
Leo nataka niseme juu ya KILIO. Kuna tofauti ya kulia kwa machozi ya
nje na kulia kwa machozi ya ndani. Mtu anapotendewa kitu na ndani yake
akasikia KUNYANYASIKA na akasikia uchungu sana, mara nyingi anatoa
machozi ya nje (atalia). Lakini sio kila mara mtu atalia kwa machozi,
ila kuna ule UCHUNGU wa ndani ambao watu mbalimbali wamekua nao na
wameenda mbele za Mungu kwa maombi au
hata wametamka tu maneno na Mungu AMESIKIA (“nipo pamoja nanyi katika
mipango yenu, kabla ya kuomba mimi Bwana nitasikia na mkiwa katika
kunena mimi Bwana nitajibu”). Chunga hii kitu, Mungu anasikia KILIO
kuliko unavyodhani. Na mara nyingi sana hiki KILIO hata kama mtu sio
mlokole nakwambia UKIMDHULUMU, UKIMNYANYASA, UKIMTENDA JEURI mtu na
akalia kwa UCHUNGU mbele za Mungu hata kama hakumwambia mtu au hata kama
hajui kama Mungu anasika, nakwambia Mungu husikia VILIO.
Wakati Mungu anamtokea Musa na anamtuma Misri kuwakomboa wana wa Israel
kutoka UTUMWANI, Mungu alisema “nimesikia kilio chao nami nimeshuka
kuwakomboa”. Mungu hakusikia maombi bali KILIO! Sasa ninataka uone huu
mfumo vizuri. Pale Misri wana wa Israel walikua watumwa, na juu yao
kulikua na VIONGOZI na WASIMAMIZI na kule juu kabisa alikuwepo Mfalme
Farao. Kiutawala hawa watumwa walikua chini kabisa, ila walikua WANA wa
MUNGU aliye hai. Kumbuka “hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na ile
iliyopo imeamriwa na Mungu”. Kwa lugha ya kawaida BOSS mkubwa sana
katika “utawala wowote” hapa duniani ni Mungu. Sasa kama mtu mwenye
HAKI, amefika mahali pa gumu sana na amelia kwa MATESO mbalimbali, akiwa
hajui huu mfumo bado BOSS mkubwa hushuka hapo na kurekebisha mambo,
haleluya! Kwa wale wanajua hii SIRI na kusimama katika nafasi na zamu
zao vizuri, HAWATAMSUJUDU boss wao wa duniani na kufanya NGONO, nk., na
kumkosea Mungu kwa sababu ya kulinda MASLAHI yao ya kikazi. Watapambana
kwa “NIA ya kushinda UOVU na KUTII kwao kutakapotimia MAMLAKA yao katika
ulimwengu wa roho dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wa baya
ITAONGEZEKA sana”. Na KILIO chao Mungu atasikia na ATASHUKA kuwaokoa.
Kumbuka, Mungu ndio boss mkubwa pale juu ila maandiko yanatuonya TUTII
mamlaka iliyo kuu. Na usithubutu kumwambia kiongozi wako kuwa wewe sio
boss ila boss ni Mungu. Jua hilo moyoni na mtizame Mungu kama Mkuu wako
wa kazi na chapa kazi kwa moyo, acha uvivu.
Nebkadneza mfalme
wa Babeli alikwenda kula majani miaka/misimu 7 kwa kosa la kujisifia
kwamba “huu mji ni mkono wangu umejenga?” Akatizama mafanikio ya Ufalme
(kampuni yake) akajiinua ndani ya moyo wake! Mungu akasema sasa utajua
kwamba mimi natawala pamoja na wanadamu, sio wewe Nebkadneza, ni Mimi!
Hii siri watu “wachache” wanaijua na wamehusika kuwapiga “transfer”
(uhamisho) mabosi wao kwa sabababu wameleta shida kwenye KAMPUNI na jina
la Mungu linatukanwa au watu wamenyanyaswa. Transfer inaweza kuwa
kulala, kushushwa cheo (kula majani), kuhama kituo cha kazi, nk. Ila
vita vyetu sio juu ya DAMU na NYAMA. Ni katika roho, na tunapata NGUVU
tukiwa na NIA thabiti ya kupinga UOVU wote na KUTII kwetu
kutakapotimilika (2Kor. 10:4-6). CHUNGA sana usije ukafanya mambo kwa
HUSUDA, WIVU au MASHINDANO, utashindwa. Mamlaka ya Mungu haifanyi kazi
hapo. LAZIMA usimame katika KWELI na HAKI na sio maslahi binafsi.
Usikubali kumkosea Mungu kwa kisingizio eti “sasa huyu ni MHESHIMIWA na
mimi ningefanya je?”, mwite Yesu hapo akuokoe na KILA (hata kama sio
mlokole) atakayeliitia jina la BWANA ataokoka katika hali anayopitia.
NEEMA ya BWANA izidi KWENU. AMEN
Frank Philip.
Kipimo cha UDHIHIRISHO (MANIFESTATION) wa Mungu kwenye HADHIRA
(PUBLIC) ni MUDA, BIDII na HALI ya MOYO wako UKIJIHUDHURISHA mbele Zake
mkiwa wenyewe wewe na Mungu pekeyenu (SIRINI).
Kama
UKIJIHUDHURISHA mbele za Mungu wako kwa BIDII na kwa UELEKEVU mahali pa
SIRI, basi Mungu ATAJIDHIHIRISHA mbele ya WATU hadharani.
Ukitaka Mungu aji-present kwa watu basi jifunze kuji-present kwa Mungu.
Ni aheri ukose MUDA wa kuandaa PRESENTATION kwa watu na sio MUDA wa
kuji-present kwa Mungu, kwa maana unaweza ku-present kitu chochote mbele
za watu ILA HUWEZI kum-present Mungu! Ndio maana kazi ya Mitume ilikua
KUHUBIRI na KAZI ya Mungu likua KULITHIBITISHA hilo Neno kwa ISHARA na
MAAJABU.
Kazi ya Musa ilikua kuji-present kwa Mungu na kupata
maelekezo na KAZI ya Mungu ilikua KUTENDA miujiza (kuji-present) mbele
za Farao!
Frank Philip.

Katika maisha yetu ya kila siku tumetamani MAMBO mengi mbalimbali
yatokee. Mengi ya haya MAMBO yako nje ya uwezo wetu na IMETUPASA
kuhitaji msaada wa Mungu au watu wengine. Mara nyingi utagundua ni
vigumu sana KUTEGEMEA misaada ya watu KUTIMIZA mahitaji yetu ya kila
siku. Njia rahisi ni kujua jinsi ya kujipanga vizuri na Baba yako wa
Mbinguni na kwa kupitia Yeye, anaweza
kuinua watu mbalimbali kuja kuingilia kati hali unazopitia na
kukusaidia. Ikishindikana kabisa, Mungu anaweza kuinua kunguru, mawe au
Malaika kuja kukupigania, na hii imetokea kwa wengi hata kwako pia
inawezekana.
Kusudi la somo hili fupi ni kutaka kuhusianisha
USHINDI wako na (i) NAFASI yako katika Kristo na KUZAA kwako MATUNDA, na
(ii). KIWANGO chako cha MAOMBI na pia ujue (iii). VIKWAZO vya Majibu ya
maombi yako, (iv). Kutofautisha imani ya KUOMBA na KUPOKEA, na (v).
