Saturday, May 19, 2012

SOMO LA WIKENDI......SABABU ZA KUFELI NA KUSHINDWA


SABABU ZA KUFELI NA KUSHINDWA
(FACTORS OF FAILURE)

Kwanini watu wa Mungu wanafeli au wanashindwa au wanakwama?
Hili ni swali la muhimu sana ambalo linaweza kuwa kama funguo ya dhahadu katika mlango wa mafanikio a maisha yetu. Kama tukilifungua swali hili vizuri, tutaweza kupata majibu ya matatizo mengi katika maisha yetu sisi watoto wa Mungu. Kulingana na ukweli (Neno la Mungu – Biblia) sisi wana wa Mungu ni “washindi na zaidi ya washindi, katika mambo yote (Warumi 8:37;   1Wakorintho 15:57).

Kulingana na Ukweli wa Neno la Mungu, watu wa Mungu tumeshabarikiwa na kukabidhiwa vitu vyote tunavyohitaji kwa ajili ya maisha yetu yote ya mwilini na rohoni (Efe 1:3; 2Pet 13-4). Kama ni ushindi juu ya dhambi na dunia, uwezo huo tumeshapewa na Bwana. Mtu wa Mungu akikumbwa na tamaa za dunia hii, ina maana kwamba, yeye mwenyewe ameruhusu au amekubali kumtii shetani kuliko Mungu (Wagalatia 1:3-4; 1Yohana 2:15-17). Kama ni ushindi dhidi ya nguvu za giza, mapepo na wachawi; Mungu amekwishatupa uwezo huo wa kuwashinda watenda kazi wote wa ibilisi shetani (Wakolosai 1:13; Luka 10:19)

Kama ni ushindi katika afya, tumepewa na tumeponywa tangu damu ya Yesu ilipomwagika msalabani kwa ajili yetu, na kwa kupigwa kwake sisi tulikwishaponywa tayari (1Petro 2:24; Mathayo 8:17). Kama ni jambo la uchimu na utajiri, watu wa Mungu tulkwishafanywa matajiri na Kristo, kwa kifo chake. Yeye alichukua umaskini wetu akatupa utajiri wake (2Wakorintho 8:9; 2Wakorintho 9:11). Kama ni suala la akili an hekima, watu wa Mungu tumekwishapewa uwezo mkubwa wa kiakili na fikra, kwa Roho Mtakatifu wa Mungu anayeishi ndani yetu. Sisi wana wa Mungu tuna akili na ufahamu wa kiungu. (Isaya 11:2; Zaburi 111:10; Matendo 6:8-10; 2Timotheo 2:7)

Kama ni baraka katika mikono yetu, tumekwishapewa na Mungu kwa ajili ya shughuli zetu (Kumbukumbu 28:1-8; Zaburi 1:1-3) Kama ni ulinzi juu yetu na nyumba zetu na mali zetu, Bwana amekwisha waagiza malaika zake watuzunguke kwa panga za moto, farasi, magari ya moto (kufanya ukuta mzito wa moto) kutuzunguka (Zaburi 34:7; 2Wafalme 6:15-17; Zaburi 121:1-8; Zaburi 91;1-11-12).

SABABU ZA KUFELI NA KUSHINDWA

Kila kitu ambacho watu wa Mungu tunachohitaji katika maisha yetu yote ya mwilini an rohoni, tumekwisha kupewa na Baba yetu aliye mbinguni, ili tuweze kuishi maisha ya ushindi katika kila eneo linalotuhusu au linalotuzunguka. Kama ukweli ndio huu basi, kwanini watu wa Mungu wengine wana maisha ya kushindwa na kufeli? Kwanini watu wa Mungu wengine wanaishi maisha ya kuhangaika na kukosa? Ni lazima kuna sababu.

