Saturday, November 30, 2013

JIFUNZE KUWA KONDOO!!!


Kama kuna vitu vya kushangaza ni jinsi ambavyo Yesu amemtumia mnyama Kondoo kujifunua au kutufundisha SIRI za Mungu. Yeye mwenyewe amejiita “Mwana-kondoo” sio KONDOO DUME MKUBWA! No! yeye ni kifaranga/kitoto cha kondoo tu! Mwana-kondoo au mtoto wa kondoo! (alama ya unyeyekevu wa hali ya juu). Nataka tujifunze nini maana ya kuwa Kondoo japo sitaweza kumaliza maana yake kwa sababu ni kubwa.

Jina la Mwana-kondoo lilitumika kwa mara ya kwanza Mbinguni (Ufunuo 5:1-14). Pale ambapo Mungu alitafuta “wa kwenda kuokoa Ulimwengu”, WOTE wakakaa kimya! Lakini akonaekana MWANA-KONDOO kutoka kabila ya YUDA naye AMECHINJWA! (kusulubiwa) na kwa Damu ya huyu MWANA-KONDOO Ulimwengu umeokolewa! Hii ni Damu ya thamani isiyoharibika iwezayo KUKUNUNUA kutoka katika hali yoyote na BEI zako MBAYA na kukufanya kiumbe KIPYA cha thamani kwa Mungu.

Sasa hatua ya kwanza, jua Yesu ni Mwana-kondoo. Hatua ya pili jua kwamba alipodhihirika katika mwili alitufundisha kuwa YEYE ni MCHUNGAJI mkuu wa Kondoo. Na sisi watu wake akatuita kondoo wa MALISHO yake. Kazi ya mchungaji ni KULISHA, KULINDA na KUTUNZA kondoo. KAZI ya kondoo ni KULA, KUKUA, KUMSIKILIZA mchungaji, na KUZAA (kuleta faida kwa Mchungaji).

Tabia ya Mchungaji wa kondoo (Yesu) ni KUTANGULIA kondoo na sio kukaa nyuma. Amejiita MLANGO wa kondoo. Sio tu KUKUTANGULIA katika mambo yote ila HAKUNA kitu kinapita kukuangamiza kikakatiza MLANGONI kama uko ndani ya Yesu! Kwanini? Yesu ni Mlango wa kondoo! Sifa nyingine ya muhimu hapa ni ile inayomtofautisha Yesu na Wachungaji wa MSHAHARA! Anasema “maisha ya kondoo kwa hao wachungaji wa mshahara sio kitu”, akija MBWA MWITU mchungaji wa mshahara hukimbia, ILA Mchungaji wa kondoo (YESU) anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake! Sasa jua neno hili, kabla ADUI hajakuua wewe ni lazima amuue au amshinde kwanza Yesu kama wewe ni kondoo wa zizi lake! Kwanini? Sababu wewe uko NDANI yake na YESU ni Mlango! Haya maandiko NDIVYO YALIVYO kama huyaamini omba IMANI zaidi Mungu akusaidie “kutokuamini kwako”. Kama kuna mahali salama ni kwa YESU.

Sasa haisaidii sana kujiita wewe ni kondoo halafu uko nje ya ZIZI. Lazima Uwe na UHAKIKA juu ya mambo mawili. 1. WEWE ni KONDOO, na 2. WEWE ni KONDOO wa ZIZI la YESU. Ya 3 sio muhimu kwa maana Yesu anajua kazi yake kwamba YEYE ni “MCHUNGAJI wako na hutapungukiwa na kitu na anajua atakulisha majani safi, atakuchunga kwa fimbo yake atakulinda na kukufariji kwa gongo lake na ujapopita kwenye bonde la uvuli wa mauti hutaogopa mabaya..,nk” Anajua kazi yake huna haja ya KUMWOMBA wala KUMFUNDISHA maana ALIJIPA mwenyewe hii kazi na AKAAHIDI “kulitizama NENO lake na KULITIMIZA”. Kazi yako wewe ni kuwa KONDOO wa ZIZI lake, basi! Mengine ni “kukumbushana na kuhojiana na unaeleza shida zako na hoja zako na Bwana anakupa haki na haja za moyo yako”. Na kama UMEJIKUTA nje ya ZIZI kwa namna fulani MCHUNGAJI anakuambia “njoo tusemezane, dhambi zako zijapokua nyekundu kama damu, bendera, nk zitakua nyeupe kama dheluji, sufu, nk..” Anasamehe na kukukaribisha TENA.