Ujue jinsi ya KUJITEGEMEA kimaombi.
i. NAFASI yako katika Kristo
Mambo kadhaa ni ya LAZIMA: (a) kukaa ndani ya Yesu, (b). Neno kukaa
ndani yako, na (c). Omba lolote utapewa. Yesu alitufananisha na yeye
akiwa mzabibu, akasema“ sisi ni matawi ya mzabibu na yeye ni Mzabibu.
pasipo yeye sisi hatuwezi jambo lolote”. Pamoja na kwamba Yesu alikuwa
anazungumzia KUZAA matunda, utagundua pia mistari iliyofuata alisema juu
ya MAOMBI. Kwa upande mwingine kuna uhusianao kati ya KUZAA matunda na
KUJIBIWA maombi yako. (Yohana 15:1-6).
ii. KIWANGO cha maombi
Yesu alipowatuma wanafunzi wake kwenye HUDUMA mambo mengine yalikuwa
magumu, japo wametumwa na Bwana! Walipomuuliza kwanini mambo mengine
yanagoma? Yesu alijibu “mambo mengine hayawezekani bila KUFUNGA na
KUOMBA”. Hapa tunapata picha kwamba kuna kiwango fulani cha maombi
kinaweza kukuvusha hadi hatua fulani. Ukifikia hiyo hatua inahitaji GIA
nyingine ya maombi ya kiwango cha juu zaidi ili uvuke kwenda kwenye
hatua ya juu zaidi.
Pamoja na BIDII (diligence) na KUDUMU
(persistance), haya mambo mawili ni ya muhimu sana KUPIMA kiwango cha
USHINDI wako katika yale unayoyaombea. Kuna wakati itakupasa kuongeza
NGUVU/KIASI cha kuomba ili kuvuka mahali ulipo. Hata kama wewe ni TAWI
na UKO ndani ya Yesu vizuri na Neno (imani) limejaa ndani. (Luka 18)
iii. VIKWAZO vya MAJIBU ya Maombi yako
Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUPOKEA majibu ya MAOMBI na HALI ya
MUOMBAJI mwenyewe pamoja na KUTIMIZA viwango vingine kama (i) na (ii)
hapo juu. Kila mtu anajua kwamba tukiomba sio mara zote mambo hutokea
wakati huo-huo. Kuna kipindi cha KUSUBIRI na wakati mwingine kinakuwa
kirefu. Ili uweze KUPOKEA majibu yako angalia usikate tamaa kwa maana
“Mtavuna kwa wakati msipozimia roho.” Huhitaji IMANI kubwa kupokea
MAJIBU ya Maombi yako. “Imani kidogo sana kama chembe ya haradali tu,
inaweza kuhamisha milima na kufanya mambo makubwa sana maishani mwako
ila usipokuwa na SHAKA juu ya yale mambo uombayo”. MASHAKA ni KIKWAZO
kikubwa cha kupokea uombayo hata kama una IMANI. Kwa lugha nyepesi,
mashaka ni sumu ya IMANI yako. Adui anajua ukiomba kwa imani utapokea,
sasa akishindwa kukuzuia usiombe, basi ataleta MASHAKA katika yale
uyaombayo ili USIPOKEE. Ukiwa makini utamsikia katika “mawazo yako”
akikukukatisha tamaa na saa nyingine akikuzomea kabisa. Pambana na hayo
mawazo maana ni vita inayoweza kuathiri IMANI yako na majibu ya maombi
yako. (2 Wakorinto 10:1-6)
iv. JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA
Watu wengi sana wana IMANI ya KUOMBA ila wachache wana IMANI ya
KUPOKEA. Ukiwauliza watu juu ya maombi kwa kweli watakuambia Mungu
anajibu ila ukichunguza WANACHOONA ndani ya MIOYO yao ni KUSHINDWA zaidi
kuliko KUSHINDA. Matokeo yake hawawezi KUPOKEA majibu kwa maana hawana
IMANI ya KUPOKELEA.
Nitakupa mfano. Pamoja na kwamba Yesu ni
mponyaji na Muumbaji wa Ulimwengu, utasikia mahali anasema “imani yako
imekuponya”. Ina maana imani ya KUPOKEA ni ya MPOKEAJI na sio imani ya
Yesu japo kuna mahali ALIWAHURUMIA tu watu akafanya mambo kabla hata
hajaombwa na mtu (Luka 7:12,13). Kati ya maeneo ambayo Yesu hakufanya
miujiza ni kule mitaa ya nyumbani kwao, SABABU sio uhaba wa IMANI ya
Yesu ila IMANI ya WAPOKEAJI haikwepo. Yesu hakufanya kitu japo wengi
walikuwa na shida zao nyingi na aliwahurumia! Ndipo akasema “nabii
hakubaliki kwa watu wake.”
v. EPUKA MAOMBI TEGEMEZI
Kuna
kundi la watu wamefanya baadhi ya watumishi kama TIKETI ya kupokelea
majibu ya MAOMBI yao. Sawa, kuna kiwango cha NEEMA juu ya watumishi wa
Mungu kinachoweza kukuvusha mahali, lakini nakwambia kuna wakati hata
YESU “alipoitizama imani ya watu, ndipo alipotenda jambo” pengine
aliacha kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao! UELEKEVU wa MOYO wako kwa Yesu
utakusaidia sana katika KUPOKEA majibu ya maombi yako.

Sasa
tunakumbushwa siku zote kuomba kwa imani na kuambiwa kwamba “kuomba
kwake mwenye HAKI kwa faa sana akiomba kwa bidii”. Jifunze na uchukue
MAZOEZI ya kutumia IMANI yako kwa maana imani ina tabia ya KUKUA au
KUPUNGUA. Kumbuka KUKUZA imani ya KUPOKEA majibu ya maombi yako kwa
maana hiyo ndiyo inayokwamisha wengi. Kumbuka adui mkubwa wa imani ya
KUPOKEA anaitwa MASHAKA.
Dawa ya kupambana na MASHAKA ni
kufanya MAZOEZI ya KUOMBA wewe mwenyewe na KUPUNGUZA utegemezi wa
WATUMSHI wa Mungu. Sisemi ni vibaya kuombewa, ninachotaka kusisitiza ni
wewe kujijengea UWEZO wa kusimama kwa MIGUU yako MIWILI kumwamini Mungu
kwamba UNAWEZA kuomba na KUOPOKEA mwenyewe. Kumbuka wewe ni TAWI la
Mzabibu na mtumishi pia ni tawi tu, anayejibu maombi ni MZABIBU (Yesu).
Ukiweza kuepuka utegemezi kwa MATAWI mengine utagundua UMEVUKA hatua
nyingine ya IMANI na KUMPENDEZA Mungu pia kwa sababu “haiwezekani
kumpendeza Mungu pasipo imani”. Wengi sana tunaweza kumshangaa Petro
jinsi alivyoweza kutembea kidogo juu ya maji na ALIPOONA upepo, akazama!
Hiyo ndio kazi ya MASHAKA. Nadhani kama Petro angefanya tena mazoezi
kwa mara nyingine, angekuwa hahitaji tena Mtumbwi kwenda ng’ambo!