1            KUTOKUJUA
Mungu anasema watu wangu wanaangamia (wanateseka na kuhangaika) kwasababu ya kukosa maarifa (ufahamu na ujuzi wa mambo niliyokwisha watendea) … japo wana bidii nyingi lakini wana bidii bila maarifa (wanapoteza nguvu nyingi katika maisha) (Hosea 4:6;  Warumi 10:2) Ndio maana Paulo alikuwa anawakazania sana wanafunzi wake ili wapate Roho ya hekima na ufunuo, ili wapate “Kujua“ mambo tuliyokwisha kupewa na Mungu kupitia Yesu Kristo. Alimwambia Timotheo hivi, yafahamu sana mambo haya… (2Tim 2:7).

Ndugu yangu, mambo usiyoyajua, hutaweza kuyapata; hayatatendeka maishani mwako. Kujua ndio mwanzo, ndio ufunguo wa kuyafungulia ili yaweze kuja kwako. ndio maana tunaambiwa Neno la Kristo likae kwa wingi katika mioyo yetu, kwa hekima yote … kuyajua maandiko matakatifu kunatuhekimisha ili tupate ufahamu wa haki zet na baraka zetu (Wakolosai 3:16; 2Timotheo 3:15-17) Ukitaka ufahamu na ujuzi, soma kwa bidii Neno la Mungu. Pata maarifa.

2            KUONA VIBAYA
Kutokujua kunasababisha kuona vibaya. mtu asiyejijua kuwa yeye ni shujaa, atajiona dhaifu. asiyejijua kuwa yeye ni mzima, ayajiona mgonjwa. asiyejijua kuwa yeye ni mbarikiwa, atajiona ni maskini. Soma vizuri habari ya wana wa Israeli kitabu cha Hesabu sura ya 13 na 14 yote, utaona jinsi wana wa Isreali walijiona wao ni kama panzi mbele ya wenyeji wa Kaanani. Hii ni kwasababu hawakujua vizuri na kwa uhalisi, uwezo wa Mungu aliye pamoja nao, japo waliyaona matendo yake ya ajabu. kutokujua kunasababisha kuona vibaya.

Hii ndio sababu iliyomfanya Mtume Paulo atuombea Wakristo tupate kufunguliwa katika macho yetu ya ndani, ili tuweze kuona vizuri, mambo ya rohoni. tukiona vizuri, tutapata ufahamu sahihi wa jinsi tulivo rohoni na jinsi tunavyotakiwa kuwa katika mwili (Waefeso 1:15-19).

Gideon alikuwa anajiona yeye ni dhaifu na muoga lakini Mungu akimuangalia anamuona yeye ni shujaa, na ndio maana Mungu alimwita “ewe shujaa” japo kuwa yeye Gideoni alikuwa katika maficho kwa hofu ya maadui. Soma vizuri habari hii katika (Waamuzi 6:11-14) Bwana akamwambia “enenda kwa nguvu zako”. Maana yake ni kwamba, kumbe Gideoni alikuwa na nguvu za kutosha ndani yake, lakini hakujua! Kutokujua kunaweza kukunyima kusonga mbele. kutokujua kulimfanya ajione mnyonge mbele ya maadui wao. Mungu akusaidie kujiona sawa sawa na yeye anavyokuona na sio kama unavyojiona wewe

Kama utatumia mwanga wa manjano ndani ya nyumba yako, vitu vyote vitaonekana ni vya manjano. Kama ukitumia mwanga mwekundu, vitu vitaonekana ni vyekundu. Vivyo hivyo katika dunia, Yesu anasema kwamba yeye ndiye nuru (mwanga) wa ulimwengu (Yohana 1:7-9) Tukimtumia yeye kuangalia mambo yetu, yataonekana vizuri kuliko tunavyoyaona sasa. Yesu ni Neno (Yohana 1:1-4; Ufunuo 19:11-13). Tumia Neno la Mungu (mwanga bora na halisi) kutazamia maisha yako, utayaona kama Mungu anavyoyaona na si kama wewe unavyoyaona. Kwa Neno la Mungu, Hutajiona mgonjwa bali mzima; hutajiona maskini, bali tajiri; hutajiona dhaifu bali hodari. soma sana Neno la Mungu ubadilishe unavyojiona. Kuona sawa sawa kutakuokoa na jambo lifuatalo.


