Habari yako kijana? Naamini unasoma hapa ukiwa na utulivu
kabisa moyoni na akili timamu kichwani!
Najisikia vizuri kusema nawe kwa habari ya “KIJANA NA
MALENGO”
Kwanza natamani tuanze kwanza kwa tafakari na maana ya
maneno haya mawili:
KIJANA: Ziko tafasiri nyingi kuhusu kijana ila mimi niseme
tu, Kijana/Ujana ni hatua ya kati ya ukuuaji wa binadamu toka “Utoto” kwenda
“Utu Uzima/Uzee”; na ndio katika hatua hii mtu anakuwa na nguvu nyingi,ari kubwa
ya kufanya mambo, uwezo wa kufanya chochote na udadisi wa kutaka kujaribu kila
kitu. Kijana kwasababu anazo nguvu
anategemewa nay eye mwenyewe,familia na jamii yake, nchi yake, dunia yake na
hata Kanisa na Mungu wake.
MALENGO: Ni mipango, mikakati na matazamio yenye nia,
yanayojenga tumaini la mwongozo wa kesho ya mtu. Malengo ni shabaha ya mbali ya
kuifikia, ambayo humpa mtu ujasiri na juhudi ya kufika pale. Malengo ni ramani
na barabara ya kupita kufikia hatma yako. Unaweza kutafasiri Mipango peke yake,
lakini hakuna mipango wala mikakati bila Malengo na hakuna ndoto ya maana bila
Malengo.
Kabla ya kuianza safari malengo huwa ni mipango tu,ila mara
unapofikia mwisho wa safari hiyo, malengo huwa ni faida ya matokeo ya safari
hiyo!
SASA KWANINI KIJANA NA MALENGO?
Ujana ndio hatua amabayo mtu ana nguvu ya kupanga na
kutenda,na ni hatua ambayo mtu amepevuka kimajukumu na anategewa na kila
amtazamaye, hususani yeye mwenyewe binafsi, hivyo ni muhimu kuwa na ndoto ama
maono makubwa, si juu yake binafsi,maana huo ni ubinafsi, bali kwa ajili ya
watu wengine wanaomhusu kama jamii yake, Taifa lake na kanisa kwa ujumla!
Sasa hayo maono na ndoto kubwa haziwezi kufikiwa ama kutimia
kwa mara moja, ni hatua kwa hatua, na hapo ndio tunapata umuhimu sasa wa
kujiwekea malengo ambayo hufikiwa kupitia mipango.
Ni Zaidi ya muhimu,kwa kijana kuweka malengo kwasababu
zifuatazo;
1.
“Asiyejua aendako huwa hapotei, na kila njia
aishikayo ni sahihi kwake”
Msemo huu unamaanisha kuwa bila kujua
unakotaka kwenda kila njia iliyo mbele yako itakufikisha, uhalisia ni kuwa
ukifuata njia yoyote utafika mahali njia inakofika na sio wewe unakopaswa
kufika, huapaswi kupoteza muda, nguvu na rasilimali kubahatisha kufanya mambo,
maana maisha sio bahati nasibu na wala sio mazoezi, ila ndio yanaendelea hivyo,
kila sekunde ipitayo ndio imeshapita na kila hatua urukayo ndio umehsaruka,
sasa ili uwe makini, uwe na hakika na safari yako kuelekea kesho yako, ni
muhimu sana kujiwekea malengo, ambayo yanakuwa kama ramani yako kuifikia hatma
ya matarajio yako maishani.
2.
“Huwezi kupima kipimo chochote bila kipimio, na
huwezi kufananisha kitu chochote bila kifananishio”
Sijui kama ni lugha sahihi, lakini kimsingi
kila kipimo kinachofahamika hapa duniani kina kifaa Fulani ambacho huitwa
“kipimio” kwa mfano uzito utapimwa kwa mzani; hali kadhalika urefu,kina,
ukubwa, ujazo na vinginevyo navyo vina vipimo vyake. Pia huwezi kufananisha
kitu,bila kuwa na kingine cha kufananishia, yaani huwezi kusema huyu Anafanana
au huyu ni mfupi ama huyu ni mnene bila kwanza kuwa na mwingine aitha halisi au
kichwani mwako unayemfanisha ama kumlinganisha naye. Naam na Malengo ni kama
Kipimio cha shabaha yako na kifananishio akilini mwako ambavyo vitakusaidia uwe
na juhudi na nia thabiti ili ufike mahali ambapo unaweza sasa kupima uhalisia
na kipimio kiitwacho malengo na kufanisha na kifananishio hicho. Ukiweka
malengo ni kama unayo picha halisi kichwani ambayo bado kuifikia, na mara
utakapoendelea na kufika hatua Fulani, ni rahisi kuangalia uhalisia wa jambo
kama umefika ama unakaribia ile picha ya malengo iliyo kichwani mwako.
3.
Malengo kama picha ya shabaha, yatukusaidia
kuamua na kupanga vema juu ya mahitaji yahitajikayo kufika pale. Yaani ukiwa na
ile picha ambayo unatamani kuifikia, ni rahisi sasa kujua unahitaji nini na
unamwitaji nani kwa hatua gani na kwa muda gani ili kuitimiliza hiyo nadharia
ambayo sasa ni picha na iwe halisi.
4.
Malengo ni kichochezi chanya cha juhudi ya mtu
kutumia sawasawa uwezo wake wa juu ili kupata matokeo bora ya kile
anachokitarajia. Bila malengo mtu anaweza kubweteka na kutumia kiasi kidogo
sana cha uwezo wake wa kufikiri na kutenda, na akajikuta anapoteza muda wake na
nguvu zake kwa mambo yasiyoeleweka na yasiyo na tija.
