Thursday, July 23, 2015

“KIJANA NA MALENGO”


Shalom ndugu msomaji,yaani Amani iwe kwako!
Habari yako kijana? Naamini unasoma hapa ukiwa na utulivu kabisa moyoni na akili timamu kichwani!

Najisikia vizuri kusema nawe kwa habari ya “KIJANA NA MALENGO”
Kwanza natamani tuanze kwanza kwa tafakari na maana ya maneno haya mawili:
KIJANA: Ziko tafasiri nyingi kuhusu kijana ila mimi niseme tu, Kijana/Ujana ni hatua ya kati ya ukuuaji wa binadamu toka “Utoto” kwenda “Utu Uzima/Uzee”; na ndio katika hatua hii mtu anakuwa na nguvu nyingi,ari kubwa ya kufanya mambo, uwezo wa kufanya chochote na udadisi wa kutaka kujaribu kila kitu.  Kijana kwasababu anazo nguvu anategemewa nay eye mwenyewe,familia na jamii yake, nchi yake, dunia yake na hata Kanisa na Mungu wake.

MALENGO: Ni mipango, mikakati na matazamio yenye nia, yanayojenga tumaini la mwongozo wa kesho ya mtu. Malengo ni shabaha ya mbali ya kuifikia, ambayo humpa mtu ujasiri na juhudi ya kufika pale. Malengo ni ramani na barabara ya kupita kufikia hatma yako. Unaweza kutafasiri Mipango peke yake, lakini hakuna mipango wala mikakati bila Malengo na hakuna ndoto ya maana bila Malengo.

Kabla ya kuianza safari malengo huwa ni mipango tu,ila mara unapofikia mwisho wa safari hiyo, malengo huwa ni faida ya matokeo ya safari hiyo!

SASA KWANINI KIJANA NA MALENGO?

Ujana ndio hatua amabayo mtu ana nguvu ya kupanga na kutenda,na ni hatua ambayo mtu amepevuka kimajukumu na anategewa na kila amtazamaye, hususani yeye mwenyewe binafsi, hivyo ni muhimu kuwa na ndoto ama maono makubwa, si juu yake binafsi,maana huo ni ubinafsi, bali kwa ajili ya watu wengine wanaomhusu kama jamii yake, Taifa lake na kanisa kwa ujumla!
Sasa hayo maono na ndoto kubwa haziwezi kufikiwa ama kutimia kwa mara moja, ni hatua kwa hatua, na hapo ndio tunapata umuhimu sasa wa kujiwekea malengo ambayo hufikiwa kupitia mipango.

Ni Zaidi ya muhimu,kwa kijana kuweka malengo kwasababu zifuatazo;

1.       “Asiyejua aendako huwa hapotei, na kila njia aishikayo ni sahihi kwake”

Msemo huu unamaanisha kuwa bila kujua unakotaka kwenda kila njia iliyo mbele yako itakufikisha, uhalisia ni kuwa ukifuata njia yoyote utafika mahali njia inakofika na sio wewe unakopaswa kufika, huapaswi kupoteza muda, nguvu na rasilimali kubahatisha kufanya mambo, maana maisha sio bahati nasibu na wala sio mazoezi, ila ndio yanaendelea hivyo, kila sekunde ipitayo ndio imeshapita na kila hatua urukayo ndio umehsaruka, sasa ili uwe makini, uwe na hakika na safari yako kuelekea kesho yako, ni muhimu sana kujiwekea malengo, ambayo yanakuwa kama ramani yako kuifikia hatma ya matarajio yako maishani.

2.       “Huwezi kupima kipimo chochote bila kipimio, na huwezi kufananisha kitu chochote bila kifananishio”

Sijui kama ni lugha sahihi, lakini kimsingi kila kipimo kinachofahamika hapa duniani kina kifaa Fulani ambacho huitwa “kipimio” kwa mfano uzito utapimwa kwa mzani; hali kadhalika urefu,kina, ukubwa, ujazo na vinginevyo navyo vina vipimo vyake. Pia huwezi kufananisha kitu,bila kuwa na kingine cha kufananishia, yaani huwezi kusema huyu Anafanana au huyu ni mfupi ama huyu ni mnene bila kwanza kuwa na mwingine aitha halisi au kichwani mwako unayemfanisha ama kumlinganisha naye. Naam na Malengo ni kama Kipimio cha shabaha yako na kifananishio akilini mwako ambavyo vitakusaidia uwe na juhudi na nia thabiti ili ufike mahali ambapo unaweza sasa kupima uhalisia na kipimio kiitwacho malengo na kufanisha na kifananishio hicho. Ukiweka malengo ni kama unayo picha halisi kichwani ambayo bado kuifikia, na mara utakapoendelea na kufika hatua Fulani, ni rahisi kuangalia uhalisia wa jambo kama umefika ama unakaribia ile picha ya malengo iliyo kichwani mwako.

3.       Malengo kama picha ya shabaha, yatukusaidia kuamua na kupanga vema juu ya mahitaji yahitajikayo kufika pale. Yaani ukiwa na ile picha ambayo unatamani kuifikia, ni rahisi sasa kujua unahitaji nini na unamwitaji nani kwa hatua gani na kwa muda gani ili kuitimiliza hiyo nadharia ambayo sasa ni picha na iwe halisi.

4.       Malengo ni kichochezi chanya cha juhudi ya mtu kutumia sawasawa uwezo wake wa juu ili kupata matokeo bora ya kile anachokitarajia. Bila malengo mtu anaweza kubweteka na kutumia kiasi kidogo sana cha uwezo wake wa kufikiri na kutenda, na akajikuta anapoteza muda wake na nguvu zake kwa mambo yasiyoeleweka na yasiyo na tija.