3            KUWAZA VIBAYA
Kutokujua kunasababisha kutokuona sawa sawa; na kutokuona vizuri kunasababisha kutokuwaza sawa sawa. Kwa lugha rahisi, Kuwaza vibaya ni matokeo ya kuona vibaya. na mtu wa Mungu akitawaliwa na mawazo mabaya juu yake, anasababisha nguvu za Mungu zisifanye kazi juu yake na hiyo inaletakushindwa kimaisha kwa watoto wa Mungu wengi. Sikiliza, mawazo ni daraja lililo katika ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Ndio maana mtu anaweza kusafiri mbali sana kimawazo tu wakati mwili wake upo hapo hapo mlipo. mawazo yakihama, mtu anaweza asiwe anasikia unachosema wala asione unachodhani anaona japo macho yake yako wazi kabisa. Hii ni kwasababu, mawazo yake yamehama; mtu huyo hayupo hapo kimawazo, bali yupo sehemu nyingine kabisa japo mwili wake upo hapo hapo mlipo. Mawazo ni daraja la mambo ya rohoni na mambo ya mwilini.

Mawazo hutawala mambo ya mwili.
Kwa mfano; mtu anayetembea katika barabara ndefu yenye maduka mengi na vitu vingi, bila kuchoka hata kama ni kilometa 5, kwasababu macho yake yanaangalia vitu vingi na mawazo yake yanaona vingi (yako busy). Lakini mtu huyo huyo anapotembea katika barabara nyingine ya urefu ule ule, isiyo na maduka pamoja na vitu vingi vya kutazama, mtu huyo huyo atasikia kuchoka na ataiona safari ile imekuwa ndefu sana kuliko ile ya mwanzo. Tofauti yake ni kwamba, katika safari ya pili, mawazo ya mtu huyo hayakushughulishwa sana kwakuwa macho yake hayakuwa na mambo mengi ya mazuri ya kuvutia kutazamwa; na hali hiyo imesababisha mtu huyo, kujisikia kuchoka katika mwili. Hii inathibitisha kwamba, mawazo hutawala mwili.

Mfano mwingine; mtu aliyebanwa na haja ndogo barabarani, akiangalia kushoto na kulia, akakosa mahali penye choo, mwili wake hutulia. lakini kadri mtu huyu anavyokaribia nyumbani au mahali popote penye choo, mwili wake huanza fujo za kutaka kuachilia ile haja iliyobanwa kwa muda mrefu. kadri mawazo yanavyotambua kwamba hapo karibu kuna choo, ndivyo mwili unavyokosa nguvu ya kuendelea kujibana. mtu huyo akikimbilia chooni na kumbe akakuta kuna mtu chooni, mwili wake, kwa mara nyingine, hukubali kujibana mpaka nafasi ipatikane. Hiyo inaonyesha kuwa, mawazo hutawala mwili.

Mfano mwingine; watu wawili walipigana sokoni. Mmoja akampiga mwenzake kichwa katika upaji wa uso wake. Yule aliyepigwa, alipasuka katika upaji wa uso wake na damu nyingi ikamtoka. Fikiri mwenyewe; upaji wa uso wa mtu wa kwanza umeupasua upaji wa uso wa mtu wa pili, lakini upaji wa uso wa mtu wa kwanza haukupasuka, bali ulivimba tu kidogo. Unadhani tofauti yake ni nini? Jibu: Ni kwasababu, mawazo ya mtu wa kwanza, yalijua tunakwenda kumpiga mtu wa pili kwa kichwa;
kwahiyo, nyama za mwili wa mtu wa kwanza zilikuwa zimeshaandaliwa kwa mawazo ya huyo mtu wa kwanza; lakini mawazo ya mtu wa pili, hayakujua kuwa kuna kichwa kinakuja kutupiga, hivyo nyama za mwili wa mtu wa pili zilikuwa hazijaandaliwa kupokea kipigo; na ndio maana upaji wa mtu wa pili ukapasuliwa na upaji wa mtu wa kwanza. Hii inathibitisha kwamba, mawazo hutawala mwili.