Kwanini? Alikuwa na IMANI ya kutosha KUTEMBEA juu ya maji ila MASHAKA
yalikuwa kikwazo.
Nitakupa mfano. Nguvu ya DAUDI na UJASIRI
aliokuwa nao wakati anamkabili Goliath, haikuwa kwa sababu tu alijuwa
uweza wa Jina la Bwana wa Majeshi, ila “kama alivyofanya MAZOEZI ya
kupambana na DUBU na SIMBA”, alijuwa kwa jinsi ILE ILE, BWANA
atampigania kwa Goliathi. Hakubakia tu KUAMINI moyoni, DAUDI
alimtangazia Goliath (adui) kwa SAUTI ya juu, mambo aliyoamini. Mara
nyingi sana wakati UNAOMBA, adui akileta SAUTI ndani yako za kukutia
mashaka, kumbuka KUMTANGAZIA kwa SAUTI juu ya USHINDI wako. Kwa njia hii
utaweza kushinda MASHAKA. Msomee adui Neno, mwambie “imeandikwa”, kisha
taja Neno (imani) katika biblia unalosimamia katika hayo maombi.
Uzoefu wa kutumia IMANI yako unakupa nguvu ya kuvuka hatua nyingine ya
KUPOKEA mambo uombayo katika kiwango cha juu zaidi. Ukiwa unamtegemea
MTUMISHI fulani tu, MOYO wako unaanza kuwa dhaifu na unaona PASIPO kujua
unahamisha UELEKEVU wako kutoka kwa Mungu na kuuweka kwa huyu MTUMISHI.
Hali hii imekuwa mtego mkubwa kwa watu wengi sana, wamehamisha MACHO
yao kwa YESU na wengine wamefikia mahali pa kuona MTU mwingine anahusika
na matatizo yao ndio maana wakati ule dada zake Lazaro walimlaumu Yesu
(mtumishi) kwa kusema “ungekuwepo hapa kaka yetu asingekufa”!
Mungu atusaidie kuongeza IMANI ya KUPOKEA majibu ya maombi yetu.
Frank Philip.

Bwana Yesu alizungumza kwa mifano mingi akisisitiza UMUHIMU wa watu
wake KUKESHA. Maana halisi ya KUKESHA ni kuwa macho hasa wakati wa USIKU
ambapo watu kwa kwaida hulala. Katika maisha yetu kuna VIPINDI vya
mchana ambapo kuna mwanga na tunaona. Pia kuna vipindi vya USIKU, kuna
GIZA na hatuoni kitu kwa sababu ya giza. Mara nyingi watu wanakuwa
SALAMA katika VIPINDI vya giza kuliko
vipindi vya MCHANA kwa sababu wanachukuwa TAHADHARI na kujilinda. Lakini
pia MAANDALIZI na MAFANIKIO ya ULINZI wako yanafanyika wakati wa
MCHANA.
Vipindi vya MCHANA vina sifa nyingi. Mojawapo ni
MWANGA. Kwa sababu UNAONA vyema, basi unakuwa na AMANI na UHAKIKA kwa
sababu unaona VITU kwa jinsi ya MWILINI. Sasa tukumbuke tumeumbwa ili
KUISHI katika ULIMWENGU wa MWILI na ULIMWENGU wa ROHO. Katika vipindi
hivi tunaambiwa “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu
uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika
hawataokolewa.” (1 Thesalonike 5:1-7). Ukifuatilia mistari hii
utagundua watu wa Mungu wameitwa ni wana wa MCHANA au wana wa NURU! Kwa
lugha nyingine kundi la pili linaitwa WANA wa USIKU! Sasa, pamoja na
kwamba mistari hii ilikuwa inakumbusha KURUDI kwa Yesu kulichukuwa
Kanisa, nataka tujifunze hii TABIA ya Mungu ya KUKESHA.
Sehemu
nyingine Mungu anajiita MLINZI wa Israel, Daudi alijuwa tabia ya Mungu
ya KUKESHA na akasema “Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu
na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam,
hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.” (Zab.
121:1-4). Hii tabia ya KUKESHA ni ya MUHIMU pia kwa WANA wa NURU ndio
maana Yesu amesisitiza sana “kukesha katika kuomba” na pia akasema
“atarudi kama MWIVI ajavyo usiku” akitutaka tuwe MACHO wakati WOTE.
Pamoja na GIZA la dunia hii, Bwana anasema “tusiwe kama wale wanawali
wapumbavu, waliochukua taa zao bila MAFUTA”, huko usiku wakati watu
wamelala, ghafla! Bwana Harusi anakuja!
Kuna sababu nyingi za
KUKESHA. (i) Tuweze kushinda/kutokuanguka majaribuni. (ii) Tuwe salama
adui anapokuja kushambulia. (iii) Kujua wakati wa KUJILIWA na Bwana.
(iv) Tusibaki Yesu akija kuchukua Kanisa lake. Sifa za WAKESHAJI
utaziona hapa, “Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna
asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea.
Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pinde
zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na
gurudumu zao kama kisulisuli;” (Isaya 5:27,28). Nitazungumzia zaidi
KUJILIWA. Yesu alipoutizama Yerusalemu alilia. Akasema “laiti ungejua
yakupasayo amani”, Wakati Yesu (Baraka za Mungu) zinakuja, Israel
hawakujua na kupokea kwa shukurani, na pia wakati ADUI anakuja kuharibu,
hawakuwa na HABARI! Akalia. Maisha yetu tumejisahau sana na kuona tu
mambo yataenda kama JANA! Tumepoa au kupunguza ile kasi ya kumtafuta
Mungu na tunaishi kama MUNGU hayupo! Taratibu tunapoteza NURU na kuanza
kutembea GIZANI. Usipoangalia Ghafla! Uharibifu unakuja, kwa maana ADUI
anakuwinda na anasubiri GIZA akushambulie! “Basi tusilale usingizi kama
wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala
usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na
kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe
tumaini la wokovu.” (1 Thesalonike 5).
Sio kila mara ukiona
MWANGA (NURU) kwenye ulimwengu wa MWILI pia unaona MWANGA kwenye
Ulimwengu wa roho. Ngoja tujifunze kwa Ayubu. “Ndipo Shetani akamjibu
Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira
kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo?
Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika
nchi. (Ayubu 1:9,10). Huu uliku wa ni wakati wa MCHANA (NURU) kwa Ayubu.
Wakati Baraka ziko kila upande, mali, watoto, na mafanikio ya kila
namna. Huku unaouna mkono wa Bwana (ukingo) unakupigania, nk. Ghafla!
Giza nene linatanda! Sasa sio watu wengi sana wanapona hapa. ILA wale
ambao WANAKESHA “watayaona mabaya yakija” (1 Thesalonike 5), na Mungu
wao atawapa DAWA ya KUSHINDA. Kwa sababu wako NURUNI, MLANGO wa KUTOKA
wakati wa KUJARIBIWA kwao watauona.
Mara nyingi sana watu
katika maisha ya kawaida hawajali sana kwa sababu BANK kumenona, wanajua
hata wakifukuzwa kazi LEO hawafi njaa. VITEGA uchumi vimesimama sawia.
