Saturday, January 4, 2014

NGUVU ya VINYAGO ndani YAKO!!!


Nabii Elisha alikua mkulima na alikua na JOZI kadhaa za ng’ombe (MAKSAI). Alipoitwa katika kazi ya Bwana alichofanya ni KUCHINJA wale maksai na kutumia vifaa vya majembe yake kama kuni! Wakala nyama na kusherehekea mwisho wa HUDUMA ya UKULIMA. Elisha akamgeukia Eliya na kuanza kazi kwa nia moja. Kumbuka Elisha alikua na NJIA moja, hapakua na njia ya kurudi nyuma maana ALIANGAMIZA (vinyago) vya ya biashara ya kwanza!

Yesu alipomwita Petro kutoka katika biashara ya UVUVI, Petro alikuja na kuanza huduma kwa nguzu sana ila kwenye STOO yake alihifadhi zile NYAVU na MTUMBWI vya kuvulia samaki. Alipokua KARIBU na Yesu, Petro alikua na ujasiri mkubwa sana kuliko hata wenzake. ILA katika vipindi vigumu na Yesu akiwa hatua kidogo tu mbali naye wakati wa MATESO, Petro anamkana YESU! Tena mara tatu! Siku Yesu ameuwawa, Petro akapiga mahesabu na kukumbuka zile NYAVU na MTUMBWI kule stoo na KURUDI kwenye kazi yake ya kuvua samaki! Baada ya kufufuka, Yesu akaenda tena kwa “mara ya pili” kumtafuta Petro kule ziwani akiwa BUSY KUVUA SAMAKI. Kumbuka, Petro alikwisha jua kua yeye ni “mvuvi wa WATU” sasa ilikuaje akarudi kuvua samaki? Sababu ya msingi ilikua ni KUKATA TAMA na kuona “hii biashara ya kumfuata Yesu hailipi”, lakini pia bado alikua na NYAVU zake na VIFAA (VINYAGO) vya ile kazi ya zamani! Akarudi huko tena maana “vinyago” vilikuwepo na sio vya KUTAFUTA.

Katiaka maisha yetu ya zamani hakuna mtu yeyote ambaye “hakua” na VINYAGO ambavyo aliviabudu. Zile dhambi na kazi mbaya za Ibilisi. Watu wengi wameamua kumfuata Mungu ila kwenye stoo zao (MIOYONI) bado kuna VINYAGO wameweka akiba huko. Wakifika mahali PAGUMU walio wengi wanarudi “stoo” na kunyanyua kinyago maana ni rahisi kuchukua KINYAGO wakati wa majaribu kuliko KUFUNGA na KUOMBA ili MUNGU akuvushe na kukufikisha MAHALI pa USHINDI wako.Hatari kubwa ya VINYAGO ni kwamba huwa VINASEMA. Wakati umevijaza ndani ya MOYO wako na unaenda mbele za Mungu na KUMUULIZA juu ya “jambo maishani mwako”, Mungu anasema “nitakujibu sawa na vinyago vyako”. Kwa sababu umeishi katika TAMAA na kumbukumbu (IBADA) ya vinyago vyako unapotelea humo ukizani ni Mungu amekujibu, kumbe ni “sauti ya vinyago”! Kwani hujui kwamba Mungu aliapa kwamba hatashindana na mwanadamu? Sasa jua hili, uking’ang’ania vinyago vyako jua Mungu hakunyang’anyi kwa nguvu ila utaangamia navyo usipogeuka. EZEKIEL 14: 3“Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote? 4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake” (Umewahi kujiuliza ni kwanini maombi ya kutafuta mchumba ni MAGUMU sana, ila maombi ya HUDUMA Mungu anajibu haraka? Asikiaye na afahamu!)

Kama kuna kitu Mungu hapendi ni mtu wa nia MBILI. Joshua akawauliza wana wa Israel wachague wanamtumikia Mungu au NANI? Hakuna katikati, kama wanamfuata Mungu lazima kusema wazi na sio kujibandika LABEL mbili, moja ya Mungu na nyingine ya Ibilisi. Musa alipokua anashughulika na maasi ya Kora alisema neno hili “walio upande wa Mungu waje huku na walio upande wa Kora waende kule”. Nakwambia wale wa upande wa Kora ambao waliambudu VINYAGO vyao walijitenga kule na ardhi ikafunguka wakamezwa humo! Usisahau, mwisho wa VINYAGO ni kukuangamiza na kukumaliza bila kujua kwa sababu vinyago VINAVUTIA macho na vyafaa sana kwa CHAKULA.

Wana wa Israel walijua kabisa huko mbele kuna nchi ya ahadi inayotiririka MAZIWA na ASALI, lakini “hapa katikati” kuna KUFAULU mtihani. Lazima kupita JANGWANI miaka ya KUTOSHA, kuna mataifa kadhaa ya kupigana nayo VITA, kuna kuishi kwa kula MANA, chakula ambacho baba zao hawakukijua, na kuna masharti sio kula tu ovyo, hakuna kuokota MANA siku ya Sabato (kula kwa nidhamu). Biblia inatuambia walivaa mavazi yao na viatu vyao havikuchakaa. Inamaana hapakua na “viwalo” vya kubadili kwa wale warembo. Ghafla! watu wakakumbuka kule Misri masufuria ya nyama na kuanza kutamani VINYAGO vya zamani. Kumbuka NYOKA ZA MOTO zilikuja kuwashughuikia maana walianza manung’uniko huko jangwani. Kiu ni kali hadi Musa anamkosea Mungu maana alishindwa KUMSTAHI mbele za hao maelf ya watu ambao wako “desperate”, akakosa uvumilivu na kushindwa kufuata malekezo vizuri! Unapobanwa na mambo mengi sana ANGALIA usikose KUMSTAHI Mungu mbele za hao “watu” na kwa sababu ya VINYAGO vyako ukamvunjia Mungu heshima yake. Chunga sana maana saa ya kujaribiwa inakuja. Simama kwa uaminifu na kwa maombi na saburi. TUPA vinyago vya zamamani na uwe safi bila njia mbili mbili, Mungu atakurehemu utavuka salama la sivyo vinyago VITAKUANGAMIZA.

Kumbuka siku zote, kama ulikua na MPENZI wa zamani na sasa umeamua kumfuata Mungu, jaribu kubwa sio UZINZI tu ila ni yule jamaa/binti maana ndani yako amekua KINYAGO na kila ukifinga macho unaona kinyago “hiki hapa”. Ibilisi anajua vyema juu ya ibada ya SANAMU hivyo kila ukifunga macho, anakuletea zile VIDEO na SAUTI kwa maana VINYAGO huongea! Gafla unatamani kurudi Misri na kusahau UKOMBOZI mkuu wa MKONO wa Mungu ulionyooshwa ULIOKUOKOA. Unarudi kusujudu SANAMU na unajikuta unaingia katika mtego wa maasi ya KORA. Mambo yote yanatokea JANGWANI! Hapo ulipobanwa na UHITAJI na ADHA mbalimbali, hapo ndio KIPIMO cha UAMINIFU wako kwa Mungu wako. Jipe moyo basi maana BWANA wetu alisema “ulimwenguni mnayo dhiki laikini jipeni moyo, Mimi nimeushinda ulimwengu”, WEWE pia Utashinda. Shughulikia vinyago vyako na KUVISAHAU nawe utakua salama. AMEN.


Frank Philip

2 comments:

  1. KAKA TUNABARIKIWA SANA NA NENO TOKA KWA,,,UMEBARIKIWA KAKA...YESU YUKO NAWE...

    ReplyDelete