Kwahiyo mtu wa Mungu, Biblia inaposema tugeuzwe fikra zetu, ina maana kubwa sana. Kwasababu, fikra zako zikiwaza vibaya, uasababisha mambo yako ya mwilini kwenda vibaya, hata kama wewe ni mwombaji. Lazima ujifunze kuwaza sawa sawa kama Neno linavyosema kuhusu wewe. Mkumbuke Gideoni, alikuwa anajiona dhaifu na ndio maana alikuwa dhaifu na maisha yake yakawa ya kitumwa. Lakini Mungu alipomwambia kwamba yeye ni hodari na shujaa, Gideoni akageuza fikra zake, akajiona shujaa (kama Mungu alivyokuwa anajiona na sio kama yeye alivyokuwa anajiona mwanzoni).

Mungu hakuwa na haja ya kumpa Gideoni nguvu kutoka mbinguni, balin mawazo mazuri ya ushindi yalitosha kumpa Gideoni nguvu za ajabu. kwa lugha nyingine, mawazo mazuri ya kishujaa, yalifungulia nguvu za Mungu zilizokuwa ndani yakena Gideoni, akaweza kuwaongoza Waisraeli katika ushindi mkuu dhidi ya adui zao. Tena kitu cha kushangaza, askari 300 tu wa Israeli waliwapiga maadui waliokuwa zaidi ya elfu 30.  (Soma vizuri habari hii katika kitabu cha Waamuzi sura ya 6 na 7).

Kwahiyo, ukujiona dhaifu, utasababisha udhaifu katika maisha yako. Ukijiona maskini au huwezi, utasababisha balaa, nuksi, mikosi, kushindwa na ufukara katika maisha yako au katika biashara yako au shamba lako au mifugo yako. Badilisha unavyojiona, utajikuta unabadilisha unavyojiwazia. Tumia Neno la Mungu kugeuza fikra zako na kuzifanya mpya, kuanzia sasa. Kulingana na Biblia, wewe ni shujaa na si dhaifu (Waefeso 6:10); wewe ni mzima na si mgonjwa (2Petro 2:24); wewe ni tajiri na si maskini (2Wakorintho 8:9); wewe ni huru na si mfungwa katika nguvu za giza (Wakolosai 1:13).


Tumia Neno la Mungu kugeuza fikra zako na kuzifanya mpya, kuanzia sasa. Badilisha unavyojiona, utajikuta unabadilisha unavyojiwazia. Ukijiwazia mawazo mazuri ya ushindi na mafanikio, ndivyo utakavyosababisha katika mwili wako, kwasababu mawazo hutawala mwili.

Ndio maana Neno la Mungu linasema; fikra zetu zigeuzwe na kufanywa upya kwa Neno la Mungu (Warumi 12:2; Waefeso 4:17-23-24). Hii inatokana na kanuni ya kwamba, mawazo ya nguvu ya kutawala mambo ya mwili. Ndio maana mtu wa Mungu inakupasa uwe na mawazo safi. Mungu Baba yako mwenyewe anakuwazia mawazo mazuri ya matumaini (Yeremia 29:11) Nakushauri ujifunze kujiwazia mawazo mazuri.