Sikiliza, kwa kondoo aliyepotea (katika dhambi), Mchungaji wa KONDOO (Yesu) yuko RADHI aache kondoo wengine 99 zizini, akakusake huko ukilikopotelea na akikupata, sio tu anakurudisha ila ANAKUBEBA MABEGANI mwake wakati anakurudisha. Usifanye mchezo kabisa mtu ANAPORUDI NYUMA au KUANGUKA dhambini. Wakati kanisa na watu “wanaojihesabia haki kwa matendo yao mema” wanakuinukia, Ibilisi na VIBARAKA vyake wanapokuzomea, MCHUNGAJI Yesu anakuja huko speed! Anakunyanyua ghafla! Kabla hawajakaa sawa, ADUI zako wanagundua unaanza KUFANIKIWA tena kwa UPAKO mkubwa, kumbe safari hii uko JUU ya MABEGA ya Yesu na sio miguu yako inatembea ila ni miguu ya BWANA, Simba wa kabila la YUDA ananguruma na kuwasambaratisha ghafla! Anakurudisha zizini kwa AMANI! Hii ni NEEMA ya ajabu sana mbayo kama hujaijua bado hujamjua huyu MCHUNGAJI wa kondoo ninayesema habari zake.


Utajuaje kwamba wewe ni kondoo? Sikiliza, sifa chache sana nakupa kati ya nyingi na zitakusaidia. 1. Kondoo husikia SAUTI ya mchungaji. Kandoo anamjua mchungaji na mchungaji AKIITA kandoo wanasikia na kutii. Hawachanganyi sauti ya Mchungaji wao na sauti ya Mbwa mwitu hata siku moja. Je! Unaisikia sauti ya Yesu na kutii akuitapo au akuonyapo au akukatazapo kufanya mambo fulani katika maisha yako? Jijibu mwenyewe. 2. Mchungaji anaongoza kondoo anakotaka YEYE sio kondoo wanachagua cha kufanya wao wenyewe. Je! Katika maamuzi yako, mipango yako, njia zako, kazi, huduma, nk. Unamshirikisha Yesu KWANZA au unamshirikisha “mtumishi” au rafiki kwanza? Sio tu kumshirikisha, je! Ni wa KWANZA kushirikishwa? Na unafanya nini unapogundua hupaswi kwenda/kufanya/kukaa/kujihusisha na mambo fulani? Unamtii na kuongozwa na Mchungaji Yesu? 3. Kondoo huwa ANAZAA: kondoo wengine (ndama), sufi, mbolea kisha huchinjwa kama kitoweo. Sufi kuhudumia wanadamu na mbolea kuhudumia mimea. Huko mbele kuchinjwa (kufa) kwa sababu mbili kubwa 1. Karamu (uzima wa milele) au 2. Msiba (jahanam ya moto) Je! Katika maisha yako umezaa matunda gani katika Ufalme wa Mungu? Unautarajia ufalme wa Mungu au Jehanam ya moto? Jijibu mwenyewe maana MAISHA ni KUPANGA na KUCHAGUA.

Katika hayo mambo matatu kati ya mengi ya KUJIPIMA, jiangalie mwenyewe maana haijalishi jina la DHEHEBU au mahali unasali au watu WANAKUJUA vipi, maana tunasoma kuna MBWA MWITU wenye ngozi ya kondoo! Sasa sisi huku nje hatuoni ila unajijua huko ndani ukijiweka katika mizani ya hayo mambo matatu na mengine kujua kama wewe ni KONDOO au MBUZI au MBWA MWITU, nk. Kisha chukua hatua ikupasayo.

Siku Bwana anakuwa Mchungaji wako HUTAPUNGUKIWA na kitu. Na ukigundua kitu kimepungua UNAMKUMBUSHA hii ahadi KAMA una UHAKIKA kwamba wewe ni KONDOO wa ZIZI lake! Hii ni faida moja KUBWA ya kuwa KONDOO wa zizi la Mungu. Usiige maneno ya Zaburi 23 na kuyakiri kwa bidii kama BWANA sio Mchungaji wako, hufiki mbali! PATA uhakika ndani yako, jipange sawa sawa na upate ujasiri wa kusema kama mfalme DAUDI kwamba “Bwana ni Mchungaji wangu”!

Neema na Baraka zitokazo juu ziwajaze na kuwafundisha kukaa chini ya Mchungaji MKUU wa kondoo, Yesu Kristo tangu sasa na HATA Milele. AMEN.

Frank Philip.

Friday, November 29, 2013

EPUKA LAANA HII!!!


Kama kuna kitu KIMEUA (kimwili, kiakili, kimaendeleo, kiroho, nk.) WATU wengi ni kumfanya MTU mwingine kuwa TEGEMEO lake la kipato. Kuna tofauti ya KUMHITAJI mtu na kumfanya mtu TEGEMEO lako. Hakuna MWANADAMU ataishi chini ya jua bila KUHITAJI msaada kutoka kwa mwingine, ila Biblia inatukataza kuwafanya hawa watu kuwa TEGEMEO! Sikiliza, "Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.” (Yeremia 17:5) Sio mimi nimesema ila ni maandiko.

