Saturday, January 4, 2014

UWEZO WA NENO LA MUNGU KUKUBADILISHA!!!


(Ushindi, mafanikio ya mwili na roho, amani, furaha, nk. vimefichwa kwenye Neno. Jua ni kwanini inakua ngumu huu ushindi kudhihirika kwako.)

Mara nyingi sana watu wamekua wasikilizaji wa Neno la Mungu na kuguswa kwa namna mbalimbali ila baada ya muda utagundua bado wanaendelea na tabia, mienendo, dhambi na maisha yao ya kale. Nini kimetokea? Neno walilosikia halikuwabdilisha! Kama lingewabadilisha wangeacha njia zao mbaya.

Daudi akasema “moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije nikakutenda dhambi”. Ina maana Neno la Mungu lina NGUVU ya kukuzuia kutenda dhambi. Utauliza ni kwa namna gani. Sikiliza, mambo yafuatayo. 1. Biblia inasema “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani” na imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. 2. “Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu” ina maana ukiwa na Neno utaona mitego mingi sana ya Ibilisi na kuepuka isikunase. Kumbuka “mitego” ni vitu vilivyofichika kukunasa au kukuangusha. 3. “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa” na “watu wanapotea kwa kutokujua Neno na Nguvu za Mungu” tunapata maarifa kutoka kwenye Neno, inamaana ukiwa na Neno uko salama na maangamizi ya adui. Haya ni baadhi tu. Swali ni kwamba kwanini watu hawabadilishwi na Neno la Mungu na wanazidi kuishi katika njia zao mbaya?

Tujifunze mambo machache ya kutusaidia katika maisha yetu na kisha tuone tanaponaje. Nitatumia mfano wa MAHUSIANO (ndoa, uchumba, kifamilia, nk.). Katika mahusiano kila mmoja huwa anakua na mahitaji kutoka kwa mwenzake. Matatizo makubwa ya kijamii yako katika mahusiano. Kufanikiwa kwa UHUSIANO unatokana na KIWANGO cha kila mmoja katika uhusiano huo kutenda WAJIBU wake na KUMPENDEZA mwenzake. Sasa sikiliza. Kama kuna SHIDA ya uhusiano jua kwamba WOTE wawili mnahitaji DAWA ambao inapatikana katika Neno la MUNGU. Utasema kwa vipi, “Mungu akitaka kuliponya taifa, au watu wa taifa fulani hulituma Neno”. Watu wakilisikia na kulitii hao watu wanapona katika SHIDA yao.


Nataka nikwambie aina 3 za mioyo. Maana Daudi alisema “moyoni mwake ameweka Neno” kwa hiyo Neno linakaa Moyoni sio kichwani. Na sehemu nyingine tunasoma “kwa moyo mtu huamini na kupokea wokovu” sio kwa kichwa mtu hukumbuka na kuamini. Sawa, sasa sikiliza. Aina za mioyo: 1. Moyo wa jiwe: Huu haupokei kitu. Ni kama jiwe la mtoni liko kwenye maji lakini ndani ni KAVU, no absorption! Paulo aliuita moyo wa aina hii kwamba ni moyo wenye “ganzi”. 2. Moyo wa nyama: Huu unapokea vizuri na ni moyo mzuri unaobadilika kama Neno likiingia humo. 3. Moyo wa KIOO: Huu ni moyo ambao UNAVUTA kila NENO kwa bidii sana ila HUAKISI kwa MTU mwingine na kuhamisha hilo Neno kama lilivyo na “kioo” kubaki kitupu. KUMBUKA ukiona umesikiliza MAFUNDISHO ya watumishi mbali mbali wa Mungu na shida yako ipo hapo iwe ya uhusiano au nyingine, jua kuna shida ya MOYO wako na sio Neno au mhubiri wala upako wao.

