Sunday, January 5, 2014

SIRI ya MAFANIKIO YAKO!!



SIRI ya MAFANIKIO YAKO
(UMUHIMU wa KUJIFUNZA NENO la MUNGU)

Wakati tunatarajia MEMA katika MWAKA mpya 2014 nimeona nikupe SIRI ya jinsi haya MEMA yanaweza kukujilia maishani mwako. Kumbuka sio kila AHADI ya kwenye Biblia ni yako hata ukiikiri USIKU na MCHANA. Kuna KIWANGO cha IMANI katika KUPOKEA AHADI za Mungu. Kumbuka “imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo”. Sasa nataka ujifunze kwamba unapata ZAIDI ya IMANI pale unapojifunza Neno la Mungu.

Unapojifunza Neno la Mungu KIWANGO chako cha KUMJUA Mungu kinaongezeka. Haiishii hapo, kila unapoongeza KIWANGO cha kumjua Mungu mambo mawili yanatokea (i) AMANI yako inaongezeka (ii). Mema yanakujilia. (Ayubu 22:21)

Hakuna kitu nafurahi kama kusikia feedback kwamba kuna MTU amebarikiwa na FUNDISHO la UFALME (Mambo ya Mungu). Ukisikia umebarikiwa mara nyingi sana inamaanisha umepata UFUNUO fulani (Mungu amefunuliwa kwa njia fulani zaidi katika maisha yako kupitia hilo Neno). Sasa huku mimi najua sio tu UMEBARIKIWA na kuongeza MAARIFA ya kiroho, ila na kiwango cha AMANI na KUFANIKIWA kwako katika mambo yote na MEMA yanaongezeka katika maisha ya kila siku.

Basi tusiwe wavivu kujifunza mambo ya Mungu kwa maana ANATUFUNDISHA ili tupate FAIDA. (Isaya 48:17-19). Ukiona kwenye TV (series, movies, nk.) na kusoma NOVEL na MAGAZETI unachangamka ila hata page 3 tu za mafundisho ya Neno la Mungu unaona ni MZIGO, ujue uko karibu na HASARA kama HUJAPATA tayari.

Nawatakia HERI ya MWAKA MPYA 2014.

Frank Philip

Saturday, January 4, 2014

UWEZO WA NENO LA MUNGU KUKUBADILISHA!!!


(Ushindi, mafanikio ya mwili na roho, amani, furaha, nk. vimefichwa kwenye Neno. Jua ni kwanini inakua ngumu huu ushindi kudhihirika kwako.)

Mara nyingi sana watu wamekua wasikilizaji wa Neno la Mungu na kuguswa kwa namna mbalimbali ila baada ya muda utagundua bado wanaendelea na tabia, mienendo, dhambi na maisha yao ya kale. Nini kimetokea? Neno walilosikia halikuwabdilisha! Kama lingewabadilisha wangeacha njia zao mbaya.

Daudi akasema “moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije nikakutenda dhambi”. Ina maana Neno la Mungu lina NGUVU ya kukuzuia kutenda dhambi. Utauliza ni kwa namna gani. Sikiliza, mambo yafuatayo. 1. Biblia inasema “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani” na imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. 2. “Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu” ina maana ukiwa na Neno utaona mitego mingi sana ya Ibilisi na kuepuka isikunase. Kumbuka “mitego” ni vitu vilivyofichika kukunasa au kukuangusha. 3. “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa” na “watu wanapotea kwa kutokujua Neno na Nguvu za Mungu” tunapata maarifa kutoka kwenye Neno, inamaana ukiwa na Neno uko salama na maangamizi ya adui. Haya ni baadhi tu. Swali ni kwamba kwanini watu hawabadilishwi na Neno la Mungu na wanazidi kuishi katika njia zao mbaya?