Sasa utajuaje kwamba umefikia hii hatua mbaya ya LAANA? Nitakupa mfano. Ukijikuta UNAKWAZIKA au UNAUMIA sana kama mtu fulani HAJAKUSAIDIA au hata KUKUSIKILIZA katika shida yako jua huyo mtu kwako ni TEGEMEO! Unamlaumu kwani yeye ndio Mungu? haya basi sio Mungu, kwani yeye ndio Shetani anayeleta shida na mateso kwa watu? Ndio maana unaweza ukawa na shida nyingi sana, lakini kuna watu wala hukumbuki KUWALAUMU kwa kutokukusaidia! Sababu? Wao sio TEGEMEO kwako.

Sasa, ukijifunza kumfanya Mungu kuwa TEGEMEO lako, ukiwa na shida Yeye atakua wa kwanza kujua, maana utamshirikisha yeye na KUOMBA kama hakuna mtu pembeni...sasa Mungu akimgusa MTU kukupa kitu "huku moyoni" kitakachotokea UTAJISIKIA kumshukuru Mungu na sio huyu mtu, japo utamshukuru kweli lakini kuna HATUA unatakiwa kufika na kusema "NIMEMWONA MUNGU" na unabarikiwa (amani, furaha, mafanikio, nk.) baada ya huo MSAADA! Na utagundua huyo "mtu" aliyekusaida HAWEZI kuwa kwazo wala JARIBU kwako kwa maana moyo wako UNAJIKUTA unamwelekea Mungu na sio huyu mtu aliyekusaidia! LAKINI kama mtu ni TEGEMEO lako, huwezi kuepusha moyo wako kumfuata huyu "mtu" anayekusaidia.....jaribu utagundua moyo wako una nguvu kuliko akili yako....UKITAKA kupona na dunia hii, na KUUDHIBITI moyo wako sawasawa, mfanye MUNGU kuwa TEGEMEO lako ama sivyo jiandae kabisa kutumika, kuwa mtumwa, kudhalilika, kunyanyaswa, kutukanwa, hata kufa na majanga mbalimbali....hii ndio inaitwa LAANA! "AMELAANIWA mtu yule amtegemeaye mwanadamu..."..

Ukikuta ndani yako unasema “hii shida yangu kama isingekea fulani, sijui ingekuaje”, au “kama kuna watu duniani basi fulani sitamsahau”, au “kuna watu wana roho nzuri…” halafu humalizii au unaguna hapo mwisho mhhh.. ANGALIA unakaribia LAANA kama haijakupata tayari. Utakuta mtu hawezi kutoa USHUHUDA wa maisha yake bila kumtaja MTU fulani, na anamhusisha moja kwa moja na MAFANIKIO yake fulani katika maisha. Usije ukafikiri unamsaidia huyo mtu, UNAMWANGAMIZA! Kama kuna hatari duniani, ni kuchukua UTUKUFU wa Mungu na kumpa mtu. “20 Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. 21 Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. 22 Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho. 23 Neno la Bwana likazidi na kuenea.” (Matendo 12: 20-23)

Kama hili Neno limekufikia hapo ulipo, nakusihi kwa Neema za Bwana, tafuta mahali umemfanya mwanadamu kuwa TEGEMEO lako, na nenda mbele za Mungu kwa TOBA ukiwataja hao watu na kumshukuru Mungu kwa sababu ALIWATUMIA na KUMRUDISHIA Mungu utukufu wake, na kuomba REHEMA juu yako na juu ya hao watu ili msiishie katika LAANA na mkaangamia. Katika Jina la Yesu.

Mungu atusaidie kuelewa hii SIRI kwa sababu Ibilisi hawezi KUKULAANI ila unajilaani mwenyewe kwa kutokujua mambo ya muhimu kama haya. AMANI na NEEMA ya BWANA wetu YESU iwe juu yetu sote. AMEN.

Frank Philip.

Wednesday, November 27, 2013

UMUHIMU WA MASHABIKI!!!


Katika MASHINDANO, kwa mfano riadha, huwa kuna MCHUANO mkali na MKIMBIAJI anapokaribia MAHALI pa USHINDI huwa inakua ni ngumu sana maana NGUVU za mwili zinaisha japo MOYO u radhi.

Sasa, wakati MKIMBIAJI anajitahidi, jasho linatiririka huku kambi ya ADUI ikizomea na kambi ya Mungu ikishangilia, kwa kadri MASHABIKI wa kambi ya Mungu wanavyoshangilia MKIMBIAJI anajikuta anapata NGUVU na anaongeza mbio. Akifika mahali WASHANGILIAJI wamekaa kimya au wanazomea, huyu ndugu hujikuta anakosa NGUVU ya KUSHINDANA na anakata tamaa hata mara nyingine kuzimia moyo, kuanguka au KUJIUZULU mashindano.

Katika NJIA ya IMANI ndani ya Yesu, sio tu kwamba njia IMESONGA ila pia ni NGUMU na kuna mambo mengi sana magumu. Kama hakuna KUTIWA moyo katika hii njia nakwambia wengi sana watazimia NJIANI kwa sababu KAMBI ya ADUI imezidisha KUZOMEA na kambi ya MUNGU haishangilii au imejiunga na kambi ya ADUI kumzomea MKIMBIAJI! Wengi wamerudi nyuma kwa sababu tu hawajapata watu wa ku-appreciate ka-hatua kadogo wanakojitahidi kupiga katika UDHAIFU na UCHANGA wao.


