MAOMBI YENYE NGUVU
Imani ya Kupokelea Majibu ya Maombi Yako
Katika Mfululizo wa somo lenye kichwa “MAOMBI YENYE NGUVU”, nimeona
nizame kidogo kwenye kipengele cha ‘iv’ cha sehemu ya II ya somo hili
kinachosema “JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA”.
Mara nyingi sana watu wanachukulia SOMO la imani kwa wepesi usiostahili. Kama kuna kitu cha muhimu katika maisha ya
Mkristo ni kujua FAIDA na MADHARA ya kutokuwa na IMANI. Sijui ni
kwanini utasikia mara nyingi sana watumishi wa Mungu wakihusianisha
imani na kushindwa kupokea majibu ya maombi lakini ni mara chache
utasikia wakitia mkazo somo hili la IMANI kwa KUSUDI la KUMPENDEZA
Mungu.
Kusudi la Msingi la IMANI sio kupokea majibu ya maombi
yako ila KUMPENDEZA Mungu. Sababu ya msingi ni kwamba mahitaji
tunayoomba kwa Mungu sio ya kila saa na kila siku, ila mambo YOTE
tuyatendayo katika maisha muda wote yanahitaji IMANI ili umpendeze Mungu
kwa sababu imeandikwa “haiwezekani kumpendeza pasipo imani” (Waebrania
11:6) na “kila jambo lisilofanyika katika imani ni dhambi”. Sasa jiulize
kwamba unafanya mambo mangapi pasipo imani? Kutokana na mistari hii
miwili najifunza kwamba LENGO la msingi la IMANI ni kumpendeza Mungu na
ndipo faida zingine huja pale unapoitumia imani hiyo KUOMBA au KUPOKEA
majibu ya maombi yako.
Katika sehemu hii ya III ya somo hili
natamani tujifunze hiki kipengele cha IMANI ya kupokea majibu ya maombi
yako. Nitatumia mfano wa NDOA ya Zakaria na Elizabeth ambao ni wazazi wa
Yohana mbatizaji na Maria, mama wa Yesu.
Nitaanza na Zakaria
na Elizabeti. “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani
mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo
wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye
haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo
yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa
tasa, na wote wawili ni wazee sana” (Luka 1: 5-7). Hawa wawili walikuwa
wakiishi maisha ya KUMTUMIKIA Mungu katika usafi na utauwa. Walitamani
sana kupata mtoto na walimwomba Mungu (kwa sababu walikuwa na IMANI ya
KUOMBA) kwa muda mrefu bila majibu. Haikuwasumbua kwamba hawakujibiwa,
walizidi kukaa katika HUDUMA na UTUMISHI Mungu aliowaitia na waliendelea
na zamu zao.
Mungu akamtuma malaika Gabriel kupeleka
ujumbe kwa Zakaria akiwa madhabahuni katikati ya huduma. Malaika akasema
“Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti
atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.” (Lika 1:13).
Alipoambiwa habari za MAJIBU ya maombia yake, “Zakaria akamwambia
malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni
mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli,
nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha
habari hizi njema.Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku
ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo
yatatimizwa kwa wakati wake.” (Luka 1:18-20). Sasa nataka uone kwamba
hawa WATUMISHI waliomba kweli ila ilipofika mahali Mungu anasema
“nimesikia MAOMBI yenu na sasa najibu” bado HAWAKUSADIKI/HAWAKUAMINI
kama inawezekana! Yaani hawana imani ya kupokea MAJIBU ya maombi yao!
Sasa Malaika akamfanya bubu. Kwa haraka unaweza kuona kama ni ADHABU ya
kutokuamini kwake (Mungu hafurahishwi na mtu wa kusita-sita/mashaka/kutokuamini
kama Anaweza) ila kuna sababu ya pili ambayo ni KUHARIBU imani ile ya
KUPOKEA majibu kwa UKIRI mbaya (negative confession) basi dawa ni
kumnyima kuongea hadi majibu ya maombi yatokee.
Ukija kwa
upande wa Maria, mama wa Yesu. Gabriel huyo huyo alikuja na habari ya
kupata mtoto ila “kwa uweza wa Roho Mtakatifu”. Utagundua kwamba Maria
na yeye aliuliza swali linalofanana na la Zakaria ila hakupigwa na
ububu! Ujumbe huu ulimjia Maria miezi 5 baada ya Elizabeti kuwa
mjamzito. Sasa wakati Maria anamuuliza Gabriel haya mambo yatakuaje,
kulikuwa na SHIDA ya IMANI ya KUPOKEA huo muujiza pia. Kabla Gabriel
hajaondoka ilibidi ainue imani ya Maria kwa kumpa “Neno la Mungu
lililotamkwa kwa kinywa cha malaika kwa Zakaria” (“Imani huja kwa
kusikia Neno la Mungu”). Baada ya Gabriel kuleta ujumbe “Mariamu
akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika
akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake
Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa
yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee
wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna
neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi
wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka
akaenda zake.” (Luka 1:34-38). Huu msitari wa 38 unatuonyesha imani ya
Maria imeinukana na kuona INAWEZEKANA kisha Malaika akaondoka.
Tukiendelea kujifunza hapa utaona “basi, Mariamu akaondoka siku hizo,
akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,
akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti
aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya
tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu
akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie
mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto
kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri
aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” (Luka 1:
39-45).
Hawa wanawake wawili walimshangilia Mungu kwa pamoja
ila ukitizama kwa makini utagundua baada ya Elizabeti kujazwa Roho
Mtakatifu, alirudia yale “maneno ya kuimarisha imani ya Maria” na
mwishowe utaona kwamba anasema “aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa
aliyoambiwa na Bwana”. Ikimaanishwa kwamba kuna IMANI inatakiwa KUPOKEA
hiyo ahadi japo kweli kabisa ni Malaika/Bwana amesema. Kumbuka siku
zote, AHADI iliyoko kwenye Neno la Mungu sio yako hadi utakapokuwa na
IMANI ya KUTOSHA kuimiliki/kuipata hiyo AHADI.
Tukiendelea
kujifunza utaona Maria anaimba wimbo wa kumshukuru Mungu baada ya haya
maneno ya Elizabeti. Maneno ya wimbo wa Maria ni marudio ya yale ambayo
malaika alikwisha kusema na jinsi alikubali kusudi la Mungu kutimia
kwake, huku akiona ni UPENDELEAO wa pekee kupokea BARAKA hii kubwa. Huu
ni UKIRI wa kuimarisha na kulinda IMANI yake ya KUPOKEA mtoto.
Ukifuatilia zaidi utaona Maria alikaa kwa Elizabeti miezi 3. Yamkini
walikuwa wakitiana moyo katika kubeba MIMBA muhimu katika maisha yao na
kufikilia KUJIFUNGUA salama sawa na KUSUDI la Mungu. Sasa mara nyingi
sana katika maisha yetu tumekuwa na imani nzuri tu wakati wa kuomba, ila
HALI HALISI zimetufanya kuona HAIWEZEKANI KUPOKEA majibu ya maombi yetu
na imekuwa kikwazo. Fikiri hii hali, binti anaambiwa atapata mimba bila
kumjua mwanaume! Na upande mwingine kikongwe aliyepitiliza siku za
kuzaa anaambiwa atapata mimba! Hali halisi inasema HAIWEZEKANI. Sasa
kama mtu hatakuwa na IMANI, na hajui namna ya kuzimisha sauti za
SAYANSI, TEKINOLOJIA na ELIMU zingine, imani ya KUPOKEA inakufa. Hata
kama ni Yesu anakuja/anazaliwa, ILIBIDI Maria awe na IMANI ya KUPOKEA!
Ilibidi Malaika Gabrieli ampe Maria mfano wa “jambo lisilowezekana” na
jinsi ambavyo “limewezekana kwa Mungu” ili kuinua IMANI yake ya KUPOKEA.
Kitu cha kukusaidia kukuza/kupata IMANI ya kupokea majibu ya MAOMBI
yako ni KUJIFUNZA matendo Makuu ya Mungu katika Biblia, na kuyatafakari
usiku na mchana, na kuyataja unapotarajia MAJIBU ya maombi yako. Jifunze
KUKIRI matendo makuu unayoyajua ya Mungu wetu ukiwa katika maombi kwa
mfano, wakati Daudi anamkabili Goliath alisema maneno ya IMANI yake kwa
Mungu, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila
wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo mimi humfuata na
kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu
akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. Mimi
mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule
Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai,
atakuwa kama hao. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na
dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu” (1 Samweli 17:34-37).
Zungumza na HALI unayopitia na uitangazie USHINDI katika MAOMBI, itaje
hiyo shida kwa jina “lake” na uiambie kwa maneno kama unazungumza na
mtu, huku ukiikemea kwa Jina la Bwana wa Majeshi. Wakati huo ukitamka
matendo mengine MAKUU ya Mungu ambayo yamefanyika kwa watu wengine. Kwa
kufanya hivyo ghafla! Utaanza kuona Mungu ni MKUBWA kuliko hiyo
shida/jambo unaloomba na IMANI yako inaongezeka wakati huo MASHAKA
yakitoweka. Kumbuka Ibilisi huleta VITA katika FIKRA zetu ili kutujengea
ngome, na njia mojawapo wa kumshinda ni kwa kutumia “NENO la ushuhuda
na Damu ya Mwana-kondoo” (Ufunuo wa Yohana). Hii ni SIRI ya KUJAZA imani
ya KUPOKELEA lakini pia kumshinda Adui azuiaye.
Mungu
atusaidie kujenga IMANI zetu kwa KUJIFUNZA kwa bidii maandiko na kuomba.
Hatimaye tuweze kutenda KILA jambo kwa imani kwa kusudi la kumpendeza
Mungu na kuweza KUOMBA na KUPOKEA majibu ya maombi yetu kwa hiyo IMANI.
Roho Mtakatifu atufundishe NENO la Mungu na kutuwezesha kupata UFUNUO katika hilo Neno ili kujenga IMANI zetu. AMEN.
Frank Philip.
Kusamehe mtu aliyekukosea ni moja ya mambo magumu ya KIIMANI ambayo LAZIMA uweze kama unataka KUMUONA Mungu katika maisha yako.
Sababu na faida za kusamehe ni nyingi lakini nitataja chache. 1.
Tunasamehe watu waliotukosea ili na sisi tusamehewe DHAMBI (madeni yetu)
na Mungu. Katika sala ya Bwana kuna sehemu tunamwambia Mungu “utusamehe
dhambi (deni) zetu kama nasi tunavyowasamehe
waliotukosea (wanaotudai). [nitarudi kueleza habari ya deni hapo
baadae]. 2. Dhambi zina NGUVU ya kuficha uso wa Mungu usiuone, KUZIBA
sikio lake ASIKUSIKIE na kuzuia Mkono wake USIKUOKOE. Nabii Isaya
anasema hivi “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa
wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu
yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake
msiuone, hata hataki kusikia.” (Isaya 59:1,2).
Kumbuka KIPIMO
ya KUSAMEHEWA dhambi na madeni yako kwa Mungu UNAJIPIMIA mwenyewe kwa
JINSI unavyowasamehe wengine. Na hii unamwambia/unamwomba Mungu katika
sala ya Bwana kila unaposali. Kwa lugha nyingina UNAMSIHI Mungu
“USINISAMEHE kama jinsi ambavyo SIWASAMEHI watu walionikosea!”. Sasa,
kwanini tunasema kwamba KUSAMEHE ni VITA? Kwa sababu anayetaka
USISAMEHE sio wewe ila ni IBILISI! Mtu ataniuliza nimejuaje? Angalia
hapo juu Isaya anasemaje: kwanza, “ili Ibilisi afanikiwe KUKUZUIA wewe
kuuona USO wa Mungu anahakikisha una DHAMBI!”, pili, “ili Mkono wa Mungu
USIKUFIKILIE na kukuokoa katika SHIDA, KILIO, na MAUMIVU yako,
anakufarakanisha na Mungu kwa kuweka WINGU la uovu kati yako na Mungu na
KUZUIA SIKIO lake kukusikiliza”! Mungu anasema “SITAKI kusikia” maombi
yako. Ibilisi anachunga sana hii SIRI ili usije ukaondoa UOVU na DHAMBI
zako maana ukifanikiwa kuondoa UOVU katikati yako MKONO wa Mungu
utadhihirika katika maisha yako katika mambo YOTE na utakua UMEMSHINDA
Ibilisi. Sikiliza, Mungu “hulitizama Neno lake na kulitimiza”. Usije
ukasema Ibilisi kamdhibiti Mungu! Haiwezekani, ila Mungu ndio kasema
HUTANIONA, SITAKUSIKIA na MKONO WANGU HAUTAKUAOKOA, kama kuna UOVU
katikati yako! Na Ibilisi analikamata hilo Neno na kulitumia kukutesa.
[kama ulikua hujui Ibilisi ni mtendaji wa Neno kuliko watu wengi sana
japo huwa analitumia kinyumenyume, na kupambana naye ni LAZIMA ujue Neno
na kulitumia kama silaha yako ya VITA. Bila Neno, wewe ni mawindo
rahisi ya Ibilisi]
(Yeremia 29: 11-13) “Maana nayajua mawazo
ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya,
kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na
kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona,
mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” Madhara ya kukaa na DHAMBI ni MENGI
kuliko unavyoweza kufikiri. 1. Unajikuta unapoteza MATUMAINI (future
hope). Huko mbele kwenye maisha yako unaanza kuona giza na kukata tama
maana bila sababu, matumaini yanapotea ndani yako! Hii ni kazi ya
Ibilisi. Kama unaona unaanza kupoteza matumaini na huko mbele ya maisha
yako unaona hakuvutii usihangaike, saka WATU wa kusamehe maishani mwako!
Ondoa UOVU katikati yako! Ukiwasamahe “wote” hii hali inakwisha kwa
maana MATUMAINI ya mambo MAZURI ni ahadi ya MUNGU wa watu wake na
Ibilisi anataka kuinyakua kutoka kwako kwa KUTOSAMEHE. Kama kuna kitu
unahitaji ni MATUMAINI, hii ni nguvu ya ajabu sana inayokupa nguvu ya
kusonga mbele hata kama uko katika majaribu mazito. “Abrahamu alipoiona
ile ahadi…”, “Yesu alipoona huko mbele ya msalaba kuna nini….alishinda
msalaba na maumivu yake yote”. Lazima uone MBELE/future na huwezi kuona
kama huna MATUMAINI na Ibilisi anakuondolea MATUMAINI ili uzidi
kushindwa katika VITA naye. Kitu anachotumia kukuwekea WINGU hili la
kutokuona mbele ni nini? Jibu ni UOVU katikati yako! 2. Katika shida na
mahitaji yetu mbali mbali huwa tunamwita Mungu. Naye anasema “mtakwenda
KUNIITA na KUNIOMBA nami NITAWASIKILIZA, MTANITAFUTA na KUNIONA ila kwa
BIDII”. Bidii inatakiwa kwa sababu gani? Ni VITA, Ibilisi hataki UITE na
Mungu asikie, wala hataki UKIOMBA na KUMTAFUTA Mungu umuone. Sasa kwa
kuwa hawezi KUMZUIA Mungu, anakuja kukudhibiti wewe kwa kuhakikisha
UNASHINDWA kusamehe watu waliokukosea! Matokeo yake ni KUZUIA majibu ya
maombi yako!