Tujifunze mambo machache ya kutusaidia katika maisha yetu na kisha tuone tanaponaje. Nitatumia mfano wa MAHUSIANO (ndoa, uchumba, kifamilia, nk.). Katika mahusiano kila mmoja huwa anakua na mahitaji kutoka kwa mwenzake. Matatizo makubwa ya kijamii yako katika mahusiano. Kufanikiwa kwa UHUSIANO unatokana na KIWANGO cha kila mmoja katika uhusiano huo kutenda WAJIBU wake na KUMPENDEZA mwenzake. Sasa sikiliza. Kama kuna SHIDA ya uhusiano jua kwamba WOTE wawili mnahitaji DAWA ambao inapatikana katika Neno la MUNGU. Utasema kwa vipi, “Mungu akitaka kuliponya taifa, au watu wa taifa fulani hulituma Neno”. Watu wakilisikia na kulitii hao watu wanapona katika SHIDA yao.


Nataka nikwambie aina 3 za mioyo. Maana Daudi alisema “moyoni mwake ameweka Neno” kwa hiyo Neno linakaa Moyoni sio kichwani. Na sehemu nyingine tunasoma “kwa moyo mtu huamini na kupokea wokovu” sio kwa kichwa mtu hukumbuka na kuamini. Sawa, sasa sikiliza. Aina za mioyo: 1. Moyo wa jiwe: Huu haupokei kitu. Ni kama jiwe la mtoni liko kwenye maji lakini ndani ni KAVU, no absorption! Paulo aliuita moyo wa aina hii kwamba ni moyo wenye “ganzi”. 2. Moyo wa nyama: Huu unapokea vizuri na ni moyo mzuri unaobadilika kama Neno likiingia humo. 3. Moyo wa KIOO: Huu ni moyo ambao UNAVUTA kila NENO kwa bidii sana ila HUAKISI kwa MTU mwingine na kuhamisha hilo Neno kama lilivyo na “kioo” kubaki kitupu. KUMBUKA ukiona umesikiliza MAFUNDISHO ya watumishi mbali mbali wa Mungu na shida yako ipo hapo iwe ya uhusiano au nyingine, jua kuna shida ya MOYO wako na sio Neno au mhubiri wala upako wao.

Umewahi kujiuliza mtu anahudhuria seminara ya NDOA, na watumishi wa Mungu wanateremsha NENO kwa UPAKO wa hali ya juu na mafunuo makubwa makubwa LAKINI shida ya ndoa imesimama kama HAKUNA kilichotokea? Shida iko wapi? Shida iko Moyoni! Kama sio JIWE basi ni KIOO! Sifa ya mtu mwenye moyo wa KIOO ni kujikusanyia MAFUNDISHO ya NGUVU ili kuthibitisha UDHAIFU wa mwenzake, mfumo au jamii inayomzunguka. Mara zote Roho Mtakatifu akileta POINT ya maana utasikia mtu anasema “unaona?” au “si nilisema?” au “hata mtumishi kasema hivyo hivyo, hii ndio shida na watu hawataki kunisikia” au “hili Neno anatakiwa fulani asikie hili”, nk. Ukijikuta una-respond kwa mtindo huu jua kuna KIOO ndani yako. Pamoja na kujikusanyia MAFUNDISHO ya kila UBORA wa juu, kama una moyo wa kioo, utakua tu ukichambua “watu” wengine kwa WINGI kwa mafundisho yako na wewe binafsi kubakia na MISHIDA yako inakukodolea macho! Kwa maana “Mkono wa Mungu haukupungua urefu wala nguvu hadi ushindwe kuokoa” sasa mbona Hauokoi? Je! Neno limepungua nguvu? La! Hasha. Yesu jina lake jingine ni Neno la Mungu, na hajawahi kushindwa KITU, ila anabisha kwenye “mlango ya moyo wako”, ukifungua utaona mwenyewe atakavyo kuhudumia na kuleta DAWA katika shida zako ZOTE. Shida sio Yesu/Neno shida ni MOYO wako! Tengeneza MOYO wako na NENO litakubadilisha bila shaka.

