata katika ZAKA KAMILI! Jifunze KUTOA kwa USAHIHI maana
kuna faida NYINGI.
Warumi 13: “1 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka
hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu. 2 Kwa
maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa
sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya
mema, nawe utapata sifa kwake; 3 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu
kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana
hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi
mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu. 4 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa
sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri. 5 Kwa sababu
hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu
katika kazi iyo hiyo. 6 Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa
ushuru, ushuru; astahiliye hofu, hofu; astahiliye heshima, heshima. 7
Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye
mwenzake ameitimiza sheria.”
4. Huwezi kufanya HUDUMA na
kutumia VIPAWA vyako bila kuwa na watu wengine katika timu. Huduma
inavyozidi kukua utahitaji watu wengi zaidi. Kumbaka jambo hili siku
zote, wana wa Mungu wanapojihudhurisha mbele za Mungu wao, shetani naye
huja kati yao. Ni vigumu sana kutambua magugu yawapo pamoja na ngano na
sio kazi yetu “kuyang’oa” maana hakuna aliyepewa huo wito na BWANA wetu
ila inabidi kujichunga na kujilinda na “chachu” yao maana inaweza
kuchachusha HUDUMA yako bila kujua. Yesu alikua na wanafunzi 12 na mmoja
wao aliitwa “msaliti”! Kama Yesu alikuwa na timu na ndani yake kuna
YUDA, jua imekupasa kuwa makini na macho ya mwili na roho kujua watu wa
timu yako maana humo watakuwepo wasaliti na wengine ni hatari kuliko
YUDA. Kazi ya Yuda ilikua “mweka hazina” ila alikua akiiba vitu/matoleo!
Sasa chunga sana mienendo na tabia za watu wa timu yako maana jua kuna
roho nyuma yao na mwisho wake huwa ni KUSALITI ili huduma ife bila
kujali madhara. Kipimo kikubwa cha uaminifu wa wengi katika timu ni
TAMAA ya pesa! Hii ndio ilimfanya YUDA akasaliti huduma yao na Bwana
wake kwa sababu ya KIPATO cha vipade 30 tu vya fedha! Sasa jua neno hili
kwamba kama YUDA ambavyo hakuila ile pesa, ndivyo wengi sana
wanaomsaliti Bwana aliyewatuma huishia pasipotarajiwa kama ilivyokua kwa
YUDA au zaidi. Ndani ya vikundi vingi sana wamejipenyeza akina Delilah
na wamenyongelea chini HUDUMA nyingi na imebaki mazoea tu na nguvu ya
ugali. Imekupasa kukaa katika Maombi ya DHATI kabisa kama timu nzima na
kuwa na ratiba za KULA na kujifunza na KUSIKILIZA maagizo ya Bwana
aliyewatuma kazini ili msiingie majaribuni.
5. Chanzo cha nguvu
zetu ni Mungu aliyetutuma kwenye kazi yake. Huwezi kumchanganya Beliari
na Mungu na ukapata matokeo mazuri. Ni jambo la kustaajabisha sana
kuteremkia Misri kutafuta msaada ili usimamishe HUDUMA! Yaani unamsaidia
Mungu “kutafuta msaada au mtaji kutoka kwa mungu mwingine”! Kumbuka,
kukua kwa huduma ni hatua, ambazo huongozwa na Mungu. Na kukua huku
kunaenda sambamba na kukua kwa IMANI yako. Kama unataka kukua kwa kasi
basi kimbiza kukua kwa IMANI yako. Kwa maana “tunafanikwa katika mambo
YOTE kwa kadri roho zetu zifanikiwavyo”. Kwa MAJIRA na vipindi
alivyoamuru Mungu, ataleta mtaji na mahitaji ya kukuza huduma yako.