Mtu atauliza kwani Ibilisi anaweza kuzuia majibu
ya maombi kutoka kwa Mungu? Sikiliza, Wakati Danieli anaomba, Mungu
anamtuma malaika Gabriel kumpasha habari kwamba hizi siku 21 alizokua
busy anaomba ajue kwamba ALIJIBU “tangu” ulipoweka NIA ya KUOMBA, (sio
wakati alipoanza kuomba) ila kuna VITA hapo juu na MAJIBU ya maombi yako
yamezuiliwa, hivyo nimemtuma MIKAELI ashuke kupambana ili huyu MKUU wa
giza hapo anayekamata majibu ya maombi yako aachilie! Sasa, ukifuatilia
sehemu nyingine utaona Danieli aliomba na alianza kwa “toba” kwanini?
Ili kusafisha NJIA ya kupokea Majibu. Ndio maana tunafundishwa kwamba
“kila tusimamapo kusali sameheni”! Ayubu alijua SIRI hii pia, sio kwamba
alitubu kwa ajili yake tu, alitubu hata kwa ajili ya watoto wake,
“isije ikawa wamemkosea Mungu mahali”, (isije ikawa…maana yake anatubu
hata kama hajui dhambi iliyofanyika! Kama ipo au haipo, yeye anatubu tu
na KUACHILIA). Sasa watu wengi sana wamekwama na wameteseka na kila
namna ya SHIDA na MAUMIVU mengi kwa sababu WAMESHINDWA kusamehe. Sasa,
hebu chukua MUDA kidogo wa kutafakari ile LIST ya mambo uliyoomba na
unayotarajia Mungu kukujibu na mengine unakiri umepokea. Kisha kumbuka
WATU uliogoma kuwasamehe na ulinganishe FAIDA ya kumsamehe “huyu mtu” na
HASARA utakayopata kama ile LIST yako ya maombi HAIJIBWI na Mungu. Pima
mwenyewe na chukua hatua. Ukiamua kusikiliza uongo wa shetani ni juu
yako, Mungu analeta hili Neno AKUOKOE na KUKUHUDUMIA.
Ngoja
nikwambie kitu shetani anafanya hadi unashindwa kusamehe halafu
ntakwambia cha kufanya. 1. Ibilisi anajua DHAMBI zako kwa maana yeye
ndio amekusababisha UFANYE au amesamabisha watu WAKUKOSEE. Kwahiyo
anajua ni wapi ameweka KUFULI ya kukutesa. Ili kuimarisha ile kufuli
ikamate sawasawa, unapomwaza “yule mtu” aliye kukosea ghafla unasikia
HASIRA au UCHUNGU, halafu analeta VIDEO na PICHA hata na SAUTI ya “yale
mambo” ili KUHUISHA ule UCHUNGU na HASIRA ndani yako. Na hii inatokea
mara nyingi na UNASHINDWA kumsamehe “huyu mtu” aliyekukosea. 2. Ibilisi
anakupa SABABU na VISINGIZIO vya kutokusamehe. Utasikia mtu anasema
ndani ya moyo wake au kwa kinywa, “kama kweli uliamua kunisaliti wakati
nipo mimi nimekukosea nini?”, “yaani pamoja na kujitahidi kufanya haya
yote umeamua kunifanyia hivi?”, nk. Ukisikia SAUTI hizi ndani yako jua
ni IBILISI anakuhubiria injili MFU ili ushindwe kusamehe na afanikiwe
kukutenga na USO, SIKIO na MKONO wa Mungu na ukose MSAADA wa Mungu. 3.
Dhambi inasema! Kila ukisimama kuomba au ukijitahidi kusimama katika
BWANA unasikia “sauti ya dhambi” ikipiga kelele moyoni mwako kukuvunja
UJASIRI. Kwa lugha nyingine naiita “deni ya dhambi” (guilty)! Kama
umewahi kua na deni mtu anakudai na anakusumbua utaelewa nasema nini.
Kila ukikumbuka lile deni ni kama “linasema” na wewe huko ndani ya moyo
wako kwa sauti! Hii ni vita ya Ibilisi na HUWEZI kuzima hiyo sauti bila
MSAADA wa Mungu na Damu ya Yesu. Ndio maana utasikia “kikaribieni kiti
cha Rehema kwa UJASIRI kwa Damu ya Yesu”, huu ujasiri unapatikana kwa
DAMU ya Yesu.
Kwa sababu MAMBO yako MAZURI na Majibu ya maombi
yako kwa WATOTO, KAZI, BIASHARA, nk, yamedhibitiwa na KUTOKUSAMEHE
kwako, jua IMEKUPASA kusamehe kwa FAIDA yako KWANZA na sio ya
aliyekukosea. Tena, kama unataka uwepo wa Mungu ukutembelee na
kukufunika kila wakati na MKONO wake kua pamoja na wewe na USIPUNGUE
katika maisha yako ni LAZIMA uondoe UOVU katikati yako. Kumuona Mungu
maana yake ni “kumuona akikupigania na adui zako wakishindwa huku na
huku na wewe ukiwa mshindi BILA sababu”! Hii lugha ni ngumu lakini
sikiliza, Mungu anasema kwa kinywa cha DAUDI kwamba “hii nchi
hamkumiliki kwa sababu ya upanga wenu wala mkuki, (sio nguvu zenu, au
hamkufanya chochote) ila ni nuru ya uso wangu umewaangazia” sasa kumbuka
DHAMBI zako zinaficha USO wa Mungu usiuone! Kwa lugha nyingine pamoja
na KUPAMBANA sana na UPANGA wako bado ni NGUMU, ila Yule aliyeondoa UOVU
katikati yake nakwambia HATASHINDA kwa upanga, Mungu anatangulia mbele
zake na kumpa ushindi bure! Mungu anasema “kabla ya kuomba mimi Bwana
nitajibu, na mkiwa katika kunena Nitasikia”. Mungu anamwambia Danieli,
“ulipotia tu nia mimi nilijibu” Sasa iweje leo watu wanafunga na kuomba
na INAKWAMA? Ondoa UOVU na DHAMBI katikati yako! Sio tu kwa KUTUBU
dhambi zako ILA na KUWASAMEHE walio kukosea hata kama ni NGUMU. Kumbuka
kwa NJIA mbili zote kwa pamoja 1. Tubu (na geuka) na acha dhambi 2.
Samehe dhambi zote watu walizokutendea. HAKIKA utamwona Mungu maishani
mwako kwa namna hujawahi kutarajia.
Kwanini unapata ujasiri wa
kutenda dhambi? Hii ni SIRI nyingine nataka nikupe kabla ya kumalizia
kukupa DAWA ya kupona. Kufanya dhambi inahitaji ujasiri wa aina yake.
Umewahi kufikiri mtu anachukua KISU anamchoma mwenzake? Bila ujasiri
huwezi. Au umewahi kufikiri mtu mzima anavua NGUO zake mbele za mtu
mwingine wa JINSIA tofauti na anazini? Kwa kweli inahitaji ujasiri na
huu unaupata kwa Ibilisi. Sasa kabla ya kufanya “hii dhmbi” lazima akupe
ujasiri. Utasikia ndani yako “kama huyu jamaa hanijali basi na mimi
nafanya ngono na huyu mwingine kwa sababu angalau yeye ananijali”, “kama
kila mtu anakula rushwa kwani nini na mimi nisichukue hiki kidogo tu?”,
“kama amenirusha hela yangu na mimi simpi msaada”, “kama Fulani
alianguka katika uzinzi na yuko kanisani mi naona hii ni ngumu kwa hiyo
watu wataelewa”, “watasema mchana na usiku watalala”, “hii ni ZAWADI sio
rushwa”, nk., ghafla! unapata UJASIRI kwa kufanya KITU ambacho ni KIOVU
ndani yako UKISHUHUDIWA kwamba UNAMKOSEA Mungu ila Ibilisi kashakujaza
UJASIRI kwa hiyo unajikaza na KUFANYA. Sasa kumbuka ukifanya dhambi
“moja”, madhara huwa yanakua zaidi ya moja! 1. Unauzuia Mkono wa Mungu
kukuokoa, Uso wake usikuone, na Sikio lake lisikusikie 2. Unatengwa na
Mungu, 3. Unazuia majibu ya mombia yako. Haya mambo matatu yanatokea kwa
pamoja! Sasa kumbuka nimetaja matatu ila ni mlolongo wa mambo mengi
sana uko hapo. Kwa sababu kuzuiliwa “majibu ya maombi” yako itawaathiri
na wale waliokua wanapona kwa WEWE kuwaombea! Kwa maana ni majibu ya
maombi YOTE yamedhibitiwa. Unaanza kushangaa watoto wako wanateseka na
uko busy kuwaombea na hakuna kinatokea! kumbe kisa HUTAKI kumsamehe baba
yao, nk!
Kumbuka siku zote, Ibilisi AKIKUSUKUMA kutenda
dhambi sio ili UFAIDI, NO! ni ili akutenge na Mungu na apate nafasi ya
KUKUANGAMIZA! Sasa, Neema ya Mungu hututetea (hasa tunapokua wajinga).
LAKINI ukilijua Neno hili na ukaufanya moyo wako MGUMU, utaangamia! Kwa
maana Mungu hulituma Neno kuwaponya mataifa lakini wasipolipokea
Maangamizi hufuata, ila kabla ya HUKUMU lazima Neno litangulie. Unaweza
kushangaa nasema nini, lakini ukisoma maandiko utaona Nuhu alihubiri kwa
miaka takriban 100 akiwaambia watu watubu, na hawataki NDIPO gharika
ikaja. Sememu nyingine tunasoma “aonywaye MARA NYINGI akishupaza shingo
itavunjika na dawa hapati”. Hii ina maana KABLA ya shingo kuvunjika
Mungu anakuletea Neno MARA NYINGI kukuonya na ukikataa KUTII basi
Ibilisi anakumaliza. Sehemu nyingine tunaambiwa kwamba Yesu atakuja
kuhukumu Ulimwengu, lakini ni baada ya INJILI kuhubiriwa kwa KILA
kiumbe! Ili aije sema mtu sikusikia. Hii ndio tunaita Neema! Ndani ya
Neema kuna muda wa Mungu kukusubiri UTUBU, ukichezea huu muda na
“kikombe kikijaa” Unaangamia! SIKIA SAUTI yake LEO na UFANYE maamuzi na
KUGEUKA.
DAWA ya kupona ni KUZIUNGAMA (kutaja dhambi kwa majina
yake) kwa Mungu DHAMBI zako na KUWATANGAZIA wale watu waliokukosea
kwamba UMEWASAMEHE BURE! Sasa, sikiliza. Kuwatangazia watu MSAMAHA pia
ni VITA, tena NGUMU sana kutokana na MAJERAHA uliyopata “ulipokosewa” na
hawa watu. Ndio maana utakuta mtu ANALIA tu kila akikumbika MTESI wake,
Jipe moyo, Mungu anaona MAUMIVU yako. Anza na KUMTANGAZIA huyo mtu
msamahawa wake kwenye MAOMBI, kisha chukua hatua ya IMANI na kumtangazia
masikioni kwamba “NIMEKUSAMEHE bure”! Na ukiona ile hali inarudi huku
ndani, kimbilia magotini tena na MTANGAZIE na IBILISI kwamba hii dhambi
haipo nimesamehe na Yesu kafuta kwa Damu yake. Sisitiza hili katika
Maombi hadi usikie UHURU wa ndani. Ukivuka hapo ndio sasa kile kipengele
ya KUSAMEHE na KUSAHAU kitaanza kuwa dhahiri kwako, la sivyo ni NGUMU
kibinabadu asikudanganye mtu. Bila Mungu huwezi KUSAMEHE na KUSAHAU,
tafuta msaada wa Mungu kushinda VITA ya KUSAMEHE.
Uwezo wa
kusamehe mtu (tolerance) Kimungu ni ndefu hakuna awezaye kufikia. Yesu
alisema 7x70 kwa siku. Tena ni mtu huyo huyo anarudia kukukosea na
kuomba msamaha kwa SIKU! Unatakiwa kumsamehe, hata kama ANARUDIA makosa
yale yale. Nakubaliana na wewe kwamba unaweza kukosewa mara “moja” ikawa
kubwa kuliko “Elfu”! Sawa, ndio maana nasema ni VITA na unahitaji
msaada ya YESU kushinda na UWEZE kusamehe maana madhara ya KUTOKUSAMEHE
ni MAKUBWA kuliko unavyofikiri. Kumbuka, kama WEWE unatakiwa uwe na
UWEZO wa kusamehe mara 490 kwa siku, Je! Yesu ANAWEZA kukusamehe wewe
mara ngapi ukimkosea? Jifunze KUJISAMEHE na KUJIACHILIA mwenyewe maana
kila dhambi ULIYOITUBU Yesu alifuta ghafla! Pale ulipoanza tu kutubu.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wake Mungu Baba Ukae nanyi tangu sasa na hata milele.
Frank Philip.
(Jua uhusiano kati ya UASI kwenye MAHUSIANO ya kijamii na UPENDO wako kwa Mungu)
Ukifuatilia nyakati katika maandiko utagundua kwamba tunaishi nyakati
za mwisho. Tumekaribia mahali ambapo Yesu anarudi kulichukua Kanisa
lake. Hakuna ajuaye ni karibu kiasi gani ila ni KARIBU. Yesu anasema
yuko malangoni, anakuja.
Yesu alisema dalili ya nyakati za mwisho (Mathayo 24:3-13) na zinaonekana. Ila
nataka niongelee MAASI. Huku mwisho wa nyakati tuliko tunaambiwa
KUTAONGEZEKA MAASI na UPENDO wa wengi utapoa. Upendo ni kitu cha ajabu
sana ambacho Mungu amewaumbia wanadamu. Mtu AKIPENDA ghafla! anakua mtu
wa hatari maana huo UPENDO utamsukuma kufanya vitu bila kujali “sana”
GHARAMA wala MUDA. Kwa mfano UPENDO wa mtu kwa Mungu utamsukuma huyo
mtu kusimama kwa UAMINIFU mbele za Mungu hata kama anateseka na
ataridhika na kila kitu kigumu na cha MAUMIVU alimradi asimtende Mungu
dhambi. Sasa, UPENDO wa mtu huyu UKIPOA hutaamini vitu ataanza kufanya.
Ghafla! visingizio vingi sana vinaibuka na sababu nyingi sana za MSINGI
za kumkosea Mungu zinaibuka, ila ukifuatilia kinachotokea kwa huyu ndugu
ni kitu kimoja tu UPENDO WAKE KWA MUNGU UMEPOA!