Usijione tena duni au dhaifu au mtu wa kushindwa au mtu wa kuugua au sio mzuri. Hapana, jione tofauti; jione mzuri, jione unaweza, jione una nguvu za kushinda, jione hodari na shujaa, jione kuwa wewe ni mzima hata kama hali ya afya yako ya mwili si nzuri, jione tofauti. Jione wewe uko huru hata kama huwa unajijua unasumbuliwa na nguvu za giza. Badilika! Jione tofauti. Jione wewe ni tajiri, mtu wa mafanikio. Mawazo ni ufunguo! Ukijiona vizuri (kama Mungu anavyokuona na si kama wewe unavyojiona) utapona katika tatizo linalofuata.



4            KUONGEA VIBAYA
Kama tulivyoona, ufahamu husababisha kuona; na kuona husababisha kuwaza; na mawazo husababisha maneno. Ukiona vibaya, utawaza vibaya; na ukiwaza vibaya utaongea vibaya. kuna nguvu ya ajabu sana katika maneno yetu. maneno ya nguvu ya kuumba. Biblia inasema ulimwengu uliumbwa kwa Neno la Mungu (Waebrania 11:3) Mungu aliumba vitu kwa kusema tu. Na kwakuwa Mungu ametushirikisha tabia ya uungu (Zaburi 82:6; Yohana 10:34; 2Petro 1:3-4) Kwahivyo basi, maneno yako yana nguvu ya kuumba. Hivyo, uwe mwangalifu unaongea nini au unajitamkia nini.
 
Chanzo cha nguvu ya maneno.
Nguvu ya maneno inatoka wapi? Maneno ni malighafi ambayo hutumiwa na Roho Mtakatifu au na roho wachafu (mapepo). Biblia inasema kwamba, kila andiko lenye pumzi ya Mungu (Roho) huwa Neno zuri la kufundishia na kuadabisha maisha ya watu. (2Timotheo 3:16-17) … na Neno la Mungu li hai na lina nguvu (Waebr 4:12) Hii ina maana kwamba;

                                     Andiko  +  Roho  =  Neno (Uhai na Nguvu)
                                            (2Kor 3:6)     (Mwa 2:7)    (Ebr 4:12)

Kwahiyo, Neno likivikwa “roho” linakuwa hai na linaweza kwenda kutenda kazi fulani. Ndio maana Mungu alisema kwasababu Neno langu ni Roho (yaani limevikwa au limejazwa Roho Mtakatifu), hivyo basi … Neno langu li hai, tena lina nguvu … na litokalo katika kinywa changu, halitarudi mpaka limeyatimiza mambo niliyolituma kufanya (Yohana 6:63; Waebrania 4:12; Isaya 55:10-11).

Hii ina maana kwamba, Neno la Mungu hupewa uhai na nguvu kutoka katika Roho Mtakatifu aliyelivika hilo Neno. Kwahiyo, unapojibariki kwa maneno mazuri, Roho Mtakatifu huja kulivika uhai na nguvu hilo neno lililotoka katika kinywa chako, ili liwe hai na liweze kukutimizia kile ulichotamka (ulicholituma kufanya). Kwa mfano; siku moja Bwana Yesu aliulaani mti na baada ya masaa kama 8 hivi, ule mti ulikufa! (Marko 11:12-14; 20-23) Tunaona Yesu hakutumia shoka au msumeno kuuua ule mti, bali alitumia maneno yake tu na ule mti ukafa.

Yesu alituma neno tu na Roho Mtakatifu akavamia lile neno na kulipa nguvu na uhai, hata likaweza kutenda kile ambacho Yesu amelituma kufanya; yaani kuua. Kuna nguvu ya ajabu sana katika maneno, kwasababu ya roho zinazoweza kuvamia hayo maneno na kuyafanya hai na yenye nguvu. Ndio maana Biblia inasema mtu hushibishwa maneno ya kinywa chake na mauti na ulimi huwa katika uwezo wa ulimi; na wote waupendao, watakula matunda yake. (Mithali 18:20-21). Hivyo basi, ukitamka maneno mabaya, Roho Mtakatifu hawezi kuja kulipa hilo neno lako uhai na nguvu; kwasababu Mungu habariki udhaifu au laana (negative words). Mungu anabariki maneno ya baraka tu (positive words).