Karibia kila kitu kimekatiwa BIMA. Wanaweza kupata MATIBABU mahali
popote duniani. Mambo ni SAFI, hata wakitafuta kwamba SHIDA inaweza
kutokezea wapi hawaoni. Huwezi kuona UMUHIMU wa kukesha na KUDUMU
kumtegemea Mungu kama huna macho ya rohoni na UELEKEVU kwa Bwana kama
Ayubu. Lakini kwa wale ambao wamepitia majanga wanajua nasema nini. Kuna
habari MBAYA hata sipendi kusikia licha ya kusimulia. Utakuta watu
wameokoka tu vizuri, wamebarikiwa kuingia kwenye NDOA. Wanakuwa na
mipango mingi ya maisha na KAZI/BIASHARA zao nzuri ziko sawa. Ghafla!
Wasipotarajia, wameenda wote kazini na kabla ya jioni mmoja ametwaliwa!
Ghafla tu! Status inabadilika, mmoja anaitwa mjane. Adui kashambulia.
Wengine katika hali isiyotarajiwa, watoto wameenda shule, ghafla jioni
hawarudi! Wanapata taarifa waende chumba cha kuhifadhia maiti kukagua!
Hizi ni habari mbaya sana. Lakini haya ndio yalikuwa yanamtokea Ayubu
wakati wa GIZA ulipoanza. Anajigundua hana WATOTO hata mmoja, wamekufa
wote! Hana MALI halafu ni mgonjwa hajiwezi hapo chini. Mke wake naye
analeta mambo magumu ya kumchanganya zaidi. Huu ni wakati wa GIZA.
Kusudi la somo hili ni kukumbusha habari ya KUKESHA. Katika kukesha
kuna kujaa NGUVU na kujiandaa kupambana (Isaya 5). Nguvu za kukuwezesha
kuvuka kwenye GIZA hupatikana wakati wa MCHANA. Maisha ya Ayubu kabla
ya JARIBU ndio yalimwezesha KUSHINDA wakati wa jaribu. Watu wengi sana
wanasubiri MAJANGA (GIZA) ndio wanaanza KUFUNGA na KUOMBA kwa BIDII na
KUKEMEA kwa NGUVU. Sasa kweli wanakemea, ila nguvu iko wapi? “Ukizimia
siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.” (Mithali 24:10). “Wamtumainio
Bwana ni kama MLIMA Sayuni, hawatatikisika kamwe” lakini pia Isaya
anasema “bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu
kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa
miguu, wala hawatazimia.” (Isaya 40:31). KUSUBIRI kunahusianishwa na
tabia ya KUKESHA.
Yesu anaposema “ni rahisi ngamia kupenya
kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia Ufamle wa Mungu” aliona
hii shida KUFANYA mapenzi ya Mungu wakati watu wamezungukwa na kila
kitu. Ndio maana alipomuuliza yule kijana tajiri habari za AMRI za
Mungu, na kijana anasema ameshika ZOTE, maandiko yanasema “Yesu
akampenda”. Kwanini? Sio rahisi kukaa katika Amri za Mungu wakati HELA
inapiga kelele. Ukifanikiwa kumpendeza Mungu wakati una KILA kitu lazima
uwe KIVUTIO kwa Yesu. Sasa, Angalia maisha yako vizuri. Pale mahali
ulikuwa una SHIDA, huna hela na hujui unavukaje, ULIMTAFUTA Mungu kwa
BIDII na kukaa mbali na DHAMBI. Leo Mungu amekuvusha, umemaliza shule
salama, umepata kazi, nafasi na pesa, Ghafla! Unaanza kuwaza KUTENDA
dhambi! Ukiwa kwenye SHIDA kwako ilikuwa MCHANA, sasa Mungu amekubariki
na baraka za Mungu badala ya kuongeza NURU, zimekuwa GIZA! Na chukizo
kwa Mungu. Je! Unataka Mungu akurudishe kule kwenye DHIKI ili taa yako
iwake? Wakati unadhani ni “amani amani” angalia uharibifu uko njiani.
Neno hili linakukumbusha UAMKE na KUCHANGAMKA, rudi kwenye MKESHA na
kuishi kwa KIASI, huku ukimsubiri Bwana. Kuna faida gani “kuupata
ulimwengu wote na kupoteza nafsi yako?” Jijibu mwenyewe na uchukue
HATUA. Mungu akusaidie.
Basi Mungu atuwezeshe kukaa katika KIASI na KUKESHA kwa Jina la Yesu. AMEN
Frank Philip.
Kazi ya UVUVI ni moja ya kazi ambazo zinahitaji uzoefu lakini pia
Imani. Umewahi kujiuliza mvuvi anaposhusha nyavu zake huko chini kwenye
maji ambapo haoni kitu ila anasubiri kwa IMANI akijua samaki wataingia?
Petro alipoambiwa anabadilishiwa kazi kutoka kuvua SAMAKI kwenda kuvua
WATU ilikau inahitaji shule zaidi kidogo ili aelewe somo. Siku moja
Petro akaenda kwa UZOEFU, kumbuka sio
ZIWA/BAHARI au maeneo asiyoyajua, anajua sana na ana uzoefu nayo. Si
akakesha sasa usiku kucha na hakupata kitu! Yesu akaja, akamwambia
“Petro shusha nyavu” na akampa maelekezo ya ziada. Petro akajiuliza,
“nimehangaika usiku kucha ila sikukamata kitu na sasa unasema nishushe
nyavu?”, akapiga moyo konde na kusema, “kwa Neno lako nitashusha”. Hao
samaki aliokamata hakuweza kuvuta nyavu maana ni wengi hadi nyavu
kuchanika! Akasema “ondoka kwangu mimi mwenye dhambi”! Kwanini? [kufanya
kazi ya Mungu bila mapenzi yake ni kosa na itakugharmu].

Sikiliza. Watumishi wengi sana wa Mungu wanahangaikal na KINA na UZOEFU
wa nondo (mafundisho, nyenzo, nk.) wanazotumia na USTADI wa kupiga
MAKASIA. Bila KUSUDI la Mungu utakesha hapo nakutahadharisha. Sio katika
HUDUMA tu ila hata katika michakato ya maisha, biashara, nk. Hakikisha
unashusha NYAVU mahali ambapo unajua YESU amekuongoza. Huwezi kosa
SAMAKI asilani. Uzoefu wako na UJUAJI vitakuponza tafuta KUSUDI la Mungu
katika maisha yako na utaona MATUNDA yakimimnika maishani mwako kama
MVUA. Mafanikio ya Petro hayakutegemea KINA cha maji, AINA ya nyavu,
MTUMBI, UREFU wa MUDA, wala UZOEFU wake! Ila NENO la Yesu! Ukipata Neno
la wakati huo katika MUKTADHA (context) na MAUDHUI (content) na MUDA
(timely), mafaniko yako katika HUDUMA, BIASHARA, KAZI, SHULE, nk.,
yatakua makubwa kuliko kujitahidi kwa NGUVU zako mwenyewe na AKILI zako.
Jifunze kumshirikisha Yesu nawe utaona HATUA atakazokufikisha.
Kumbuka. Mungu hulituma Neno lake “kama mvua ishukavyo kutoka juu
kuangukia ardhi”, na LITATIMIZA makusudi yake, halitarudi bure. Ukijua
Yesu anasema nini juu ya UVUVI wako, sema kama Petro “kwa Neno lako
nitashusha nyavu” halafu tukikutana utanipa ushuhuda. Barikiwa.