Sasa tunajua
kabisa kwamba Mungu wetu ana NGUVU kuliko Ibilisi. Na hakuna siku
ibilisi atakinga MSULI kwa Yesu akafanikiwa maana Yesu yuko juu sana
katika UWEZA, sana sana ikiibuka vita atamtuma tu MIKAELI
akamshughulikie huko na yeye akaendelea kumtizama BIBI ARUSI wake
anayempenda sana ambaye ni KANISA. Ibilisi anachofanya hapa kwa wana wa
Mungu ni KUONGEZA MAASI kati yao! USALITI katika mahusiano, biashara,
familia, ndugu, huduma, nk. Huu usaliti unasababisha watu KUJERUHIWA
ndani yao na UPENDO wao UNAPOA bila wao kujua! Wengi sana wamefika
mahali pa gumu sana na wameweka SILAHA zao chini kwa sababu wamejeruhuwa
na ADUI wakiwa KAZINI. Madhara yake yanapelekea KAZI yao kusimama
shambani mwa Bwana, wamebaki KULAUMIANA na SHUHUDA MFU za watu
waliowatendea mambo “mabaya” badala ya kushuhudia MATENDO makuu ya
Mungu!
Watumishi wengi sana na wana wa Mungu wameacha zile
SHUHUDA za “kuokoa” watu na Ibilisi ameanza kuwatumia kusambaza shuhuda
KANDAMIZI za kurudisha watu nyuma! Ushuhuda ni habari NJEMA! Hili ndilo
jina jingine la INJILI, habari njema kwa watu wote! Sasa, watu wengi
sana wamewekeza kwenye habari MBAYA za watu na zimewavunja wengi sana
moyo (hasa wachanga katika imani) na kuwajeruhi badala ya kuwajenga!
Hayo MAASI ambayo yametokea, na WEWE mwana wa Mungu umejeruhiwa na
umepata UCHUNGU na kwasababu hujashughulikia uchungu wako UMENAJISI
wengi kanisani na madhara ya ule UASI “mmoja” umekua JANGA kubwa maana
umesambaa na KUZIMISHA upendo wa WENGI kwa mara moja bila wewe kujua.
Tunaonywa tuangalie “shina la UCHUNGU lisichipuke ndani yetu” maana
UCHUNGU ndani ya mtu mmoja una uwezo wa kunajisi watu WENGI ambao
hawakuhusika katika TUKIO lililosababisha huo uchungu. Chunga sana hili
ENEO maana unaweza kujikuta umegeuka kuwa mtumishi wa Ibilisi kusambaza
UCHUNGU bila kujua na ukamfanikishia Ibilisi kazi yake ya KUNAJISI watu!
Nitatoa mfano wa huduma ya Yesu. Wakati huduma ya INJILI inaendelea kwa
kasi kubwa, Petro na wenzake “wako tayari kupigana kwa upanga kumtetea
Yesu hadi kufa”, na ikafika mahali Petro anatoa upanga ALANI mwake kwa
ajili ya kumlinda Yesu, na alijikuta anakata mtu sikio ghafla, aliona
huyu jamaa anamsogelea Yesu. UPENDO kwa Bwana wake ukamsukuma “kupiga
mtu”. Kabla Petro hajakaa sawa anaona YUDA, ambaye ni MTUMISHI mwenzake
hapo pembeni anachukua RUSHWA, kabla hajakaa sawa anaona ANAMBUSU Yesu
hadharani, kabla hajakaa sawa anaona Bwana wake AMESALITIWA LIVE na sasa
ANASULUBIWA! Na aliyemsaliti ni MTUMISHI mwenzake ambaye wamefanya
HUDUMA pamoja kwa takriban mika 3! Yesu alimwamini YUDA kiasi cha
kumfanya MWEKA HAZINA wa HUDUMA yao. Leo machoni pa kila mmoja wao
katika HUDUMA na wakiwa KAZINI anamsaliti Bwana wao! Hili jambo
liliwasambaratisha wote wakatawanyika, sio kwa hofu tu ya wale waliokua
wanamsulubu Yesu lakini pia ile hali ya UASI iliyojitokeza imeathiri
UPENDO wao na WAKARUDI nyuma!
Kabla Petro hajakaa sawa
anaulizwa “wewe si ulikua na huyu jamaa”, Petro anasema SIMJUI mtu huyu!
Hataki hata kutaja jina la Yesu, safari hii anamwita “mtu huyu”! Mara
tatu anamkana YESU hadharani! ila kilichotokea kabla ya hapo ni UASI
mkuu na USALITI wa waziwazi! Wanafunzi walitawanyika kwa sababu
“mchungaji wao amepigwa”. Petro akarudi zake KUVUA samaki ziwani,
akaachana na BIASHARA ya Yesu maana UPENDO umepoa! Huyu ni Yule Petro
ambaye alisema “hata wakikuacha wote mimi sitakuacha, niko tayari kufa
kwa ajili yako, nk”. Sasa kimetokea nini? Upendo umepoa. Yesu
alipofufuka akamtafuta tena Petro, akamuuliza “Petro UNANIPENDA?”,
akarudia mara ya pili “Petro UNANIPENDA?” na mara ya tatu kurudia Petro
AKALIA! Na akamwambia “Bwana unajua nakupenda…”. Ninachotaka uone hapa
ni ile hali ya KUKATA TAMAA na KURUDI nyuma ya Petro baada ya VURUGU
nyingi kutokea katika HUDUMA yao. Na YESU alikua ANAHUISHA ule UPENDO
kati yao ambao ULIATHIRIKA. Hapo wakati Yesu anampa Petro kazi unaweza
kujiuliza kwanini amuulize kwanza “unanipenda” ndio asema “LISHA
KONDOO”, “CHUNGA KONDOO”, nk.? Sababu ya msingi hapa ni HUWEZI kufanya
kazi ya MUNGU kama HUMPENDI! Jaribu uone halafu mbwa mwitu aje kama
hujakimbia na kuacha KONDOO wanaliwa huko! Nakwambia mchungaji
ANAYEPENDA kondoo zake “itamgharimu” maisha kwa kondoo hao. Sio mimi, ni
maandiko yamesema.
Sasa katika maisha ya leo wengi wetu
tumejeruhiwa sana na “watu” katika michakato mbalimbali ya maisha na kwa
sababu UASI umeongezeka UPENDO wetu kwa Mungu na kwa “hao watu”
umeathirika kwa viwango tofauti. Wengine WAMEACHA wokovu na wengine
WAMERUDI nyuma. Sasa Ibilisi akifanikiwa kukurudisha nyuma, ukampa
nafasi ya kurudi pale alikofukuzwa wakati unampokea Yesu, huwa anaongeza
“idadi ya MAPEPO mara 7, tena wale waovu zaidi, na hali ya mtu huyu
inakua mbaya kuliko ya mwanzo”! ili akifanikiwa “akuchinje” kabisa usije
ukatubu!
Ukifahamu SIRI hii utagundua ni kwanini MTU
akisalitiwa katika MAHUSIANO ni rahisi sana kurudi nyuma katika WOKOVU
pia! Ule UASI una NGUVU ya KUPOOZA upendo wako kwa Mungu na kukumaliza
kiroho USIPOANGALIA. Katika NDOA, HUDUMA, MAKANISANI, nk. kumekua na
hiki kitu cha KUSALITIANA na kimeathiri kazi ya Mungu kwa kiwango
kikubwa sana kwa sababu kimegusa eneo nyeti la UPENDO. Ni jambo la
kusikitisha sana “mmoja” katika HUDUMA au NDOA anakua AGENT wa shetani
“kwa muda” (bila kujua) kama ilivyokua kwa YUDA. Na kwa kipindi kifupi
anatumika kufanya KITU ambacho kitasambaratisha HUDUMA au NDOA moja kwa
moja. Ibilisi akimwachia huyu mtu (kwa maana ilikua kwa kitambo tu)
akizinduka, anajuta! Ndio maana YUDA alikimbilia KITANZI na wala ile
RUSHWA hakuila! Alisikia vibaya sana baada ya KUFANYA ule UASI na
USALITI na akachukua ile HELA na kuirudisha kwa wenyewe! Too LATE! Yesu
yuko msalabani saa hizo na huku huduma ishasambaratika WATUMISHI wenzake
akina Petro nao “washaharibu” na akina Yohana na wenzake washatokomea
kusikojulikana. Yesu alipofufuka alifanya kazi ya KUWAKUSANYA hawa
wanafunzi wake kwa UPYA baada ya kusambaratika vibaya.
Angalia
mambo ya kwanza uyape umuhimu wa kwanza. Watu wengi sana wako busy na
HUDUMA na kusahau kwamba UPENDO ni msingi wa YOTE. Mungu havutiwi sana
na hayo mambo kama HUMPENDI, na utakosa Ufalme wa Mungu usipojipanga
pamoja na huduma yako kubwa nchi nzima au hata dunia nzima. Kumbuka (1
Wakorintho 13:1,2) “Tena nijapokuwa na UNABII, na kujua SIRI zote na
MAARIFA yote, nijapokuwa na IMANI TIMILIFU kiasi cha kuweza kuhamisha
milima, kama sina UPENDO, si kitu mimi. 2 Tena NIKITOA MALI ZANGU ZOTE
kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina
upendo, hainifaidii kitu.” Shughulikia eneo lako la UPENDO wa KWANZA na
Yesu. Fanya “toba” ya dhati ukikiri (kutaja kwa jina) pale “ulipoa
anguka” maana unatakiwa UPAKUMBUKE na kumwambia Yesu, na kisha omba
“maombi” yako ya dhati ili KUHUISHA ule UPENDO wa kwanza, na utaona
mabadiliko na BARAKA zikimiminika kwako kwa namna ya tofauti.
Lengo la somo hili ni kukutahadharisha kuwa tuko nyakati za hatari.
UASI ni mwingi na usipoangalia unaweza KUPOOZA UPENDO wako wa KWANZA! Na
Yesu anasema na wewe akijua “umeuacha ule UPENDO wako wa kwanza”, ule
ambao ulikuweka chini ukasoma Neno na kuomba na KUSHUHUDIA au kumtumikia
Mungu katika ngazi mbali mbali. Naye anasema “kumbuka ni wapi
ulipoanguka ukatubu”. Fanya HARAKA kwa sababu hizo njia za YUDA kweli
zitakupa HELA, ila ni vipande 30 tu! Kumbuka thamani ya DAMU ya Yesu
iliyokununua, FANYA uamuzi LEO kama UNAZIDI kumsaliti MWANA wa MUNGU au
unamrudia. Mungu atusaidie kufanya maamuzi sahihi. NEEMA ya BWANA na iwe
JUU yako tangu SASA na hata milele. AMEN.
Frank Philip.
Nimetamani sana tujifuze jambo katika ndoa ya Yusufu na Maria.
Nimechukua mfano huu kama ndoa/uhusiano wowote wa mwanaume na mwanamke
ambao lengo lake ni kuishi kama mke na mume.
Kuna mambo kadhaa
najifunza kwa maisha ya binafsi ya Yusufu na Maria. Yusufu alikuwa mtu
wa haki, mtu mwenye heshima yake na jina jema katika jamii
iliyomzunguka. Aliukuwa na kazi yake ya useremala
ambayo yamkini ilimwingizia kipato. Kwa upande mwingine hatuambiwi
Maria alikuwa anajishughulisha na nini ila alikuwa BIKIRA, ikimaanisha
alikuwa msichana aliyejitunza na kuishi maisha masafi. Hawa wawili
walikuwa wachumba na walidumu katika UHUSIANO huo katika USAFI wote.
Kuna mambo manne (4) nataka tuone hapa. (Luka 1)
i. Kipindi cha Giza
Wakati maisha yanaendelea, ghafla! Malaika analeta habari kwa Maria
kwamba atapata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu na atazaa mtoto wa
kiume. Kwa Maria ilikuwa ni habari ngumu ila alikubali kama MTUMWA kwa
Bwana wake kwa sababu alijua ni mapenzi ya Mungu. Sasa nisikilize
vizuri, wakati Malaika Gabriel analeta habari kwa Maria kwamba
AMEBARIKIWA, tena amebarikiwa kuliko wanawake wote, na kwamba mtoto
atakayezaliwa atarithi kwenye kiti cha mfalme “Daudi”, Maria anasikai
raha hadi anaenda kwa ndugu yake Elizabeth [mama yake Yohana mbatizaji],
anamshangilia Mungu kwa wimbo na wanajazwa Roho Mtakatifu pale na
Yohana naye anashangilia kwa kucheza akiwa huko tumboni kwa mama yake.
Sasa nataka uone kitu ambacho mimi nakiona. Wakati Maria anaitwa
AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote, kwa Yusufu ilikuwa sio Baraka ila ni
balaa tupu. Kwa maana binti aliyemwamini kabisa sasa ni mjamzito katika
mazingira ambayo hayaelewi, wala hajawahi kusikia kitu cha sampuli hii
kimetokea wapi (all was new experience), hakuna mahali pa kurejea
(reference) na wala hakuna mtu anaweza kumshauri kwa maana katika ELIMU
ya dunia wakati huo hakuna mahali kitu kama hicho kimeandikwa/kimetokea.
Watu hawajui nini kinaendelea. [Angalizo: Sio kila jambo kwenye
ndoa/uhusiano wako utapata mjuzi wa kukusaidia, jifunze kujipanga na
Mungu kwa mambo ya ndoa yako]
Katika hali hii ya GIZA, Yusufu
akaamua KUMWACHA Maria kwa siri! Hii ni hali ya kuchanganyikiwa ambayo
wengi wanafika katika mazingira magumu katika mahusiano yao. Ghafla tu
unaona hiki “kitu” ni kigumu na unaona hakuna njia tena na unajiambia
“basi bwana kama ndio hivi basi mimi naacha” au “mimi nimefanya sehemu
yangu ila mwenzangu amenisaliti, naachia ngazi”, au “kwani mimi ndio wa
kwanza kuachika”, “kwa vile ameenda kupata mimba huko basi na mimi sioni
tena haja ya kujitunza”, “kwanza nina kazi yangu na simtegemei, potelea
mbali maisha yataendelea”, nk. Ni hali ya kukata tamaa. Hiki ni kipindi
cha giza. Na mwili unataka kuleta majibu ya haraka (instant solutions),
kukimbia na kupotelea mbali. Lakini Malaika anakuja kusema na Yusufu na
kuugeuza Moyo wake. Sijui kama Yusufu alikuwa mwombaji ila tunaambiwa
Mungu alisema naye, akasikia na KURUDISHA moyo nyuma. Usipo jifunza
kukaa katika MAOMBI ni vigumu kuvuka hii ngazi. Hapa ni kipindi cha
KUNGOJA maana unajisikia huku ndani kwamba BADO hujapata/hujafika mahali
unataka. Kumbuka “wamngojao Bwana watapata NGUVU mpya”. Unahitaji Nguvu
mpya kila siku kuvuka hapa. Utagundua ule “upendo wa zamani umepoa”,
sasa unahitaji NGUVU mpya. Muombe Mungu akupe nguvu mpya.
ii. Kutembea katika Baraka
Mara nyingi watu wamefikiria Baraka za Mungu kwa upande mmoja tu wa
kuwa na hela, majumba, magari au kufanikiwa katika mambo ya mwilini na
kusahau upande mwingine. Utasikia watu wanasema “count your blessings”
(“hesabu Baraka zako”). Sasa unajua huwezi kuhesabu KITU ambacho hukijui
na wala hukioni. Nakwambia Leo kuna Baraka nyingi sana Mungu
anatubariki na hatuwezi kuziona wala kuzihesabu kwa maana ziko kwa jinsi
ya ROHONI na kwa sababu huzioni hujui kwamba UMEBARIKIWA na unabaki
ukilalamika na kunung’unika kwa sababu ulishamwekea Mungu vigezo na
vitu fulani kwamba “hiki kisipotokea basi sijabarikiwa bado”. Kama mambo
yako “hivi” basi bado hakijaeleweka, nk. Maria alichukuwa tu kama
Malaika alivyosema na “akayatia moyoni mwake” huku akijua kwamba
AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote. Kwanini aliweka moyoni mwake? Kwa
maana hakuna mtu wa kawaida anaweza kuelewa hii lugha ya kupata mimba
kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Akajua ni Mungu na hakuna haja ya kutoa
maelezo ya ziada au kuuliza watu au kupeleka umbea. Akakaa mimya.