Kwahiyo; ukijitamkia maneno ya mabaya ya udhaifu, laana, balaa na kushindwa, mapepo wachafu huja na kuvamia hayo maneno na kuyapa uhai na nguvu, na yatafanya kazi maishani mwako kukushibisha ulichotamka kwa ulimi wako mwenyewe. Umetegwa kwa maneno ya kinywa chako na umekamatwa kwa maneno ya midomo yako (Mithali 6:2).

Watu wengi hawajui kwanini Yesu alimtaka Petro akiri kwa  kinywa chake, tena mara tatu, kwamba anampenda Yesu (Yohana 20:1-19). Jiulize, jibu la kwanza la Petro, halikumtosha Bwana Yesu? Yesu hakuridhika? Kumbuka kwamba, Petro aliwahi kumkana Bwana Yesu kwa kinywa chake, tena mara tatu, ya kwamba yeye Petro hamjui Yesu. Hayo maneno ya Petro yalianza kuzaa matunda. Tunamuona Petro, baada ya kifo cha Yesu, Petro alianza kupata mawazo ya kuziridia nyavu zake za uvuvi wa samaki, kazi ambayo Yesu alishamwachisha.

Hayo yalikuwa matunda ya maneno yake; kwa lungha ya leo, tungesema Petro alikuwa anaacha wokovu!  Ndio maana ilimbidi Yesu kumfuata Petro na ndugu wanafunzi wengine, kule baharini. Na alipowapata, Yesu akaanza kumtamkisha Petro mara tatu ili kumsaidia Petro aweze kufuta maneno yake mabaya ya laana. Maneno ya kinywa chako yana nguvu ya kusababisha kile unachosema kitokee katika ulimwengu wa mwili, kwasababu kuna roho zinazowinda maneno ili zivae hayo maneno ya kuyaleta mwilini. Hivyo uwe mwangalifu unatamka nini. Ukitamka laana, pepo wachafu watakusaidia na utapokea laana. Lakini ukitamka baraka, Roho Mtakatifu pamoja na malaika (Waebrania 1:14) watakusaidia, na utapokea baraka, ushindi na mafanikio.

Ikikulazimu kutamka maneno ya udhaifu, usiyaache yananing’inia hivyo hivyo, mapepo yatakushibisha; bali hakikisha unayafuta kwa maneno mengine mazuri ya naraka na ushindi. Kwa mfano; Umetoka kwenye mtihani mgumu sana, watu wakikuuliza habari za mtihani, unaweza kuwajibu kwa ushindi tu kwamba ‘mtihani ulikuwa mzuri tu’ ingawamoyoni unajua mambo yalikuwa magumu. Lakini ikikulazimu, wee sema tu kwamba ‘mtihani kwakweli ulikuwa mgumu sana, lakini Mungu atanipigania’. Hapo utakuwa umeshafuta ule udhaifu kama Petro.

Kama unaumwa na hali bado si nzuri, unaweza kusema ‘namshukuru Mungu ninaendelea vizuri’ japo wewe binafsi unajua hali bado ni ngumu. Huo ushindi na uzima unaoukiri, utakuwa malighafi kwa Roho Mtakatifu, kukuletea uzima wako katika mwili. Lakini ikikulazimu, wee sema tu hali ‘hali yangu bado lakini Mungu ataniponya’. Hapo utakuwa umefuta ule udhaifu ulioutamka. Hili tunajifunza kwa Bwana Yesu mwenye; alisema udhaifu lakini hakuacha maneno yake dhaifu yananing’inia, bali aliyafuta kwa kutamka maneno mengi ya baraka na ushindi kwa nyuma yake.

