Monday, December 30, 2013

MAOMBI YENYE NGUVU.......SEHEMU ya III



 MAOMBI YENYE NGUVU
Imani ya Kupokelea Majibu ya Maombi Yako

Katika Mfululizo wa somo lenye kichwa “MAOMBI YENYE NGUVU”, nimeona nizame kidogo kwenye kipengele cha ‘iv’ cha sehemu ya II ya somo hili kinachosema “JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA”.

Mara nyingi sana watu wanachukulia SOMO la imani kwa wepesi usiostahili. Kama kuna kitu cha muhimu katika maisha ya Mkristo ni kujua FAIDA na MADHARA ya kutokuwa na IMANI. Sijui ni kwanini utasikia mara nyingi sana watumishi wa Mungu wakihusianisha imani na kushindwa kupokea majibu ya maombi lakini ni mara chache utasikia wakitia mkazo somo hili la IMANI kwa KUSUDI la KUMPENDEZA Mungu.

Kusudi la Msingi la IMANI sio kupokea majibu ya maombi yako ila KUMPENDEZA Mungu. Sababu ya msingi ni kwamba mahitaji tunayoomba kwa Mungu sio ya kila saa na kila siku, ila mambo YOTE tuyatendayo katika maisha muda wote yanahitaji IMANI ili umpendeze Mungu kwa sababu imeandikwa “haiwezekani kumpendeza pasipo imani” (Waebrania 11:6) na “kila jambo lisilofanyika katika imani ni dhambi”. Sasa jiulize kwamba unafanya mambo mangapi pasipo imani? Kutokana na mistari hii miwili najifunza kwamba LENGO la msingi la IMANI ni kumpendeza Mungu na ndipo faida zingine huja pale unapoitumia imani hiyo KUOMBA au KUPOKEA majibu ya maombi yako.

Katika sehemu hii ya III ya somo hili natamani tujifunze hiki kipengele cha IMANI ya kupokea majibu ya maombi yako. Nitatumia mfano wa NDOA ya Zakaria na Elizabeth ambao ni wazazi wa Yohana mbatizaji na Maria, mama wa Yesu.

Nitaanza na Zakaria na Elizabeti. “Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana” (Luka 1: 5-7). Hawa wawili walikuwa wakiishi maisha ya KUMTUMIKIA Mungu katika usafi na utauwa. Walitamani sana kupata mtoto na walimwomba Mungu (kwa sababu walikuwa na IMANI ya KUOMBA) kwa muda mrefu bila majibu. Haikuwasumbua kwamba hawakujibiwa, walizidi kukaa katika HUDUMA na UTUMISHI Mungu aliowaitia na waliendelea na zamu zao.

Mungu akamtuma malaika Gabriel kupeleka ujumbe kwa Zakaria akiwa madhabahuni katikati ya huduma. Malaika akasema “Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.” (Lika 1:13). Alipoambiwa habari za MAJIBU ya maombia yake, “Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.” (Luka 1:18-20). Sasa nataka uone kwamba hawa WATUMISHI waliomba kweli ila ilipofika mahali Mungu anasema “nimesikia MAOMBI yenu na sasa najibu” bado HAWAKUSADIKI/HAWAKUAMINI kama inawezekana! Yaani hawana imani ya kupokea MAJIBU ya maombi yao! Sasa Malaika akamfanya bubu. Kwa haraka unaweza kuona kama ni ADHABU ya kutokuamini kwake (Mungu hafurahishwi na mtu wa kusita-sita/mashaka/kutokuamini kama Anaweza) ila kuna sababu ya pili ambayo ni KUHARIBU imani ile ya KUPOKEA majibu kwa UKIRI mbaya (negative confession) basi dawa ni kumnyima kuongea hadi majibu ya maombi yatokee.

Ukija kwa upande wa Maria, mama wa Yesu. Gabriel huyo huyo alikuja na habari ya kupata mtoto ila “kwa uweza wa Roho Mtakatifu”. Utagundua kwamba Maria na yeye aliuliza swali linalofanana na la Zakaria ila hakupigwa na ububu! Ujumbe huu ulimjia Maria miezi 5 baada ya Elizabeti kuwa mjamzito. Sasa wakati Maria anamuuliza Gabriel haya mambo yatakuaje, kulikuwa na SHIDA ya IMANI ya KUPOKEA huo muujiza pia. Kabla Gabriel hajaondoka ilibidi ainue imani ya Maria kwa kumpa “Neno la Mungu lililotamkwa kwa kinywa cha malaika kwa Zakaria” (“Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu”). Baada ya Gabriel kuleta ujumbe “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.” (Luka 1:34-38). Huu msitari wa 38 unatuonyesha imani ya Maria imeinukana na kuona INAWEZEKANA kisha Malaika akaondoka.


