SABABU ZA KUFELI
NA KUSHINDWA
(FACTORS OF
FAILURE)
Kwanini watu wa Mungu wanafeli
au wanashindwa au wanakwama?
Hili
ni swali la muhimu sana ambalo linaweza kuwa kama funguo ya dhahadu katika mlango wa mafanikio a
maisha yetu. Kama tukilifungua swali hili vizuri,
tutaweza kupata majibu ya matatizo mengi katika maisha yetu sisi watoto wa
Mungu. Kulingana na ukweli (Neno la
Mungu – Biblia) sisi wana wa Mungu ni “washindi” na zaidi ya washindi, katika
mambo yote (Warumi 8:37;
1Wakorintho 15:57).
Kulingana
na Ukweli wa Neno la Mungu, watu wa Mungu tumeshabarikiwa na kukabidhiwa vitu vyote
tunavyohitaji kwa ajili ya maisha yetu yote ya mwilini na rohoni (Efe 1:3; 2Pet
13-4). Kama ni ushindi juu ya dhambi
na dunia, uwezo huo tumeshapewa na Bwana. Mtu wa Mungu akikumbwa na tamaa za
dunia hii, ina maana kwamba, yeye mwenyewe ameruhusu au amekubali kumtii
shetani kuliko Mungu (Wagalatia 1:3-4;
1Yohana 2:15-17). Kama ni ushindi dhidi ya nguvu za giza, mapepo na wachawi; Mungu amekwishatupa
uwezo huo wa kuwashinda watenda kazi wote wa ibilisi shetani (Wakolosai 1:13; Luka 10:19)
Kama ni ushindi katika afya, tumepewa na tumeponywa tangu
damu ya Yesu ilipomwagika msalabani kwa ajili yetu, na kwa kupigwa kwake sisi
tulikwishaponywa tayari (1Petro 2:24;
Mathayo 8:17). Kama ni jambo la uchimu na
utajiri, watu wa Mungu tulkwishafanywa matajiri na Kristo, kwa kifo chake. Yeye
alichukua umaskini wetu akatupa utajiri wake (2Wakorintho 8:9; 2Wakorintho 9:11). Kama
ni suala la akili an hekima, watu wa Mungu tumekwishapewa uwezo mkubwa wa
kiakili na fikra, kwa Roho Mtakatifu wa Mungu anayeishi ndani yetu. Sisi wana
wa Mungu tuna akili na ufahamu wa kiungu. (Isaya
11:2; Zaburi 111:10; Matendo 6:8-10; 2Timotheo 2:7)
Kama
ni baraka katika mikono yetu, tumekwishapewa na Mungu kwa ajili ya shughuli
zetu (Kumbukumbu 28:1-8; Zaburi 1:1-3) Kama
ni ulinzi juu yetu na nyumba zetu na mali zetu, Bwana amekwisha waagiza malaika
zake watuzunguke kwa panga za moto, farasi, magari ya moto (kufanya ukuta mzito
wa moto) kutuzunguka (Zaburi 34:7; 2Wafalme
6:15-17; Zaburi 121:1-8; Zaburi 91;1-11-12).
SABABU ZA KUFELI
NA KUSHINDWA
Kila
kitu ambacho watu wa Mungu tunachohitaji katika maisha yetu yote ya mwilini an
rohoni, tumekwisha kupewa na Baba yetu aliye mbinguni, ili tuweze kuishi maisha
ya ushindi katika kila eneo linalotuhusu au linalotuzunguka. Kama
ukweli ndio huu basi, kwanini watu wa Mungu wengine wana maisha ya kushindwa na
kufeli? Kwanini watu wa Mungu wengine wanaishi maisha ya kuhangaika na kukosa?
Ni lazima kuna sababu.