Kwa mfano; Yesu aliwahi kusema “ulimwenguni mnayo dhiki (hili si neno zuri. lakini kahuishia hapo, bali alifuta udhaifu/kushindwa kwa neno la ushindi, akasema) lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu (yaani; alikuwa anatuambia kwamba, kama yeye ameshinda, na sisi tutashinda tu) Yohana 16:33. Pia aliwahi kusema “mwana wa Adam atauwawa (halafu akafuta kwa kusema) lakini siku ya tatu atafufuka (Marko 16:21).  Ndio Mungu anasema “aliye dhaifu na aseme mimi ni hodari” (Joel 3:10). Kwahiyo; kama unataka kubadilisha hiyo hali uliyonayo, usiseme jinsi hali ilivyo, bali tamka vile unavyotaka hali yako iwe katika mwili.

Tumia nguvu ya maneno yako, hata kama hali si ya kutia moyo sana, lakini usiseme wewe ni dhaifu, bali  sema ‘mimi ni hodari katika jina la Yesu’ (Yoel 3:10); usiseme wewe ni mgonjwa, sema ‘mimi ni mzima katika jina la Yesu’ (1Petro 2:24); usiseme wewe ni maskini, bali sema ‘mimi ni tajiri katika jina la Yesu’ (2Wakorintho 8:9); usiseme kwamba hutaweza, bali kiri kwamba ‘mimi ninayaweza yote katika Kristo anitiaye nguvu’ (Wafilipi 4:19). Hivyo ndivyo watu wa imani tunavyoshinda na zaidi ya kushinda katika dunia hii hii mbovu. Kwwahiyo umegundua kwamba, watu wa Mungu wengi wanafeli na kushindwa kimaisha kwasababu ya maneno yao wenyewe.


5            KUOMBA VIBAYA
Jambo jingine linalosababisha watu wa Mungu ambao ni wabarikiwa lakini wanaishi maisha ya shida na taabu ni suala zima la kutokuomba ipasavyo au kuomba vibaya. Katika sura ya tatu na sura ya nne, nimeongelea sana juu ya watu wa Mungu kutokuwa waombaji. Katika pointi hii, siongelei kutokuomba, bali naongelea kuomba vibaya. Kwahiyo utagundua kwamba, baadhi ya watu w Mungu, wana bidii sana katika kuomba lakini bado hawapokei yale wanayoyaomba, kwasababu wanaomba vibaya. Mungu anailalamikia hii hali kwa kusema kwamba, mnaomba lakini hampati, kwasababu mnaomba vibaya (Yakobo 4:3).

Mtume Paulo pia anasema watu wa Mungu wanabidii sanakatika mabo ya Mungu lakini si katika maarifa (Warumi 10:2; Hosea 4:6). Maana yake ni kwamba; watu wa Mungu wanavuja jasho sana lakini matunda wanayoambulia ni kidogo. Yesu naye anasema ninawashangaa, mbona mnavyohangaikia maisha, kula na kunywa na kuvaa, kama mataifa wasi na Mungu (Mathayo 6:31-32)

Maana yake ni kwamba, wana wa Mungu hatutakiwi kuhangaika na kuhenyeka duniani kwa ajili ya maisha na mahitaji yake kama mataifa, bali tunatakiwa kupata msaada wa Mungu katika kila eneo la maisha yetu, kwasababu sisi ni wa thamani kuliko maua na ndege na yeye Mungu ndiye anayetuhudumia sisi (kama anavyowahudumia ndege na maua). Maneno haya hayamaanishi tusiende kulima na kufuga au kusomana kufanya kazi; haimaanishi tusiende kufanya biashara, NO! Maana yake sio hiyo, bali alikuwa na maana hii; twende tukafanya kazi kwasababu kufanya kazi ni agizo la Mungu;