Frank Philip

Katika mambo ya muhimu sana kwa maisha ya IMANI, moja wapo ni kujua NIA
yako katika mambo fulani ya kimwili na kiroho. Kwa lugha nyepesi ni
muhimu kujua MOYO wako “unasema nini juu ya jambo fulani” (nimetumia
KUSEMA kwa maana Moyo unatoa sauti ya yale uwazayo mbele za Mungu). Au
kwa lugha nyingine ni vizuri kujua “MTIZAMO wako juu ya mambo fulani”
(Kuna picha/kitu halisi kinajengwa ndani yako na mawazo yako na ndicho Mungu anachokiona).
Sababu ya msingi ya kujua NIA (makusudi ya Moyo) yako ni kupima kiwango
cha MUNGU kuhusika na hayo mambo UWAZAYO/UNAYOHITAJI ambayo mengi
yanapita MOYONI mwako kama MAWAZO tu. Majibu ya maombi yako hayaji kwa
yale mambo ambayo ULIMI wako ulitamka wakati wa maombi, bali yale mambo
ambayo NIA (makusudi ya moyo) yako imetamka wakati wa kuomba. Sasa
unaweza ukafikiri nataka kusema nini hapa ila ukitafakari kwa makini
utagundua kwamba “unaweza kuomba au kunena jambo tofauti na unavyo NIA
ndani yako (unavyo sikia/ona hilo jambo NDANI yako)”. Sikia, “Kwa MOYO
mtu huamini hata akapata HAKI”, ticket ya kupokea inaitwa IMANI, na
hukaa moyoni. Moyo wako ukinena (NIA) kwa imani UNAPOKEA majibu ya
maombi yako! “Kinywa kinapitisha tu yaujazayo moyo wako”!
NIA
yako ikisema KITU tofauti na ULIMI wako unachokisema, katika kuchagua
kati ya haya MAWILI, Mungu anasikiliza NIA (makusudi ya moyo) yako na
sio ULIMI (mambo yatokeayo akilini mwako) wako! Ndio maana Suleiman
alisema “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka
kwa Bwana.” (Mithali 16:1). Haijalishi ULIMI wako umekiri sana mangapi,
je! Nia yako imejipanga sawasawa na KUSUDI la Bwana? Ukitaka MAJIBU
mazuri, maandalio ya MOY O ni wewe unafanya sio Mungu, JAWABU la ULIMI
kwa uombapo ni kazi ya Mungu kujibu.
Kutokana na UMUHIMU wa
NIA (makusudi ya moyo) ndani ya mtu ndio maana “Mungu anachunguza moyo
na kujaribu viuno”. Na katika vitu 6, naam 7 achukiavyo Mungu mojawapo
ni “moyo uwazao mabaya” (Mithali 6:18). Sasa sisi tunapambana na watu
kwa MATENDO au MANENO yao lakini kwa MUNGU hata ULIMI usiposema, MOYO
unasema na Mungu anasikia na KUONA. Yesu akasisitiza, “sio alacho mtu
hunajisi ila kimtokacho”, kwa maana kinatoka ndani ya MOYO na NIA yako
inasema moyo ULICHOKUSUDIA kufanya. Kabla dhambi haijafanyika kwa jinsi
ya mwili, ilianza kufanyika ndani ya moyo wako kisha UNAITIMIZA kwa
MAKUSUDI ya MOYO wako (NIA).
Jifunze kudhibiti NIA yako kwa
sababu hapo ndipo penye NGUVU ya kushinda au kushindwa kwako. Kama
unataka kufanikwa zingatia “kulinda sana moyo wako kuliko vyote
ulindavyo”. Watu wengi sana wanasahau kwamba MAWAZO ya mioyo yao
yanapiga KELELE kwa SAUTI japo ULIMI haujasema kitu! Kwa Mungu hayo
mawazo yanapita kama PICHA/SANAMU ndio maana Mungu anasema “umechukua
vinyago na kuvitia moyoni”, yaani kule ndani yako Mungu anaweza kuona
OBJECTS au PICHA japo wewe UNAWAZA tu. Yesu akasema “amwangaliaye
mwanamke kwa kumtamni MOYONI mwake amezini”, sasa kila mtu anajua tamaa
ni kama WAZO tu ndani ya mtu ila Mungu akiangalia kama umefuga hayo
mawazo, Yeye anaona KITENDO/SAUTI/PICHA/SANAMU! Ndio maana Mungu anasema
“anachukia MOYO uwazayo mabaya” kwa sabubu kwake ni VITU HALISI kuliko
sisi tunavyofikiri na mara nyingi tunapuuzia tu.
Mungu
alipomtokea Sulemain na kumwambia aombe kitu chochote, NDANI ya Sulemani
kulikuwa na MENGI ila aliomba KUSUDI la Mungu juu ya KAZI aliyoitwa
kufanya ili AMPENDEZE Mungu. Jambo hili LIKAMPENDEZA Mungu. Nataka uone
kitu cha tofauti hapa. Usije ukafikiri Sulemani alikuwa na AKILI sana
ndio maana ALISEMA hivyo. KUMBUKA, ilikuwa ni NDOTO tu! (1 Wafalme 3:8).
Kila mtu anajua kwamba tukilala hatutumii AKILI kama tukiwa macho, sasa
Sulemani aliwezaje KUOMBA kitu sahihi kwenye NDOTO? Inamaana MOYO wa
Suleiman ulikuwa UKITAMANI kumpendeza Mungu (alikuwa na NIA) ambayo
Mungu alipomtembelea japo ULIMI wake haukunena, NIA iliyoko ndani yake
ILINENA na Mungu akajibu.
Ukisoma sehemu nyingine Bwana
anasema “niko pamoja nanyi katika mipango yenu, KABLA ya kuomba mimi
Bwana nitajibu, na mkiwa katika KUNENA nitasikia”! Sasa watu
watakubaliana na mimi kwamba kila mmoja wetu huwa ana mipango ndani ya
MOYO. Ukiwa na NIA (makusudi ya moyo) safi mbele za Mungu, hiyo MIPANGO
yako katika MAWAZO yako, Mungu anasema NINASIKIA! Kabla HUJAOMBA, Mungu
anajibu! Ukisoma kitabu cha Ayubu utaelewa vizuri NGUVU ya mawazo yako.
Tunaambiwa Ayubu “hakumwazia Mungu kwa upumbavu”. Hili ni jambo KUBWA na
Ibilisi amelificha kwa watu wengi ukiangalia ndani yao ni MAWAZO
machafu tu na kuwaza vitu vya AIBU na wao hawajui kwamba mambo mawili
yanatokea: i. Moyo wako unakua chukizo kwa Bwana ii. Unadhoofisha
kiwango cha kupokea majibu ya maombi yako kwa maana MOYO wako unanena
tofauti na ULIMI wako. Umepoteza UELEKEVU! “Na macho ya Mungu
yanakimbia-kimbia diniani kote, anatafuta huo uelekevu ndani yako ili
ajionyeshe mwenye NGUVU”
Petro akasema “kwa hiyo VIFUNGENI
VIUNO VYA NIA ZENU, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile
neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii
msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu” (1Petro1:12,13).