Ukifika mahali “unakopa” na kujitaabisha sana ili “uwekeze” kwenye
huduma kwa malengo ya KUKUA KWA HARAKA, jua unakaribia mahali sio
pazuri. Kama wewe ni “mtumwa” na Bwana wako anataka ulime hatua 10 kwa
siku, kwanini ushindane naye na kutaka kulima hatua 100? Je! Hizo hatua
90 za zaidi ulifanya kwa msukumo wa kumzalishia Bwana wako au
“kujiongezea kipato”. Jiulize kinachokusukuma ni BIASHARA au HUDUMA?
Sasa usiwe MLEGEVU katika kazi ya BWANA maana Mungu amekataa UVIVU na
ULEGEVU ila tuwe na BIDII katika KUTAFUTA na KUTENDA mapenzi ya Mungu
peke yake.
6. Ukiona UNAMTUMIKIA Mungu, na umefika mahali
ukitaka PESA kwa ajili ya jambo fulani, na unajikuta UNACHANGISHA watu,
au kuomba watu PESA “kabla” ya kumwomba “kwanza” Mungu hiyo PESA, jua
unakaribia mahali pa GUMU. Epuka kua OMBAOMBA na jifunze kumtegemea
Mungu kama kweli UNAMTUMIKIA Yeye. Yesu alipotaka “pesa” alituma mtu
akavue samaki na kisha ampasue atoe huko sarafu! Unadhani wakati wa Yesu
akina ZAKAYO hawakuwepo? Unadhani alishindwa kuwambia tu kwa URAHISI
walete SADAKA/MBEGU na wakamjazia kila mahali MIJI-HELA? Angalia basi
Mtumishi wa Mungu usije ukahamisha TEGEMEO lako kwa wanadamu bila kujua.
Ni kweli Mungu atainua hata “mawe” yafanye kazi yake, ila chunga usije
ukaanza na kutafuta misaada kwa “mawe” kama hayo ndio yamekuita katika
kazi ya HUDUMA. Muombe Mungu kwa bidii, tafuta USO wake kwa bidii zote,
kama atatuma MALAIKA kukuletea “mkate na gudulia la maji” au kama
atatumia KUNGURU kukuletea “mkate” kama kwa Elia Mtishibi, sio juu yako
kuchagua. Mtumaini yeye na kaa katika KUSUDI lake. Mojawapo ya sifa za
watu wanaomtegemea Mungu katika VIPATO vyoa ni KUOGOPA sadaka na
KUIHESHIMU! Yamkini hujawahi kukutana na mtumishi wa Mungu anakataa
SADAKA lakini wapo wengi tu, Kumbuka habari za Elisha baada ya kumponya
mtu ukoma! Ingekua leo tungeita “sadaka ya shukurani” na tungeshangilia
kupokea! Sasa sisemi sadaka za shukurani ni mbaya, ila nataka uone hii
KIU ghafla ya kutaka KUPOKEA kirahisi kutoka kwa WANADAMU na KUDAI kwa
nguvu au kijanjajnja saa nyingine kwa kutishia watu kwa maandiko.
Hatukuitwa KUKUSANYA pesa na sadaka ila kuleta ROHO za watu kwa Mungu.
Pesa ikija ni sawa, ni CHAKULA CHA SAFARI tu kutuwezesha kufikilia
MAKUSUDI ya Mungu na wala Pesa yenyewe sio MAKUSUDI ya MSINGI ya HUDUMA
zetu labda kama tunafanya BIASHARA.