Mfalme Daudi yeye hakuomba UTAKASO wa moyo, aliomba moyo MPYA! Aliona hizi toba zimekua nyingi na mambo hayaendi sasa, akamwambia Mungu “niumbie moyo safi (“create” in me a clean heart!)”. Kama kuna eneo unatakiwa kushughulika nalo sana ni Moyo! Ndio maana maandiko yanasema “linda SANA moyo wako KULIKO vitu vyote ulindavyo”. Kwanini? Huko ndiko kuna SIRI ya kushinda au kushindwa kwako! Uzima unatokea humo, na mauti inatoke humo pia! Ndio maana Yesu akasema “sio kile akilacho mtu HUMNAJISI ila kile kimtokacho”. Kutokea wapi? Jibu ni MOYONI. Uzinzi, uongo, ufisadi wa kila namna, tamaa, nk, makao yao ni moyoni mwako. Shughulika na moyo nakwambia “viungo” vingine vya mwili ni mateka tu na vinatumika kama watumwa ila bwana wao anaitwa MOYO! Shughulika na bwana mkubwa “moyo” na kila kitu kitakia kimya!

Sasa watu wengi sana wako busy kujitakasa kwa Damu ya Yesu. Kweli inatakasa, lakini ukifuatilia maandiko utagundua Neno la Mungu linafanya hiyo kazi pia. “Uwatakase kwa Kweli yako, Neno lako ndio Kweli!” Ibilisi anakuweka mbali na Neno la Mungu akijua lina NGUVU ya kukutakasa na KUKUPONYA, sio tu magonjwa ila hata na matatizo na shida ZOTE za duniani (formula ya maisha yako imefichwa kwenye NENO). Ufumbuzi wa matatizo yako yote uko kwenye NENO asikudanganye mtu, unachohitaji ni UFUNUO kwenye hilo Neno, na hapo ndipo pa GUMU ila OMBA na tafuta KUSUDI la Mungu katika KILA unachokifanya itakusaidia kuwekeza nguvu na muda wako. {kwa ufafanuzi zaidi soma somo jingine humu lenye kichwa “KAZI YA MVUVI”} uone jinsi Yesu ambavyo sio mvuvi wa samaki lakini anamsaidia mvuvi mzoefu kwa kumpa NENO la maelekezo na kazi inakua rahisi na ya mafanikio makubwa.

Sasa ili Ibilisi akutese lazima akuweke mbali na Neno la Mungu, au akishindwa anashughulika na moyo wako. Kama hatupii “jiwe” basi anatupia “kioo” (lugha ya kwenye Agano jipya ina sema Ibilisi “hulinyakua Neno”), unasikia lakini ganzi tupu! ILI usije ukaamini “ukaokoka”! Hii ni vita KAMILI na ni KALI sio utani. Ndio maana sio kuombea tu ugali kabla ya kula, ombea hata Neno la Mungu kabla ya kusoma ili lizame mahali pake, upata UFUNUO na lifanye mabadiliko katika maisha yako. Usisahau uwezo wa kupokea Neno na kuleta mabadiliko ni katika moyo wako kwa hiyo ombea na moyo wako uwe kama “udongo tifutifu”, ili kila Neno likidondoka hapo lizae 1:100, 1:60, 1:30, nk. Haiwezekani usome, usikie au ukutane na Neno HALISI la Mungu uwe kama ULIVYO haiwezekani! Lazima kuna shida mahali. Mungu atusaidie kujua siri hii. AMANI na BARAKA zizidi kwenu.

Frank Philip

NGUVU ya VINYAGO ndani YAKO!!!


Nabii Elisha alikua mkulima na alikua na JOZI kadhaa za ng’ombe (MAKSAI). Alipoitwa katika kazi ya Bwana alichofanya ni KUCHINJA wale maksai na kutumia vifaa vya majembe yake kama kuni! Wakala nyama na kusherehekea mwisho wa HUDUMA ya UKULIMA. Elisha akamgeukia Eliya na kuanza kazi kwa nia moja. Kumbuka Elisha alikua na NJIA moja, hapakua na njia ya kurudi nyuma maana ALIANGAMIZA (vinyago) vya ya biashara ya kwanza!