Hebu mfikirie Yusufu. Wakati anajua kabisa hii mimba sio yangu ila
anamhudumia Maria. Wanaenda huko mbali mji mwingine kuhesabiwa na mama
hajiwezi mimba ni kubwa. Yamkini huko njiani Yusufu alitembea kwa mguu
wakati mkewe mjamzito yuko juu ya punda na yeye anakokota huku mbele,
ila mimba sio yake! Yule mama anajifungua hapo, Yusufu anamsaidia, ila
mimba sio yake! Ni mambo magumu kuelewa ila Yusufu alikaza USO kufanya
MAPENZI ya Mungu kama Malaika alivyosema. Hapo hampendezi Maria, ila
Mungu, kwa maana yeye alichagua kitu cha kumfanyia Maria tayari, yaani
KUMWACHA kwa SIRI! Sasa huu mpango wa kubaki ni mpango mpya ambao
anaambiwa na Malaika na anaamua kuutimiza mpango huu japo haelewi
vizuri. Mimba sio yake! Na sio hivyo tu, hajawahi kumgusa kabisa huyu
mama! Analea mimba miezi 9, akijua kabisa sio yeye!
Kumbuka
sio kila kitu Mungu atafanya juu ya maisha yako UTAELEWA. Baraka nyingi
sana tunapata sio BINAFSI. Mungu amelenga KUWABARIKI wengi kupitia
BARAKA alizokupa. Katika kubariki wengi LAZIMA kuna UDHIA. Ndio maana
Yesu alisema “hakuna mtu aliyeacha ndugu, wazazi, shamba, nk. na
kumfuata asipate hivyo “vitu” mara 100 hapa duniani ila na UDHIA pia”.
Watu wengi sana wanapenda BARAKA ila BINAFSI, wanasahau kwamba Mungu
akishusha Baraka mara nyingi sana hulenga wengi sana kwa Baraka hiyo
hiyo, na imekuwa udhia. Kwa maana sio UPENDAVYO wewe ila sasa ni kama
WAPENDAVYO wengine pia kupitia Baraka hiyo hiyo. Hebu fikiri wewe ni
Maria (mama wa Yesu), unaitwa MBARIKIWA kuliko wanawake wote, ila kijana
hakai nyumbani, anapita mitaani KUHUBIRI vitu hata huelewi, ukimuuliza
anasema anafanya MAPENZI ya Baba yake! Huku Yusufu naye haelewi pia.
Ghafla! Watu wanajaa kila mahali hata hakuna muda wa kula na kuongea
kama familia! Huwezi tena kusema huyu ni MWANANGU kwa maana hata yeye
anasema “hawa wa hekaluni ndio mama na ndugu zangu”. Kijana anasema
lugha ngumu-ngumu tu kila saa! Huku mtaani wanasema kachanganyikiwa
(karukwa na akili) na wengine wanasema kijana ana pepo! Hebu fikiri hii
ndio ile kitu Mungu anasema ni BARAKA!
iii. Machozi kwenye Baraka Yako
Bila shaka Maria na Yusufu walikuwa na vipindi vigumu na Yesu, japo
waliitwa WABARIKIWA. Ghafla wanaambiwa wahame nchi kwa maana Herode
anataka kumuua mtoto! Wanakimbilia Misri, sijui walikuwa na usafiri gani
ila najua haikuwa rahisi. Hebu fikiri ghafla! unajikuta unaanza kupiga
mahesabu ya kuacha kazi yako kama Yusufu kwa sababu ya hii BARAKA
iliyokuja kwenye familia. Hebu fikiri wale wateja wake ambao alikuwa
anawatengenezea furniture, anawaagaje? Hebu fikiri wale ndugu zake sasa
hapo mtaani anawaagaje? Eti, anahama nchi! Maana sio tu hawamwelewi, ila
wanamwona kachanganyikiwa pia. Hii ni BARAKA imeingia katika familia na
watu wanaanza kuhangaika. Sasa ukifika mahali pa kukata tamaa jua
UNAHARIBU ile Baraka ya Mungu kwa maana sasa inakuja kwa MTINDO ambao
haujautarajia. Nakwambia kila mtu atakuelewa ukiamua kuitupilia mbali
hiyo BARAKA isipokuwa Mungu. Lakini nakwambia ni aheri KILA mtu
asikuelewe ila Mungu akuelewe inapofika kufanya MAPENZI yake.
Ndoa nyingi sana ni BARAKA katika maisha ya watu na pia Mungu amelenga
hizi ndoa ziweze kuwa BARAKA kwa watu wengine. Utakuta hapo katikati
kumetokea MAMBO magumu na watu wamesamabaratika na KUTOKA nje ya kusudi
la Mungu. Sawa watu watakuelewe kwa maana kwa kweli “huyu jamaa” amekuwa
kama kichaa kabisa, ila kusudi la Mungu ni nini? Nakwambia kuna BARAKA
ambayo Mungu alitarajia watu wengine waipate kupitia NDOA yako ila sasa
Ibilisi ameisambaratisha na amefuta BARAKA kubwa ambayo wengi wangeipata
kupitia NDOA yako! Sio kila KUACHANA ni suluhisho hata kama mazingira
yote ya KISHERIA na KIJAMII yamekaa sawasawa na kila mtu anakuunga
mkono. Kumbuka Yusufu angeweza kumwacha Maria mapema tu akiwa kama mtu
wa HAKI, ila alikaza uso kutimiza Mapenzi ya Mungu. Je! Unajua mapenzi
ya Mungu kwa NDOA yako? Je! Kila mmoja anajua WITO wake na mlichoitiwa
kufanya shambani mwa Bwana? LAZIMA kipo. Hebu fikiri hii MISUKOSUKO yote
ya NDOA ya Yusufu na Maria halafu hawajui WITO wao ingekuaje? Mkijua
kila mmoja alichoitiwa mtapona kwa urahisi zaidi katika VITA vya adui.
iv. Mahali pa Ushindi
Wakati Maria na Yusufu wanapita nyakati mbalimbali ngumu na BARAKA ya
mtoto Yesu, inafika takriban miaka 30 ambapo sasa KIJANA anakomaa kuwa
mtu mzima. Mara kijana anakuja na agenda za KUFA kwa ajili ya ULIMWENGU!
Maria haelewi wakati kijana anasema “mkila mwili wangu na kunywa damu
yangu mnauzima wa milele”! Pamoja na kupita hivi vipindi vizito sasa
kijana anataka KUFA! Eti yeye ni kondoo wa SADAKA. Matarajio ya Maria
alijua siku moja yeye atakuwa mama wa MFALME, mtu tajiri mtaani na watu
wote, wakubwa kwa wadogo wanamwamkia na kumheshimu. Maria anapiga picha
ya KIONGOZI mkubwa kwa jinsi ya mwili lakini KIJANA anakuja na AGENDA za
kusulubiwa sasa. Yamkini nguvu ya kushinda mambo yote magumu ilikuwa
kwenye matumaini kwamba SIKU MOJA huyu kijana atakuwa mfalme kwenye kiti
cha Mfalme Daudi na hapa nitapumzika. Mambo yanakuja kinyume na
matarajio yake japo anajua kuwa AMEBARIKIWA. Huyu mama anafuata kila
hatua, anaona kijana anakamatwa, anapelekwa Golgotha kusulubiwa kama
MHALIFU. Hebu fikiri hapo. Mama anamjua mwanae vizuri sana. Anajua ni
mcha Mungu leo ghafla tu anasingiziwa vitu VIGUMU na sasa wamempiga
vibaya damu inatiririka kila mahali na wanampeleka kumgongomelea
MASALABANI. Mama analia Yesu anasema “USINILILIE mama, jililieni
wenyewe!” Yesu alijua ili hii BARAKA ikamilike ni LAZIMA asulubiwe kwa
maana yeye ni “Mwana-kondoo wa Mungu achukuaye dhambi za ulimwengu”. Hii
ni Baraka kubwa ila haijakaa kwa namna watu wengi wataiona kama Baraka!
Wengi wangelalamika na kuona ni BALAA kubwa kwenye familia! Kama
unatarajia UZIMA wa Milele jifunze kusoma LUGHA za rohoni katika Baraka
zako kwa maana nyingine zinakuja kwa mtindo ambao unaweza kukemea
ukidhani ni Ibilisi au jaribu. (Luka 23)
Lengo la somo hili ni
kutaka kukufungua macho juu ya mambo ambayo Mungu anafanya katika maisha
yetu na tukumbuke kumshukuru hata kama hatuelewi kila kitu kwa maana
“Mungu amekusudia mambo mema kwa ajili ya watoto wake kila siku”.
Angalia usibebe roho ya KISASI kwa mambo yatakayokukuta katika MAHUSIANO
kwa maana KILA uhusiano/ndoa itapita katika VIPINDI vigumu na vyepesi,
vipindi vya huzuni na furaha, vicheko na vilio, nk. Angalia sana katika
VIPINDI hivi usimkosee Mungu kwa sababu tu HUELEWEI mwenzako anafanya
nini. Yamkini ameamua kukusaliti na wanawake/wanaume wengine na umejua.
Kwa maana kama wewe ni mtu wa Mungu “hutakosa kuzijua HILA za Ibilisi na
Mungu hatawaficha watu wake jambo”, na umefika mahali UMEJUA. Chunga
USIMKOSEE Mungu kwa sababu mwenzako amemkosea Mungu. Uhusiano/NDOA ina
mwisho ila uhusiano wako na Mungu hauna mwisho. Ukijua kwamba MATESO
yako ni ya KITAMBO tu, usikubali KUPOTEZA hatma yako (mambo ya milele)
kwa sababu ya mambo ya kitambo tu. Kaza uso wako kwa Mungu na kaa katika
KUSUDI lake na WITO ulioitiwa ili ile BARAKA Mungu aliyoweka katika
maisha yako ISIPOTELEE njiani. Tafakari yaliyo juu aliko Kristo kwa
maana huku Duniani kuna ufisadi mwingi. Angalia MWISHO wa safari yako na
ujitie moyo katika Bwana. Mambo yanayotokea kwenye uhusiano wako
yasiujaze moyo wako hata ukakosa shukrani kwa Mungu wako.
Neema na Rehema zitokazo juu ziwahifadhi NIA zetu tangu sasa na hata milele. Bwana yu karibu.
Frank Philip.
Kibaraka ni mtu anayefanya kazi kwa kutaka kumpendeza BWANA wake au mtu
mwingine MWENYE NGUVU. Kibaraka haishi kwa matakwa yake ila ya MWENYE
NGUVU.
Kibaraka anasifa nyingi za kuvutia. Nataja chache:
Kibaraka hua na nguvu nyingi bila kuhesabu gharama ya kile afanyacho
alimradi bwana wake ameridhika. Mara nyingi kibaraka halalamiki
anapotumikishwa, na hata akilalamika bado
huendelea kumtumikia bwana wake tu. Kibaraka haangalii muda, mahali
wala kuwaza sana juu ya matokeo ya matendo yake japo mara nyingine
hapendi afanyacho. Kwa sababu hii ya “ku-take risk” vibaraka hufanikiwa
saana katika wayatendayo japo ni kwa ajili ya kumpendeza MWENYE NGUVU na
sio Mungu!
Kuna sifa mbaya kadhaa za kibaraka. Nitazitaja
chache. Kibaraka hua katika hali ya UHITAJI na KUPUNGUKIWA kila siku.
Siku zote ni dhaifu kwa MWENYE NGUVU! Sifa nyingine mbaya zaidi
inayomfanya kibaraka azidi kua kibaraka ni ile hali ya ‘kutojua kua yeye
ni kibaraka’ na akiambiwa hukasirika na kubisha kwa nguvu!
Katika organizational structure ya Mungu, MUNGU yuko pale juu, punde
kidogo akamweka mwanadamu na kisha malaika watakatifu. Kumbuka Shetani
na mapepo yote yalikua katika ngazi ya malaika kabla ya kuasi. Hii
inamaana Mwanadamu yuko juu ya shetani na mapepeo yote na juu ya malaika
pia! Shetani na mapepo yote yatazidi kua CHINI yako daima kama unaishi
maisha MATAKATIFU na kumtii Mungu.
Nitatoa mfano. Kila mtu,
mvulana au msichana, anakua na nguvu kubwa ya kupambana na ‘uzinzi’ na
kuupinga hata kama “hajaokoka”. Asili ya hiyo nguvu sio jina la Yesu,
kwa maana hata hajui kuomba na wala sio Mkristo, ila asili ya nguvu hiyo
ni ile ngazi ya juu Mungu aliyomweka katika ulimwengu wa roho kuliko
mapepo. Siku anajaribiwa na “tamaa zake” na kufungulia ‘uzinzi’, kuna
package ya mapepo yanahusika hapo na yanamfanya sasa kua KIBARAKA wa
ngono! Anakua dhaifu wa ngono na anaanza sasa kutenda kwa mfano wa
KIBARAKA na mapepo ya ngono yakiwa kama MWENYE NGUVU! Ushindi wa mtu
huyu dhidi ya ngono sio natural na automatic tena, sasa atatumia jina la
Yesu, tena kwa nguvu na kupambana na MWENYE NGUVU kwa maana mwenye
nguvu ameshaingia ndani, sharti “umfunge kwanza ndio uweze
kuchukua/kutawala vilivyo vyako” la sivyo utabaki kua kibaraka na
utatumikishwa kweli hadi mauti. (Warumi 7)
Umewahi kufikiri
gharama ambayo KIBARAKA anaweka katika salon, mavazi, viatu, vipodozi,
simu na mawasiliano, gym, nk. Kwa lengo tu la kukaa katika “mkao fulani”
ili kumpendezesha MWENYE NGUVU wake? Nakwambia kwenda fellowship na
bible study ni bure ila KIBARAKA hataenda huko maana ‘anaswagwa’ kama
ng’ombe na mwenye nguvu [“asije akasikia Neno akapona/akaokoka”],
atapata muda na hela ya kulipa gym, eti ana-keep shape na tumbo lake
liwe dogo! Au anajenga kifua na mkono kwa maana wadada wanapenda hiyo!
