Bwana Yesu alizungumza kwa mifano mingi akisisitiza UMUHIMU wa watu wake KUKESHA. Maana halisi ya KUKESHA ni kuwa macho hasa wakati wa USIKU ambapo watu kwa kwaida hulala. Katika maisha yetu kuna VIPINDI vya mchana ambapo kuna mwanga na tunaona. Pia kuna vipindi vya USIKU, kuna GIZA na hatuoni kitu kwa sababu ya giza. Mara nyingi watu wanakuwa SALAMA katika VIPINDI vya giza kuliko vipindi vya MCHANA kwa sababu wanachukuwa TAHADHARI na kujilinda. Lakini pia MAANDALIZI na MAFANIKIO ya ULINZI wako yanafanyika wakati wa MCHANA.
Vipindi vya MCHANA vina sifa nyingi. Mojawapo ni MWANGA. Kwa sababu UNAONA vyema, basi unakuwa na AMANI na UHAKIKA kwa sababu unaona VITU kwa jinsi ya MWILINI. Sasa tukumbuke tumeumbwa ili KUISHI katika ULIMWENGU wa MWILI na ULIMWENGU wa ROHO. Katika vipindi hivi tunaambiwa “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.” (1 Thesalonike 5:1-7). Ukifuatilia mistari hii utagundua watu wa Mungu wameitwa ni wana wa MCHANA au wana wa NURU! Kwa lugha nyingine kundi la pili linaitwa WANA wa USIKU! Sasa, pamoja na kwamba mistari hii ilikuwa inakumbusha KURUDI kwa Yesu kulichukuwa Kanisa, nataka tujifunze hii TABIA ya Mungu ya KUKESHA.
Sehemu nyingine Mungu anajiita MLINZI wa Israel, Daudi alijuwa tabia ya Mungu ya KUKESHA na akasema “Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.” (Zab. 121:1-4). Hii tabia ya KUKESHA ni ya MUHIMU pia kwa WANA wa NURU ndio maana Yesu amesisitiza sana “kukesha katika kuomba” na pia akasema “atarudi kama MWIVI ajavyo usiku” akitutaka tuwe MACHO wakati WOTE. Pamoja na GIZA la dunia hii, Bwana anasema “tusiwe kama wale wanawali wapumbavu, waliochukua taa zao bila MAFUTA”, huko usiku wakati watu wamelala, ghafla! Bwana Harusi anakuja!
Kuna sababu nyingi za KUKESHA. (i) Tuweze kushinda/kutokuanguka majaribuni. (ii) Tuwe salama adui anapokuja kushambulia. (iii) Kujua wakati wa KUJILIWA na Bwana. (iv) Tusibaki Yesu akija kuchukua Kanisa lake. Sifa za WAKESHAJI utaziona hapa, “Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pinde zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli;” (Isaya 5:27,28). Nitazungumzia zaidi KUJILIWA. Yesu alipoutizama Yerusalemu alilia. Akasema “laiti ungejua yakupasayo amani”, Wakati Yesu (Baraka za Mungu) zinakuja, Israel hawakujua na kupokea kwa shukurani, na pia wakati ADUI anakuja kuharibu, hawakuwa na HABARI! Akalia. Maisha yetu tumejisahau sana na kuona tu mambo yataenda kama JANA! Tumepoa au kupunguza ile kasi ya kumtafuta Mungu na tunaishi kama MUNGU hayupo! Taratibu tunapoteza NURU na kuanza kutembea GIZANI. Usipoangalia Ghafla! Uharibifu unakuja, kwa maana ADUI anakuwinda na anasubiri GIZA akushambulie! “Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.” (1 Thesalonike 5).
Sio kila mara ukiona MWANGA (NURU) kwenye ulimwengu wa MWILI pia unaona MWANGA kwenye Ulimwengu wa roho. Ngoja tujifunze kwa Ayubu. “Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. (Ayubu 1:9,10). Huu uliku wa ni wakati wa MCHANA (NURU) kwa Ayubu. Wakati Baraka ziko kila upande, mali, watoto, na mafanikio ya kila namna. Huku unaouna mkono wa Bwana (ukingo) unakupigania, nk. Ghafla! Giza nene linatanda! Sasa sio watu wengi sana wanapona hapa. ILA wale ambao WANAKESHA “watayaona mabaya yakija” (1 Thesalonike 5), na Mungu wao atawapa DAWA ya KUSHINDA. Kwa sababu wako NURUNI, MLANGO wa KUTOKA wakati wa KUJARIBIWA kwao watauona.