Yesu alipomwita Petro kutoka katika biashara ya UVUVI, Petro alikuja na kuanza huduma kwa nguzu sana ila kwenye STOO yake alihifadhi zile NYAVU na MTUMBWI vya kuvulia samaki. Alipokua KARIBU na Yesu, Petro alikua na ujasiri mkubwa sana kuliko hata wenzake. ILA katika vipindi vigumu na Yesu akiwa hatua kidogo tu mbali naye wakati wa MATESO, Petro anamkana YESU! Tena mara tatu! Siku Yesu ameuwawa, Petro akapiga mahesabu na kukumbuka zile NYAVU na MTUMBWI kule stoo na KURUDI kwenye kazi yake ya kuvua samaki! Baada ya kufufuka, Yesu akaenda tena kwa “mara ya pili” kumtafuta Petro kule ziwani akiwa BUSY KUVUA SAMAKI. Kumbuka, Petro alikwisha jua kua yeye ni “mvuvi wa WATU” sasa ilikuaje akarudi kuvua samaki? Sababu ya msingi ilikua ni KUKATA TAMA na kuona “hii biashara ya kumfuata Yesu hailipi”, lakini pia bado alikua na NYAVU zake na VIFAA (VINYAGO) vya ile kazi ya zamani! Akarudi huko tena maana “vinyago” vilikuwepo na sio vya KUTAFUTA.

Katiaka maisha yetu ya zamani hakuna mtu yeyote ambaye “hakua” na VINYAGO ambavyo aliviabudu. Zile dhambi na kazi mbaya za Ibilisi. Watu wengi wameamua kumfuata Mungu ila kwenye stoo zao (MIOYONI) bado kuna VINYAGO wameweka akiba huko. Wakifika mahali PAGUMU walio wengi wanarudi “stoo” na kunyanyua kinyago maana ni rahisi kuchukua KINYAGO wakati wa majaribu kuliko KUFUNGA na KUOMBA ili MUNGU akuvushe na kukufikisha MAHALI pa USHINDI wako.



Hatari kubwa ya VINYAGO ni kwamba huwa VINASEMA. Wakati umevijaza ndani ya MOYO wako na unaenda mbele za Mungu na KUMUULIZA juu ya “jambo maishani mwako”, Mungu anasema “nitakujibu sawa na vinyago vyako”. Kwa sababu umeishi katika TAMAA na kumbukumbu (IBADA) ya vinyago vyako unapotelea humo ukizani ni Mungu amekujibu, kumbe ni “sauti ya vinyago”! Kwani hujui kwamba Mungu aliapa kwamba hatashindana na mwanadamu? Sasa jua hili, uking’ang’ania vinyago vyako jua Mungu hakunyang’anyi kwa nguvu ila utaangamia navyo usipogeuka. EZEKIEL 14: 3“Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote? 4 Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake” (Umewahi kujiuliza ni kwanini maombi ya kutafuta mchumba ni MAGUMU sana, ila maombi ya HUDUMA Mungu anajibu haraka? Asikiaye na afahamu!)

Kama kuna kitu Mungu hapendi ni mtu wa nia MBILI. Joshua akawauliza wana wa Israel wachague wanamtumikia Mungu au NANI? Hakuna katikati, kama wanamfuata Mungu lazima kusema wazi na sio kujibandika LABEL mbili, moja ya Mungu na nyingine ya Ibilisi. Musa alipokua anashughulika na maasi ya Kora alisema neno hili “walio upande wa Mungu waje huku na walio upande wa Kora waende kule”. Nakwambia wale wa upande wa Kora ambao waliambudu VINYAGO vyao walijitenga kule na ardhi ikafunguka wakamezwa humo! Usisahau, mwisho wa VINYAGO ni kukuangamiza na kukumaliza bila kujua kwa sababu vinyago VINAVUTIA macho na vyafaa sana kwa CHAKULA.

