Saturday, January 26, 2013
HII NI TAARIFA YA MWIMBAJI WA KITANZANIA WA NYIMBO ZA INJILI "RACHEL SCHARP" ANAYEISHI NCHINI SWEEDEN KWA WATANZANIA WOTE KUPITIA VYOMBO VYA HABARI WEEKEND HII!!
Press release
KARUBUNI sana wanahabari katika hafla yetu hii fupi yenye lengo la kumpa Mungu wetu utukufu.
Mimi ninaitwa Rachel Scharp, ni Mwimbaji wa nyimbo za Injili, ninaishi Malmo, Sweden. Lakini kwa
sasa nipo nyumbani kwa ajili ya utambulisho wa Albamu yangu ya Muziki wa injili.
Uimbaji kwangu ni maisha kwa kuwa nilianza kuupenda muziki na kuimba kuimba nikiwa mdogo sana,
nilikuwa nikitunga nyimbo na kuwafundisha wadogo zangu. Tuliimba nyimbo hizo jioni, haswa kipindi
kile cha ugawaji ikiwa zamu ya Kaya yetu, ile foleni ya kununua mchele ilivyokuwa ndefu chakula
kilikuwa kinachelewa, ili wadogo zangu wasilale bila kula na furaha ya kusubiria ubwabwa na maharage
basi tunaimba kusubiria msosi, Wakati huo hakukiuwa na Tv. kama ilivyo sasa.
Niliimba Kwaya ya shule pale “Jangwani Secondary” pia niliongoza sifa na kuabudu Kwenye fellowship
katika kanisa la Msewe Lutheran . Nilikuwa nikiandika nyimbo nyingi nikitegemea kupata fursa ya
kurekodi au kuimba na Kwaya nyimbo zangu, lakini sikupata fursa hiyo.
Kwa sasa ninaimba Kwaya kanisa la Elim Pentecostal huko Malmo kusini mwa Sweden, ninaongoza sifa
na kuabudu. Ninaimba pia kwenye kundi linaloitwa Shalom International ambalo ni muunganiko wa
waimbaji kutoka makanisa mbalimbali ya kiroho yaliyopo mjini Malmo. Nilipata fursa ya kurekodi album
yangu ya kwanza mwaka 2008 ikazinduliwa huko Sweden, Mai mwaka, 2009 nikisindikizwa na dada
Upendo Kilahiro. Album hiyo niliita 'Naringa na Yesu' yenye nyimbo 9, iko Kwenye mfumo wa sauti tu.
Leo ninatambulisha album yangu ya pili yenye jina la 'Ni Mungu wa ajabu'. Album hii Ina nyimbo kumi
zilizo Kwenye mfumo wa sauti (audio), na 8 Kwenye mfumo wa picha na sauti (DVD).
Nimerekodi album hii Oktoba mwaka 2011 nchini Sweden, kwa upande wa mpangilio wa vyombo na
muziki nikisaidiwa na Paalab Nyarko, kutoka Ghana na producer Zolile Matikinga(Zorro) - kutoka South
Afrika.
Mwanzoni mwa mwaka 2012 niliongeza baadhi ya vionjo vya muziki kwenye studio za New Life band
Arusha, vionjo nilivyoingiza ni gitaa la solo lililopigwa na Godlucky Matingisa wa New life band Arusha,
Base Gitaa limepigwa na Wilsson Godfrey Mtangoo. Ngoma zilipigwa na Fujo Makaranga . Na sauti pia
niliingiza hapo Arusha nikisaidiwa na Jackson Benty, chini usimamizi na uangalizi wa producer Wilsson
Mtangoo. Mwalimu wa sauti mchungaji David Nkone.
Video imerekodiwa na UMU production Arusha chini ya uongozi wa Jojo Jose Mwakajila. Video hii
imerekodiwa Sweden (Malmo), Ujerumani (Berlin), Tanzania (Dar es Salaam, Bagamoyo, Arusha ,Moshi,
Serengeti).