1
KUTOKUJUA
Mungu anasema watu
wangu wanaangamia (wanateseka na kuhangaika) kwasababu ya kukosa maarifa
(ufahamu na ujuzi wa mambo niliyokwisha watendea) … japo wana bidii nyingi
lakini wana bidii bila maarifa (wanapoteza nguvu nyingi katika maisha) (Hosea
4:6; Warumi 10:2) Ndio maana
Paulo alikuwa anawakazania sana wanafunzi wake ili wapate Roho ya hekima na ufunuo, ili
wapate “Kujua“ mambo tuliyokwisha kupewa na Mungu kupitia Yesu
Kristo. Alimwambia Timotheo hivi, yafahamu sana mambo haya… (2Tim 2:7).
Ndugu yangu, mambo
usiyoyajua, hutaweza kuyapata; hayatatendeka maishani mwako. Kujua ndio mwanzo,
ndio ufunguo wa kuyafungulia ili yaweze kuja kwako. ndio maana tunaambiwa Neno
la Kristo likae kwa wingi katika mioyo yetu, kwa hekima yote … kuyajua maandiko
matakatifu kunatuhekimisha ili tupate ufahamu wa haki zet na baraka zetu
(Wakolosai 3:16; 2Timotheo 3:15-17) Ukitaka ufahamu na ujuzi, soma kwa
bidii Neno la Mungu. Pata maarifa.
2
KUONA VIBAYA
Kutokujua
kunasababisha kuona vibaya. mtu asiyejijua kuwa yeye ni shujaa, atajiona
dhaifu. asiyejijua kuwa yeye ni mzima, ayajiona mgonjwa. asiyejijua kuwa yeye
ni mbarikiwa, atajiona ni maskini. Soma vizuri habari ya wana wa Israeli kitabu
cha Hesabu sura ya 13 na 14 yote,
utaona jinsi wana wa Isreali walijiona wao ni kama
panzi mbele ya wenyeji wa Kaanani. Hii ni kwasababu hawakujua vizuri na kwa
uhalisi, uwezo wa Mungu aliye pamoja nao, japo waliyaona matendo yake ya ajabu.
kutokujua kunasababisha kuona vibaya.
Hii
ndio sababu iliyomfanya Mtume Paulo atuombea Wakristo tupate kufunguliwa katika
macho yetu ya ndani, ili tuweze kuona vizuri, mambo ya rohoni. tukiona vizuri,
tutapata ufahamu sahihi wa jinsi tulivo rohoni na jinsi tunavyotakiwa kuwa
katika mwili (Waefeso 1:15-19).
Gideon
alikuwa anajiona yeye ni dhaifu na muoga lakini Mungu akimuangalia anamuona
yeye ni shujaa, na ndio maana Mungu alimwita “ewe shujaa” japo kuwa
yeye Gideoni alikuwa katika maficho kwa hofu ya maadui. Soma vizuri habari hii katika (Waamuzi
6:11-14) Bwana akamwambia “enenda kwa nguvu zako”. Maana yake ni
kwamba, kumbe Gideoni alikuwa na nguvu za kutosha ndani yake, lakini hakujua!
Kutokujua kunaweza kukunyima kusonga mbele. kutokujua kulimfanya ajione mnyonge
mbele ya maadui wao. Mungu akusaidie kujiona sawa sawa na yeye anavyokuona na
sio kama unavyojiona wewe
Kama utatumia mwanga wa manjano ndani ya nyumba yako, vitu
vyote vitaonekana ni vya manjano. Kama
ukitumia mwanga mwekundu, vitu vitaonekana ni vyekundu. Vivyo hivyo katika
dunia, Yesu anasema kwamba yeye ndiye
nuru (mwanga) wa ulimwengu (Yohana 1:7-9) Tukimtumia yeye kuangalia mambo
yetu, yataonekana vizuri kuliko tunavyoyaona sasa. Yesu ni Neno (Yohana 1:1-4; Ufunuo 19:11-13). Tumia Neno la Mungu
(mwanga bora na halisi) kutazamia maisha yako, utayaona kama Mungu anavyoyaona
na si kama wewe unavyoyaona. Kwa Neno la Mungu, Hutajiona mgonjwa
bali mzima; hutajiona maskini, bali tajiri; hutajiona dhaifu bali hodari. soma sana Neno la Mungu
ubadilishe unavyojiona. Kuona sawa sawa kutakuokoa na jambo lifuatalo.