[Sasa biblia inasema “mazoezi ya mwili yafaa, ila utaua wafaa zaidi”]
Shida sio mazoezi, vipodozi wala jitihada zingine, shida iko katika
chanzo na sababu na makusudi ya kufanya “hivyo vitu” ndio inayopima
kwamba ufanyacho ni dhambi au la!, the motive behind! Je! Kuna mwenye
NGUVU anakusukuma katika jitihada zako ziwazo zote? Je! Wewe ni kibaraka
wa mwenye nguvu katika maeneo mbalimbali? Tafuta UKOMBOZI WA DAMU YA
YESU nawe utakua huru..
Warumi 7: 14 “Tunafahamu kwamba sheria ni
ya kiroho. Lakini mimi si wa kiroho; mimi nimeuzwa utumwani, ni mtumwa
wa dhambi. 15. Sielewi nitendalo: kwa maana lile ninalotaka kulifanya,
sifanyi; badala yake, ninafanya lile ambalo nachukia kulifanya. 16 Kwa
hiyo kama ninafanya lile nisilopenda kufanya, hii ina maana kwamba
nakubali kuwa sheria ni njema. 17 Basi, kwa kweli si mimi hasa nitendaye
lile nisilolipenda bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.18 Kwa maana
ninafahamu kwamba hakuna wema wo wote ndani yangu mimi, yaani katika
mwili wangu wa asili. Ingawa nina nia ya kutenda lililo jema, lakini
ninashindwa kulitenda. 19 Sitendi lile jema nipendalo bali lile ovu
nisilopenda, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninafanya lile nisilopenda
kufanya, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani
yangu. 21 Kwa hiyo imekuwa kama ni sheria: kila ninapotaka kufanya jambo
jema, jambo ovu hujitokeza. 22 Kwa maana ndani yangu ninaifurahia
sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyin gine mwilini mwangu
inayopingana na ile sheria ninayoikubali akilini mwangu. Sheria hii
inanifanya kuwa mateka wa sheria ya dhambi ambayo inafanya kazi mwilini
mwangu. 24 Ole wangu, mimi mnyonge! Ni nani atakayeniokoa na huu mwili
wa kifo? 25 Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa
hiyo basi, mimi kwa moyo wangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa
mwili wangu wa asili ninaitumikia sheria ya dhambi.”
Frank Philip.
Leo nataka niseme juu ya KILIO. Kuna tofauti ya kulia kwa machozi ya
nje na kulia kwa machozi ya ndani. Mtu anapotendewa kitu na ndani yake
akasikia KUNYANYASIKA na akasikia uchungu sana, mara nyingi anatoa
machozi ya nje (atalia). Lakini sio kila mara mtu atalia kwa machozi,
ila kuna ule UCHUNGU wa ndani ambao watu mbalimbali wamekua nao na
wameenda mbele za Mungu kwa maombi au
hata wametamka tu maneno na Mungu AMESIKIA (“nipo pamoja nanyi katika
mipango yenu, kabla ya kuomba mimi Bwana nitasikia na mkiwa katika
kunena mimi Bwana nitajibu”). Chunga hii kitu, Mungu anasikia KILIO
kuliko unavyodhani. Na mara nyingi sana hiki KILIO hata kama mtu sio
mlokole nakwambia UKIMDHULUMU, UKIMNYANYASA, UKIMTENDA JEURI mtu na
akalia kwa UCHUNGU mbele za Mungu hata kama hakumwambia mtu au hata kama
hajui kama Mungu anasika, nakwambia Mungu husikia VILIO.
Wakati Mungu anamtokea Musa na anamtuma Misri kuwakomboa wana wa Israel
kutoka UTUMWANI, Mungu alisema “nimesikia kilio chao nami nimeshuka
kuwakomboa”. Mungu hakusikia maombi bali KILIO! Sasa ninataka uone huu
mfumo vizuri. Pale Misri wana wa Israel walikua watumwa, na juu yao
kulikua na VIONGOZI na WASIMAMIZI na kule juu kabisa alikuwepo Mfalme
Farao. Kiutawala hawa watumwa walikua chini kabisa, ila walikua WANA wa
MUNGU aliye hai. Kumbuka “hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na ile
iliyopo imeamriwa na Mungu”. Kwa lugha ya kawaida BOSS mkubwa sana
katika “utawala wowote” hapa duniani ni Mungu. Sasa kama mtu mwenye
HAKI, amefika mahali pa gumu sana na amelia kwa MATESO mbalimbali, akiwa
hajui huu mfumo bado BOSS mkubwa hushuka hapo na kurekebisha mambo,
haleluya! Kwa wale wanajua hii SIRI na kusimama katika nafasi na zamu
zao vizuri, HAWATAMSUJUDU boss wao wa duniani na kufanya NGONO, nk., na
kumkosea Mungu kwa sababu ya kulinda MASLAHI yao ya kikazi. Watapambana
kwa “NIA ya kushinda UOVU na KUTII kwao kutakapotimia MAMLAKA yao katika
ulimwengu wa roho dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wa baya
ITAONGEZEKA sana”. Na KILIO chao Mungu atasikia na ATASHUKA kuwaokoa.
Kumbuka, Mungu ndio boss mkubwa pale juu ila maandiko yanatuonya TUTII
mamlaka iliyo kuu. Na usithubutu kumwambia kiongozi wako kuwa wewe sio
boss ila boss ni Mungu. Jua hilo moyoni na mtizame Mungu kama Mkuu wako
wa kazi na chapa kazi kwa moyo, acha uvivu.
Nebkadneza mfalme
wa Babeli alikwenda kula majani miaka/misimu 7 kwa kosa la kujisifia
kwamba “huu mji ni mkono wangu umejenga?” Akatizama mafanikio ya Ufalme
(kampuni yake) akajiinua ndani ya moyo wake! Mungu akasema sasa utajua
kwamba mimi natawala pamoja na wanadamu, sio wewe Nebkadneza, ni Mimi!
Hii siri watu “wachache” wanaijua na wamehusika kuwapiga “transfer”
(uhamisho) mabosi wao kwa sabababu wameleta shida kwenye KAMPUNI na jina
la Mungu linatukanwa au watu wamenyanyaswa. Transfer inaweza kuwa
kulala, kushushwa cheo (kula majani), kuhama kituo cha kazi, nk. Ila
vita vyetu sio juu ya DAMU na NYAMA. Ni katika roho, na tunapata NGUVU
tukiwa na NIA thabiti ya kupinga UOVU wote na KUTII kwetu
kutakapotimilika (2Kor. 10:4-6). CHUNGA sana usije ukafanya mambo kwa
HUSUDA, WIVU au MASHINDANO, utashindwa. Mamlaka ya Mungu haifanyi kazi
hapo. LAZIMA usimame katika KWELI na HAKI na sio maslahi binafsi.
Usikubali kumkosea Mungu kwa kisingizio eti “sasa huyu ni MHESHIMIWA na
mimi ningefanya je?”, mwite Yesu hapo akuokoe na KILA (hata kama sio
mlokole) atakayeliitia jina la BWANA ataokoka katika hali anayopitia.
NEEMA ya BWANA izidi KWENU. AMEN
Frank Philip.
Kipimo cha UDHIHIRISHO (MANIFESTATION) wa Mungu kwenye HADHIRA
(PUBLIC) ni MUDA, BIDII na HALI ya MOYO wako UKIJIHUDHURISHA mbele Zake
mkiwa wenyewe wewe na Mungu pekeyenu (SIRINI).
Kama
UKIJIHUDHURISHA mbele za Mungu wako kwa BIDII na kwa UELEKEVU mahali pa
SIRI, basi Mungu ATAJIDHIHIRISHA mbele ya WATU hadharani.
Ukitaka Mungu aji-present kwa watu basi jifunze kuji-present kwa Mungu.
Ni aheri ukose MUDA wa kuandaa PRESENTATION kwa watu na sio MUDA wa
kuji-present kwa Mungu, kwa maana unaweza ku-present kitu chochote mbele
za watu ILA HUWEZI kum-present Mungu! Ndio maana kazi ya Mitume ilikua
KUHUBIRI na KAZI ya Mungu likua KULITHIBITISHA hilo Neno kwa ISHARA na
MAAJABU.
Kazi ya Musa ilikua kuji-present kwa Mungu na kupata
maelekezo na KAZI ya Mungu ilikua KUTENDA miujiza (kuji-present) mbele
za Farao!
Frank Philip.
Katika maisha yetu ya kila siku tumetamani MAMBO mengi mbalimbali
yatokee. Mengi ya haya MAMBO yako nje ya uwezo wetu na IMETUPASA
kuhitaji msaada wa Mungu au watu wengine. Mara nyingi utagundua ni
vigumu sana KUTEGEMEA misaada ya watu KUTIMIZA mahitaji yetu ya kila
siku. Njia rahisi ni kujua jinsi ya kujipanga vizuri na Baba yako wa
Mbinguni na kwa kupitia Yeye, anaweza
kuinua watu mbalimbali kuja kuingilia kati hali unazopitia na
kukusaidia. Ikishindikana kabisa, Mungu anaweza kuinua kunguru, mawe au
Malaika kuja kukupigania, na hii imetokea kwa wengi hata kwako pia
inawezekana.
Kusudi la somo hili fupi ni kutaka kuhusianisha
USHINDI wako na (i) NAFASI yako katika Kristo na KUZAA kwako MATUNDA, na
(ii). KIWANGO chako cha MAOMBI na pia ujue (iii). VIKWAZO vya Majibu ya
maombi yako, (iv). Kutofautisha imani ya KUOMBA na KUPOKEA, na (v).
Ujue jinsi ya KUJITEGEMEA kimaombi.
i. NAFASI yako katika Kristo
Mambo kadhaa ni ya LAZIMA: (a) kukaa ndani ya Yesu, (b). Neno kukaa
ndani yako, na (c). Omba lolote utapewa. Yesu alitufananisha na yeye
akiwa mzabibu, akasema“ sisi ni matawi ya mzabibu na yeye ni Mzabibu.
pasipo yeye sisi hatuwezi jambo lolote”. Pamoja na kwamba Yesu alikuwa
anazungumzia KUZAA matunda, utagundua pia mistari iliyofuata alisema juu
ya MAOMBI. Kwa upande mwingine kuna uhusianao kati ya KUZAA matunda na
KUJIBIWA maombi yako. (Yohana 15:1-6).
ii. KIWANGO cha maombi
Yesu alipowatuma wanafunzi wake kwenye HUDUMA mambo mengine yalikuwa
magumu, japo wametumwa na Bwana! Walipomuuliza kwanini mambo mengine
yanagoma? Yesu alijibu “mambo mengine hayawezekani bila KUFUNGA na
KUOMBA”. Hapa tunapata picha kwamba kuna kiwango fulani cha maombi
kinaweza kukuvusha hadi hatua fulani. Ukifikia hiyo hatua inahitaji GIA
nyingine ya maombi ya kiwango cha juu zaidi ili uvuke kwenda kwenye
hatua ya juu zaidi.
Pamoja na BIDII (diligence) na KUDUMU
(persistance), haya mambo mawili ni ya muhimu sana KUPIMA kiwango cha
USHINDI wako katika yale unayoyaombea. Kuna wakati itakupasa kuongeza
NGUVU/KIASI cha kuomba ili kuvuka mahali ulipo. Hata kama wewe ni TAWI
na UKO ndani ya Yesu vizuri na Neno (imani) limejaa ndani. (Luka 18)
iii. VIKWAZO vya MAJIBU ya Maombi yako
Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUPOKEA majibu ya MAOMBI na HALI ya
MUOMBAJI mwenyewe pamoja na KUTIMIZA viwango vingine kama (i) na (ii)
hapo juu. Kila mtu anajua kwamba tukiomba sio mara zote mambo hutokea
wakati huo-huo. Kuna kipindi cha KUSUBIRI na wakati mwingine kinakuwa
kirefu. Ili uweze KUPOKEA majibu yako angalia usikate tamaa kwa maana
“Mtavuna kwa wakati msipozimia roho.” Huhitaji IMANI kubwa kupokea
MAJIBU ya Maombi yako. “Imani kidogo sana kama chembe ya haradali tu,
inaweza kuhamisha milima na kufanya mambo makubwa sana maishani mwako
ila usipokuwa na SHAKA juu ya yale mambo uombayo”. MASHAKA ni KIKWAZO
kikubwa cha kupokea uombayo hata kama una IMANI. Kwa lugha nyepesi,
mashaka ni sumu ya IMANI yako. Adui anajua ukiomba kwa imani utapokea,
sasa akishindwa kukuzuia usiombe, basi ataleta MASHAKA katika yale
uyaombayo ili USIPOKEE. Ukiwa makini utamsikia katika “mawazo yako”
akikukukatisha tamaa na saa nyingine akikuzomea kabisa. Pambana na hayo
mawazo maana ni vita inayoweza kuathiri IMANI yako na majibu ya maombi
yako. (2 Wakorinto 10:1-6)
iv. JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA
Watu wengi sana wana IMANI ya KUOMBA ila wachache wana IMANI ya
KUPOKEA. Ukiwauliza watu juu ya maombi kwa kweli watakuambia Mungu
anajibu ila ukichunguza WANACHOONA ndani ya MIOYO yao ni KUSHINDWA zaidi
kuliko KUSHINDA. Matokeo yake hawawezi KUPOKEA majibu kwa maana hawana
IMANI ya KUPOKELEA.
Nitakupa mfano. Pamoja na kwamba Yesu ni
mponyaji na Muumbaji wa Ulimwengu, utasikia mahali anasema “imani yako
imekuponya”. Ina maana imani ya KUPOKEA ni ya MPOKEAJI na sio imani ya
Yesu japo kuna mahali ALIWAHURUMIA tu watu akafanya mambo kabla hata
hajaombwa na mtu (Luka 7:12,13). Kati ya maeneo ambayo Yesu hakufanya
miujiza ni kule mitaa ya nyumbani kwao, SABABU sio uhaba wa IMANI ya
Yesu ila IMANI ya WAPOKEAJI haikwepo. Yesu hakufanya kitu japo wengi
walikuwa na shida zao nyingi na aliwahurumia! Ndipo akasema “nabii
hakubaliki kwa watu wake.”
v. EPUKA MAOMBI TEGEMEZI
Kuna
kundi la watu wamefanya baadhi ya watumishi kama TIKETI ya kupokelea
majibu ya MAOMBI yao. Sawa, kuna kiwango cha NEEMA juu ya watumishi wa
Mungu kinachoweza kukuvusha mahali, lakini nakwambia kuna wakati hata
YESU “alipoitizama imani ya watu, ndipo alipotenda jambo” pengine
aliacha kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao! UELEKEVU wa MOYO wako kwa Yesu
utakusaidia sana katika KUPOKEA majibu ya maombi yako.