Mara nyingi sana watu katika maisha ya kawaida hawajali sana kwa sababu BANK kumenona, wanajua hata wakifukuzwa kazi LEO hawafi njaa. VITEGA uchumi vimesimama sawia. Karibia kila kitu kimekatiwa BIMA. Wanaweza kupata MATIBABU mahali popote duniani. Mambo ni SAFI, hata wakitafuta kwamba SHIDA inaweza kutokezea wapi hawaoni. Huwezi kuona UMUHIMU wa kukesha na KUDUMU kumtegemea Mungu kama huna macho ya rohoni na UELEKEVU kwa Bwana kama Ayubu. Lakini kwa wale ambao wamepitia majanga wanajua nasema nini. Kuna habari MBAYA hata sipendi kusikia licha ya kusimulia. Utakuta watu wameokoka tu vizuri, wamebarikiwa kuingia kwenye NDOA. Wanakuwa na mipango mingi ya maisha na KAZI/BIASHARA zao nzuri ziko sawa. Ghafla! Wasipotarajia, wameenda wote kazini na kabla ya jioni mmoja ametwaliwa! Ghafla tu! Status inabadilika, mmoja anaitwa mjane. Adui kashambulia. Wengine katika hali isiyotarajiwa, watoto wameenda shule, ghafla jioni hawarudi! Wanapata taarifa waende chumba cha kuhifadhia maiti kukagua! Hizi ni habari mbaya sana. Lakini haya ndio yalikuwa yanamtokea Ayubu wakati wa GIZA ulipoanza. Anajigundua hana WATOTO hata mmoja, wamekufa wote! Hana MALI halafu ni mgonjwa hajiwezi hapo chini. Mke wake naye analeta mambo magumu ya kumchanganya zaidi. Huu ni wakati wa GIZA.
Kusudi la somo hili ni kukumbusha habari ya KUKESHA. Katika kukesha kuna kujaa NGUVU na kujiandaa kupambana (Isaya 5). Nguvu za kukuwezesha kuvuka kwenye GIZA hupatikana wakati wa MCHANA. Maisha ya Ayubu kabla ya JARIBU ndio yalimwezesha KUSHINDA wakati wa jaribu. Watu wengi sana wanasubiri MAJANGA (GIZA) ndio wanaanza KUFUNGA na KUOMBA kwa BIDII na KUKEMEA kwa NGUVU. Sasa kweli wanakemea, ila nguvu iko wapi? “Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.” (Mithali 24:10). “Wamtumainio Bwana ni kama MLIMA Sayuni, hawatatikisika kamwe” lakini pia Isaya anasema “bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.” (Isaya 40:31). KUSUBIRI kunahusianishwa na tabia ya KUKESHA.
Yesu anaposema “ni rahisi ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia Ufamle wa Mungu” aliona hii shida KUFANYA mapenzi ya Mungu wakati watu wamezungukwa na kila kitu. Ndio maana alipomuuliza yule kijana tajiri habari za AMRI za Mungu, na kijana anasema ameshika ZOTE, maandiko yanasema “Yesu akampenda”. Kwanini? Sio rahisi kukaa katika Amri za Mungu wakati HELA inapiga kelele. Ukifanikiwa kumpendeza Mungu wakati una KILA kitu lazima uwe KIVUTIO kwa Yesu. Sasa, Angalia maisha yako vizuri. Pale mahali ulikuwa una SHIDA, huna hela na hujui unavukaje, ULIMTAFUTA Mungu kwa BIDII na kukaa mbali na DHAMBI. Leo Mungu amekuvusha, umemaliza shule salama, umepata kazi, nafasi na pesa, Ghafla! Unaanza kuwaza KUTENDA dhambi! Ukiwa kwenye SHIDA kwako ilikuwa MCHANA, sasa Mungu amekubariki na baraka za Mungu badala ya kuongeza NURU, zimekuwa GIZA! Na chukizo kwa Mungu. Je! Unataka Mungu akurudishe kule kwenye DHIKI ili taa yako iwake? Wakati unadhani ni “amani amani” angalia uharibifu uko njiani. Neno hili linakukumbusha UAMKE na KUCHANGAMKA, rudi kwenye MKESHA na kuishi kwa KIASI, huku ukimsubiri Bwana. Kuna faida gani “kuupata ulimwengu wote na kupoteza nafsi yako?” Jijibu mwenyewe na uchukue HATUA. Mungu akusaidie.
Basi Mungu atuwezeshe kukaa katika KIASI na KUKESHA kwa Jina la Yesu. AMEN
Frank Philip.
No comments:
Post a Comment