3
KUWAZA VIBAYA
Kutokujua
kunasababisha kutokuona sawa sawa; na kutokuona
vizuri kunasababisha kutokuwaza sawa sawa. Kwa lugha rahisi, Kuwaza
vibaya ni matokeo ya kuona vibaya. na mtu wa Mungu akitawaliwa na mawazo mabaya
juu yake, anasababisha nguvu za Mungu zisifanye kazi juu yake na hiyo inaletakushindwa
kimaisha kwa watoto wa Mungu wengi. Sikiliza, mawazo ni daraja lililo katika ya
ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Ndio
maana mtu anaweza kusafiri mbali sana
kimawazo tu wakati mwili wake upo hapo hapo mlipo. mawazo yakihama, mtu anaweza
asiwe anasikia unachosema wala asione unachodhani anaona japo macho yake yako
wazi kabisa. Hii ni kwasababu, mawazo yake yamehama; mtu huyo hayupo hapo
kimawazo, bali yupo sehemu nyingine kabisa japo mwili wake upo hapo hapo mlipo.
Mawazo ni daraja la mambo ya rohoni na mambo ya mwilini.
Mawazo hutawala mambo ya
mwili.
Kwa
mfano; mtu anayetembea katika barabara ndefu yenye maduka mengi na vitu vingi,
bila kuchoka hata kama ni kilometa 5,
kwasababu macho yake yanaangalia vitu vingi na mawazo yake yanaona vingi (yako busy). Lakini mtu huyo huyo
anapotembea katika barabara nyingine ya urefu ule ule, isiyo na maduka pamoja
na vitu vingi vya kutazama, mtu huyo huyo atasikia kuchoka na ataiona safari
ile imekuwa ndefu sana
kuliko ile ya mwanzo. Tofauti yake ni kwamba, katika safari ya pili, mawazo ya
mtu huyo hayakushughulishwa sana
kwakuwa macho yake hayakuwa na mambo mengi ya mazuri ya kuvutia kutazamwa; na
hali hiyo imesababisha mtu huyo, kujisikia kuchoka katika mwili. Hii
inathibitisha kwamba, mawazo hutawala mwili.
Mfano
mwingine; mtu aliyebanwa na haja ndogo barabarani, akiangalia kushoto na kulia,
akakosa mahali penye choo, mwili wake hutulia. lakini kadri mtu huyu
anavyokaribia nyumbani au mahali popote penye choo, mwili wake huanza fujo za
kutaka kuachilia ile haja iliyobanwa kwa muda mrefu. kadri mawazo yanavyotambua
kwamba hapo karibu kuna choo, ndivyo mwili unavyokosa nguvu ya kuendelea
kujibana. mtu huyo akikimbilia chooni na kumbe akakuta kuna mtu chooni, mwili
wake, kwa mara nyingine, hukubali kujibana mpaka nafasi ipatikane. Hiyo
inaonyesha kuwa, mawazo hutawala mwili.
Mfano
mwingine; watu wawili walipigana sokoni. Mmoja akampiga mwenzake kichwa katika
upaji wa uso wake. Yule aliyepigwa, alipasuka katika upaji wa uso wake na damu
nyingi ikamtoka. Fikiri mwenyewe; upaji wa uso wa mtu wa kwanza umeupasua upaji
wa uso wa mtu wa pili, lakini upaji wa uso wa mtu wa kwanza haukupasuka, bali
ulivimba tu kidogo. Unadhani tofauti yake ni nini? Jibu: Ni kwasababu, mawazo
ya mtu wa kwanza, yalijua tunakwenda kumpiga mtu wa pili kwa kichwa;
kwahiyo,
nyama za mwili wa mtu wa kwanza zilikuwa zimeshaandaliwa kwa mawazo ya huyo mtu
wa kwanza; lakini mawazo ya mtu wa pili, hayakujua kuwa kuna kichwa kinakuja
kutupiga, hivyo nyama za mwili wa mtu wa pili zilikuwa hazijaandaliwa kupokea
kipigo; na ndio maana upaji wa mtu wa pili ukapasuliwa na upaji wa mtu wa
kwanza. Hii inathibitisha kwamba, mawazo hutawala mwili.