Hapa napata picha kwamba tunaweza KUAMUA kushughulika na NIA zetu na
kizidhibiti, ndio maana tunaambiwa TUZIFUNGE NIA zotu viuno na kua na
kiasi!
Kuna maswali mengi huwa najiluza. Hivi Mungu
akiniangalia huku ndani ANAONA nini? Watu wengi sana utawakuta wamepiga
MAGOTI kwenye IBADA kanisani/sehemu mbalimbali, lakini ndani ya MIOYO
yao kwa kweli WAMESIMAMA. Jiulize tu, kwamba kweli kuna UWIANO
(synchronization) kati ya USEMAYO, UTENDAYO na UWAZAYO? Watu hawatuoni
lakini nakwambia kuna watu MIOYO yao inavurumisha matusi kwa nguvu kama
wafanyavyo wavuta bangi. Sawa, watu hawasikii lakini nakuhakikishia leo
Mungu wako anasikia SAUTI! Basi AMUA leo, katika dunia hii iliyojaa UOVU
na HARUFU ya UVUNDO inayopanda kwa Mungu kila siku, wewe uwe MANUKATO
na KITU cha kupendeza Mungu anapo CHUNGUZA moyo wako. Jifunze KUMBARIKI
MUNGU kwa MAWAZO ya MOYO wako. Ukifanikiwa hili Mungu atajibu HAJA ya
MOYO wako kabla hujaomba kwa sababu NIA yako husema kwa SAUTI mbele za
Mungu.
Ukitaka kujua UMEFANANAJE mbele za Mungu, angalia
NAFSINI mwako, kile kitu unachokiona ndani yako NDIVYO ULIVYO mbele za
Mungu, kwa maana imeandikwa "mtu aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo".
Roho Mtakatifu tusaidie. AMEN.
Frank Philip.

Kama kuna kitu unahitaji kujua kama Mkiristo ni kuomba VIZURI.
Wanafunzi wa Yesu walimwomba Bwana awafundishe kuomba kwa maana waliona
wanafunzi wa Yohana wanavyoomba wakajua lazima kuna namna ya kuomba na
sio kufurumuka tu na maneno bila utaratibu (Luka 11).
Kama kuna swali gumu nilikuwa najiuliza ni hili la kuomba kwa muda mrefu. Yesu anasema “KESHENI mkiomba msiingie majaribuni”,
sehemu nyingine anauliza “hamkuweza kukesha nami hata saa moja tu?”.
Katika Agano la Kale utaona neno “WALINZI” limetumika. Bwana anasema
“Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana
wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya” (Isaya 62:6).
Sasa kwa WAOMBAJI watajua hii lugha ya “KUMKUMBUSHA” Bwana maana yake
ni nini. Unapoomba sio kwamba Bwana hajui, unamkumbusha tu, ndio maana
“Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama
itupasavyo”. Sio tu kwamba hatujui kuomba ila hata cha kuomba mara
nyingi hatujui hadi Roho atusaidie. Kumbuka, unapoomba hutakiwi kukaa
kimya hadi utakapoona majibu ya maombi yako. Hii TABIA ya KUDUMU/KUKESHA
katika maombi imejirudia tena wakati Yesu anafundisha wanafunzi wake
FAIDA za kuomba BILA KUKOMA. Yesu “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa
kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na
kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji
huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema,
Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema
moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa
mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa
kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na
Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku,
naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini,
atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:1-8).
Nilinachotaka uone hapa ni aina ya UOMBAJI unaotakiwa na jinsi unapaswa
kujipanga na kuwa na nguvu za kuomba kwa muda mrefu. Nitakupa moja ya
SIRI muhimu za kukusadia kuwa na nguvu za kukusukuma angalau muda zaidi
kidogo katika maombi.
Kuna mambo mawili nataka uone. La kwanza
ni BIDII na la pili ni MUDA. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na
kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba
kwa BIDII. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba
kwa BIDII mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka
mitatu na miezi sita.”(Yakobo 5:15,16). Ukiona mtu “anajifanya” eti
anatamka neno “moja tu” na mambo yanatokea, anataka kuonyesha kwamba
yeye yuko juu sana na karibu sana na Mungu na miujiza ni kama tu switch
ya umeme, ON/OFF matatizo kwisha! Huwa najiuliza swali hili, je! Huyu
jamaa huwa anakesha na kuomba sana na sasa anamalizia tu kile alichokuwa
ameomba/anomba kwa muda mrefu? Na kama sio mwombaji, je! Hii nguvu ya
ON/OFF na huku ameshika kiuno imetoka wapi? Naishia hapo. Usifike mahali
ukaona watumishi wa Mungu wanatumika kwa mtindo ambao hujawahi kuona
ukakimbilia kusema ni PEPO. Utaingia kwenye matata MAKUBWA kama ni Mungu
kweli anawatumia. Lakini pia UJUE sio kila atendaye MIUJIZA anatoka kwa
Mungu.

Biblia inasema Eliya aliomba kwa BIDII! Sasa wewe
unasema hapa ni kuamuru tu mambo kama ON/OFF na huna TABIA ya kukesha
kwenye maombi! Kumbuka Yesu aliamuru mambo kwa mtindo huu, just ON/OFF
mambo yanatokea, wanafunzi wake wakajitahidi kuiga, “IKAGOMA”!
Wakamwendea wakamuuliza “mbona sisi inagoma?” Yesu akasema “mambo
mengine hayawezekani ila kwa KUFUNGA na KUOMBA”. Tunasoma kwenye
maandiko kwamba Yesu alikesha milimani akiomba na asubuhi anaingia
hekaluni kuhudumu. Anasema “sifanyi kitu ambacho sikumwona Baba yangu
akifanya!” Swali je! Aliona saa ngapi? Kama Yesu ALIFUNGA na KUOMBA,
halafu wewe HUTAKI kujifunza tabia hii na unataka tu usimame kama
“AFANDE” na kutoa tu ishara kwa mkono mambo yanatokea, watu wanarushwa
huku na kule. Jua unakaribia MAHALI pa GUMU.
Hatua SABA za
maombi zitakusaidia kuomba kwa MUDA mrefu. Kumbuka siku zote MAOMBI
hayaendi bila NENO. Ukitaka kufanikiwa kuomba ni LAZIMA uwe msomaji wa
NENO pia. Jipe angalau milango (chapters) 2 kwa siku. Asubuhi na jioni
au muda wa kusubiri (ukiwa kwenye gari, bank, nk.) Hizi hatua SABA sio
ubunifu wangu ila ni SALA ya BWANA.
Hatua ya kwanza: Liitie Jina la Bwana wa Majeshi.
Yesu alisema “mkiomba neno LOLOTE kwa Jina langu nitafanya”. Pamoja na
kwamba Daudi alimkabili Goliath kwa kombeo, fimbo na jiwe, alitumia
“Jina la Bwana”. Hiyo ndio siri ya ushindi wake. Sehemu nyingine Daudi
akasema “hawa wanataja magari na farasi lakini mimi nitalitaja jina la
Bwana Mungu wangu”. NGUVU zako za kuomba na MAFANIKIO ya uombayo yapo
katika Jina la Yesu.