7. Majaribu lazima yaje
ili kupunguza kasi ya huduma yako japo ukiyashinda UNAPANDA cheo. Kwa
Ayubu shetani alisema “nikigusa kitu cha karibu naye” huyu jamaa lazima
ashindwe. Ibilisi akashughulikia watoto na mali zote! Usidhani ilikua
mahali pa rahisi hapo kusimama tu katika UAMINIFU na Mungu. Wakati
watoto wanaangamia na mali zinaporomoka wanakuja MARAFIKI “wataabishaji”
wakileta injili pori na maneno “kandamizi”. Lakini Ayubu akakaza macho
kumtizama Bwana wake na akafika MAHALI pa USHINDI wake, japo ilikua ni
raundi ya kwanza. Raundi ya pili Ibilisi anataka kumgusa Ayubu “karibu
zaidi” ili kumchanganya na kumpotezea mwelekeo. Ibilisi anasema “mwili
bwana, mwili, mtu akiguswa mwilini ataachia tu ngazi”, Mungu akatoa “go
ahead”. Wakati Ayubu anapambana na MAJIPU mwili mzima, anajikuna kwa
kigae maana yamkini akijikuna usaha ulikua unamwagika na kigae ndio cha
kukingia, huku ananuka na kwa kawaida watu wanakaa mbali, hatamaniki,
MKE wake anakuja na mpya! Akidhani anamwonea huruma, akitazama haoni
tena mtu ila “maiti” na anamshauri “amkufuru Mungu” kuharakisha kufa
maana anaona jamaa kilichobaki ni kifo tu na anateseka bure! Ayubu
alijua bado mara hii tena atafika “MAHALI pa USHINDI” wake! Kumbuka
alishinda mara dufu, na alirudishiwa kila kilichopotea maradufu!
Watumishi wengi sana wameshindwa kusimama kwasababu Ibilisi amegusa
vitu vya “karibu” nao. Wengine wakati wako Busy na Mungu, huku nyuma
mke/mume anakamatana na makahaba! Na ibilisi ataweka “mtu wa kuleta
habari” kama ilivyokua kwa AYUBU! Ili uumie na uvunjike moyo na upunguze
KASI ya huduma yako. Mara nyingine “karibu” inaweza kua watoto, wazazi,
ndugu, mali au ajira alimradi ni mahali PATAKAPOKUGHARIMU na PANAUMA.
Lengo ni kukukatisha tamaa mtu wa Mungu ili ukose mwelekeo na ushindwe
kutimiza HUDUMA au kuzaa MATUNDA sawa na wito au KIPAWA chako. Chunga
sana hili eneo maana ni gumu na limefisha HUDUMA nyingi sana za
watumishi wa Mungu na wameshindwa kuzaa MATUNDA yawapasayo. Sikiliza
MTUMISHI wa Mungu, KILA kitu kitapita, usiangalie kushoto wala kulia,
kama ni mume au mke amekusaliti kwa kumsikiliza Ibilisi na kwa
“kutokujua saa ya kujaribiwa kwake”, wewe USIKATE tamaa, SONGA mbele!
Mwangalie Mungu aliyekuita na uzidi katika nguvu zake na mapenzi yake
maana hapo ndipo MAHALI pa USHINDI wako.
Kwa sababu kila mtu
katika Mwili wa Kristo ameitwa kwa kazi maalumu kama ilivyo viungo vya
miili yetu, basi jua kama UNASHIKA njia za SHETANI sio tu kwamba
UNAHARIBU huduma yako, ila pia UNAANGAMIZA huduma ya watu wa “karibu”
wanaokuhusu kwa sababu kwa KUTENDA hayo MAOVU unawaumiza na kupunguza
KASI ya utumishi wao. Kumbuka kuukomboa wakati maana hizi ni nyakati za
uovo. Msikae tu kugombana na kubishania mambo yasiyo ya msingi na
kusahau kua mna KAZI shambani mwa Bwana. Mtakapo shughulika na MAMBO ya
Mungu jua HAKIKA Mungu atashughulika na mambo yenu pia na BARAKA na
FURAHA vitaongezeka kwenu na kwa watu wenu wa KARIBU.
Matendo
ya Mitume 20: 19 “nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa
machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; 20 ya kuwa
sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali
naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, 21 nikiwashuhudia
Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu
Kristo. 22 Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali
nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;
23
isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba
vifungo na dhiki vyaningoja. 24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu
cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile
niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.