Hawa walio tutangulia, ambao mara nyingi wameishia KUJIGAMBA kwa MEDALI zao na kuhesabu madhaifu ya hawa WAKIMBIAJI wachanga, imekua KWAZO na ndio maana Yesu anasema OLE wake AKWAZAYE “mmoja kati ya WADOGO hao” kwa maana ni aheri angefungiwe jiwe la kusagia na KUTUPILIWA mbali kwenye vilindi vya bahari. Sasa mara nyingi sana watu wanadhani vita kali katika Injili ni ya WAMATAIFA, No! Katika maandiko fuatilia waliokua wanampa shida YESU kwenye huduma yake ni akina nani? Ni WAKUU wa DINI! Wakati Bwana anatandika Injili, wao wanakuja na VITABU vyao KUPIMA ujumbe ili wapate mahali pa KUMHUKUMU badala ya kujifunza au kumsaidia KIHUDUMA! Hakuna mahali tunaambiawa WAKUU wa DINI walijikusanya kwa MAOMBI kwa ajili ya huyu “dogo” wa Nazareti aliyeibuka hapa JUZI. Walitafuta kumhukumu! Nikodemu akagundua SIRI, ila kwa kuogopa, akajisalimisha kwa siri. Sasa usifikiri ilikua rahisi, maana Yesu alikuwa kijana mdogo sana tu, wa takriban miaka 30, na hawa WAKUU wa DINI ni MIJIBABA ya NGUVU iliyobobea katika KILA ELIMU. Na haikua rahisi kupenya hapo. Wakamsulubisha Bwana wangu ili wazimishe CHANAGAMOTO kubwa aliyokua akiibua katika ile jamii hadi wale WAKUU wakaona UMAARUFU wao unapata shida.

Nazungumza na TAWI changa muda huu. Kumbuka SIRI ya kuzaa ni kukaa katika MZABIBU (Yesu). Na Kuzaa MATUNDA ni LAZIMA! Ila pamoja na UCHAFU wako na UNYONGE wako usikatishwe tamaa. Jipe moyo. Hivyo hivyo usikatishwe tamaa kwa maana BWANA alisema “ukizaa” UTASAFISHWA ili uzae zaidi. Kwanini USAFISHWE kama wewe ni SAFI tayari? Hakuna asiye na MADHAIFU, ila usiangalie udaifu wako au wa wengine ukashindwa KUSIMAMA katika nafasi yako na KUZAA matunda. Mara nyingine UTAZOMEWA badala ya KUSHANGILIWA sio tu na Ibilisi ila hata na wale waliopaswa KUKU-SUPPORT nao watakaa kimya au kukufanyia FITNA! Kaza uso wako kwa BWANA kama STEFANO, usihesabu MAWE unayopigwa, Mtizame BWANA aliyekuita, na USISAHAU kuwasamehe wanaokurushia MAWE. Njia imesonga, ukisikia kubanwa jua hujapotea njia. UWE na AMANI TELE.

Frank Philip.

Tuesday, November 26, 2013

UMUHIMU WA MWANA MPOTEVU!!!


Mara nyingi sana kumekua na hali ya kujihesabia haki kati ya wana wa Mungu kwa sababu eti fulani kaanguka kwenye dhambi, karudi nyuma, nk., na mimi niko fit! Hii hali imelifikisha kanisa mahali ambapo “kurejezana kwa roho ya upole” kumepungua ila wengi “wanajaribiwa” nafsini mwao kwa sababu ya MWANA mpotevu na UZINZI wake.

Sikiliza, pamoja na kwamba MWANA mpotevu ni MPOTEVU lakini bado ana haki kama MWANA! Pamoja na kwamba ndugu zake wanamshangaa anavyo kengeuka na kumwasi BABA yao hadharani, BADO baba yake anampenda. Kama kuna fumbo duniani ni kujua tofauti ya WALIOITWA na WATEULE. Maandiko yanasema WALIOITWA ni wengi ila WATEULE ni wachache. Kukuweka mahali pagumu zaidi kibinadamu, maandiko yanasema MTEULE ataanguka mara saba ila atainuka! Ndo maana utasikia “usifurahi ee adui yangu, niangukapo mimi nitainuka tena” na utukufu wa mwisho utakua mkubwa kuliko wa kwanza. Wakati ADUI za Mungu wanashangilia KUANGUKA kwa mteule, ghafla! Anainuka na upako mwingine tena MKUBWA! Haleluyaa. Usikose kujua UMUHIMU wa mwana mpotevu, kwa maana Mungu anamwita CHOMBO KITEULE!