Sasa, unaposimama na kuanza “Baba
yetu/yangu uliye Mbinguni. JINA lako LITUKUZWE”. Jiulize, litukuzwe na
nani? Kama ni wewe basi anza kulitukuza jina la Bwana. Usikurupuke na
kuanza tu kukemea pepo bila utaratibu hapo, No! Mtukuze Mungu kwanza.
Kukemea ni hatua ya 6 huko mwisho wakati umeshajaa NGUVU. Yesu akasema
“huwezi kuchukua vitu vya mwenye nguvu mpaka umemfunga kwanza”. Sasa
unamfungaje mwenye nguvu wakati huna NGUVU?
Watu wanajiuliza
sasa nitamtukuzaje Mungu? Sikiliza. Wana wa Israel walipovuka mto
Yordani na maji yakatindika mbele yao, waliambiwa waokote mawe 12 hapo
mtoni wayaweke iwe ukumbusho huko mbele kwamba “Mungu alifanya matendo
makuu”. Mungu anapenda hiki kitu. Taja “matendo makuu ya Mungu” yoyote
unayoyajua huko kwenye Biblia, mshangilie na kumshukuru kwa sababu ya
UWEZA na NGUVU zake. Unavyozidi KUZAMA katika kutafakari na KUTAJA
matendo makuu ya Mungu, taratibu utagundua kuna kitu kinatokea, unaanza
kujaa CHARGE! Unavyozidi kutaja na kumtukuza Mungu, NGUVU inaongezeka na
unaanza kuwa mwepesi ghafla. Hii hatua ukipita vizuri, inakupa NGUVU ya
kusogea hatua ya 2.
Hatua ya pili: Ita Ufalme wa Mungu.
Hakuna ufalme usio na mfalme! Ndani ya MFALME kuna MAMLAKA na NGUVU.
Sasa unapoita Ufalme wa Mungu uje, kimsingi umeagiza MAMLAKA za Mbinguni
zishuke kukuhudumia wewe na mambo unayoyaombea. Ndani ya ufalme wa
Mungu kuna KILA kitu unachokitaka. Mahitaji yako yote yanapatikana humo.
Lakini jipange na MOYO wako vizuri maana ukiomba vitu kwa tamaa yako
hupati kitu (fuatilia somo kwenye “Mafundisho ya Neno la Mungu LIKE
page” lenye kichwa “Jinsi ya kumwona Mungu akijidhihirisha kwako”).
Jifunze kwamba NENO la Mfalme ndio NENO la MWISHO. Huwezi kumfundisha
Mfalme chakufanya kama hataki. Wewe UNAMSIHI kwamba MAPENZI yake
yatimizwe . Ukifika hapo unaingia hatua ya 3.
Hatua ya 3: Jua Mapenzi ya Mungu kwa unachokiombea.
Mapenzi ya Mungu yapo katika NENO la Mungu. Huwezi kupokea kama unaomba
pasipo IMANI. Na tunajua kwamba “imani huja kwa kusikia, na kusikia
huja kwa NENO la Kristo”. Sasa ukiwa na Neno la Mungu juu ya “hicho”
unachoombea, jua una mtaji wa IMANI. Sasa kumbuka. Unapoenda mbele za
Mungu uwe kama yule mama mjane ambaye alienda BILA KUCHOKA,
“akirudi-rudi kudai haki yake” (Luka 18). Ukijua AHADI zako na NENO juu
ya kitu unachoomba, kaa hapo usiondoke, omba na dai ahadi yako kwa UPOLE
na UNYEYEKEVU mbele za Bwana, tena bila kuchoka (usipayuke kama mtu
asiye na imani). Ukirudi-rudi hadi upokee kumbuka siku zote, “Mungu
huliangalia Neno lake akalitimize, na Yeye hulituma Neno kama mvua
ishukavyo juu ya Nchi, Litaenda (halikosi shabaha) kwa YALE mambo
aliyoliagiza na halitamrudia bure”. Hakuna faida kama unajua KITU
unachoomba kipo kwenye MAANDIKO. Hapo ndio nguvu na mafanikio yako
yalipo. Kama una jambo “nyeti” unataka Mungu akutendee, hakikisha
unachukua kalamu na karatasi na unatafuta mistari ya KUSIMAMIA. Imani ya
KUPOKEA uombacho imejikita katika UFUNUO wa hilo Neno.
Hatua ya nne: Omba mahitaji yako.
Maombi ya unachokihitaji yamejengwa kwenye hatua ya 3 hapo juu.
Unapoomba RIZIKI au mahitaji mbalimbali ya mwilini na rohoni, kwako au
kwa mtu mwingine, yote yamejikita katika MAPENZI ya Mungu ambayo
unayapata katika Neno. Neno hilo hilo linakupa imani ya kupokea majibu
ya maombi yako. Sasa kumbuka siku zote kwamba majibu ya maombi yetu yako
ya aina mbili tu. NDIO au HAPANA! Jifunze kwamba hata HAPANA imo katika
mapenzi ya Mungu pia. Mungu anakuwazia mema siku zote, hakunyimi kitu
bila SABABU. Na imetupasa kumshukuru Mungu katika Mambo yote. Kama
tumepokea au hatujapokea yote ni mapenzi ya Mungu kwetu. Ukisikia mtu
anakuhakikishia kwamba “LAZIMA” jambo fulani litatokea kwa MUDA anaotaka
yeye, jiulize swali hili, Je! Mungu alimhakikishia hilo jambo kwa namna
hiyo? Na kama hajahakikishiwa na Mungu, jiulize tena swali hili, je!
Ukiri tu ushindi NJE ya MAPENZI ya Mungu ili “kumpinda” Mungu afuate
matakwa yako? Ukijua majibu, jifunze UMUHIMU wa kujipanga kwenye mapenzi
ya Mungu na KUMSHUKURU kwa KILA jambo.
Hatua ya tano: Toba.
Hii hatua huwa inakuwa ya tano kama tu wewe unadumu katika maombi muda
wote, ila mara nyingi sana inakuwa ya kwanza pia. Mungu ni mtakatifu,
“ujasiri wa kukariba Kiti cha rehema tunaupata katika Damu ya Yesu tu”
mara nyingi sana ukianza kuomba unaweza KUSUKUMWA kujitakasa.
Sizungumzii hii hatua ya kujitakasa ambayo inaweza kutokea mwanzo wa
maombi. Nazungumzia hii hata ya 5 ambayo sasa unazama kwenye TOBA kwa
UPANA wake. Hii hatua ukiifaya vizuri itakuwa ni UFUNGUO wa matatizo
mengi sana na KIPOKELEO cha maombi yako. Yesu anaagiza “kila tusimamapo
kusali tusamehe ili na sisi tusamehewe”. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo
yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa
yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya
mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe
ninyi makosa yenu.]” (Marko11:24-26). Ili uweze KUPOKEA jifunze
KUACHILIA watu waliokukosea/wadeni wako! Nakwambia jitahidi KUSAKA
“huko” ndani yako KILA mtu ambaye ukimuwaza moyoni unasikia UCHUNGU na
ukimpata, MSAMEHE na KUOMBA kwa ajili yake hadi upate UHURU. Kama bado
una FUNDO ukimuwaza huyo mtu jua BADO hujavuka hapo hatua ya tano. Watu
wengi sana wameshindwa “kupokea wanayoamini” (Marko 11) kwa sababu
wameshindwa kuvuka hatua ya tano! Omba NEEMA ya KUSAMEHE kama inakuwa
Ngumu na Yesu atakusaidia kumsamehe Mtu. Kama Yesu aliweza kuwasamehe
WALIOMSULUBISHA katikati ya mijeledi, misumari, taji ya miba na
kuangikwa msalabani huku anatukanwa na kutemewa mate, wakati yote
yanaendelea ANAWASAMEHE na kumwomba Baba awasamehe! Yaani anapigwa, ila
yeye yuko kwenye maombi! Huyu Yesu anaweza kukupa NEEMA hii ya KUSAMEHE
mwenzako kwa faida yako WEWE mwenyewe KUVUKA hatua nyingine.