25 Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria
ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. 26 Kwa hiyo
nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya
mtu awaye yote. 27 Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya
kusudi lote la Mungu. 28 Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo,
ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate
kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”
8. USHUHUDA. Kama kuna kitu kimekwamisha kazi ya Mungu ni USHUHUDA
mmbaya wa watumi wa Mungu. Kumbuka, unapotenda “KITUKO” chochote
hadharani au kwa SIRI ila Ibilisi amefanikiwa kukichomoza hadharani,
watu wataanza kukutizama kama wewe ni mtu wa “namna ile” sawa na KITUKO
ulichofanya, hata kama ilikua mara moja. Ile LEBO unayobandikwa ya hiki
KITUKO ina tabia ya KUDUMU na ni NGUMU sana kuifuta kwa jinsi ya
kibinadamu. Sababu ya msingi hapa ni kwamba Mungu ANASAMEHE na hakumbuki
kama UKITUBU, ila wanadamu HAWASAHU hata kama umetubu. Kama ulifanya
UZINZI bado watu watakutizama tu kama MZINZI kwa muda mrefu. Ibilisi
naye atahakikisha habari MABAYA inaenea kwa KASI kwa sababu yeye ni
“mshitaki”. Watu wengi sana wamesahau kwamba USHUHUDA ni silaha ya
MUHIMU kumshinda Ibilisi, ndio maana tunasoma “nao wakamshinda kwa Damu
ya Mwana-kondoo na kwa neno la ushuhuda wao..” Kama kuna kitu Ibilisi
anawinda ni kupata USHUHUDA wako mmbaya na KUUSAMBAZA kila mahali.
Unaposimama KUHUDUMU anawakumbusha watu na kuwaambia “msimsikilize huyu
jamaa kwanza ni tapeli/mzinzi/mrushi/mwizi” nk. Mara nyingi sana watu
wameshindwa kupokea Neema ya Mungu iokoayo na hata kusema kwa ujasiri
“hakuna wokovu duniani” kwa sababu wanajua WALICHOONA kwa wana wa Mungu.
Makosa ya ZAMANI yana NGUVU ya kuzuia MAFANIKIO yako ya sasa na ya
baadae KIHUDUMA kama hujawa makini na kutafuta Neema ya kupona na MAMBO
ya KALE.
Kwa upande mwingine, sio kila jambo jema laweza kuwa
na USHUHUDA mzuri. Kwa lugha nyingine, sio tu kwamba USHUHUDA mmbaya ni
kuanguka dhambini. Kuna mambo mengi sana katika mienendo na tabia
ambayo Paulo alisema katika kitabu cha Warumi kua makini nayo. Kuna
mambo IMEKUPASA kuacha kufanya kwa sababu ya UDHAIFU wa imani ya mtu
mwingine sio imani yako. Mfano rahisi ni namna ya UVAAJI wa nguo. Watu
wengi wameonekana kama WAHUNI tu kwa sababu ya aina ya nguo walizovaa na
MUONEKANO wao katika mavazi hayo. Na wengine wamekua wabishi na kiburi
hata wakiambiwa au wakionywa! Mungu atusaidie tusiwe KWAZO kwa namna
yoyote. KUMBUKA kumpokea dhaifu wa imani na kumsaidia sio kumwangamiza
kwa UDHAIFU wa imani yake eti kwa sababu sisi ni MIAMBA ya Imani. Hicho
ni KIBURI.
NEEMA ya BWANA na IZIDI KWENU TANGU SASA na HATA MILELE. AMEN.
Frank Philip

Ukitaka kujua umbali au kimo utakachofikia kiroho angalia aliko
kiongozi wako wa KIROHO. Kwa maana yatosha mwanafunzi kulingana na
mkufunzi wake ila hampiti.
