Wednesday, March 6, 2013

MISINGI YA UHUSIANO MZURI (O1)


SEHEMU YA KWANZA

MISINGI YA UHUSIANO MZURI

1) Upendo
2) Msamaha
3) Mawasilano
4) Uaminifu

1. UPENDO
“Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa mungu; na kila
apendaye amezaliwa na mungu naye anamjua mungu.Yeye asiyependa
hakumjua mungu, kwa maana mungu ni upendo.”
Yohana 4:7-8

Naamini karibia kila mmoja wetu anapenda kupendwa, ila sina hakika kama ni wote tunaopenda kupenda. Ili uhusiano wowote uwe mzuri, utengeneze mizizi na ustawi vizuri na kutoa matunda mema, uhusiano huo unaitaji kuwa na upendo ndani yake. Upendo ni kitu cha kwanza muhimu kwenye aina yoyote ya mahusiano. Yawezekana umetamani kusikia mtu akikuambia nakupenda lakini umemkosa; yawezekana hata wazazi wako wameshimdwa kukuaambia au kuonyesha upendo wao kwako, yawezekana umekaa na kujiona ni mtu wa kuchukiwa na watu wote. Neno nakupenda limekuwa bidhaa adimu kwako, umefikia hatua ya kujikataa. Nina habari njema kwako, kuwa kuna mtu anakupenda, anaitwa Yesu. Yesu alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu, akafa kifo cha aibu pale fuvu la kichwa, juu ya msalaba kwa ajili yako. Hata sasa Yesu anasema anakupenda. Upendo wake hauna kipimo. Upendo wake kwako ni wa gharama ya damu na kifo. Ili akuonyeshe ni jinsi gani anakupenda, aliiacha mbingu akaja duniani aishi na sisi, akala vyakula vyetu, akavaa mavazi yetu, akalala na kutembea nasi. Yeye hakuona kukaa mbinguni kuwa kitu akashuka kutufuaata wanadamu.


Hii ni baada ya mwanadamu wa kwanza Adamu kupoteza uhusiano wetu mzuri na Mungu, Mungu hakuweza kutulia mbinguni, maana masikani yake ni pamoja na wanadamu. Baada ya mwanadamu kupoteza uhusiano wake mzuri na Mungu kilichofanya arudishe uhusiano wake na mwanadamu huyo ni upendo wake mkubwa. “KWA MAANA NJISI HII MUNGU ALIUPENDA ULIMWENGU”. Aliupendaje ulimwengu? Ni kwa kumtoa mwana wake pekee awe daraja, awe patanisho kati yetu na Mungu. Yesu akaamua kulipa gharama ya upatanisho huo, gharama hiyo haikuwa nyingine ila damu isiyokuwa na hatia, uzao wa mwanamke bikira, hakuna mwengine ye yote ambaye angeweza ilipa gharama hiyo zaidi ya Bwana wetu Yesu.
Ambaye kwa uweza wa Roho matakatifu kupitia bikira Mariamu alizaliwa.

“Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika
ndoto, akisema, Yusufu mwana wa Daudi, usohofu kumchukua Mariamu
mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa
mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakaye waokoa
watu wake na dhambi zao.” Mathayo 1:20-21.

Biblia inatuthibitishia kwamba Yesu alikuja kwa ajili yetu, kutuokoa, kurudisha uhusiano wetu mzuri na Baba yetu wa mbinguni. Maana sisi ni watu wake kama vile ambavyo malaika alimwambia Yusufu kwamba yeye ndiye atakaye waokoa watu wake. inafurahisha kujijua kuwa sisi ni watu wake Mungu, sio watu wake tu bali watoto wake, pia ni rafiki zake kama
tutakavyo kuja kuona huko mbele tutakapo zungumzia urafiki.

MAANA YA UPENDO
Upendo una maana nyingi, lakini maana zote zinakaribiana;
• Kuumia kwa ajili ya mwengine. Isaya 53:3-10
• Kuhesabu wengine kuwa bora kuliko wewe
• Kuwa tayari kupoteza maisha yako kwa ajili ya mwengine.

“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye
sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa
wala hatukumhesabu kuwa kitu.
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu;
Lakini tulidhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake
mwenyewe;
Na BWANA ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.
Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama
mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,
Na kama vile kondoo anyamazavyo
Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.
Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;
Na maisha yake ni nani atakaye simulia?
Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;
Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;
Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;
Ingawa hakutenda jeuri. Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.
Lakini BWANA aliridhika kumchubua; Amemuhuzunisha;
Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,
Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,
Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake.
Isaya 53:3-10

Maandiko haya yanayoelezea maana ya upendo kwa undani sana. Mtu akikuambia anataka kujua maana ya upendo mwambie asomee Isaya 53. Nabii Isaya anaelezea upendo wa Mungu kwetu ulivyo au kwa lugha nyingine anaelezea na kutoa maana halisi ya upendo. Je, ni watu wangapi wanakuambia wanakupenda lakini hawapo tayari kuumia kwa ajili yako, wanaishia kukupenda kwa maneno tu? Huo sio upendo. Tutaona ni jinsi gani upendo unavyoambatana na vitendo.
Yesu alikuwa tayari kuumia kwa ajili yetu. Alikuwa tayari kuyapotezamaisha yake kwa ajili yetu. Alipigwa ili sisi tupone. Alizaliwa katika hali ya umasikini ili sisi tuwe matajiri, hata kama asingesema kwa manenokwamba anatupenda,vitendo vyake vinonyesha na kusema ‘nakupenda, sipendi kuona ukiishi maisha ya utumwa wa dhambi, maisha ya kuteswa na magonjwa, kusumbuliwa na kuteswa na nguvu za giza akasema basi imekwisha!; Hata leo yawezekana bado unamfanya Yesu aendelee kuumia kwa sababu hutaki kumpa maisha yako ayaongoze. Unaufanya moyo wako kuwa mgumu, lakini bado anakuita anatamka kwa nguvu nakupende! Nakupenda! Nakupenda

......SOMO LINAENDELEA!!!

No comments:

Post a Comment