Hatua ya sita: Shughulika na ADUI.
Watu wengi sana wamejifunza njia moja tu ya kushughulika na Ibilisi.
Kila mmoja yuko busy KUKEMEA kwa Jina la Yesu! Sawa, ni muhimu lakini
nataka ujifunze Neno hili. Yesu alimwona Petro jinsi anakavyo mkana
kabla hajamkana! Hakikumsumbua Yesu kwa sababu “huko” katika MAOMBI yake
alikwisha omba kwamba “imani ya Petro isitindike wakati Ibilisi
anampepeta kama ngano”. Yesu hakumkemea Ibilisi “asimpepete Petro ila
aliomba Petro ASIANGUKE kwenye hilo JARIBU na akisimama awasaidie
wenzake”. Majaribu ni package (kivunge/kifurushi) sio kitu kimoja. Sasa
ukiwa na utaalamu wa kukemea kuna kitu kwenye hicho kifurushi kitakuwia
kigumu. Kifurushi cha jaribu kina mambo makubwa matatu. Kwanza,
jambo/kitu utakachojaribiwa nacho. Pili, kitakachotokea wakati unakutana
na hicho “kitu” (kupepetwa kama ngano) na tatu, kusudi la jaribu.
Ufanye nini baada ya jaribu (simama na imarisha wenzako). Hakuna
mwanadamu atakemea MAJARIBU yasije maana majaribu yamo katika mapenzi ya
Mungu. Unapaswa kutambua mambo haya matatu kwa makini sana: jaribu
(kitu kinachokujaribu), namna ya kujaribiwa, na kusudi la jaribu. Sasa
ukikazana tu na kukema huwezi kufanikiwa kila kitu kwa maana katika hilo
jaribu, japo ni Ibilisi anakujaribu lakini ni Roho Mtakatifu katoa
kibali kwa KIPIMO! Na huwezi kumkemea Roho Mtakatifu kwa maana ndani ya
hilo JARIBU kuna KUSUDI la Mungu!
Kumbuka aliyempeleka Yesu
Nyikani kujaribiwa hakuwa Ibilisi. Alipelekwa na Roho Mtakatifu! Sasa
nataka ujifunze KUOMBA na sio KUKEMEA tu! Omba Mungu kwamba “usianguke
majaribuni na uokolewe na yule Mwovu”. Jifunze kumshinda Ibilisi kwa
Maombi sio kumkemea tu. Mara nyingi sana ukikuta mambo magumu na
unawekwa kwenye “kona” badala ya kukemea pia unamwambia Ibilisi
“imeandikwa”, halafu unamsomea msitari wa Biblia na Ibilisi anaachilia
mara moja! Kumbuka “nao wakamshinda kwa Damu ya Mwana-kondoo na NENO la
ushuhuda wao”, Neno lina nguvu ya kumshinda Ibilisi. Kwanini? Yesu ni
Neno! Na tumehakikishiwa kwamba ni “aheri dunia iondoshwe kuliko yodi
moja ya andiko kuondoshwa”. Sasa unaweza kuona kwamba hakuna UJANJA
ibilisi anaweza kufanya kushindana na Neno la Mungu. Kwa mfano ni rahisi
Ibilisi kuangamiza dunia ila sio Neno la Mungu! [japo dunia inalindwa
na hakuna uharibifu wa kuangamiza dunia yote ambao utatokea kama Mungu
hajaruhusu. Kumbuka agano la upinde wa mvua, nk. hii dunia imewekwa
akiba..]
Hatua ya saba: Rudisha Utukufu kwa Mungu.
Hii
hatua ni ya muhimu sana kama hatua nyingine zilizotangulia. “kwa kuwa
wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”. Ulianza na
“Jina lako Litukuzwe” na kuita “Ufalme wa Mungu uje”, sasa
ukishahudumiwa na Mfalme na kuamini kwamba KILA ulichoomba kimesikika
kwa Mfalme sasa lazima utoe HESHIMA kwa Mfalme! Unamalizia kwa kusema
“kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”
Kumbuka kumshukuru Mungu kabla ya kupokea uliyoomba kwa sababu “imani ni
hakika ya mambo YATARAJIWAYO na ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana”.
Mambo yatarajiwayo maana yake hujayapata ila UNAJUA yanakuja. Haya mambo
yakiwa BAYANA unapata ujasiri wa KUKIRI kwa maana una UDHIHIRISHO wa
NDANI kwamba umepokea ulichoomba. Usiiishie hapo, rudi-rudi kama yule
mama mjane, kukumbusha hadi uhitimishe maombi yako kwa kuona sasa kwa
jinsi ya mwilini jambo limetokea.
HITIMISHO
Kama
utakuwa umefuata hizi hatua saba, na kujimimina utagundua kumbe saa
nzima imeisha na unataka kuendelea kuomba. Fanya mazoezi halafu unipe
ushuhuda. Najua hutaanza kupiga masaa tu kwa mara moja, ila angalau
utavuka hatua kwa hatua.
Jambo la muhimu sana la kujifunza
katika maombi ni juu ya MAHALI na MUDA. Watu wengi sana wamesindwa
kuomba kwa sababu ya kufungwa na MAHALI na/au MUDA. Ukijifunza kuomba
kila mahali, ukitembea, ukipika, ukifua, ukiwa darasani, ukiwa safarini,
nk., utagundua unaweza kuombea mambo mengi sana kwa siku na kurudi-rudi
kwa Mungu mara kadhaa “kumkumbusha jambo” kwa sababu huhitaji
kujifungia mahali. Kama unaweza kuomba kwa “kunena” ni nzuri sana hasa
unapokuwa katika michakato ambayo inachukua attention yako. Mtume Paulo
anatufundisha kwamba tutumie mbinu zote mbili. Kuomba kwa lugha na kwa
akili pia. “usikae kimya usiku wala mchana” (Isaya 62) usifungwe na
muda.
Ukisikia unasukumwa KUFUNGA, fanya hivyo kwa kipimo cha
mambo unayojihusisha nayo kama umetingwa na KAZI au aina ya MAJUKUMU
yanahitaji sana nguvu za mwili. Ikiwezekana jipe siku malumu katikati ya
wiki na kama kazi yako inahitaji nguvu nyingi za mwili jaribu kufanya
maombi ya namna hii wakati wa mapumziko ya wiki, nk. Kila mtu afanye
kama Roho Mtakatifu atakavyomongoza.
Neema ya Bwana wetu Yesu na izidi kwenu mnapojifunza na KUYATENDA haya. AMEN.
Frank Philip.