Lakini, katika kafanya kazi kwetu, tuudhihirishie ulimwengu kuwa, sisi wana wa Mungu, tuna msaada wa Mungu katika kila tunachofanya. Kama Mungu anakusaidia katika kila unachofanya, hautakiwi kuhangaika na kuhenyeka. Msaada wa Mungu unakusaidia kupata mahitaji yako yote katikati ya dunia hii mbovu iliyoharibika. Lakini ukiangalia maisha ya baadhi ya watoto wa Mungu, ni ya kuhangaika na kuhenyeka kama vile hatuna Mungu. Hali hiyo haitutofautishi na mataifa wasiomjua Mungu. Mungu anataka iwepo tofauti kati ye watoto wa Mungu na watoto wa shetani (1Yohana 3:10; Kutoka 11:7; Kutoka 8:23; Kutoka 9:4)

Kwahiyo, Mungu anatamani kuona watoto wake tunarithi baraka zote alizotuwekea katika ulimwengu wa roho. Mungu anatamani sana kuona damu ya Yesu imemwagika kwa thamani yake, kwamba watoto wake tumepata vyote ambavyo damu ya yesu ilitununua navyo. Lakini sivyo ililivyo; na moja ya sababu ni kwamba, watu wa Mungu wanabidii sana katika mambo ya Mungu lakini si katika maarifa (Warumi 10:2; Hosea 4:6). Maana yake ni kwamba; watu wa Mungu wanavuja jasho sana lakini matunda wanayoambulia ni kidogo. Katika pointi hii, siongelei kutokuomba, bali naongelea kuomba vibaya.

Kwahiyo utagundua kwamba, baadhi ya watu wa Mungu, wana bidii sana katika kuomba, kwenye mikesha wapo, kwenye kufunga swaumu, wapo; lakini bado hawapokei yale wanayoyaomba. Hii ni kwasababu wanaomba vibaya. Mungu anailalamikia hii hali kwa watoto wake kwa kusema; mnaomba lakini hampati, kwasababu mnaomba vibaya (Yakobo 4:3).


Tunakosea wapi katika kuomba?

a)   Kuomba Mambo manyonge (Isaya 41:21)
     Isaya 43:26, Zaburi 2:7-8,  2Wakorintho 9:6, Wagalatia 6:7

b)   Kuomba Pasipo uhakika (imani) (Yakobo 1:5-7)
Waebrnia 11:1, 6,   Waebrania 10:38

c)    Kuomba nje ya mapenzi ya Mungu  (1Yohana 5:14-15) < Kitu / Muda / Mahali >
Mathayo 26:36-44, Warumi 8:26-27;  Waefeso 6:18,    Yuda 1:10

d)   Kuomba kwa kukatisha (1Wathes 5:17)
(1) Luka 18:1-7,  (2) Yakobo 5:17-18  (1Waflme 18:41-44), (3) Wagalt 1:6 / 4:19
(Wakolosai 4:2,   Waefes 6:18)

e)   Kuomba kwa msimu  (Walawi 6:12-13)
Luka 10:1, 9, 17;  Mathayo 17:14-16-21; 1Wafalme 20:19-22
Mfano; Mathayo 26:36-46 Linganisha na Matendo 2:43-47, 42 / 3:1- 4:1-13-18-20-31 

f)    Kuomba bila kumpinga shetani  (Yakobo 4:7)
Ufunuo 5:8-10, Ufunuo 1:5-6,  1Pet 2:9
Mwanzo 1:26-28,  Zaburi 8:4-8, 1Yoh 4:13,17,
Mathayo 28:18;  Luka 10:19, Yeremia 1:10/ 51:20
Waefes 6:12-13, 10-11;   Joshua 1:3, 6-9, 5.

g)    Kumpinga shetani wakati una vitu vyake (Yohana 14:33)
Yakobo 4:3-7;  Marko 11:25-26;  Mathyo 6:14-15;  Isaya 59:1-2;  Yohana 9:31.




No comments:

Post a Comment