Saturday, January 12, 2013

UHUSIANO WA MTU NA MUNGU


Na Emmanuel Makwaya

UHUSIANO WA MTU NA MUNGU

WAEBRANIA 12:14

Uhusiano ni jambo muhimu katika maisha yetu ya kila siku. Kwa sababu hatuwezi kuishi bila kuhusiana au kushirikiana kwa namna moja ama nyingine. Mtu huhitaji mtu mwengine ili aweze kufanikisha jambo fulani.
Mkulima anamuhitaji mwanasayansi amtengenezee mbolea mwanasayansi anamuhiitaji mkulima ili apate chakula; daktari anamwitaji muhandisi ili ajenge majengo na muhandisi anamuhitaji dakitari ili atibiwe hivyo
hatuwezi kukwepa mahusiano. Tunapokuwa makanisani, mchungaji anawahitaji waimbaji ambao nao wanawahitaji waombaji, ambao nao wanawahitaji wakarimu, watoaji, n.k. Ili kazi ya Mungu iende mbele kama Kanisa tunahitajika kuhusiana. Paulo anasema sisi ni viungo katika mwili wa Kristo, kama vile viungo vinavyotegemeana na kuhusiana hali kadhalika na sisi tunapaswa kuwa hivyo.
Neno la msingi lilonifanya niandike kitabu hiki ambapo kutokea hapo Mungu amenifundisha mambo mengi ni “Tafuteni kwa bidii kuwa na amanina watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana
asipokuwa nao.” Waebrania 12:14. Hatuwezi kuwa na amani na watu wote kama hatuna uhusiano mzuri na Mungu. Biblia inatuonyesha mifano ya watu wengi waliokuwa na uhusiano mzuri na Mungu jinsi walivyokuwa na amani na watu wote. Tukianza na Yusufu mwana wa Yakobo, pamoja na kuuzwa utumwani na ndugu zakeambao walikuwa wakimchukia, bado aliendelea kuwa na amani nao pale walipomkuta ni kiongozi mkubwa nchini Misri (Mwanzo 37, 38, 39). Pia tunamuona mtumishi wa Mungu Stefano katikati ya maumivu ya kupigwa na mawe hata kufa bado na yeye alikuwa na amani na watu wale waliokuwa wakimpiga na kuwaombea kwa Mungu asiwahesabie dhambi ile. Hata Bwana wetu Yesu Kristo katikati ya mateso makubwa ya dhihaka na aibu, alipongongomewa msalabani na kuchomwa mkuki ubavuni bado aliendelea kuwa na amani na watu wote naye akawaombea kwa Baba. “Yesu akasema, Baba uwasamehe,kwa kuwa hawajui walitendalo...” Luka 23:34.
Ni maombi yangu kwa Mungu kwamba mimi na wewe unayesoma kitabu hiki tujifunze na zaidi sana tuwe na uhusiano mzuri na Mungu ili tuwezekuwa na amani na watu wote pamoja na utakatifu na siku moja tumwone
Bwana Mungu mbinguni. Kama viumbe tumeumbwa tuhusiane kwa namna moja au nyingine ili
kufanya dunia iwe sehemu nzuri ya kuishi.Kama wanadamu tunahusiana na watu, vitu, viumbe hai na visivyo hai pamoja na mazingira yanayotuzunguka. Basi uhusiano ni kitu cha muhimu sana kujifunza.
Uhusiano wa mtu na rafiki zake
Uhusiano ni ile hali ya vitu vyenyewe kwa vyenyewe kuwiana, hivyo basi ili tufurahie maisha yetu ya kimwili na kiroho hatuna budi kuwa na uhusiano mzuri. Pamoja na kwamba kuna aina mbalimbali za uhusiano kama :-
• Uhusiano wa mtu na nchi yake
• Uhusiano wa mtu na familia yake
• Uhusiano wa mtu na rafiki zake
• Uhusiano wa mtu na mchumba wake. Nk
Uhusiano wa mtu na Mungu ni ufunguo wa aina zote za mahusiano.