Sasa
tunakumbushwa siku zote kuomba kwa imani na kuambiwa kwamba “kuomba
kwake mwenye HAKI kwa faa sana akiomba kwa bidii”. Jifunze na uchukue
MAZOEZI ya kutumia IMANI yako kwa maana imani ina tabia ya KUKUA au
KUPUNGUA. Kumbuka KUKUZA imani ya KUPOKEA majibu ya maombi yako kwa
maana hiyo ndiyo inayokwamisha wengi. Kumbuka adui mkubwa wa imani ya
KUPOKEA anaitwa MASHAKA.
Dawa ya kupambana na MASHAKA ni
kufanya MAZOEZI ya KUOMBA wewe mwenyewe na KUPUNGUZA utegemezi wa
WATUMSHI wa Mungu. Sisemi ni vibaya kuombewa, ninachotaka kusisitiza ni
wewe kujijengea UWEZO wa kusimama kwa MIGUU yako MIWILI kumwamini Mungu
kwamba UNAWEZA kuomba na KUOPOKEA mwenyewe. Kumbuka wewe ni TAWI la
Mzabibu na mtumishi pia ni tawi tu, anayejibu maombi ni MZABIBU (Yesu).
Ukiweza kuepuka utegemezi kwa MATAWI mengine utagundua UMEVUKA hatua
nyingine ya IMANI na KUMPENDEZA Mungu pia kwa sababu “haiwezekani
kumpendeza Mungu pasipo imani”. Wengi sana tunaweza kumshangaa Petro
jinsi alivyoweza kutembea kidogo juu ya maji na ALIPOONA upepo, akazama!
Hiyo ndio kazi ya MASHAKA. Nadhani kama Petro angefanya tena mazoezi
kwa mara nyingine, angekuwa hahitaji tena Mtumbwi kwenda ng’ambo!
Kwanini? Alikuwa na IMANI ya kutosha KUTEMBEA juu ya maji ila MASHAKA
yalikuwa kikwazo.
Nitakupa mfano. Nguvu ya DAUDI na UJASIRI
aliokuwa nao wakati anamkabili Goliath, haikuwa kwa sababu tu alijuwa
uweza wa Jina la Bwana wa Majeshi, ila “kama alivyofanya MAZOEZI ya
kupambana na DUBU na SIMBA”, alijuwa kwa jinsi ILE ILE, BWANA
atampigania kwa Goliathi. Hakubakia tu KUAMINI moyoni, DAUDI
alimtangazia Goliath (adui) kwa SAUTI ya juu, mambo aliyoamini. Mara
nyingi sana wakati UNAOMBA, adui akileta SAUTI ndani yako za kukutia
mashaka, kumbuka KUMTANGAZIA kwa SAUTI juu ya USHINDI wako. Kwa njia hii
utaweza kushinda MASHAKA. Msomee adui Neno, mwambie “imeandikwa”, kisha
taja Neno (imani) katika biblia unalosimamia katika hayo maombi.
Uzoefu wa kutumia IMANI yako unakupa nguvu ya kuvuka hatua nyingine ya
KUPOKEA mambo uombayo katika kiwango cha juu zaidi. Ukiwa unamtegemea
MTUMISHI fulani tu, MOYO wako unaanza kuwa dhaifu na unaona PASIPO kujua
unahamisha UELEKEVU wako kutoka kwa Mungu na kuuweka kwa huyu MTUMISHI.
Hali hii imekuwa mtego mkubwa kwa watu wengi sana, wamehamisha MACHO
yao kwa YESU na wengine wamefikia mahali pa kuona MTU mwingine anahusika
na matatizo yao ndio maana wakati ule dada zake Lazaro walimlaumu Yesu
(mtumishi) kwa kusema “ungekuwepo hapa kaka yetu asingekufa”!
Mungu atusaidie kuongeza IMANI ya KUPOKEA majibu ya maombi yetu.
Frank Philip.
Bwana Yesu alizungumza kwa mifano mingi akisisitiza UMUHIMU wa watu
wake KUKESHA. Maana halisi ya KUKESHA ni kuwa macho hasa wakati wa USIKU
ambapo watu kwa kwaida hulala. Katika maisha yetu kuna VIPINDI vya
mchana ambapo kuna mwanga na tunaona. Pia kuna vipindi vya USIKU, kuna
GIZA na hatuoni kitu kwa sababu ya giza. Mara nyingi watu wanakuwa
SALAMA katika VIPINDI vya giza kuliko
vipindi vya MCHANA kwa sababu wanachukuwa TAHADHARI na kujilinda. Lakini
pia MAANDALIZI na MAFANIKIO ya ULINZI wako yanafanyika wakati wa
MCHANA.
Vipindi vya MCHANA vina sifa nyingi. Mojawapo ni
MWANGA. Kwa sababu UNAONA vyema, basi unakuwa na AMANI na UHAKIKA kwa
sababu unaona VITU kwa jinsi ya MWILINI. Sasa tukumbuke tumeumbwa ili
KUISHI katika ULIMWENGU wa MWILI na ULIMWENGU wa ROHO. Katika vipindi
hivi tunaambiwa “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu
uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika
hawataokolewa.” (1 Thesalonike 5:1-7). Ukifuatilia mistari hii
utagundua watu wa Mungu wameitwa ni wana wa MCHANA au wana wa NURU! Kwa
lugha nyingine kundi la pili linaitwa WANA wa USIKU! Sasa, pamoja na
kwamba mistari hii ilikuwa inakumbusha KURUDI kwa Yesu kulichukuwa
Kanisa, nataka tujifunze hii TABIA ya Mungu ya KUKESHA.
Sehemu
nyingine Mungu anajiita MLINZI wa Israel, Daudi alijuwa tabia ya Mungu
ya KUKESHA na akasema “Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu
na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam,
hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.” (Zab.
121:1-4). Hii tabia ya KUKESHA ni ya MUHIMU pia kwa WANA wa NURU ndio
maana Yesu amesisitiza sana “kukesha katika kuomba” na pia akasema
“atarudi kama MWIVI ajavyo usiku” akitutaka tuwe MACHO wakati WOTE.
Pamoja na GIZA la dunia hii, Bwana anasema “tusiwe kama wale wanawali
wapumbavu, waliochukua taa zao bila MAFUTA”, huko usiku wakati watu
wamelala, ghafla! Bwana Harusi anakuja!
Kuna sababu nyingi za
KUKESHA. (i) Tuweze kushinda/kutokuanguka majaribuni. (ii) Tuwe salama
adui anapokuja kushambulia. (iii) Kujua wakati wa KUJILIWA na Bwana.
(iv) Tusibaki Yesu akija kuchukua Kanisa lake. Sifa za WAKESHAJI
utaziona hapa, “Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna
asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea.
Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pinde
zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na
gurudumu zao kama kisulisuli;” (Isaya 5:27,28). Nitazungumzia zaidi
KUJILIWA. Yesu alipoutizama Yerusalemu alilia. Akasema “laiti ungejua
yakupasayo amani”, Wakati Yesu (Baraka za Mungu) zinakuja, Israel
hawakujua na kupokea kwa shukurani, na pia wakati ADUI anakuja kuharibu,
hawakuwa na HABARI! Akalia. Maisha yetu tumejisahau sana na kuona tu
mambo yataenda kama JANA! Tumepoa au kupunguza ile kasi ya kumtafuta
Mungu na tunaishi kama MUNGU hayupo! Taratibu tunapoteza NURU na kuanza
kutembea GIZANI. Usipoangalia Ghafla! Uharibifu unakuja, kwa maana ADUI
anakuwinda na anasubiri GIZA akushambulie! “Basi tusilale usingizi kama
wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala
usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na
kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe
tumaini la wokovu.” (1 Thesalonike 5).
Sio kila mara ukiona
MWANGA (NURU) kwenye ulimwengu wa MWILI pia unaona MWANGA kwenye
Ulimwengu wa roho. Ngoja tujifunze kwa Ayubu. “Ndipo Shetani akamjibu
Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira
kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo?
Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika
nchi. (Ayubu 1:9,10). Huu uliku wa ni wakati wa MCHANA (NURU) kwa Ayubu.
Wakati Baraka ziko kila upande, mali, watoto, na mafanikio ya kila
namna. Huku unaouna mkono wa Bwana (ukingo) unakupigania, nk. Ghafla!
Giza nene linatanda! Sasa sio watu wengi sana wanapona hapa. ILA wale
ambao WANAKESHA “watayaona mabaya yakija” (1 Thesalonike 5), na Mungu
wao atawapa DAWA ya KUSHINDA. Kwa sababu wako NURUNI, MLANGO wa KUTOKA
wakati wa KUJARIBIWA kwao watauona.
Mara nyingi sana watu
katika maisha ya kawaida hawajali sana kwa sababu BANK kumenona, wanajua
hata wakifukuzwa kazi LEO hawafi njaa. VITEGA uchumi vimesimama sawia.
Karibia kila kitu kimekatiwa BIMA. Wanaweza kupata MATIBABU mahali
popote duniani. Mambo ni SAFI, hata wakitafuta kwamba SHIDA inaweza
kutokezea wapi hawaoni. Huwezi kuona UMUHIMU wa kukesha na KUDUMU
kumtegemea Mungu kama huna macho ya rohoni na UELEKEVU kwa Bwana kama
Ayubu. Lakini kwa wale ambao wamepitia majanga wanajua nasema nini. Kuna
habari MBAYA hata sipendi kusikia licha ya kusimulia. Utakuta watu
wameokoka tu vizuri, wamebarikiwa kuingia kwenye NDOA. Wanakuwa na
mipango mingi ya maisha na KAZI/BIASHARA zao nzuri ziko sawa. Ghafla!
Wasipotarajia, wameenda wote kazini na kabla ya jioni mmoja ametwaliwa!
Ghafla tu! Status inabadilika, mmoja anaitwa mjane. Adui kashambulia.
Wengine katika hali isiyotarajiwa, watoto wameenda shule, ghafla jioni
hawarudi! Wanapata taarifa waende chumba cha kuhifadhia maiti kukagua!
Hizi ni habari mbaya sana. Lakini haya ndio yalikuwa yanamtokea Ayubu
wakati wa GIZA ulipoanza. Anajigundua hana WATOTO hata mmoja, wamekufa
wote! Hana MALI halafu ni mgonjwa hajiwezi hapo chini. Mke wake naye
analeta mambo magumu ya kumchanganya zaidi. Huu ni wakati wa GIZA.
Kusudi la somo hili ni kukumbusha habari ya KUKESHA. Katika kukesha
kuna kujaa NGUVU na kujiandaa kupambana (Isaya 5). Nguvu za kukuwezesha
kuvuka kwenye GIZA hupatikana wakati wa MCHANA. Maisha ya Ayubu kabla
ya JARIBU ndio yalimwezesha KUSHINDA wakati wa jaribu. Watu wengi sana
wanasubiri MAJANGA (GIZA) ndio wanaanza KUFUNGA na KUOMBA kwa BIDII na
KUKEMEA kwa NGUVU. Sasa kweli wanakemea, ila nguvu iko wapi? “Ukizimia
siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.” (Mithali 24:10). “Wamtumainio
Bwana ni kama MLIMA Sayuni, hawatatikisika kamwe” lakini pia Isaya
anasema “bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu
kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa
miguu, wala hawatazimia.” (Isaya 40:31). KUSUBIRI kunahusianishwa na
tabia ya KUKESHA.
Yesu anaposema “ni rahisi ngamia kupenya
kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia Ufamle wa Mungu” aliona
hii shida KUFANYA mapenzi ya Mungu wakati watu wamezungukwa na kila
kitu. Ndio maana alipomuuliza yule kijana tajiri habari za AMRI za
Mungu, na kijana anasema ameshika ZOTE, maandiko yanasema “Yesu
akampenda”. Kwanini? Sio rahisi kukaa katika Amri za Mungu wakati HELA
inapiga kelele. Ukifanikiwa kumpendeza Mungu wakati una KILA kitu lazima
uwe KIVUTIO kwa Yesu. Sasa, Angalia maisha yako vizuri. Pale mahali
ulikuwa una SHIDA, huna hela na hujui unavukaje, ULIMTAFUTA Mungu kwa
BIDII na kukaa mbali na DHAMBI. Leo Mungu amekuvusha, umemaliza shule
salama, umepata kazi, nafasi na pesa, Ghafla! Unaanza kuwaza KUTENDA
dhambi! Ukiwa kwenye SHIDA kwako ilikuwa MCHANA, sasa Mungu amekubariki
na baraka za Mungu badala ya kuongeza NURU, zimekuwa GIZA! Na chukizo
kwa Mungu. Je! Unataka Mungu akurudishe kule kwenye DHIKI ili taa yako
iwake? Wakati unadhani ni “amani amani” angalia uharibifu uko njiani.
Neno hili linakukumbusha UAMKE na KUCHANGAMKA, rudi kwenye MKESHA na
kuishi kwa KIASI, huku ukimsubiri Bwana. Kuna faida gani “kuupata
ulimwengu wote na kupoteza nafsi yako?” Jijibu mwenyewe na uchukue
HATUA. Mungu akusaidie.
Basi Mungu atuwezeshe kukaa katika KIASI na KUKESHA kwa Jina la Yesu. AMEN
Frank Philip.
Kazi ya UVUVI ni moja ya kazi ambazo zinahitaji uzoefu lakini pia
Imani. Umewahi kujiuliza mvuvi anaposhusha nyavu zake huko chini kwenye
maji ambapo haoni kitu ila anasubiri kwa IMANI akijua samaki wataingia?
Petro alipoambiwa anabadilishiwa kazi kutoka kuvua SAMAKI kwenda kuvua
WATU ilikau inahitaji shule zaidi kidogo ili aelewe somo. Siku moja
Petro akaenda kwa UZOEFU, kumbuka sio
ZIWA/BAHARI au maeneo asiyoyajua, anajua sana na ana uzoefu nayo. Si
akakesha sasa usiku kucha na hakupata kitu! Yesu akaja, akamwambia
“Petro shusha nyavu” na akampa maelekezo ya ziada. Petro akajiuliza,
“nimehangaika usiku kucha ila sikukamata kitu na sasa unasema nishushe
nyavu?”, akapiga moyo konde na kusema, “kwa Neno lako nitashusha”. Hao
samaki aliokamata hakuweza kuvuta nyavu maana ni wengi hadi nyavu
kuchanika! Akasema “ondoka kwangu mimi mwenye dhambi”! Kwanini? [kufanya
kazi ya Mungu bila mapenzi yake ni kosa na itakugharmu].