Kwahiyo
mtu wa Mungu, Biblia inaposema tugeuzwe fikra zetu, ina maana kubwa sana. Kwasababu, fikra
zako zikiwaza vibaya, uasababisha mambo yako ya mwilini kwenda vibaya, hata kama wewe ni mwombaji. Lazima ujifunze kuwaza sawa sawa kama Neno linavyosema kuhusu wewe. Mkumbuke Gideoni,
alikuwa anajiona dhaifu na ndio maana alikuwa dhaifu na maisha yake yakawa ya
kitumwa. Lakini Mungu alipomwambia kwamba yeye ni hodari na shujaa, Gideoni
akageuza fikra zake, akajiona shujaa (kama Mungu alivyokuwa anajiona na sio kama yeye alivyokuwa anajiona mwanzoni).
Mungu
hakuwa na haja ya kumpa Gideoni nguvu kutoka mbinguni, balin mawazo mazuri ya
ushindi yalitosha kumpa Gideoni nguvu za ajabu. kwa lugha nyingine, mawazo
mazuri ya kishujaa, yalifungulia nguvu za Mungu zilizokuwa ndani yakena
Gideoni, akaweza kuwaongoza Waisraeli katika ushindi mkuu dhidi ya adui zao.
Tena kitu cha kushangaza, askari 300 tu wa Israeli waliwapiga maadui waliokuwa
zaidi ya elfu 30. (Soma vizuri habari hii katika kitabu cha Waamuzi sura ya 6 na 7).
Kwahiyo,
ukujiona dhaifu, utasababisha udhaifu katika maisha yako. Ukijiona maskini au
huwezi, utasababisha balaa, nuksi, mikosi, kushindwa na ufukara katika maisha
yako au katika biashara yako au shamba lako au mifugo yako. Badilisha
unavyojiona, utajikuta unabadilisha unavyojiwazia. Tumia Neno la Mungu kugeuza
fikra zako na kuzifanya mpya, kuanzia sasa. Kulingana na Biblia, wewe ni shujaa
na si dhaifu (Waefeso 6:10); wewe ni mzima na si mgonjwa (2Petro 2:24); wewe ni
tajiri na si maskini (2Wakorintho 8:9); wewe ni huru na si mfungwa katika nguvu
za giza (Wakolosai 1:13).
Tumia
Neno la Mungu kugeuza fikra zako na kuzifanya mpya, kuanzia sasa. Badilisha
unavyojiona, utajikuta unabadilisha unavyojiwazia. Ukijiwazia mawazo mazuri ya
ushindi na mafanikio, ndivyo utakavyosababisha katika mwili wako, kwasababu
mawazo hutawala mwili.
Ndio
maana Neno la Mungu linasema; fikra zetu zigeuzwe na kufanywa upya kwa
Neno la Mungu (Warumi 12:2; Waefeso 4:17-23-24). Hii inatokana na
kanuni ya kwamba, mawazo ya nguvu ya kutawala mambo ya mwili. Ndio maana
mtu wa Mungu inakupasa uwe na mawazo safi.
Mungu Baba yako mwenyewe anakuwazia mawazo mazuri ya matumaini (Yeremia 29:11) Nakushauri ujifunze
kujiwazia mawazo mazuri.