AINA ZA UHUSIANO

Kuna aina kuu mbili za uhusiano ambamo ndani yake mahusiano yote yapo.
1. Uhusiano mbaya
2. Uhusiano mzuri
 
Uhusiano mbaya
Ni ule uhusiano au hali ya kutokuwa na ushirika mzuri, maelewano mazuri baina ya vitu vinavyohusiana. Mfano:-mwenye dhambi na Mungu, mafisadi
na nchi yao, nk
 

Uhusiano wa mume na mke

Uhusiano mzuri
Ni ule uhusiano au hali ya kuwa na ushirika mzuri, maelewano mazuri baina ya vitu vinavyohusiana. Mfano:- Uhusiano kati ya Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Ni wazi kwamba wengi wetu tunapenda kuwa na mahusiano mazuri katika maisha yetu, hivyo basi vifuatavyo na vitu muhimu katika uhusiano wa mtu na Mungu na mahusiano mengine yeyote, upendo, msamaha, mawasiliano, uaminifu, imani, uvumilivu, zawadi, shukurani pamoja ahadi . Pamoja na kwamba vitu hivyo tisa juu vinawezakutufanya tuwe na uhusiano mzuri na Mungu, bado tunahitaji kujua au kujifunza vitu vya kuvitilia mkazo au kuwa waangalifu kwavyo ili mahusiano yetu yaendelee kuwa mazuri. Vitu hivyo ni rafiki, ulimi na makwazo, ambapo ukijumlisha na mambo tisa tutakuwa na mambo kumi na mbili ya kujifunza. Karibu tunapoanza kujifunza kwa pamoja kuhusu uhusiano wa mtu na Mungu


Baada yakuangalia utangulizi wa uhusiano wa mtu na Mungu tuanze kuingia ndani zaidi. kwa kuangalia misingi ya uhusiano mzuri.


SEHEMU YA KWANZA
MISINGI YA UHUSIANO MZURI
1) Upendo
2) Msamaha
3) Mawasilano
4) Uaminifu

1. UPENDO
“Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa mungu; na kila
apendaye amezaliwa na mungu naye anamjua mungu.Yeye asiyependa
hakumjua mungu, kwa maana mungu ni upendo.”
Yohana 4:7-8

Naamini karibia kila mmoja wetu anapenda kupendwa, ila sina hakika kama ni wote tunaopenda kupenda. Ili uhusiano wowote uwe mzuri, utengeneze mizizi na ustawi vizuri na kutoa matunda mema, uhusiano huo unaitaji kuwa na upendo ndani yake. Upendo ni kitu cha kwanza muhimu kwenye aina yoyote ya mahusiano. Yawezekana umetamani kusikia mtu akikuambia nakupenda lakini umemkosa; yawezekana hata wazazi wako wameshimdwa kukuaambia au kuonyesha upendo wao kwako, yawezekana umekaa na kujiona ni mtu wa kuchukiwa na watu wote. Neno nakupenda limekuwa bidhaa adimu kwako, umefikia hatua ya kujikataa. Nina habari njema kwako, kuwa kuna mtu anakupenda, anaitwa Yesu.

Yesu alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu, akafa kifo cha aibu pale fuvu la kichwa, juu ya msalaba kwa ajili yako. Hata sasa Yesu anasema anakupenda. Upendo wake hauna kipimo. Upendo wake kwako ni wa gharama ya damu na kifo. Ili akuonyeshe ni jinsi gani anakupenda, aliiacha mbingu akaja duniani aishi na sisi, akala vyakula vyetu, akavaa mavazi yetu, akalala na kutembea nasi. Yeye hakuona kukaa mbinguni kuwa kitu akashuka kutufuaata wanadamu.