Wana wa Israel walijua kabisa huko mbele kuna nchi ya ahadi inayotiririka MAZIWA na ASALI, lakini “hapa katikati” kuna KUFAULU mtihani. Lazima kupita JANGWANI miaka ya KUTOSHA, kuna mataifa kadhaa ya kupigana nayo VITA, kuna kuishi kwa kula MANA, chakula ambacho baba zao hawakukijua, na kuna masharti sio kula tu ovyo, hakuna kuokota MANA siku ya Sabato (kula kwa nidhamu). Biblia inatuambia walivaa mavazi yao na viatu vyao havikuchakaa. Inamaana hapakua na “viwalo” vya kubadili kwa wale warembo. Ghafla! watu wakakumbuka kule Misri masufuria ya nyama na kuanza kutamani VINYAGO vya zamani. Kumbuka NYOKA ZA MOTO zilikuja kuwashughuikia maana walianza manung’uniko huko jangwani. Kiu ni kali hadi Musa anamkosea Mungu maana alishindwa KUMSTAHI mbele za hao maelf ya watu ambao wako “desperate”, akakosa uvumilivu na kushindwa kufuata malekezo vizuri! Unapobanwa na mambo mengi sana ANGALIA usikose KUMSTAHI Mungu mbele za hao “watu” na kwa sababu ya VINYAGO vyako ukamvunjia Mungu heshima yake. Chunga sana maana saa ya kujaribiwa inakuja. Simama kwa uaminifu na kwa maombi na saburi. TUPA vinyago vya zamamani na uwe safi bila njia mbili mbili, Mungu atakurehemu utavuka salama la sivyo vinyago VITAKUANGAMIZA.

Kumbuka siku zote, kama ulikua na MPENZI wa zamani na sasa umeamua kumfuata Mungu, jaribu kubwa sio UZINZI tu ila ni yule jamaa/binti maana ndani yako amekua KINYAGO na kila ukifinga macho unaona kinyago “hiki hapa”. Ibilisi anajua vyema juu ya ibada ya SANAMU hivyo kila ukifunga macho, anakuletea zile VIDEO na SAUTI kwa maana VINYAGO huongea! Gafla unatamani kurudi Misri na kusahau UKOMBOZI mkuu wa MKONO wa Mungu ulionyooshwa ULIOKUOKOA. Unarudi kusujudu SANAMU na unajikuta unaingia katika mtego wa maasi ya KORA. Mambo yote yanatokea JANGWANI! Hapo ulipobanwa na UHITAJI na ADHA mbalimbali, hapo ndio KIPIMO cha UAMINIFU wako kwa Mungu wako. Jipe moyo basi maana BWANA wetu alisema “ulimwenguni mnayo dhiki laikini jipeni moyo, Mimi nimeushinda ulimwengu”, WEWE pia Utashinda. Shughulikia vinyago vyako na KUVISAHAU nawe utakua salama. AMEN.


Frank Philip

HERI YA MWAKA MPYA 2014!!!!

Shalom!!!
Habari zenu wapendwa wasomaji wa blog hii!!
Tulikuwa kimya na sasa tumerudi tena na huu ni msimu mpya!
Naamini mmekuwa na wakati mzuri wakati wa Sikukuu ya Noeli na hata shamrashamra za kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014!

NENO LA KINABII KWA 2014;
*PAMOJA NA MISUKOSUKO MINGI SANA ITAKAYOKUWEPO MWAKA HUU KISIASA,KIJAMII, KIUCHUMI NA KIIMANI BADO WALE WAMTUMAINIO BWANA WATAUONA MKONO WA MUNGU....NAAM HUU NI MWAKA WA KIBALI KIKUBWA KUTOKA KWA BWANA (A YEAR OF MEGA FAVOUR)
>>>NA KAMA VILE MUNGU ALIVYOWASHINDIA WANA ISRAELI NA KUWAVUSHA BAHARI YA SHAMU,NDIVYO ITAKAVYOKUWA KWA WANA WA MUNGU!!!

*LAKINI PIA NI MWAKA WA KUVUKA KWENDA NG'AMBO YA PILI...A YEAR OF CROSSING OVER!!!

TUNAYO MENGI YA KUJIFUNZA NA KUSHIRIKISHANA HAPA!
TAFADHALI USIONDOKE HAPA NA KAMA BADO HUJAJIUNGA NA BLOG HII BASI JIUNGE SASA!!

KWA NIABA YA TIMU NZIMA YA "GOSPEL STANDARD BASE" NINAKUTAKIA KILA BARAKA NDANI YA MWAKA HUU NA MAFANIKIO MENGI SANA!!

KAA MKAO WA KUMSIKIA BWANA WAKATI WOTE!

Fredy E. Chavala
President
(c)2014

Thursday, January 2, 2014

NGUVU katika MATENDO yako!!!