Pamoja na yote hayo, malengo sio bima ya kufikia hatma ya jambo lako, unaweza ukashindwa na kuanguka mara kadhaa katika jambo hilo, naam hata ukaamua kubadilisha namna ya kufanya jambo hilo, lakini bado Malengo yanabaki kuwa dira, ama shabaha ambayo kwa njia yeyote ile lazima uifikie na labda na kuipitiliza kabisa.

Ili upange malengo vema yanaweza kufikiwa ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;

i.Ni lazima Uwe na taarifa sahihi na za kutosha kuhusu jambo hilo unalolipangia malengo, na hata kama sio zote basi zile za msingi zinazokupa ujasiri wa kuamini kuwa inawezekana;

ii. Kama ni jambo la kitaalamu, basi uwe na hakika na ujuzi ulio nao, ama uwe na hakika na wataalamu ulio nao na ujiridhishe na ujuzi ama taarifa walizo nazo kuwa zimethibitishwa.

iii. Lazima uzingatie matumizi mazuri ya muda, upange mipango inayoweza kutekelezeka katika muda unaoamini unafaa, usijibane sana ukalipua na usijipe mwingi kupitiliza ukabweteka.

iv. Lazima uwe na hakika na mahitaji pamoja rasilimali zinazohitajika ili kufikia malengo yako, na hapa namaanisha zote, yaani rasilimali watu, rasilimali vitu na fedha.

v. Lazima mazingira yawe yanaruhusu bila shida jambo hilo, yaani mazingira asili pamoja mazingira ya utawala wa nchi. Lazima uwe na hakika kuwa unalotaka kufanya haligombani na mazingira wa sharia na taratibu za nchi.

Lakini pia malengo humfanya mtu azidi kujifunza na kutafuta taarifa Zaidi kuhusu jambo ambalo ameanza kulifanya, pia malengo yanamsaidia mtu kupata watu sahihi wa kushirikiana nao, mahali sahihi pa kufanya jambo kwa wakati sahihi.

Najua unayo maono na ndoto nyingi sana kijana, na unatamani kama zingetimia hata kesho, najua unatamani kuishi maisha Fulani hivi yasiyo na bugudha na unatamani kuwa akina Fulani wenye hela zao, ni sawa inawezekana kabisa kuwa vyovyote utakavyo, na Mungu ameweka uwezo ndani yako kutimiza chochote ukusudiacho kufanya, sasa ili ufike huko utakapo, kwanza imekupasa kujitambua vema na kujikubali, kuwa wewe mwenyewe halisi na wala usitamani kuwa kama yeyote yule umtamaniye, maana hata ufanye juhudi gani hautaweza; Usishindane na yeyote wala usigombane na mtu, wewe tazama mbele yako, ona ile picha kicwani mwako unayotaka kuwa, kisha panga mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ambayo itakuwezesha kuyafikia malengo yako. Usitamani kufika haraka, uwe na subira na usiruke hatua wala kutaka njia za mkato, tembea hatua kwa hatua, ongeza juhudi, imarisha Imani yako na nia na kaa mahali sahihi na watu sahihi kila siku, na mimi ninayo hakika kuwa lazima utayafikia tu malengo yako siku moja.

Kijana malengo yatakusaidia kuwa na adabu na muono wa mbali katika yale uyafanyayo sasa, unataka kuwa mwandishi mzuri, jiwekee malengo ya kusoma vitabu kadhaa kila mwezi; Unataka kuwa kiongozi, jiwekee malengo ya kufanya jambo moja la kijamii kila baada ya wakati Fulani; Ama niseme unacheza mpira sawa, basi jiwekee malengo ya kucheza mpira Afrika ama duniani na anza juhudi ya zoezi sasa, Una malengo ya kuajiriwa mahali Fulani, basi anza kujifunza kidogo kidogo kuhusu watu hao, naam ukipata nafasi ya kufanya mazoezi hapo, fanya Zaidi yaw engine, kwa uaminifu na juhudi kubwa nao hawatakusahau hata iweje. Unatamani kujiajiri ama kuja kuwa mfanya biashara mkubwa duniani, ni vema, basi jiwekee malengo ya kuweka akiba na kuanza kuzungusha hela kidogo kidogo na uone kama hautayafikia malengo yako.

Najua unaweza kuwa unatamani kuwa maarufu, sijui ni kwanini na yamkini hata wewe mwenyewe hujui hasa kwanini unatamani, ila nataka nikwambie kitu kimoja tu, kama ukiwa halisi, ukiwa makini na nia thabiti katika yale uyafanyayo kwa juhudi na uthabiti mkubwa, basi uwe na hakika, kazi yako itakutangaza tu, na kwakuwa hakuna pilau nzuri ipikwayo isinukie, basi nawe kupitia hayo uyatendayo utakuwa maarufu tu, hata kama hutaki!

Mungu akubariki na kukuwezesha katika yote ufanyayo, naam na Roho wake wa Ufahamu akufundishe na kukufunulia yale yote unayohitaji kuyajua ili kutimiliza kusudi la kuishi kwako hapa duniani kwa faida yako na wote wanaokutegemea….Nenda sasa kijana ukajiwekee MALENGO, Na saa ile ikifika YAKATIMIE! Amen!



Na
 Fredy Erasto Chavala (King Chavala-MC)
(Mwalimu na Mshauri wa Vijana/ Mzungumzaji wa hadhira/Mshereheshaji/Mchekeshaji/Mwandishi na Mtaalamu wa Biashara na Utawala kitaaluma)
+255 713 883 797

Barua pepe: lacs.project@gmail.com