Sasa nisikilize vizuri. Kila
ajikwezaye atadhiliwa naye ajidhiliye atakwezwa. Ninazungumzia tabia ya
ndani ya unyenyekevu ambayo Mungu anaipenda. Kupitia tabia hii mtu
huinuliwa na kuwa MKUU kuliko wenzake kwa kukubali kuwa
MDOGO kuliko wenzake. Kuna kundi dogo la watu ndani ya Kanisa ambao wao
watanyenyekea chini ya Mkono wa Mungu na viongozi wao. Kama
wamezingatia mambo matatu yafuatayo kati ya mengi watafika mbali: 1.
watautafuta uso wa Mungu kwa BIDII, 2. wataacha uovu na kusafisha njia
zao mbaya 3. watatafuta kusudi la Mungu hata kama hawapati faida kwa
jinsi ya mwilini. Sasa hili kundi dogo, kwa maana ni dogo kweli,
litajikuta na nguvu nyingi sana za kiroho na watafanikiwa kwa jinsi ya
rohoni na mwilini kwa kadri watakavyokaa katika kusudi la Mungu.
Mambo kadhaa yatajitokeza.
1. VITA na VIPINGAMIZI kutoka kwa viongozi wao na watu wengine kwa
sababu ya wivu. Hali hii ya kuinuliwa ikiibuka katika kundi hili dogo,
wapo watakaovumilia na kunyenyekea na kudumu hapo chini ya viongozi wao
na wengine wataondoka na kuanzisha huduma au kujiunga na viongozi
wengine. Sasa hii ni hali ya kawaida sana kwa nyakati tulizo nazo kuwa
na makundi ya namna hii.TAHADHARI! kwa lile kundi linalohama kwa sababu
ya MADHAIFU ya walikotoka. Angalia usihame kwa KIBURI ila uhakikishe ni
makusudi ya Mungu juu ya maamuzi unayofanya maana unaweza kujikuta
umepoteza ile nguvu uliyodhani unayo. Katika hili twajifunza pale ambapo
Yesu alipoanza huduma, na nguvu za Mungu kudhihirika sana katika maisha
yake, vita iliibuka kwa wakuu wa DINI. Kumbuka, Yesu hakufanya kitu
ambacho hakumwona Baba yake anafanya, ilikua ni mapenzi ya Mungu kabisa
ila VITA ilikuwa kali. Kila mtu asimamaye katika mapenzi ya Mungu kwa
uelekevu na kumpendeza LAZIMA Mungu atajidhihirisha kwa maana “jicho la
Mungu linakimbia-kimbia duniani kote kumsaka mtu wa namna hii ili
Ajionyeshe mwenye nguvu”. Usistushwe uonapo vita wakati unajua ufanyacho
ni mapenzi ya Mungu. Simama katika nafasi yako kwa unyeyekevu na fanya
huduma uliyoitiwa kwa uaminifu.
2. Mungu atawapa hili kundi dogo
nguvu za maamuzi katika kanisa au huduma wanakotumika. Kwa kadri hili
kundi dogo linavyojinyenyekesha na kumtii Mungu, Mungu atawapa hekima na
maarifa hata na nguvu za kiuchumi kiasi kwamba hawa VIONGOZI
watawatafuta kwa ushauri, msaada na mambo mengine ya kihuduma na
mwishowe kama hawa WAKUU wanazidi “kulala”, maamuzi mengi au makubwa
yatategemea hili kundi dogo la watu walioamua kumpendeza Mungu na
kuutafuta uso wake kwa bidii hata kama majina yao hayapo kwenye orodha
ya mashemasi, au watu wowote wenye vyeo kanisani. Kumbuka mfano wa
Paulo. Japo alikuwa mfungwa kati ya wafungwa wengine na wasimamizi wao,
wakati wanasafirishwa baharini yeye alikuwa ndio anasema cha kufanya na
watu wanamsikiliza kwa sababau kwa wakati huo ndiye aliyekuwa amesimama
na mapenzi ya Mungu peke yake na anatenda makusudi ya Mungu hata kama ni
mfungwa.

Wakati VIONGOZI wengi sana wanasahu kazi ya
“mchungaji wa kondoo” na wanageuza hiyo huduma kama “mchungaji wa
mshahara”, hawatajua ni saa ngapi hili kundi dogo limekamata usukani na
kusukuma kazi ya Mungu mbele wao wakiwa busy na miradi yao. Jipange
katika nafasi yako na ni MARUFUKU kumnyooshea mtumishi wa Mungu kidole.