Usijione
tena duni au dhaifu au mtu wa kushindwa au mtu wa kuugua au sio mzuri. Hapana,
jione tofauti; jione mzuri, jione unaweza, jione una nguvu za kushinda, jione
hodari na shujaa, jione kuwa wewe ni mzima hata kama
hali ya afya yako ya mwili si nzuri, jione tofauti. Jione wewe uko huru hata
kama huwa unajijua unasumbuliwa na nguvu za giza. Badilika! Jione tofauti. Jione wewe ni
tajiri, mtu wa mafanikio. Mawazo ni ufunguo! Ukijiona vizuri (kama Mungu
anavyokuona na si kama wewe unavyojiona)
utapona katika tatizo linalofuata.
4
KUONGEA VIBAYA
Kama tulivyoona, ufahamu husababisha kuona; na kuona
husababisha kuwaza; na mawazo
husababisha maneno. Ukiona vibaya, utawaza vibaya; na ukiwaza vibaya
utaongea vibaya. kuna nguvu ya ajabu sana
katika maneno yetu. maneno ya nguvu ya kuumba. Biblia inasema ulimwengu
uliumbwa kwa Neno la Mungu (Waebrania 11:3) Mungu aliumba vitu kwa
kusema tu. Na kwakuwa Mungu ametushirikisha tabia ya uungu (Zaburi 82:6; Yohana
10:34; 2Petro 1:3-4) Kwahivyo basi, maneno yako yana nguvu ya kuumba. Hivyo,
uwe mwangalifu unaongea nini au unajitamkia nini.
Chanzo cha nguvu ya maneno.
Nguvu
ya maneno inatoka wapi? Maneno ni malighafi ambayo hutumiwa na Roho Mtakatifu
au na roho wachafu (mapepo). Biblia inasema kwamba, kila andiko lenye pumzi ya Mungu
(Roho) huwa Neno zuri la kufundishia na kuadabisha maisha ya watu. (2Timotheo
3:16-17) … na Neno la Mungu li hai na lina nguvu (Waebr 4:12) Hii ina
maana kwamba;
Andiko + Roho
= Neno (Uhai na Nguvu)
(2Kor 3:6) (Mwa 2:7) (Ebr 4:12)
Kwahiyo, Neno likivikwa “roho”
linakuwa hai na linaweza kwenda kutenda kazi fulani. Ndio maana Mungu alisema
kwasababu Neno langu ni Roho (yaani limevikwa au limejazwa Roho Mtakatifu), hivyo
basi … Neno langu li hai, tena lina nguvu … na litokalo katika kinywa changu,
halitarudi mpaka limeyatimiza mambo niliyolituma kufanya (Yohana 6:63;
Waebrania 4:12; Isaya 55:10-11).
Hii ina maana kwamba, Neno la Mungu
hupewa uhai na nguvu kutoka katika Roho Mtakatifu aliyelivika hilo Neno. Kwahiyo, unapojibariki kwa maneno
mazuri, Roho Mtakatifu huja kulivika uhai na nguvu hilo neno lililotoka katika kinywa chako, ili
liwe hai na liweze kukutimizia kile ulichotamka (ulicholituma kufanya). Kwa
mfano; siku moja Bwana Yesu aliulaani mti na baada ya masaa kama
8 hivi, ule mti ulikufa! (Marko
11:12-14; 20-23) Tunaona Yesu hakutumia shoka au msumeno kuuua ule mti,
bali alitumia maneno yake tu na ule mti ukafa.
Yesu alituma neno tu na Roho
Mtakatifu akavamia lile neno na kulipa nguvu na uhai, hata likaweza kutenda
kile ambacho Yesu amelituma kufanya; yaani kuua. Kuna nguvu ya ajabu sana katika maneno,
kwasababu ya roho zinazoweza kuvamia hayo maneno na kuyafanya hai na yenye
nguvu. Ndio maana Biblia inasema mtu hushibishwa maneno ya kinywa chake na
mauti na ulimi huwa katika uwezo wa ulimi; na wote waupendao, watakula matunda
yake. (Mithali 18:20-21). Hivyo basi, ukitamka maneno mabaya, Roho
Mtakatifu hawezi kuja kulipa hilo
neno lako uhai na nguvu; kwasababu Mungu habariki udhaifu au laana (negative words). Mungu anabariki maneno
ya baraka tu (positive words).