NGUVU katika MATENDO yako
(Umri, mlango wa misaada kwako, uheri (less trouble) wa maisha, baraka na utajiri)

Kuna msemo uliozoeleka sana unaosema “malipo ni hapa hapa duniani”. Na kwa wenzetu wa Magharibi wanasema “what goes around comes around”. Lakini Bwana wetu alitufundisha kwamba “yale mambo tunayotaka watu watutendee inatupasa sisi pia kuwatendea hivyo”, ikiwezekana tuwatendee kwanza na bila masharti. Na “kipimo tunachowapimia wengine hicho hicho na sisi tutapimiwa”. Kumbuka sio KIPIMO hicho umetumia kumpimia mtu mmoja ila ndio KIPIMO umejichagulia watu WOTE au hata Mungu kukupimia wewe!

Ni rahisi sana kumtendea mtu WEMA baada ya yeye kukutendea wewe kwanza (kulipa wema kwa wema), ila pia ni NGUMU kumtendea wema ADUI yako au mtu USIYEMPENDA. Ndio maana Yesu alisema, “Haki yenu isipozidi ya Mafarisayo, hakika hamtauingia Ufalme wa Mungu”. Kumbuka hii HAKI haimaanishi IMANI tu ila na KUTIMIZA mambo ya KIJAMII yanayotuhusu! Yesu akazidi kufundisha akisema “kunatofauti gani kufanya jema wa watu uwapendao?” maana KILA mtu anaweza kufanya hivyo hivyo! Lakini Akatufundisha namna ya KUWEZA kwa maana ni NGUMU sana kutenda kwa namana hii. Akatufundisha KUWAPENDA adui zetu na KUWAOMBEA wanotuudhi! Huwezi kumtendea wema ADUI na mtu ANAYEKUUDHI kama HUJAJIPANGA kumowmbea! Jaribu uone, ni ngumu na hata ukiweza utaishia kunung’unika ndani yako. Mara nyingi tumesikia watu wanasema “ulinifanyia hivi na vile lakini mimi bado nakusaidi”! Hii kitu acha mara moja kwa sababu hailipi! Inaonyesha hukutoa kwa moyo mweupe ambayo ni kutoa kwa hasara! Omba kama unaona unapaswa kumsaidia mtu na ni ADUI au MTESI wako.

Mfalme Hezekia alipoambiwa na nabii kwamba “tengeneza mambo ya nyuma yako maana utakufa”, Hezekia aligeukia ukuta. Akaomba na KUMKUMBUSHA Mungu matendo yake MAZURI aliyofanya huko nyuma, Mungu akampa BONUS ya miaka 15 mbele ya kuishi. Unaweza ukashindwa kuhuasinisha UREFU wa MAISHA ya mtu na MATENDO yake moja kwa moja lakini ukiangalia kwenye maandiko utagundua kuna AMRI ya Mungu ina sema “waheshimu baba yako na mama yako ili siku zako zipate kua nyingi katika nchi, na uheri pia”. Sasa naamini huwezi kumheshimu mzazi wako MOYONI tu bila kufanya kitu. Heshima inaonyeshwa kwa matendo fulani na hayo matendo basi yana NGUVU ya kuongeza UMRI wako na kusababisha UGUMU au WEPESI (uheri) wa maisha yako hapa Duniani. Kumbuka hatuongelei majaribu wala kazi ya Ibilisi, ila ni WEWE na MATENDO yako ambayo mengi yamejikita katika TABIA yako nzuri au mbaya.

Doricas alikua mama mmoja ambaye alijitoa sana kusaidia wajane wakati ule wa Mitume. Akafa. Wale wanawake wakaona haiwezekani huyu mama afe hivi hivi tu jisi walimpenda na kufaidi vipwa vyake mbalimbali. Wakamlaza Ghorofani. Wakamwita Petro wakampa kazi ya KUFUFUA mtu “wa matendo mema” ili azidi kutenda KAZI njema! Mungu akamfufua Doricas, akampa siku zaidi za kuishi. Connection iko katika “matendo yake kwa ile jamii”.