Wakati SAULI wa Tarso “anatesa na kuharibu” kanisa, watu walimuona muuaji, pepo mchafu, adui, nk. Mungu alikuwa anaona “chombo kiteule”! Sasa wako wengi sana leo ni WAHARIBIFU kanisani na nje ya kanisa. Waangalie sana maana kuna ghadhabu ya Mungu, na kikombe cha ghadabu yake kikijaa na kumiminwa juu yao hawataamini kitakachotokea, ila tunaomba ile NEEMA iliyomfundisha SAULI wa Tarso (mtume PAULO), iwatembelee hawa ndugu. Na sisi wengine humo tukikumbuka KUWAOMBEA watakatifu ili wasimame katika wito wao na kazi ya INJILI isonge mbele na MWILI wa Kristo ujengwe.

MWANA mpotevu (huyu mpendwa) alipodai sehemu ya URITHI (tunapomwomba Mungu mali huku duniani kwa sababu sisi ni WARITHI wa Baraka za Ibrahim), na kupata PESA, MALI, UMAARUFU, nk., alienda NCHI ya mbali (akakaa mbali na Baba yake na ndugu zake [dhambi inamtenga mtu na Mungu]. Mwili wa Kristo na kama ndugu katika familia moja na baba yetu ni Mungu). Huko katika NCHI ya mbali, akazini na kutapanya mali hadi AKAFILISIKA! Sasa anarudi kwa BABA yake na kutamani kuwa MTUMISHI potelea mbali hata kama sio MWANA! Anatamani tena ile kazi ya HUDUMA kule “Shambani mwa Baba”, Sasa sikiliza. BABA alimuona kwa “mbali” akapiga mbio kumlaki, kumbusu na kumvika VAZI jipya (wokovu) na PETE (mamlaka) kidoleni, na kufanya KARAMU. Ndugu zake (wapendwa) wanalalamika “sisi tuko hapa hata hatujazini, wala kumkosea BABA ila huyu MWASHERATI anakuja na kufanyiwa PARTY! Tuko busy hapa tunazaa matunda huyu jamaa alikuwa na MAKAHABA huko sasa anapata MUALIKO kama MTU wa MUHIMU!” Chunga hili eneo na UJIFUNZE kuwarejesha wenzako kwa UPOLE na UNYENYEKEVU huku ukijiangalia USIJARIBIWE na KUMKOSEA Mungu kwa sababu wengine wamemkosea! Huyu mwana mpotevu ni MUHIMU kwa BABA!

Amani, Baraka, Furaha, Upendo na Neema vizidi kwenu.

Frank Philip.

Friday, November 22, 2013

UJUMBE kwa WANAFUNZI!!!



Elimu ya kawaida tunayosoma mashuleni ni sehemu ya makusudi ya Mungu ili uweze kuishi maisha BORA na uweze KUFANIKIWA kwa urahisi katika shughuli za kila siku ikiwemo na kumtumikia Mungu. Mungu hapendi “mbumbumbu” Soma kwa bidii.

Kuna vitu vya msingi nataka niweke hapa. Kwanza jua kuna uhusiano wa MAFANIKO yako ya kielimu na TABIA yako. Tabia ni mjumuisho wa mwenendo wako ambao unajidhihirisha katika matendo, maneno, mawazo na hisia zako. Tunajifunza katika Neno la Mungu kwamba “maneno mabaya huharibu tabia njema”. Kama unataka kuchunga tabia yako, jifunze kuchunga “makundi” ya watu na mambo wanayoongea katika makundi hayo. Imani yoyote huja kwa “kusikia” au kwa kuona, na hicho unachokisikia/kiona ndicho kitakujengea imani fulani ambayo ina athari kubwa katika utendaji wako wa kila siku. Ukisikiliza sana Neno la Mungu utakua na IMANI ya kiungu, ukisikiliza sana mambo ya KICHAWI utajikuta unaanza kuamini katika ushirikina, nk. Tengeneza imani yako na ilinde sana maana itakupa ushindi katika VITA mbalimbali za kitaaluma.

Biblia inaita elimu ni “uzima wako” na inasema umshike sana na usimwache aende zake huyu mdudu anaitwa Elimu, kwa maana kuna faida kubwa. Na kwanini unshike sana? Kwa sababu anateleza! Ni ngumu kukamata, inahitaji jitihada na Elimu “hakungoji”. Changamoto kubwa ya elimu ni MUDA, kila kiwango cha elimu kinapimwa kwa muda na muda haukungoji.

Kabala Mungu haja mtumia Musa kufanya kazi kubwa sana ya Ukombozi wa taifa la Israel alikaa kwanza shule, akasoma elimu “yote” ya Misri! Sio elimu ya DINI, No. Elimu ya Misri. Kuna wale vijana watatu mashujaa sana majina yao ni Shedrack, Meshak na Abednego, pamoja na Daniel, wakiwa huko Babeli kitu kimojawapo walichofanya ni kujifunza shule kwanza, miaka 3 darasani! Usije ukadhani walikua mabingwa wa KUSALI tu, hapana walikua WANAPIGA kitabu kwa msuli mkubwa pia. Baada ya kufuzu ndio wakapata AJIRA IKULU.