Hii ni baada ya mwanadamu wa kwanza Adamu kupoteza uhusiano wetu mzuri na Mungu, Mungu hakuweza kutulia mbinguni, maana masikani yake ni pamoja na wanadamu. Baada ya mwanadamu kupoteza uhusiano wake mzuri na Mungu kilichofanya arudishe uhusiano wake na mwanadamu huyo ni upendo wake mkubwa. “KWA MAANA NJISI HII MUNGU ALIUPENDA ULIMWENGU”. Aliupendaje ulimwengu? Ni kwa kumtoa mwana wake pekee awe daraja, awe patanisho kati yetu na Mungu. Yesu akaamua kulipa gharama ya upatanisho huo, gharama hiyo haikuwa nyingine ila damu isiyokuwa na hatia, uzao wa mwanamke bikira, hakuna mwengine ye yote ambaye angeweza ilipa gharama hiyo zaidi ya Bwana wetu Yesu.
Ambaye kwa uweza wa Roho matakatifu kupitia bikira Mariamu alizaliwa.

“Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika
ndoto, akisema, Yusufu mwana wa Daudi, usohofu kumchukua Mariamu
mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa
mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakaye waokoa
watu wake na dhambi zao.” Mathayo 1:20-21.

Biblia inatuthibitishia kwamba Yesu alikuja kwa ajili yetu, kutuokoa, kurudisha uhusiano wetu mzuri na Baba yetu wa mbinguni. Maana sisi ni watu wake kama vile ambavyo malaika alimwambia Yusufu kwamba yeye ndiye atakaye waokoa watu wake. inafurahisha kujijua kuwa sisi ni watu wake Mungu, sio watu wake tu bali watoto wake, pia ni rafiki zake kama
tutakavyo kuja kuona huko mbele tutakapo zungumzia urafiki.

MAANA YA UPENDO
Upendo una maana nyingi, lakini maana zote zinakaribiana;
• Kuumia kwa ajili ya mwengine. Isaya 53:3-10
• Kuhesabu wengine kuwa bora kuliko wewe
• Kuwa tayari kupoteza maisha yako kwa ajili ya mwengine.

“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye
sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa
wala hatukumhesabu kuwa kitu.
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu;
Lakini tulidhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake
mwenyewe;
Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama
mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,
Na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;
Na maisha yake ni nani atakaye simulia?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;
Ingawa hakutenda jeuri. Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
Lakini BWANA aliridhika kumchubua; Amemuhuzunisha;
Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,
Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake.
Isaya 53:3-10

Maandiko haya yanayoelezea maana ya upendo kwa undani sana. Mtu akikuambia anataka kujua maana ya upendo mwambie asomee Isaya 53. Nabii Isaya anaelezea upendo wa Mungu kwetu ulivyo au kwa lugha nyingine anaelezea na kutoa maana halisi ya upendo. Je, ni watu wangapi wanakuambia wanakupenda lakini hawapo tayari kuumia kwa ajili yako, wanaishia kukupenda kwa maneno tu? Huo sio upendo. Tutaona ni jinsi gani upendo unavyoambatana na vitendo.
Yesu alikuwa tayari kuumia kwa ajili yetu. Alikuwa tayari kuyapotezamaisha yake kwa ajili yetu. Alipigwa ili sisi tupone. Alizaliwa katika hali ya umasikini ili sisi tuwe matajiri, hata kama asingesema kwa manenokwamba anatupenda,vitendo vyake vinonyesha na kusema ‘nakupenda, sipendi kuona ukiishi maisha ya utumwa wa dhambi, maisha ya kuteswa na magonjwa, kusumbuliwa na kuteswa na nguvu za giza akasema basi imekwisha!; Hata leo yawezekana bado unamfanya Yesu aendelee kuumia kwa sababu hutaki kumpa maisha yako ayaongoze. Unaufanya moyo wako kuwa mgumu, lakini bado anakuita anatamka kwa nguvu nakupende! Nakupenda! Nakupenda

ASILI YA UPENDO
Ili tuweze kupenda hatunabudi kujua asili ya upendo ni wapi. Maana ni wazi kwamba kila mtu anatamani kupendwa. Ingawa sio lazima kila mtu akupende. Watu wengi tunautafuta upendo kwa watu, tunajitaidi kuwapenda watu lakini tunashindwa. Inawezekana ni kwa sababu hatujui
asili ya upendo. Hatufahamu chanzo cha upendo. Wengine tunaamini tutaupata upendo kutoka kwa wake zetu, marafiki zetu, au watu ambao tunaona kuwa ni wa karibu nasi. Hivyo pale inapotokea tukaukosa upendo huo tunaishia kulaumu.