Kwahiyo; ukijitamkia maneno ya mabaya
ya udhaifu, laana, balaa na kushindwa, mapepo wachafu huja na kuvamia hayo
maneno na kuyapa uhai na nguvu, na yatafanya kazi maishani mwako kukushibisha
ulichotamka kwa ulimi wako mwenyewe. Umetegwa kwa maneno ya kinywa chako na
umekamatwa kwa maneno ya midomo yako (Mithali 6:2).
Watu wengi hawajui kwanini Yesu
alimtaka Petro akiri kwa kinywa chake,
tena mara tatu, kwamba anampenda Yesu (Yohana
20:1-19). Jiulize, jibu la kwanza la Petro, halikumtosha Bwana Yesu? Yesu
hakuridhika? Kumbuka kwamba, Petro aliwahi kumkana Bwana Yesu kwa kinywa chake,
tena mara tatu, ya kwamba yeye Petro hamjui Yesu. Hayo maneno ya Petro yalianza
kuzaa matunda. Tunamuona Petro, baada ya kifo cha Yesu, Petro alianza kupata
mawazo ya kuziridia nyavu zake za uvuvi wa samaki, kazi ambayo Yesu
alishamwachisha.
Hayo yalikuwa matunda ya maneno yake;
kwa lungha ya leo, tungesema Petro alikuwa anaacha wokovu! Ndio maana ilimbidi Yesu kumfuata Petro na
ndugu wanafunzi wengine, kule baharini. Na alipowapata, Yesu akaanza kumtamkisha
Petro mara tatu ili kumsaidia Petro aweze kufuta maneno yake mabaya ya laana.
Maneno ya kinywa chako yana nguvu ya kusababisha kile unachosema kitokee katika
ulimwengu wa mwili, kwasababu kuna roho zinazowinda maneno ili zivae hayo
maneno ya kuyaleta mwilini. Hivyo uwe mwangalifu unatamka nini. Ukitamka laana,
pepo wachafu watakusaidia na utapokea laana. Lakini ukitamka baraka, Roho
Mtakatifu pamoja na malaika (Waebrania 1:14) watakusaidia, na utapokea baraka,
ushindi na mafanikio.
Ikikulazimu kutamka maneno ya
udhaifu, usiyaache yananing’inia hivyo hivyo, mapepo yatakushibisha; bali
hakikisha unayafuta kwa maneno mengine mazuri ya naraka na ushindi. Kwa mfano;
Umetoka kwenye mtihani mgumu sana, watu wakikuuliza habari za mtihani, unaweza
kuwajibu kwa ushindi tu kwamba ‘mtihani ulikuwa mzuri tu’ ingawamoyoni unajua
mambo yalikuwa magumu. Lakini ikikulazimu, wee sema tu kwamba ‘mtihani kwakweli
ulikuwa mgumu sana,
lakini
Mungu atanipigania’. Hapo utakuwa umeshafuta ule udhaifu kama
Petro.
Kama unaumwa na
hali bado si nzuri, unaweza kusema ‘namshukuru Mungu ninaendelea vizuri’ japo
wewe binafsi unajua hali bado ni ngumu. Huo ushindi na uzima unaoukiri, utakuwa
malighafi kwa Roho Mtakatifu, kukuletea uzima wako katika mwili. Lakini
ikikulazimu, wee sema tu hali ‘hali yangu bado lakini Mungu
ataniponya’. Hapo utakuwa umefuta ule udhaifu ulioutamka. Hili tunajifunza kwa
Bwana Yesu mwenye; alisema udhaifu lakini hakuacha maneno yake dhaifu
yananing’inia, bali aliyafuta kwa kutamka maneno mengi ya baraka na ushindi kwa
nyuma yake.