Fanya kazi ya huduma na ONGOZWA na Mungu. Kama jinsi DAUDI alivyosimama
katika nafasi yake wala hakushindana na Mfalme SAULI japo alitaka
kumwangamiza, kaza macho yako katika WITO wako na acha VITA na wanadamu.
ADUI yetu ni Ibilisi peke yake! Daudi hakufurahia kuanguka kwa Sauli
japo kibinadamu Sauli alikuwa ADUI kwa Daudi! Alijua japo yeye amepakwa
MAFUTA ila alihehimu nafasi ya SAULI hadi wakati wa Bwana ulipotimia. Na
aliomboleza KIFO cha SAULI, hakufanya SHEREHE kwa sababu alijua kwamba
pamoja na madhaifu ya SAULI, bado alikuwa ni MASIHI wa BWANA! Uwe makini
Mungu anapokuruhusu kuona MADHAIFU ya watumishi wa Mungu!
Mara nyingi sana watu wamejisahau na kufikiri MUSA atadumu milele!
Yamkini wewe ni Joshua au Kaleb na hujitambui. Na mara nyingine kuna
watumishi kama Eliya ambao wanadhani wengine wote wamekwisha na wako
wenyewe kwenye HUDUMA, kumbe Bwana amejisazia Elfu saba wasiopiga goti
kwa Baali. Hapa nazungumza na hawa Elfu saba, Joshua na Kaleb. Wamo
katika kundi kubwa la WALIOITWA na watafuata kuchukua MIKOBA ya VIONGOZI
wao na kupeleka kazi ya Mungu mbele. Mara nyingi hawa watu hawaandaliwi
na mtu, Mungu huwaandaa mwenyewe na atakupaka mafuta huko huko
MACHUNGANI kama Daudi. Wakati unapambana na DUBU na SIMBA, jua
unaandaliwa KUMSHUGHULIKIA Goliath katika KIZAZI chako. Baadhi watakulia
miguuni pa Makuhani kama Eli kama ilivyokuwa kwa Nabii Samweli.
Vyovyote itakavyokua, kama Mungu anakuaanda huko VICHAKANI kama Daudi au
HEKALUNI kama Samweli, kaa katika kusudi la Mungu na jipange sawaswa
maana kwa jinsi ya MWILINI wengi hawakuoni na yamkini wanakudharau kwa
sabau wewe ni kijana wa kuchunga mbuzi tu ila siku UPAKO wa DAUDI
unadhihirika juu yako ndipo watakapojua kuwa UKIMYA wako ulikuwa MBELE
za Bwana ukijifunza na kukuwa kwa NDANI.
Neema na Rehema zitokazo juu ziwe nanyi tangu sasa na hata Milele. AMEN.
Frank Philip.
Ukienda mnadani na ukaona NG'OMBE aliyenona na wengine wanaonekana afya
mbovu. Jua yule aliyenona zaidi yuko KARIBU na KUCHINJWA kuliko huyu
mwingine ambaye havutii.
Sasa unapoanza hatua za kutaka
kumpendeza Mungu (KUNONA KIROHO), utashangaa ghafla watu wanakuita
HANDSOME/BEAUTIFUL na wanaanza kukufanyia mambo ambayo yanakuvuta
KUTENDA dhambi. Jua ADUI anataka KUKUCHINJA! Jitambe na UPONE.
Sasa, unavyozidi kua karibu sana na MUNGU unakua KIVUTIO cha ADUI na
unakua mawindo. ILA kama wewe tayari ni MALI ya adui, hana haja sana
KUWINDA kilicho chake! Hao watu wanaokutaka ufanye dhmbi HAWAKUPENDI ila
hawakutakii MEMA! Mtu anayetaka UFANYE DHAMBI anakuangamiza na sio
KUKUPENDA.
Jifunze KUJIFUNIKA kwa DAMU ya YESU na kujificha NDANI ya Yesu ili ADUI akija asikuone wewe ila Yesu. Utakua salama.
Frank Philip.