Pamoja na yote hayo, malengo sio bima ya kufikia hatma ya
jambo lako, unaweza ukashindwa na kuanguka mara kadhaa katika jambo hilo, naam
hata ukaamua kubadilisha namna ya kufanya jambo hilo, lakini bado Malengo
yanabaki kuwa dira, ama shabaha ambayo kwa njia yeyote ile lazima uifikie na
labda na kuipitiliza kabisa.
Ili upange malengo vema yanaweza kufikiwa ni muhimu
kuzingatia mambo yafuatayo;
i.Ni lazima Uwe na taarifa sahihi na za kutosha kuhusu jambo
hilo unalolipangia malengo, na hata kama sio zote basi zile za msingi
zinazokupa ujasiri wa kuamini kuwa inawezekana;
ii. Kama ni jambo la kitaalamu, basi uwe na hakika na ujuzi
ulio nao, ama uwe na hakika na wataalamu ulio nao na ujiridhishe na ujuzi ama
taarifa walizo nazo kuwa zimethibitishwa.
iii. Lazima uzingatie matumizi mazuri ya muda, upange
mipango inayoweza kutekelezeka katika muda unaoamini unafaa, usijibane sana
ukalipua na usijipe mwingi kupitiliza ukabweteka.
iv. Lazima uwe na hakika na mahitaji pamoja rasilimali
zinazohitajika ili kufikia malengo yako, na hapa namaanisha zote, yaani
rasilimali watu, rasilimali vitu na fedha.
v. Lazima mazingira yawe yanaruhusu bila shida jambo hilo,
yaani mazingira asili pamoja mazingira ya utawala wa nchi. Lazima uwe na hakika
kuwa unalotaka kufanya haligombani na mazingira wa sharia na taratibu za nchi.
Lakini pia malengo humfanya mtu azidi kujifunza na kutafuta
taarifa Zaidi kuhusu jambo ambalo ameanza kulifanya, pia malengo yanamsaidia
mtu kupata watu sahihi wa kushirikiana nao, mahali sahihi pa kufanya jambo kwa
wakati sahihi.
Najua unayo maono na ndoto nyingi sana kijana, na unatamani
kama zingetimia hata kesho, najua unatamani kuishi maisha Fulani hivi yasiyo na
bugudha na unatamani kuwa akina Fulani wenye hela zao, ni sawa inawezekana
kabisa kuwa vyovyote utakavyo, na Mungu ameweka uwezo ndani yako kutimiza
chochote ukusudiacho kufanya, sasa ili ufike huko utakapo, kwanza imekupasa
kujitambua vema na kujikubali, kuwa wewe mwenyewe halisi na wala usitamani kuwa
kama yeyote yule umtamaniye, maana hata ufanye juhudi gani hautaweza;
Usishindane na yeyote wala usigombane na mtu, wewe tazama mbele yako, ona ile
picha kicwani mwako unayotaka kuwa, kisha panga mikakati ya muda mfupi, wa kati
na mrefu ambayo itakuwezesha kuyafikia malengo yako. Usitamani kufika haraka,
uwe na subira na usiruke hatua wala kutaka njia za mkato, tembea hatua kwa
hatua, ongeza juhudi, imarisha Imani yako na nia na kaa mahali sahihi na watu
sahihi kila siku, na mimi ninayo hakika kuwa lazima utayafikia tu malengo yako
siku moja.
Kijana malengo yatakusaidia kuwa na adabu na muono wa mbali
katika yale uyafanyayo sasa, unataka kuwa mwandishi mzuri, jiwekee malengo ya
kusoma vitabu kadhaa kila mwezi; Unataka kuwa kiongozi, jiwekee malengo ya
kufanya jambo moja la kijamii kila baada ya wakati Fulani; Ama niseme unacheza
mpira sawa, basi jiwekee malengo ya kucheza mpira Afrika ama duniani na anza
juhudi ya zoezi sasa, Una malengo ya kuajiriwa mahali Fulani, basi anza
kujifunza kidogo kidogo kuhusu watu hao, naam ukipata nafasi ya kufanya mazoezi
hapo, fanya Zaidi yaw engine, kwa uaminifu na juhudi kubwa nao hawatakusahau
hata iweje. Unatamani kujiajiri ama kuja kuwa mfanya biashara mkubwa duniani,
ni vema, basi jiwekee malengo ya kuweka akiba na kuanza kuzungusha hela kidogo
kidogo na uone kama hautayafikia malengo yako.
Najua unaweza kuwa unatamani kuwa maarufu, sijui ni kwanini
na yamkini hata wewe mwenyewe hujui hasa kwanini unatamani, ila nataka
nikwambie kitu kimoja tu, kama ukiwa halisi, ukiwa makini na nia thabiti katika
yale uyafanyayo kwa juhudi na uthabiti mkubwa, basi uwe na hakika, kazi yako
itakutangaza tu, na kwakuwa hakuna pilau nzuri ipikwayo isinukie, basi nawe
kupitia hayo uyatendayo utakuwa maarufu tu, hata kama hutaki!
Mungu akubariki na kukuwezesha katika yote ufanyayo, naam na
Roho wake wa Ufahamu akufundishe na kukufunulia yale yote unayohitaji kuyajua
ili kutimiliza kusudi la kuishi kwako hapa duniani kwa faida yako na wote
wanaokutegemea….Nenda sasa kijana ukajiwekee MALENGO, Na saa ile ikifika
YAKATIMIE! Amen!
Na
Fredy Erasto Chavala
(King Chavala-MC)
(Mwalimu na Mshauri wa Vijana/ Mzungumzaji wa
hadhira/Mshereheshaji/Mchekeshaji/Mwandishi na Mtaalamu wa Biashara na Utawala
kitaaluma)
+255 713 883 797
Barua pepe: lacs.project@gmail.com