Sikiliza. Watumishi wengi sana wa Mungu wanahangaikal na KINA na UZOEFU
wa nondo (mafundisho, nyenzo, nk.) wanazotumia na USTADI wa kupiga
MAKASIA. Bila KUSUDI la Mungu utakesha hapo nakutahadharisha. Sio katika
HUDUMA tu ila hata katika michakato ya maisha, biashara, nk. Hakikisha
unashusha NYAVU mahali ambapo unajua YESU amekuongoza. Huwezi kosa
SAMAKI asilani. Uzoefu wako na UJUAJI vitakuponza tafuta KUSUDI la Mungu
katika maisha yako na utaona MATUNDA yakimimnika maishani mwako kama
MVUA. Mafanikio ya Petro hayakutegemea KINA cha maji, AINA ya nyavu,
MTUMBI, UREFU wa MUDA, wala UZOEFU wake! Ila NENO la Yesu! Ukipata Neno
la wakati huo katika MUKTADHA (context) na MAUDHUI (content) na MUDA
(timely), mafaniko yako katika HUDUMA, BIASHARA, KAZI, SHULE, nk.,
yatakua makubwa kuliko kujitahidi kwa NGUVU zako mwenyewe na AKILI zako.
Jifunze kumshirikisha Yesu nawe utaona HATUA atakazokufikisha.
Kumbuka. Mungu hulituma Neno lake “kama mvua ishukavyo kutoka juu
kuangukia ardhi”, na LITATIMIZA makusudi yake, halitarudi bure. Ukijua
Yesu anasema nini juu ya UVUVI wako, sema kama Petro “kwa Neno lako
nitashusha nyavu” halafu tukikutana utanipa ushuhuda. Barikiwa.
Frank Philip
Katika mambo ya muhimu sana kwa maisha ya IMANI, moja wapo ni kujua NIA
yako katika mambo fulani ya kimwili na kiroho. Kwa lugha nyepesi ni
muhimu kujua MOYO wako “unasema nini juu ya jambo fulani” (nimetumia
KUSEMA kwa maana Moyo unatoa sauti ya yale uwazayo mbele za Mungu). Au
kwa lugha nyingine ni vizuri kujua “MTIZAMO wako juu ya mambo fulani”
(Kuna picha/kitu halisi kinajengwa ndani yako na mawazo yako na ndicho Mungu anachokiona).
Sababu ya msingi ya kujua NIA (makusudi ya Moyo) yako ni kupima kiwango
cha MUNGU kuhusika na hayo mambo UWAZAYO/UNAYOHITAJI ambayo mengi
yanapita MOYONI mwako kama MAWAZO tu. Majibu ya maombi yako hayaji kwa
yale mambo ambayo ULIMI wako ulitamka wakati wa maombi, bali yale mambo
ambayo NIA (makusudi ya moyo) yako imetamka wakati wa kuomba. Sasa
unaweza ukafikiri nataka kusema nini hapa ila ukitafakari kwa makini
utagundua kwamba “unaweza kuomba au kunena jambo tofauti na unavyo NIA
ndani yako (unavyo sikia/ona hilo jambo NDANI yako)”. Sikia, “Kwa MOYO
mtu huamini hata akapata HAKI”, ticket ya kupokea inaitwa IMANI, na
hukaa moyoni. Moyo wako ukinena (NIA) kwa imani UNAPOKEA majibu ya
maombi yako! “Kinywa kinapitisha tu yaujazayo moyo wako”!
NIA
yako ikisema KITU tofauti na ULIMI wako unachokisema, katika kuchagua
kati ya haya MAWILI, Mungu anasikiliza NIA (makusudi ya moyo) yako na
sio ULIMI (mambo yatokeayo akilini mwako) wako! Ndio maana Suleiman
alisema “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka
kwa Bwana.” (Mithali 16:1). Haijalishi ULIMI wako umekiri sana mangapi,
je! Nia yako imejipanga sawasawa na KUSUDI la Bwana? Ukitaka MAJIBU
mazuri, maandalio ya MOY O ni wewe unafanya sio Mungu, JAWABU la ULIMI
kwa uombapo ni kazi ya Mungu kujibu.
Kutokana na UMUHIMU wa
NIA (makusudi ya moyo) ndani ya mtu ndio maana “Mungu anachunguza moyo
na kujaribu viuno”. Na katika vitu 6, naam 7 achukiavyo Mungu mojawapo
ni “moyo uwazao mabaya” (Mithali 6:18). Sasa sisi tunapambana na watu
kwa MATENDO au MANENO yao lakini kwa MUNGU hata ULIMI usiposema, MOYO
unasema na Mungu anasikia na KUONA. Yesu akasisitiza, “sio alacho mtu
hunajisi ila kimtokacho”, kwa maana kinatoka ndani ya MOYO na NIA yako
inasema moyo ULICHOKUSUDIA kufanya. Kabla dhambi haijafanyika kwa jinsi
ya mwili, ilianza kufanyika ndani ya moyo wako kisha UNAITIMIZA kwa
MAKUSUDI ya MOYO wako (NIA).
Jifunze kudhibiti NIA yako kwa
sababu hapo ndipo penye NGUVU ya kushinda au kushindwa kwako. Kama
unataka kufanikwa zingatia “kulinda sana moyo wako kuliko vyote
ulindavyo”. Watu wengi sana wanasahau kwamba MAWAZO ya mioyo yao
yanapiga KELELE kwa SAUTI japo ULIMI haujasema kitu! Kwa Mungu hayo
mawazo yanapita kama PICHA/SANAMU ndio maana Mungu anasema “umechukua
vinyago na kuvitia moyoni”, yaani kule ndani yako Mungu anaweza kuona
OBJECTS au PICHA japo wewe UNAWAZA tu. Yesu akasema “amwangaliaye
mwanamke kwa kumtamni MOYONI mwake amezini”, sasa kila mtu anajua tamaa
ni kama WAZO tu ndani ya mtu ila Mungu akiangalia kama umefuga hayo
mawazo, Yeye anaona KITENDO/SAUTI/PICHA/SANAMU! Ndio maana Mungu anasema
“anachukia MOYO uwazayo mabaya” kwa sabubu kwake ni VITU HALISI kuliko
sisi tunavyofikiri na mara nyingi tunapuuzia tu.
Mungu
alipomtokea Sulemain na kumwambia aombe kitu chochote, NDANI ya Sulemani
kulikuwa na MENGI ila aliomba KUSUDI la Mungu juu ya KAZI aliyoitwa
kufanya ili AMPENDEZE Mungu. Jambo hili LIKAMPENDEZA Mungu. Nataka uone
kitu cha tofauti hapa. Usije ukafikiri Sulemani alikuwa na AKILI sana
ndio maana ALISEMA hivyo. KUMBUKA, ilikuwa ni NDOTO tu! (1 Wafalme 3:8).
Kila mtu anajua kwamba tukilala hatutumii AKILI kama tukiwa macho, sasa
Sulemani aliwezaje KUOMBA kitu sahihi kwenye NDOTO? Inamaana MOYO wa
Suleiman ulikuwa UKITAMANI kumpendeza Mungu (alikuwa na NIA) ambayo
Mungu alipomtembelea japo ULIMI wake haukunena, NIA iliyoko ndani yake
ILINENA na Mungu akajibu.
Ukisoma sehemu nyingine Bwana
anasema “niko pamoja nanyi katika mipango yenu, KABLA ya kuomba mimi
Bwana nitajibu, na mkiwa katika KUNENA nitasikia”! Sasa watu
watakubaliana na mimi kwamba kila mmoja wetu huwa ana mipango ndani ya
MOYO. Ukiwa na NIA (makusudi ya moyo) safi mbele za Mungu, hiyo MIPANGO
yako katika MAWAZO yako, Mungu anasema NINASIKIA! Kabla HUJAOMBA, Mungu
anajibu! Ukisoma kitabu cha Ayubu utaelewa vizuri NGUVU ya mawazo yako.
Tunaambiwa Ayubu “hakumwazia Mungu kwa upumbavu”. Hili ni jambo KUBWA na
Ibilisi amelificha kwa watu wengi ukiangalia ndani yao ni MAWAZO
machafu tu na kuwaza vitu vya AIBU na wao hawajui kwamba mambo mawili
yanatokea: i. Moyo wako unakua chukizo kwa Bwana ii. Unadhoofisha
kiwango cha kupokea majibu ya maombi yako kwa maana MOYO wako unanena
tofauti na ULIMI wako. Umepoteza UELEKEVU! “Na macho ya Mungu
yanakimbia-kimbia diniani kote, anatafuta huo uelekevu ndani yako ili
ajionyeshe mwenye NGUVU”
Petro akasema “kwa hiyo VIFUNGENI
VIUNO VYA NIA ZENU, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile
neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii
msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu” (1Petro1:12,13).
Hapa napata picha kwamba tunaweza KUAMUA kushughulika na NIA zetu na
kizidhibiti, ndio maana tunaambiwa TUZIFUNGE NIA zotu viuno na kua na
kiasi!
Kuna maswali mengi huwa najiluza. Hivi Mungu
akiniangalia huku ndani ANAONA nini? Watu wengi sana utawakuta wamepiga
MAGOTI kwenye IBADA kanisani/sehemu mbalimbali, lakini ndani ya MIOYO
yao kwa kweli WAMESIMAMA. Jiulize tu, kwamba kweli kuna UWIANO
(synchronization) kati ya USEMAYO, UTENDAYO na UWAZAYO? Watu hawatuoni
lakini nakwambia kuna watu MIOYO yao inavurumisha matusi kwa nguvu kama
wafanyavyo wavuta bangi. Sawa, watu hawasikii lakini nakuhakikishia leo
Mungu wako anasikia SAUTI! Basi AMUA leo, katika dunia hii iliyojaa UOVU
na HARUFU ya UVUNDO inayopanda kwa Mungu kila siku, wewe uwe MANUKATO
na KITU cha kupendeza Mungu anapo CHUNGUZA moyo wako. Jifunze KUMBARIKI
MUNGU kwa MAWAZO ya MOYO wako. Ukifanikiwa hili Mungu atajibu HAJA ya
MOYO wako kabla hujaomba kwa sababu NIA yako husema kwa SAUTI mbele za
Mungu.
Ukitaka kujua UMEFANANAJE mbele za Mungu, angalia
NAFSINI mwako, kile kitu unachokiona ndani yako NDIVYO ULIVYO mbele za
Mungu, kwa maana imeandikwa "mtu aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo".
Roho Mtakatifu tusaidie. AMEN.
Frank Philip.
Kama kuna kitu unahitaji kujua kama Mkiristo ni kuomba VIZURI.
Wanafunzi wa Yesu walimwomba Bwana awafundishe kuomba kwa maana waliona
wanafunzi wa Yohana wanavyoomba wakajua lazima kuna namna ya kuomba na
sio kufurumuka tu na maneno bila utaratibu (Luka 11).
Kama kuna swali gumu nilikuwa najiuliza ni hili la kuomba kwa muda mrefu. Yesu anasema “KESHENI mkiomba msiingie majaribuni”,
sehemu nyingine anauliza “hamkuweza kukesha nami hata saa moja tu?”.
Katika Agano la Kale utaona neno “WALINZI” limetumika. Bwana anasema
“Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana
wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya” (Isaya 62:6).
Sasa kwa WAOMBAJI watajua hii lugha ya “KUMKUMBUSHA” Bwana maana yake
ni nini. Unapoomba sio kwamba Bwana hajui, unamkumbusha tu, ndio maana
“Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama
itupasavyo”. Sio tu kwamba hatujui kuomba ila hata cha kuomba mara
nyingi hatujui hadi Roho atusaidie. Kumbuka, unapoomba hutakiwi kukaa
kimya hadi utakapoona majibu ya maombi yako. Hii TABIA ya KUDUMU/KUKESHA
katika maombi imejirudia tena wakati Yesu anafundisha wanafunzi wake
FAIDA za kuomba BILA KUKOMA. Yesu “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa
kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na
kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji
huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema,
Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema
moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa
mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa
kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na
Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku,
naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:1-8).
Nilinachotaka uone hapa ni aina ya UOMBAJI unaotakiwa na jinsi unapaswa
kujipanga na kuwa na nguvu za kuomba kwa muda mrefu. Nitakupa moja ya
SIRI muhimu za kukusadia kuwa na nguvu za kukusukuma angalau muda zaidi
kidogo katika maombi.
Kuna mambo mawili nataka uone. La kwanza
ni BIDII na la pili ni MUDA. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na
kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba
kwa BIDII. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba
kwa BIDII mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka
mitatu na miezi sita.”(Yakobo 5:15,16). Ukiona mtu “anajifanya” eti
anatamka neno “moja tu” na mambo yanatokea, anataka kuonyesha kwamba
yeye yuko juu sana na karibu sana na Mungu na miujiza ni kama tu switch
ya umeme, ON/OFF matatizo kwisha! Huwa najiuliza swali hili, je! Huyu
jamaa huwa anakesha na kuomba sana na sasa anamalizia tu kile alichokuwa
ameomba/anomba kwa muda mrefu? Na kama sio mwombaji, je! Hii nguvu ya
ON/OFF na huku ameshika kiuno imetoka wapi? Naishia hapo. Usifike mahali
ukaona watumishi wa Mungu wanatumika kwa mtindo ambao hujawahi kuona
ukakimbilia kusema ni PEPO. Utaingia kwenye matata MAKUBWA kama ni Mungu
kweli anawatumia. Lakini pia UJUE sio kila atendaye MIUJIZA anatoka kwa
Mungu.
Biblia inasema Eliya aliomba kwa BIDII! Sasa wewe
unasema hapa ni kuamuru tu mambo kama ON/OFF na huna TABIA ya kukesha
kwenye maombi! Kumbuka Yesu aliamuru mambo kwa mtindo huu, just ON/OFF
mambo yanatokea, wanafunzi wake wakajitahidi kuiga, “IKAGOMA”!
Wakamwendea wakamuuliza “mbona sisi inagoma?” Yesu akasema “mambo
mengine hayawezekani ila kwa KUFUNGA na KUOMBA”. Tunasoma kwenye
maandiko kwamba Yesu alikesha milimani akiomba na asubuhi anaingia
hekaluni kuhudumu. Anasema “sifanyi kitu ambacho sikumwona Baba yangu
akifanya!” Swali je! Aliona saa ngapi? Kama Yesu ALIFUNGA na KUOMBA,
halafu wewe HUTAKI kujifunza tabia hii na unataka tu usimame kama
“AFANDE” na kutoa tu ishara kwa mkono mambo yanatokea, watu wanarushwa
huku na kule. Jua unakaribia MAHALI pa GUMU.
Hatua SABA za
maombi zitakusaidia kuomba kwa MUDA mrefu. Kumbuka siku zote MAOMBI
hayaendi bila NENO. Ukitaka kufanikiwa kuomba ni LAZIMA uwe msomaji wa
NENO pia. Jipe angalau milango (chapters) 2 kwa siku. Asubuhi na jioni
au muda wa kusubiri (ukiwa kwenye gari, bank, nk.) Hizi hatua SABA sio
ubunifu wangu ila ni SALA ya BWANA.