Yesu alimwambia yule mwnamke kisimani kwamba angekunywa maji anayoyatoa yeye asingepata kiu kamwe kwa lugha nyingine anamwambia yeye ndiyo chanzo cha maji, yeye ni chemichemi ya uzima, yeye ndiyo chanzo, hivyo hata upendo unatoka kwake. Asili ya upendo ni Mungu. Mtume Yohana analielezea hilo katika nyaraka zake tatu alizoandika alipotoka kisiwani Patimo, ameongelea kuhusu upendo, najua yeye aliufahamu upendo wa Yesu kwa namna ya kipekee kwa sababu alikuwa karibu sana na Yesu, hivyo aliupata upendo, alikaa na upendo na akaishi na upendo mwisho akaandika kuhusu upendo

“Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa mungu; na kila
apendaye amezaliwa na mungu naye anamjua mungu.Yeye asiyependa
hakumjua mungu, kwa maana mungu ni upendo.”
I.yohana 4:7-8

Vitu vya kuviangalia

i. Pendo latoka kwa Mungu
Jambo la kwanza kulizingatia Yohana anataka tupendane kwa sababu pendo limetoka kwaMungu. Kwa hiyo hatuwezi kupendana kama hatujapata upendo kutoka kwa huyo Mungu. Huwezi kusema unampenda jirani yako kama humpendi Mungu, ndivyo ilivyo pia kwamba huwezi kumpenda Mungu kama humpendi jirani yako. Hapo kuna vitu viwili; Mungu na jirani.
Mungu ndiye upendo wenyewe au yeye ndiye chanzo cha upendo na anatupa huo upendo ili na sisi tupendane, hivyo ukiwa na upendo huo ndio unaweza kumpenda jirani yako. Na ili uupata upendo kwa ajili ya jirani yako huna budi kumpenda Mungu ili akupe huo upendo

ii. Apendaye na asiyependa
Watu wengi tunatamani na tunapenda kupendwa lakini hatufikirii kuhusu kupenda. Kama hatuwezi kupenda basi hatujatokana na Mungu. Na kama hatujatokana na Mungu tumetokana na kitu kingine tofauti na yeye, kupenda wengine ni moja ya dalili za kumjua Mungu. Kama
vile tunavyopenda kupendwa ndivyo hivyo hivyo yatupasa kuwapenda wengine. Tukumbuke chochote apandacho mtu ndicho atakacho vuna, ukipanda upendo utavuna upendo na kadhalika ukipanda chuki utavuna chuki, fanya uchunguzi kwa watu wapendao kusema mimi simpendi fulani, simpendi huyu au yule mara nyingi watu hao huchukiwa na wengine hata
kama hakuna atakaye mwambia kwa Maneno kuwa nakuchukia

iii. Mungu ni Upendo
Biblia inatuambia kuwa Mungu mwenyewe ndio upendo, kwa hiyo asili ya upendo ni Mungu mwenyewe. Sheteni anawadanganya watu wengi kwa sababu anajua thamani ya upendo na asili ya upendo kuwa ni Mungu. Tukumbuke kuwa shetani alitaka kuwa kama Mungu hivyo pamoja na kushindwa na kuondolewa mbinguni bado anataka aabudiwe kama Mungu, ndio sababu anatolewa sadaka ambazo tunaziita kafara. Bado anataka kuabudiwa, tunaita ibada hizo kuwa ni ibada za sanamu. Vitu ambavyo anavitumia sana kupotosha watu wengi ni muziki na upendo ambao tunautambua kama mapenzi

1 comment:

  1. Mtumishi umeeleza vizuri lakini hatujaona ukimalizia somo lako,maana umeacha vipengele vingi hewani. MF misingi ya upendo umeelezea mmoja tu na mingine hujaelezea kama vile msamaha,mawasiliano n.k pia na vipengele vingine Vingi tu umeviacha hivyo malizia somo lako maan tunahitaji kujifunza zaid.umetupa utamu alafu ukautoa gafra.

    ReplyDelete