Ukiangalia kwenye again Jipya. Yesu alijifunza kusoma ndio maana alipoingia hekaluni aliomba Gombo la chuo na akasoma Mlango wa 61 wa kitabu cha nabii Isaya. Ukifuatilia idadi ya machapisho kwenye Agano jipya utagundua Mtume Paulo aliandika karibia ¾ (robo tatu) ya Agano jipya, kwanini? Alikua msomi kuliko wenzake! Alikaa chini ya Mafarisayo nguli akasoma sheria na Torati na alikau msomi kamili.

Sasa Vijana wengi sana wanafikiri wataenda chuo kuu kwa IMANI! Ni sawa kabisa, LAKINI imani bila matendo imekufa. Lazima ujichimbie na uwe na nidhamu ya kukaa LIBRARY/MAHALI na KUSOMA kwa ADABU na kwa BIDII. Achana na michezo ya kupoteza muda na mafariki wabaya. Komboa muda wako maana hizi ni saa za uovu. Ibilisi ameharibu watu wengi sana wakiwa katika ngazi ya UANAFUNZI kwa sababu mbalimbali. Kwa mfano, uwezo mdogo wa wazazi kukupa hela za matumizi na “tamaa” ya kula na kumiliki vitu vizuri inakuzonga. Waswahili wanasema “tamaa inaua” lakini katika maandiko imo hiyo kwamba “Mungu hamjaribu mtu, ILA mtu hujaribiwa na tamaa zake mwenyewe, na tamaa ikikomaa huzaa dhambi na dhambi ikishakukomaa huzaa MAUTI”. Kila mtenda dhambi ni MTUMWA wa zambi, na sifa ya mtumwa ni kutokua na uhuru wake! Sasa sikiliza MWANAFUNZI, ukianza kuishi maisha ya dhambi, ghafla unakua “mtumwa” wa hiyo dhambi na unaanza kuitumikia kwa AKILI na MAWAZO yako na shule inakua NGUMU. Mara nyingi mtu aliyeko katika ngazi hii hajui kiwango cha madhara hadi yatokee ndo maana naleta huu ujumbe ili ufanye uamuzi LEO.

Kama mtu angerudisha miaka 20 nyuma kwa watu wote, nakwambia hutaamini jinsi watu wangesafisha “DIVISION” zao na yamkini idadi ya Division ZERO ingekua ndogo sana au hakuna aliyefeli. Kwanini? Majuto ni mjukuu. Wengi wamechezea MUDA wao wakiwa shuleni na wamefeli na maisha yanawachapa FIMBO kila siku na wamekosa nafasi za muhimu kwa sababu ya kigezo cha ELIMU! Wangepata nafasi ya kurekebisha UFAULU wao nakwambia asingekuwepo hata mmoja angefeli baada ya “kichapo kikali cha maisha”. Ila pia kwa bahati mbaya sana wengine wamejikuta wamepata “magnjwa magumu sana” wakiwa shuleni, Mungu awarehemu tu na bado Mungu ana DAWA ya kuwasaidia hata hao, waje tu watapata REHEMA.

Kumbuka mwanafunzi. Anayelala sasa akiwa shuleni atarajie kukesha kwa ugumu wa maisha na anayekesha sasa hivi akijitahidi na kufaulu ajue huko mbele atafaidi matunda manono. Jua pia kwamba MFUMO wa Elimu umewekwa ili KUBAGUA nani afanye kazi chafu/ngumu kwa mapato KIDUNCHU na nani afanye kazi safi/nzuri kwa mapato MANONO. Chagua unataka nini na anza kujipanga kwa maombi na kufanya kazi kwa bidii. Chunga simu za mkononi, Internet, magazeti, tamthilia, TV, michezo mbalimbali, nk. Hivi vitu ni vya muhimu sana ila uwe na HEKIMA maana vimepoteza wengi. HATIMA YAKO IKO MIKONONI MWAKO. MUNGU ATUSAIDIE. AMEN

Frank Philip

Wednesday, November 20, 2013

JUMAPILI HII HAPATATOSHA CCC-UPANGA KWA UJIO NA MOTO MPYA WA CHRISTINA SHUSHO!!!!!