Hatua ya kwanza: Liitie Jina la Bwana wa Majeshi.
Yesu alisema “mkiomba neno LOLOTE kwa Jina langu nitafanya”. Pamoja na
kwamba Daudi alimkabili Goliath kwa kombeo, fimbo na jiwe, alitumia
“Jina la Bwana”. Hiyo ndio siri ya ushindi wake. Sehemu nyingine Daudi
akasema “hawa wanataja magari na farasi lakini mimi nitalitaja jina la
Bwana Mungu wangu”. NGUVU zako za kuomba na MAFANIKIO ya uombayo yapo
katika Jina la Yesu.
Sasa, unaposimama na kuanza “Baba
yetu/yangu uliye Mbinguni. JINA lako LITUKUZWE”. Jiulize, litukuzwe na
nani? Kama ni wewe basi anza kulitukuza jina la Bwana. Usikurupuke na
kuanza tu kukemea pepo bila utaratibu hapo, No! Mtukuze Mungu kwanza.
Kukemea ni hatua ya 6 huko mwisho wakati umeshajaa NGUVU. Yesu akasema
“huwezi kuchukua vitu vya mwenye nguvu mpaka umemfunga kwanza”. Sasa
unamfungaje mwenye nguvu wakati huna NGUVU?
Watu wanajiuliza
sasa nitamtukuzaje Mungu? Sikiliza. Wana wa Israel walipovuka mto
Yordani na maji yakatindika mbele yao, waliambiwa waokote mawe 12 hapo
mtoni wayaweke iwe ukumbusho huko mbele kwamba “Mungu alifanya matendo
makuu”. Mungu anapenda hiki kitu. Taja “matendo makuu ya Mungu” yoyote
unayoyajua huko kwenye Biblia, mshangilie na kumshukuru kwa sababu ya
UWEZA na NGUVU zake. Unavyozidi KUZAMA katika kutafakari na KUTAJA
matendo makuu ya Mungu, taratibu utagundua kuna kitu kinatokea, unaanza
kujaa CHARGE! Unavyozidi kutaja na kumtukuza Mungu, NGUVU inaongezeka na
unaanza kuwa mwepesi ghafla. Hii hatua ukipita vizuri, inakupa NGUVU ya
kusogea hatua ya 2.
Hatua ya pili: Ita Ufalme wa Mungu.
Hakuna ufalme usio na mfalme! Ndani ya MFALME kuna MAMLAKA na NGUVU.
Sasa unapoita Ufalme wa Mungu uje, kimsingi umeagiza MAMLAKA za Mbinguni
zishuke kukuhudumia wewe na mambo unayoyaombea. Ndani ya ufalme wa
Mungu kuna KILA kitu unachokitaka. Mahitaji yako yote yanapatikana humo.
Lakini jipange na MOYO wako vizuri maana ukiomba vitu kwa tamaa yako
hupati kitu (fuatilia somo kwenye “Mafundisho ya Neno la Mungu LIKE
page” lenye kichwa “Jinsi ya kumwona Mungu akijidhihirisha kwako”).
Jifunze kwamba NENO la Mfalme ndio NENO la MWISHO. Huwezi kumfundisha
Mfalme chakufanya kama hataki. Wewe UNAMSIHI kwamba MAPENZI yake
yatimizwe . Ukifika hapo unaingia hatua ya 3.
Hatua ya 3: Jua Mapenzi ya Mungu kwa unachokiombea.
Mapenzi ya Mungu yapo katika NENO la Mungu. Huwezi kupokea kama unaomba
pasipo IMANI. Na tunajua kwamba “imani huja kwa kusikia, na kusikia
huja kwa NENO la Kristo”. Sasa ukiwa na Neno la Mungu juu ya “hicho”
unachoombea, jua una mtaji wa IMANI. Sasa kumbuka. Unapoenda mbele za
Mungu uwe kama yule mama mjane ambaye alienda BILA KUCHOKA,
“akirudi-rudi kudai haki yake” (Luka 18). Ukijua AHADI zako na NENO juu
ya kitu unachoomba, kaa hapo usiondoke, omba na dai ahadi yako kwa UPOLE
na UNYEYEKEVU mbele za Bwana, tena bila kuchoka (usipayuke kama mtu
asiye na imani). Ukirudi-rudi hadi upokee kumbuka siku zote, “Mungu
huliangalia Neno lake akalitimize, na Yeye hulituma Neno kama mvua
ishukavyo juu ya Nchi, Litaenda (halikosi shabaha) kwa YALE mambo
aliyoliagiza na halitamrudia bure”. Hakuna faida kama unajua KITU
unachoomba kipo kwenye MAANDIKO. Hapo ndio nguvu na mafanikio yako
yalipo. Kama una jambo “nyeti” unataka Mungu akutendee, hakikisha
unachukua kalamu na karatasi na unatafuta mistari ya KUSIMAMIA. Imani ya
KUPOKEA uombacho imejikita katika UFUNUO wa hilo Neno.
Hatua ya nne: Omba mahitaji yako.
Maombi ya unachokihitaji yamejengwa kwenye hatua ya 3 hapo juu.
Unapoomba RIZIKI au mahitaji mbalimbali ya mwilini na rohoni, kwako au
kwa mtu mwingine, yote yamejikita katika MAPENZI ya Mungu ambayo
unayapata katika Neno. Neno hilo hilo linakupa imani ya kupokea majibu
ya maombi yako. Sasa kumbuka siku zote kwamba majibu ya maombi yetu yako
ya aina mbili tu. NDIO au HAPANA! Jifunze kwamba hata HAPANA imo katika
mapenzi ya Mungu pia. Mungu anakuwazia mema siku zote, hakunyimi kitu
bila SABABU. Na imetupasa kumshukuru Mungu katika Mambo yote. Kama
tumepokea au hatujapokea yote ni mapenzi ya Mungu kwetu. Ukisikia mtu
anakuhakikishia kwamba “LAZIMA” jambo fulani litatokea kwa MUDA anaotaka
yeye, jiulize swali hili, Je! Mungu alimhakikishia hilo jambo kwa namna
hiyo? Na kama hajahakikishiwa na Mungu, jiulize tena swali hili, je!
Ukiri tu ushindi NJE ya MAPENZI ya Mungu ili “kumpinda” Mungu afuate
matakwa yako? Ukijua majibu, jifunze UMUHIMU wa kujipanga kwenye mapenzi
ya Mungu na KUMSHUKURU kwa KILA jambo.
Hatua ya tano: Toba.
Hii hatua huwa inakuwa ya tano kama tu wewe unadumu katika maombi muda
wote, ila mara nyingi sana inakuwa ya kwanza pia. Mungu ni mtakatifu,
“ujasiri wa kukariba Kiti cha rehema tunaupata katika Damu ya Yesu tu”
mara nyingi sana ukianza kuomba unaweza KUSUKUMWA kujitakasa.
Sizungumzii hii hatua ya kujitakasa ambayo inaweza kutokea mwanzo wa
maombi. Nazungumzia hii hata ya 5 ambayo sasa unazama kwenye TOBA kwa
UPANA wake. Hii hatua ukiifaya vizuri itakuwa ni UFUNGUO wa matatizo
mengi sana na KIPOKELEO cha maombi yako. Yesu anaagiza “kila tusimamapo
kusali tusamehe ili na sisi tusamehewe”. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo
yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa
yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya
mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe
ninyi makosa yenu.]” (Marko11:24-26). Ili uweze KUPOKEA jifunze
KUACHILIA watu waliokukosea/wadeni wako! Nakwambia jitahidi KUSAKA
“huko” ndani yako KILA mtu ambaye ukimuwaza moyoni unasikia UCHUNGU na
ukimpata, MSAMEHE na KUOMBA kwa ajili yake hadi upate UHURU. Kama bado
una FUNDO ukimuwaza huyo mtu jua BADO hujavuka hapo hatua ya tano. Watu
wengi sana wameshindwa “kupokea wanayoamini” (Marko 11) kwa sababu
wameshindwa kuvuka hatua ya tano! Omba NEEMA ya KUSAMEHE kama inakuwa
Ngumu na Yesu atakusaidia kumsamehe Mtu. Kama Yesu aliweza kuwasamehe
WALIOMSULUBISHA katikati ya mijeledi, misumari, taji ya miba na
kuangikwa msalabani huku anatukanwa na kutemewa mate, wakati yote
yanaendelea ANAWASAMEHE na kumwomba Baba awasamehe! Yaani anapigwa, ila
yeye yuko kwenye maombi! Huyu Yesu anaweza kukupa NEEMA hii ya KUSAMEHE
mwenzako kwa faida yako WEWE mwenyewe KUVUKA hatua nyingine.
Hatua ya sita: Shughulika na ADUI.
Watu wengi sana wamejifunza njia moja tu ya kushughulika na Ibilisi.
Kila mmoja yuko busy KUKEMEA kwa Jina la Yesu! Sawa, ni muhimu lakini
nataka ujifunze Neno hili. Yesu alimwona Petro jinsi anakavyo mkana
kabla hajamkana! Hakikumsumbua Yesu kwa sababu “huko” katika MAOMBI yake
alikwisha omba kwamba “imani ya Petro isitindike wakati Ibilisi
anampepeta kama ngano”. Yesu hakumkemea Ibilisi “asimpepete Petro ila
aliomba Petro ASIANGUKE kwenye hilo JARIBU na akisimama awasaidie
wenzake”. Majaribu ni package (kivunge/kifurushi) sio kitu kimoja. Sasa
ukiwa na utaalamu wa kukemea kuna kitu kwenye hicho kifurushi kitakuwia
kigumu. Kifurushi cha jaribu kina mambo makubwa matatu. Kwanza,
jambo/kitu utakachojaribiwa nacho. Pili, kitakachotokea wakati unakutana
na hicho “kitu” (kupepetwa kama ngano) na tatu, kusudi la jaribu.
Ufanye nini baada ya jaribu (simama na imarisha wenzako). Hakuna
mwanadamu atakemea MAJARIBU yasije maana majaribu yamo katika mapenzi ya
Mungu. Unapaswa kutambua mambo haya matatu kwa makini sana: jaribu
(kitu kinachokujaribu), namna ya kujaribiwa, na kusudi la jaribu. Sasa
ukikazana tu na kukema huwezi kufanikiwa kila kitu kwa maana katika hilo
jaribu, japo ni Ibilisi anakujaribu lakini ni Roho Mtakatifu katoa
kibali kwa KIPIMO! Na huwezi kumkemea Roho Mtakatifu kwa maana ndani ya
hilo JARIBU kuna KUSUDI la Mungu!
Kumbuka aliyempeleka Yesu
Nyikani kujaribiwa hakuwa Ibilisi. Alipelekwa na Roho Mtakatifu! Sasa
nataka ujifunze KUOMBA na sio KUKEMEA tu! Omba Mungu kwamba “usianguke
majaribuni na uokolewe na yule Mwovu”. Jifunze kumshinda Ibilisi kwa
Maombi sio kumkemea tu. Mara nyingi sana ukikuta mambo magumu na
unawekwa kwenye “kona” badala ya kukemea pia unamwambia Ibilisi
“imeandikwa”, halafu unamsomea msitari wa Biblia na Ibilisi anaachilia
mara moja! Kumbuka “nao wakamshinda kwa Damu ya Mwana-kondoo na NENO la
ushuhuda wao”, Neno lina nguvu ya kumshinda Ibilisi. Kwanini? Yesu ni
Neno! Na tumehakikishiwa kwamba ni “aheri dunia iondoshwe kuliko yodi
moja ya andiko kuondoshwa”. Sasa unaweza kuona kwamba hakuna UJANJA
ibilisi anaweza kufanya kushindana na Neno la Mungu. Kwa mfano ni rahisi
Ibilisi kuangamiza dunia ila sio Neno la Mungu! [japo dunia inalindwa
na hakuna uharibifu wa kuangamiza dunia yote ambao utatokea kama Mungu
hajaruhusu. Kumbuka agano la upinde wa mvua, nk. hii dunia imewekwa
akiba..]
Hatua ya saba: Rudisha Utukufu kwa Mungu.
Hii
hatua ni ya muhimu sana kama hatua nyingine zilizotangulia. “kwa kuwa
wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”. Ulianza na
“Jina lako Litukuzwe” na kuita “Ufalme wa Mungu uje”, sasa
ukishahudumiwa na Mfalme na kuamini kwamba KILA ulichoomba kimesikika
kwa Mfalme sasa lazima utoe HESHIMA kwa Mfalme! Unamalizia kwa kusema
“kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”
Kumbuka kumshukuru Mungu kabla ya kupokea uliyoomba kwa sababu “imani ni
hakika ya mambo YATARAJIWAYO na ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana”.
Mambo yatarajiwayo maana yake hujayapata ila UNAJUA yanakuja. Haya mambo
yakiwa BAYANA unapata ujasiri wa KUKIRI kwa maana una UDHIHIRISHO wa
NDANI kwamba umepokea ulichoomba. Usiiishie hapo, rudi-rudi kama yule
mama mjane, kukumbusha hadi uhitimishe maombi yako kwa kuona sasa kwa
jinsi ya mwilini jambo limetokea.
HITIMISHO
Kama
utakuwa umefuata hizi hatua saba, na kujimimina utagundua kumbe saa
nzima imeisha na unataka kuendelea kuomba. Fanya mazoezi halafu unipe
ushuhuda. Najua hutaanza kupiga masaa tu kwa mara moja, ila angalau
utavuka hatua kwa hatua.
Jambo la muhimu sana la kujifunza
katika maombi ni juu ya MAHALI na MUDA. Watu wengi sana wamesindwa
kuomba kwa sababu ya kufungwa na MAHALI na/au MUDA. Ukijifunza kuomba
kila mahali, ukitembea, ukipika, ukifua, ukiwa darasani, ukiwa safarini,
nk., utagundua unaweza kuombea mambo mengi sana kwa siku na kurudi-rudi
kwa Mungu mara kadhaa “kumkumbusha jambo” kwa sababu huhitaji
kujifungia mahali. Kama unaweza kuomba kwa “kunena” ni nzuri sana hasa
unapokuwa katika michakato ambayo inachukua attention yako. Mtume Paulo
anatufundisha kwamba tutumie mbinu zote mbili. Kuomba kwa lugha na kwa
akili pia. “usikae kimya usiku wala mchana” (Isaya 62) usifungwe na
muda.
Ukisikia unasukumwa KUFUNGA, fanya hivyo kwa kipimo cha
mambo unayojihusisha nayo kama umetingwa na KAZI au aina ya MAJUKUMU
yanahitaji sana nguvu za mwili. Ikiwezekana jipe siku malumu katikati ya
wiki na kama kazi yako inahitaji nguvu nyingi za mwili jaribu kufanya
maombi ya namna hii wakati wa mapumziko ya wiki, nk. Kila mtu afanye
kama Roho Mtakatifu atakavyomongoza.
Neema ya Bwana wetu Yesu na izidi kwenu mnapojifunza na KUYATENDA haya. AMEN.
Frank Philip.