Kwa mfano; Yesu aliwahi kusema “ulimwenguni mnayo dhiki (hili si neno
zuri. lakini kahuishia hapo, bali alifuta udhaifu/kushindwa kwa neno la
ushindi, akasema) lakini jipeni moyo, mimi
nimeushinda ulimwengu (yaani;
alikuwa anatuambia kwamba, kama yeye
ameshinda, na sisi tutashinda tu) Yohana
16:33. Pia aliwahi kusema “mwana wa Adam atauwawa (halafu akafuta kwa
kusema) lakini siku ya tatu atafufuka (Marko 16:21). Ndio Mungu
anasema “aliye dhaifu na aseme mimi ni hodari” (Joel 3:10). Kwahiyo; kama unataka kubadilisha hiyo hali uliyonayo, usiseme
jinsi hali ilivyo, bali tamka vile unavyotaka hali yako iwe katika mwili.
Tumia nguvu ya maneno yako, hata kama
hali si ya kutia moyo sana, lakini usiseme wewe ni dhaifu, bali sema ‘mimi ni hodari katika jina la Yesu’
(Yoel 3:10); usiseme wewe ni mgonjwa, sema ‘mimi ni mzima katika jina la Yesu’
(1Petro 2:24); usiseme wewe ni maskini, bali sema ‘mimi ni tajiri katika jina
la Yesu’ (2Wakorintho 8:9); usiseme kwamba hutaweza, bali kiri kwamba ‘mimi
ninayaweza yote katika Kristo anitiaye nguvu’ (Wafilipi 4:19). Hivyo ndivyo
watu wa imani tunavyoshinda na zaidi ya kushinda katika dunia hii hii mbovu.
Kwwahiyo umegundua kwamba, watu wa Mungu wengi wanafeli na kushindwa kimaisha
kwasababu ya maneno yao
wenyewe.
5
KUOMBA VIBAYA
Jambo jingine linalosababisha watu wa Mungu ambao ni
wabarikiwa lakini wanaishi maisha ya shida na taabu ni suala zima la kutokuomba
ipasavyo au kuomba vibaya. Katika sura ya tatu na sura ya nne, nimeongelea sana juu ya watu wa Mungu
kutokuwa waombaji. Katika pointi hii, siongelei kutokuomba, bali naongelea kuomba
vibaya. Kwahiyo utagundua kwamba, baadhi ya watu w Mungu, wana bidii sana katika kuomba lakini
bado hawapokei yale wanayoyaomba, kwasababu wanaomba vibaya. Mungu anailalamikia
hii hali kwa kusema kwamba, mnaomba lakini hampati, kwasababu mnaomba
vibaya (Yakobo 4:3).
Mtume Paulo pia anasema watu wa Mungu wanabidii
sanakatika mabo ya Mungu lakini si katika maarifa (Warumi 10:2; Hosea 4:6). Maana
yake ni kwamba; watu wa Mungu wanavuja jasho sana lakini matunda wanayoambulia ni kidogo.
Yesu naye anasema ninawashangaa, mbona mnavyohangaikia maisha, kula na kunywa na
kuvaa, kama mataifa wasi na Mungu (Mathayo
6:31-32)
Maana yake ni kwamba, wana wa Mungu hatutakiwi kuhangaika
na kuhenyeka duniani kwa ajili ya maisha na mahitaji yake kama mataifa, bali
tunatakiwa kupata msaada wa Mungu katika kila eneo la maisha yetu, kwasababu
sisi ni wa thamani kuliko maua na ndege na yeye Mungu ndiye anayetuhudumia sisi
(kama anavyowahudumia ndege na maua). Maneno haya hayamaanishi tusiende kulima
na kufuga au kusomana kufanya kazi; haimaanishi tusiende kufanya biashara, NO!