Maandiko yanasema wazi sana kua Mungu hana upendeleo, lakini nakwambia sio kila mtu anapokea sawa na mwingine kutoka kwa Mungu huyo huyo. Sehemu ya sababu hii ni MAKUSIDI na WITO wako mbele za Mungu ila na KIASI cha utii wako katika mambo mengine ya Mungu na unavyo WATENDEA watu wengine. Yesu akasema “heri wenye rehema maana watapata rehema”. Rehema ni huruma kwa matendo. Kwa mfano, watu wawili wana shida sawa, mmoja kabla hajalia shida, watu managombania kuleta michango na misaada, huku mwingine anajitahidi kuomba na kutafuta misaada ila watu “hawaguswi” na hakuna anayemrehemu hadi anakufa na shida yake! Kumbuka, ukiwarehemu watu “wowote” nawe utapata rehema kutoka “kokote”!

Korinelio alikua “akiwapa watu VITU vingi” na alikua akisali daima. Hakua mlokole, ila alikua mtu wa MATENDO mema. Biblia inasema zile “SADAKA” zilifika Mbinguni na zikawa UKUMBUSHO mbele za Kiti cha Enzi! Kumbuka huwezi kutoa kwa kiwango hiki kama huna REHEMA ndani yako. Kwa MATENDO ya Kornelio, jinsi alivyo WAREHEMU watu, Mungu akamrehemu na kumpa zawadi ya WOKOVU yeye na NYUMBA yake! Kumbuka, wakati anatoa hivyo vitu na misaada alivyovitoa vyote viliitwa “vitu” na sio “sadaka”. LAKINI kwa Mungu unapotoa hata kama umempa mtu offer ya soda katika “kutoa kwema”, hiyo ni sadaka kamili na inaenda Mbinguni “kule ambako hakuna wezi, nondo, wala kutu iharibuyo”, na Mungu huachilia BARAKA juu yako na hutajua kwamba ni ile soda tu!

Kuna uhusiano mkubwa sana wa maisha ya kawaida ya mtu na mafanikio yake ya kiroho na hata uwezekano wa kuingia Mbinguni au kutokuingia. Dhambi iko upande mmoja, ila kuna upande wa pili ambao ni ngumu kuupima. Kwa mfano, yule kijana tajiri aliyemfuata Yesu na kumuuliza afanyeje ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu aliambiwa “Je! Umezishika amri?” Kijana akasema NDIO, “Yesu akampenda!” ila akamwambia “uza ulivyo navyo na uwape masikini”. Kijana akageuka na kuondoka kwa maana alikua na mali nyingi. Sasa kumbuka, ninachotaka uone hapa ni 1. Kumshika Mungu ni muhimu, 2. Je! Hao jirani zako na watu waliojaa kila kona wajane, yatima, masikini, wenye shida mbali mbali umefanyaje? Yesu akasema “ni vyepesi kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko TAJIRI kuingia katika Ufalme wa Mungu”! Wengi humu watajiona ni SALAMA kwa maana wanajiita wao sio MATAJIRI. Sikiliza, Utajiri una awamu zake. Utajiri unakua au kupungua kutokana na nini UNAFANYA au HUFANYI. Kila mtu kwa awamu yake aliyo sasa ni TAJIRI kwa hivyo vitu Mungu alivyokupa, na utajiri huu UNAKUA au KUPUNGUA kwa kadri unavyojipanga na Mungu ua na JAMII inayokuzunguka. Kumbuka, ukijipanga sawasawa na Mungu na Jamii kwa pamoja utabarikiwa DUNIANI na UZIMA wa milele. Ukijipanga KIJAMII zaidi utafanikiwa pia na utakua tajiri kwa maana “KILA apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu na KILA apandaye haba atavuna haba”. Mbegu ni mbegu usidanganyike ikipandwa ITAOTA tu! Hata kama aliyepanda ni Korinelio ambaye hajaokoka wala hajajazwa Roho mtakatifu, tofauti tu ni kwamba haendi mbinguni.

Lengo la somo hili ni kukufungua macho juu ya MATENDO yako ya kila siku kwa WATU wengine katika JAMII, ili uweze kuona jinsi ambavyo matendo yako yanaweza 1. Kuathiri umri wako wa kuishi 2. Uheri wa maisha yako 3. Kufungua misaada (rehema) kutoka kwa watu mbalimbali na Mungu pia, na 4. Kubarikiwa kwa Baraka za aina nyingi.

Frank Philip.