KAMA HABARI HII HAIJAKUFIKIA BASI NAOMBA NIKUJUZE RASMI!
MWANAMAMA ANAYETAMBA NA MAHADHI YA KIPEKEE KATIKA MUZIKI WA INJILI TANZANIA NA AFRIKA MASHARIKI,IKIWA TU BAADA YA KUJINYAKULIA TUZO YA MWANAMUZIKI BORA WA INJILI AFRIKA UKANDA WA AFRIKA MASHARIKI KWA 2013,SASA ANAKUJA KIVINGINE,ANAKUJA UPYA,NDIO AMEAMUA KUHAMA KABISA TOKA KUIMBA KWA KUTUMIA CD MPAKA KUIMBA MOJA KWA MOJA......NI JUMAPILI HII NDANI YA UKUMBI WA CCC-UPANGA!
JUKWAANI ATAIMBA PAMOJA NA BAHATI BUKUKU,UPENDO KILAHIRO,JOSHUA MLELWA,AMANI KAPAMA,PAUL CLEMENT,THE VOICE ACAPELLA PAMOJA NA KINONDONI REVIVAL CHOIR!
MAJIRA YA SAA NANE GETI LITAKUWA WAZI NA SAA TISA TAMASHA LITAANZA RASMI,KAMA WEWE NI MGENI MAHALI HAPO BASI FIKA POSTA MPYA SAA NANE NA HAPO UTAPATA GARI MPAKA UKUMBINI KWA BEI YA KAWAIDA!
UTAKUWA SEHEMU YA HISTORIA HII KWA KUCHANGIA KWA KUNUNUA TIKETI TSH 10,000/= KAWAIDA,20,000/=VIP NA 3000/= KWA WATOTO!
NI VIZURI KUPATA TIKETI YAKO MAPEMA PALE SILVERSPOON-MLIMANICITY,MWENGE-PUMA KITUO CHA MAFUTA NA STEERS-POSTA,INGAWA HATA MLANGONI ZITAKUWEPO!
ZINGATIA KUWAHI,ZINGATIA KUWATAARIFU WENGINE NA KWA JAMBO LOLOTE LA ZIADA BASI USISITE KUWASILIANA KUPITIA
0713883 797 AU 0713 905 118

Tuesday, November 5, 2013

MILITARY COMMANDOES IN ACTION!!!


(A commando is a soldier specially trained to carry out raids and ‘special missions’)

Mara nyingi tumesikia habari za vita na matetesi ya vita au mashambulizi ya kigaidi amabayo ni magumu na yanahitaji UJUZI na SILAHA malumu katika kukabiliana nayo.

Sio kila askari au mtu anaweza kuhusika na ‘kushinda’ katika baadhi ya “mission” fulani dhidi ya adui. Kuna mission ambazo zinahitaji Ma-COMMANDO tu! Kibaya zaidi adui akija anaangamiza bila huruma. Kazi ya adui ni: KUIBA, KUHARIBU na KUCHINJA (Yohana 10:10), huja kama “simba angurumaye na huzunguka akimtafuta askari aliyekaa vibaya ili ammeze”(1Petro 5:8)

Mafanikio ya askari yeyote KATIKA UAWANJA WA VITA yanategemea mambo kadha:
1. Kujua uwezo wa silaha zake na wapi zinafanya kazi: “Maana silaha za vita vyetu SI ZA MWILI, bali ZINA UWEZO KATIKA MUNGU hata kuangushya ngome; tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, KIJIINUACHO JUU YA ELIMU YA MUNGU; na tukiteka nyara kila FIKIRA ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, KUTII KWENU KUTAKAPOTIMIA” (2 Wakor. 10:3-6).
2. Maarifa: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa”, Askari akikosa maarifa anaangamizwa na adui, (Hosea 6:4).
3. Kujua Neno na Nguvu za Mungu: “ Askari asipojua hilo anapotea katika uwanja wa vita” (Yesu)
4. Ushuhuda: “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao..” (Ufunuo 12:11a)
5. Damu ya Yesu: Simply like a bullet proof! (Ufunuo 12:11)
6. Silaha zote: Helmet (wakovu), mkanda (kweli), Dirii ya kukinga kifua/moyo (haki), upanga/bunduki (Neno la Mungu), boot (Injili), ngao (imani).
7. Jina la Yesu: “KILA atakayeliitia JINA hili ataokoka”. “Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa UWALINDE hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. 12 Nilipokuwapo pamoja nao, MIMI NALIWALINDA KWA JINA LAKO ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. (Yohana 17:11b, 12)

Waefeso 6: 10 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu Zake. 11Vaeni silaha zote za Mungu ILI kwamba mweze kuzipinga hila za Shetani. 12 Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13 Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14 Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16 Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18Mkiomba kwa Roho sikuzote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.”

Je! Wewe umejifunza kutumia silaha ngapi na kwa uhodari gani? IDADI, UMAHIRI na UZOEFU wa kutumia silaha NYINGI zadi kwa USAHIHI, pamoja na kujua MBINU za adui, SIRI na MAARIFA ya uwanja wa VITA vitakufanya uwe mmojawapo wa ma-COMANDO wa Yesu!
 
Na Fank Philip 

KWA MARA YA KWANZA "CHRISTINA SHUSHO" KUIMBA LIVE KATIKA TAMASHA LAKE LA "NATAKA NIMJUE" 24/11/2013 PALE CCC-UPANGA!!!!