Midundo ya nyimbo hizi ni ya kiasili (kitamaduni), Napenda nyimbo zenye vionjo vya Kiafrika na
kitanzania zaidi. Nimeimba kwa kiswahili na kiingereza pia. Na nyimbo nyingi ni za kiswahili, hii
haimaanishi kwamba soko liko nchi wanazoongea kiswahili tu. cha kushangaza ni kwamba pia nch za
Scandinavia wanapenda sana kiswahili na kukithamini, na nafikiri kuliko hata sisi wenye lugha.
Wanasema kwamba ni lugha yenye sauti tamu nami sina budi kujivunia na kuiendeleza na huku
nikimsifu Mungu na kupeleka ujumbe kwa Watu wake.
Nyimbo hizi zimebeba jumbe mbalimbali, kuna za kumsifu Mungu na matendo yake makuu, kuna za
maonyo na kuna za kutia moyo kwa safari hii ngumu ya kwenda mbinguni.
Ningependa sana watu wapate ujumbe huu na wakutane na Mungu katika maeneo hayo tofauti kama
nilivyoeleza mwanzoni kuwa kuna kumsifu na kumwabudu Mungu, kuonywa na kutiwa moyo pia.
Inategemea mtu yuko kwenye hali gani na ana mahitaji gani.
WITO WANGU KWA JAMII
kwanza ni kupenda na kuthamini kile tulicho nacho Mungu alicho tupatia.
Kwanza kwa sisi wakristo tumepewa Neema hii ya wokovu tunatakiwa tuipende, tuithamini, tuitunze na
tuiendeleze, tusiichezee na tuwafanye wengine pia waijue na waipate.
Kama tusipoipenda, tusipoithamini, kujivunia na kuilinda, wengine hawatajua thamani yake.
Nikaja kwenye jamii yetu kwa sasa tunapenda sana kuiga kutoka nje tunaacha ya kwetu, sikatai kuiga
yale yaletayo maendeleo, na tunahitaji kujifunza kutoka kwa walioendelea, lakini si kwamba tuvipuuzie
vya kwetu. Kuna vyetu vinavyohitaji mwendelezo.na tena vikawa vizuri sana na wa nje wakaiga kutoka
kwetu. Kwa Mfano; muziki wetu , lugha yetu na vingine vingi.
Kwa upande wa muziki, watanzania siku hizi wanapenda sana muziki kutoka Afrika kusini, ni mzuri sana
hata mimi napendezwa nao. Naona sasa waimbaji wengi wanapenda kupiga mtindo huo. Ule ni muziki
wa asili wa ngoma zao za kienyeji ukawekwa/ukaongozewa vionjo vya kisasa.
Sasa na sisi tutakapopiga muziki huo hautakuwa mzuri kama wanavyopiga Joyous Celebration kwa kuwa
ndio asili yao. Swali ni kwamba, kwa nini na sisi watanzania tusitengeneze lizombe letu au Mdumange au
Sindimba na hata Mdundiko tukaweka vionjo vya kisasa ukawa mzuri tu na wao waige kutoka kwetu?
Nilazima tujitahidi jamani tuwe na utambulisho wetu (identity). Kwamba ukisikika muziki uutambue
mmmh Huu ni muziki wa Tanzania, tunahitaji ubunifu tu kuondoa uvivu wa kufikiri. Kama tukitulia na
kubuni na kutumia vipawa tulivyopewa na Mungu tutafika mbali sana na sio kupita njia ya mkato ya
kuiga tu.
Namalizia kwa kuwaambia watanzania, tusiende kwa mazoea eti watu wamezoea hivi. Huu ni wakati wa
mabadiliko, tubadilike turudi kwetu. Tutafika mbali. watanzania tunaweza, na kuleta mabadiliko ni mimi
na wewe.
Asanteni sana kwa kuja kushiriki pamoja nami tukio hili la Baraka. Mungu awabariki sana.
Rachel Scharp
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
WAIMBAJI WOTE WA AFRIKA YA MASHARIKI WANAHITAJI UJUMBE HUU.
ReplyDeleteNI KWELI KABISA,UJUMBE HUU UNAPASWA UWAFIKIE WOTE AMBAO WANAMAANISHA KUIFANYA KAZI HII NA IKIWA WAMEKUSUDIA KUUFIKIA ULIMWENGU WOTE!!
ReplyDelete