Maana yake sio hiyo, bali alikuwa na maana hii; twende tukafanya kazi kwasababu
kufanya kazi ni agizo la Mungu;
Lakini, katika kafanya kazi kwetu, tuudhihirishie
ulimwengu kuwa, sisi wana wa Mungu, tuna msaada wa Mungu katika kila
tunachofanya. Kama Mungu anakusaidia katika kila unachofanya, hautakiwi
kuhangaika na kuhenyeka. Msaada wa Mungu unakusaidia kupata mahitaji yako yote
katikati ya dunia hii mbovu iliyoharibika. Lakini ukiangalia maisha ya baadhi
ya watoto wa Mungu, ni ya kuhangaika na kuhenyeka kama
vile hatuna Mungu. Hali hiyo haitutofautishi na mataifa wasiomjua Mungu. Mungu
anataka iwepo tofauti kati ye watoto wa Mungu na watoto wa shetani (1Yohana
3:10; Kutoka 11:7; Kutoka 8:23; Kutoka 9:4)
Kwahiyo, Mungu anatamani kuona watoto wake tunarithi
baraka zote alizotuwekea katika ulimwengu wa roho. Mungu anatamani sana kuona damu ya Yesu
imemwagika kwa thamani yake, kwamba watoto wake tumepata vyote ambavyo damu ya
yesu ilitununua navyo. Lakini sivyo ililivyo; na moja ya sababu ni kwamba, watu
wa Mungu wanabidii sana
katika mambo ya Mungu lakini si katika maarifa (Warumi 10:2; Hosea 4:6). Maana
yake ni kwamba; watu wa Mungu wanavuja jasho sana lakini matunda wanayoambulia ni kidogo.
Katika pointi hii, siongelei kutokuomba, bali naongelea kuomba vibaya.
Kwahiyo utagundua kwamba, baadhi ya watu wa Mungu,
wana bidii sana
katika kuomba, kwenye mikesha wapo, kwenye kufunga swaumu, wapo; lakini bado
hawapokei yale wanayoyaomba. Hii ni kwasababu wanaomba vibaya. Mungu
anailalamikia hii hali kwa watoto wake kwa kusema; mnaomba lakini hampati, kwasababu
mnaomba vibaya (Yakobo 4:3).
Tunakosea wapi katika kuomba?
a)
Kuomba Mambo manyonge (Isaya
41:21)
Isaya
43:26, Zaburi 2:7-8, 2Wakorintho 9:6,
Wagalatia 6:7
b)
Kuomba Pasipo uhakika (imani)
(Yakobo 1:5-7)
Waebrnia 11:1, 6,
Waebrania 10:38
c)
Kuomba nje ya mapenzi ya
Mungu (1Yohana 5:14-15) < Kitu / Muda
/ Mahali >
Mathayo 26:36-44, Warumi 8:26-27; Waefeso 6:18, Yuda 1:10
d)
Kuomba kwa kukatisha (1Wathes
5:17)
(1) Luka 18:1-7,
(2) Yakobo 5:17-18 (1Waflme
18:41-44), (3) Wagalt 1:6 / 4:19
(Wakolosai 4:2,
Waefes 6:18)
e)
Kuomba kwa msimu (Walawi 6:12-13)
Luka 10:1, 9, 17;
Mathayo 17:14-16-21; 1Wafalme 20:19-22
Mfano; Mathayo 26:36-46 Linganisha na Matendo 2:43-47, 42 / 3:1- 4:1-13-18-20-31
f)
Kuomba bila kumpinga
shetani (Yakobo 4:7)
Ufunuo 5:8-10, Ufunuo 1:5-6, 1Pet 2:9
Mwanzo 1:26-28,
Zaburi 8:4-8, 1Yoh 4:13,17,
Mathayo 28:18; Luka
10:19, Yeremia 1:10/ 51:20
Waefes 6:12-13, 10-11; Joshua 1:3, 6-9, 5.
g)
Kumpinga shetani wakati una
vitu vyake (Yohana 14:33)
Yakobo 4:3-7;
Marko 11:25-26; Mathyo
6:14-15; Isaya 59:1-2; Yohana 9:31.