Shalom Tanzania!
Baada ya kimya kirefu, mizunguko mingi ya ndani na nje ya nchi kihuduma, Hatimaye Mwanamama, Mtumishi, Mwimbaji alijinyakulia tuzo ya Uanamuziki bora wa nyimbo za injili Ukanda huu wa Afrika Mashariki, CHRISTINA SHUSHO, Sasa amekuja na jambo kubwa la kipee na hili ni TAMASHA LA KUSIFU NA KUMWABUDU MUNGU!
katika TAMASHA hili lililopewa jina "NATAKA NIMJUE", CHRISTINA SHUSHO ATAIMBA LIVE (BILA KUTUMIA CD) na atasindikizwa na Waimbaji kama
1.BAHATI BUKUKU
BAHATI BUKUKU

HUYU NI MWANAMUZIKI ANAYETAMBA NA ALBUM YAKE MPYA KWA SASA IITWAYO "DUNIA HAINA HURUMA"
2.UPENDO KILAHIRO
Pia Vijana wanaochipukia kwa sasa, hapa ninamzungumzia PAUL CLEMENT na mpiga DRUM maarufu mjini na mwimbaji AMANI KAPAMA
PAUL CLEMENT

AMANI KAPAMA
Mkongwe na Muasisi wa Live JOHN LISSU Ambaye amefanya LIVE RECORDING yake kipindi sio kirefu lilichopita mwaka huu!
CHRISTINA SHUSHO & JOHN LISSU

JAMBO KUBWA ZAIDI NI KUWA TAMASHA HILI LITAONGEZEWA VIONJO VYA kwaya ya KINONDONI REVIVAL, watu waliouvuma sana na ule wimbo wao wa "KWANINI UNATAKA KUJIUA?" pamoja vijana wa THE VOICE Acapella!
KINONDONI REVIVAL CHOIR

THE VOICE
TAMASHA HILI LINATARAJIWA KUFANYIKA KATIKA UKUMBI WA CITY CHRISTIAN CENTRE, TAREHE 24/11/2013 KUANZIA SAA NANE MCHANA MPAKA MOJA JIONI KWA VIINGILIO VYA TSH 10,000(Kawaida) na 20,000 (VIP)
Tiketi zinapatikana SILVERSPOON-mlimani city
Kituo cha MAfuta Mwenge-PUMA,kwenye baadhi ya makanisa pamoja na
Banana kwa Giddo
CCC-Mlangoni.....Kumbuka Usafiri kutoka Posta utakuwepo kuwaleta watu tamashani kwa wale wasiopafahu.

Na King Chavala-MC
Publicity & Protocal Manager

KWA MAELEZO ZAIDI
Piga 0713905118 au 0713883797

Monday, November 4, 2013

NEEMA MBISE KUZINDUA ALBUM YAKA YA SAUTI NA VIDEO TAR 17 NOV MOSHI MJINI!!!

MWANAMUZIKI WA INJILI ANAYECHIPUKIA, ANAYEVUMA SANA PANDE ZA KASKAZINI MWA TANZANIA, BAADA YA KUREKODI SAUTI NA KUFANYA VIDEO YA ALBUM YAKE IJULIKANAYO KAMA "SINA CHA KUKUPA"
HATIMAYE YUKO TAYARI KWA AJILI YA KUIWEKA WAKFU AMA KUZINDUA KAMA WENGI WALIVYOZOEA KUITA...TAMASHA HILI KUBWA LA KIPEKEE LINATARAJIA KUWAKUSANYA WAKAZI WA MOSHI NA ARUSHA PAMOJA NA VITONGOJI VYAKE, NEEMA MBISE ATASINDIKIZWA NA WAIMBAJI KAMA VILE
1.AMBWENE MWASONGWE
2.AMBELE CHAPANYOTA
3.LEMBO JUNIOR
4.DANIEL SAFARI
5.GRACE WAGANA
6. ANTONY FRANK NKONDOLA
7.ARUSHA MASS CHOIR NA
8.THE SPRING OF PRAISE
NA WENGINE WENGI BILA KUMSAHAU MISE ANAEL ANAYEABUDU NA KUSIFU KWA KUTUMIA KIFAA KIITWACHO SAKSAFONI!

TAMASHA HILI LITAFANYIKA JUMAPILI YA TAREHE 17/11/2013 PALE UKUMBI WA MR PRICE CITY MOSHI-MKABALA NA TANESCO, KUANZIA SAA NANE MCHANA

MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO, MHESHIMIWA LEONIDAS GAMA NDIYE ANAYETARAJIWA KUWA MGENI RASMI NA TAMASHA HILO LITAENDESHWA NA MSHEREHESHAJI NA MCHEKESHAJI MAARUFU TANZANIA, KING CHAVALA-MC TOKA DAR ES SALAAM!!

NI MUHIMU SANA NA WEWE KUWA SEHEMU YA TAMASHA HILI....TIKETI NI 2000 TU KWA WATU WAZIMA NA 1000 KWA WATOTO!

NEEMA MBISE NI MWIMBAJI WA MAZINGIRA YETU YA NYUMBANI...HEKO WATU WOTE WA MOSHI TUJITOKEZE KUMPA MKONO WA KUMTIA MOYO BINTI YETU!!

GOSPEL STANDARD BASE INAWATAKIENI MAANDALIZI MEMA NA TAMASHA JEMA!!!