Umewahi kujiuliza mtu anahudhuria seminara ya NDOA, na watumishi wa Mungu wanateremsha NENO kwa UPAKO wa hali ya juu na mafunuo makubwa makubwa LAKINI shida ya ndoa imesimama kama HAKUNA kilichotokea? Shida iko wapi? Shida iko Moyoni! Kama sio JIWE basi ni KIOO! Sifa ya mtu mwenye moyo wa KIOO ni kujikusanyia MAFUNDISHO ya NGUVU ili kuthibitisha UDHAIFU wa mwenzake, mfumo au jamii inayomzunguka. Mara zote Roho Mtakatifu akileta POINT ya maana utasikia mtu anasema “unaona?” au “si nilisema?” au “hata mtumishi kasema hivyo hivyo, hii ndio shida na watu hawataki kunisikia” au “hili Neno anatakiwa fulani asikie hili”, nk. Ukijikuta una-respond kwa mtindo huu jua kuna KIOO ndani yako. Pamoja na kujikusanyia MAFUNDISHO ya kila UBORA wa juu, kama una moyo wa kioo, utakua tu ukichambua “watu” wengine kwa WINGI kwa mafundisho yako na wewe binafsi kubakia na MISHIDA yako inakukodolea macho! Kwa maana “Mkono wa Mungu haukupungua urefu wala nguvu hadi ushindwe kuokoa” sasa mbona Hauokoi? Je! Neno limepungua nguvu? La! Hasha. Yesu jina lake jingine ni Neno la Mungu, na hajawahi kushindwa KITU, ila anabisha kwenye “mlango ya moyo wako”, ukifungua utaona mwenyewe atakavyo kuhudumia na kuleta DAWA katika shida zako ZOTE. Shida sio Yesu/Neno shida ni MOYO wako! Tengeneza MOYO wako na NENO litakubadilisha bila shaka.

Mfalme Daudi yeye hakuomba UTAKASO wa moyo, aliomba moyo MPYA! Aliona hizi toba zimekua nyingi na mambo hayaendi sasa, akamwambia Mungu “niumbie moyo safi (“create” in me a clean heart!)”. Kama kuna eneo unatakiwa kushughulika nalo sana ni Moyo! Ndio maana maandiko yanasema “linda SANA moyo wako KULIKO vitu vyote ulindavyo”. Kwanini? Huko ndiko kuna SIRI ya kushinda au kushindwa kwako! Uzima unatokea humo, na mauti inatoke humo pia! Ndio maana Yesu akasema “sio kile akilacho mtu HUMNAJISI ila kile kimtokacho”. Kutokea wapi? Jibu ni MOYONI. Uzinzi, uongo, ufisadi wa kila namna, tamaa, nk, makao yao ni moyoni mwako. Shughulika na moyo nakwambia “viungo” vingine vya mwili ni mateka tu na vinatumika kama watumwa ila bwana wao anaitwa MOYO! Shughulika na bwana mkubwa “moyo” na kila kitu kitakia kimya!

Sasa watu wengi sana wako busy kujitakasa kwa Damu ya Yesu. Kweli inatakasa, lakini ukifuatilia maandiko utagundua Neno la Mungu linafanya hiyo kazi pia. “Uwatakase kwa Kweli yako, Neno lako ndio Kweli!” Ibilisi anakuweka mbali na Neno la Mungu akijua lina NGUVU ya kukutakasa na KUKUPONYA, sio tu magonjwa ila hata na matatizo na shida ZOTE za duniani (formula ya maisha yako imefichwa kwenye NENO). Ufumbuzi wa matatizo yako yote uko kwenye NENO asikudanganye mtu, unachohitaji ni UFUNUO kwenye hilo Neno, na hapo ndipo pa GUMU ila OMBA na tafuta KUSUDI la Mungu katika KILA unachokifanya itakusaidia kuwekeza nguvu na muda wako. {kwa ufafanuzi zaidi soma somo jingine humu lenye kichwa “KAZI YA MVUVI”} uone jinsi Yesu ambavyo sio mvuvi wa samaki lakini anamsaidia mvuvi mzoefu kwa kumpa NENO la maelekezo na kazi inakua rahisi na ya mafanikio makubwa.

Sasa ili Ibilisi akutese lazima akuweke mbali na Neno la Mungu, au akishindwa anashughulika na moyo wako. Kama hatupii “jiwe” basi anatupia “kioo” (lugha ya kwenye Agano jipya ina sema Ibilisi “hulinyakua Neno”), unasikia lakini ganzi tupu! ILI usije ukaamini “ukaokoka”! Hii ni vita KAMILI na ni KALI sio utani. Ndio maana sio kuombea tu ugali kabla ya kula, ombea hata Neno la Mungu kabla ya kusoma ili lizame mahali pake, upata UFUNUO na lifanye mabadiliko katika maisha yako. Usisahau uwezo wa kupokea Neno na kuleta mabadiliko ni katika moyo wako kwa hiyo ombea na moyo wako uwe kama “udongo tifutifu”, ili kila Neno likidondoka hapo lizae 1:100, 1:60, 1:30, nk. Haiwezekani usome, usikie au ukutane na Neno HALISI la Mungu uwe kama ULIVYO haiwezekani! Lazima kuna shida mahali. Mungu atusaidie kujua siri hii. AMANI na BARAKA zizidi kwenu.

Frank Philip

No comments:

Post a Comment