Tukiendelea kujifunza hapa utaona “basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana” (Luka 1: 39-45).

Hawa wanawake wawili walimshangilia Mungu kwa pamoja ila ukitizama kwa makini utagundua baada ya Elizabeti kujazwa Roho Mtakatifu, alirudia yale “maneno ya kuimarisha imani ya Maria” na mwishowe utaona kwamba anasema “aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”. Ikimaanishwa kwamba kuna IMANI inatakiwa KUPOKEA hiyo ahadi japo kweli kabisa ni Malaika/Bwana amesema. Kumbuka siku zote, AHADI iliyoko kwenye Neno la Mungu sio yako hadi utakapokuwa na IMANI ya KUTOSHA kuimiliki/kuipata hiyo AHADI.

Tukiendelea kujifunza utaona Maria anaimba wimbo wa kumshukuru Mungu baada ya haya maneno ya Elizabeti. Maneno ya wimbo wa Maria ni marudio ya yale ambayo malaika alikwisha kusema na jinsi alikubali kusudi la Mungu kutimia kwake, huku akiona ni UPENDELEAO wa pekee kupokea BARAKA hii kubwa. Huu ni UKIRI wa kuimarisha na kulinda IMANI yake ya KUPOKEA mtoto.

Ukifuatilia zaidi utaona Maria alikaa kwa Elizabeti miezi 3. Yamkini walikuwa wakitiana moyo katika kubeba MIMBA muhimu katika maisha yao na kufikilia KUJIFUNGUA salama sawa na KUSUDI la Mungu. Sasa mara nyingi sana katika maisha yetu tumekuwa na imani nzuri tu wakati wa kuomba, ila HALI HALISI zimetufanya kuona HAIWEZEKANI KUPOKEA majibu ya maombi yetu na imekuwa kikwazo. Fikiri hii hali, binti anaambiwa atapata mimba bila kumjua mwanaume! Na upande mwingine kikongwe aliyepitiliza siku za kuzaa anaambiwa atapata mimba! Hali halisi inasema HAIWEZEKANI. Sasa kama mtu hatakuwa na IMANI, na hajui namna ya kuzimisha sauti za SAYANSI, TEKINOLOJIA na ELIMU zingine, imani ya KUPOKEA inakufa. Hata kama ni Yesu anakuja/anazaliwa, ILIBIDI Maria awe na IMANI ya KUPOKEA! Ilibidi Malaika Gabrieli ampe Maria mfano wa “jambo lisilowezekana” na jinsi ambavyo “limewezekana kwa Mungu” ili kuinua IMANI yake ya KUPOKEA.

Kitu cha kukusaidia kukuza/kupata IMANI ya kupokea majibu ya MAOMBI yako ni KUJIFUNZA matendo Makuu ya Mungu katika Biblia, na kuyatafakari usiku na mchana, na kuyataja unapotarajia MAJIBU ya maombi yako. Jifunze KUKIRI matendo makuu unayoyajua ya Mungu wetu ukiwa katika maombi kwa mfano, wakati Daudi anamkabili Goliath alisema maneno ya IMANI yake kwa Mungu, “Mimi mtumishi wako nimezoea kuchunga kondoo wa baba yangu. Kila wakati simba au dubu akija na kukamata mwanakondoo mimi humfuata na kumshambulia, nikamwokoa mwanakondoo kinywani mwake. Kama simba au dubu akinishambulia, mimi humshika ndevu zake, nikamwangusha na kumuua. Mimi mtumishi wako nimekwisha ua simba wengi na dubu wengi. Sasa, hata yule Mfilisti asiyetahiriwa, ambaye ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai, atakuwa kama hao. Mwenyezi-Mungu ambaye ameniokoa makuchani mwa simba na dubu, ataniokoa kutoka kwa Mfilisti huyu” (1 Samweli 17:34-37). Zungumza na HALI unayopitia na uitangazie USHINDI katika MAOMBI, itaje hiyo shida kwa jina “lake” na uiambie kwa maneno kama unazungumza na mtu, huku ukiikemea kwa Jina la Bwana wa Majeshi. Wakati huo ukitamka matendo mengine MAKUU ya Mungu ambayo yamefanyika kwa watu wengine. Kwa kufanya hivyo ghafla! Utaanza kuona Mungu ni MKUBWA kuliko hiyo shida/jambo unaloomba na IMANI yako inaongezeka wakati huo MASHAKA yakitoweka. Kumbuka Ibilisi huleta VITA katika FIKRA zetu ili kutujengea ngome, na njia mojawapo wa kumshinda ni kwa kutumia “NENO la ushuhuda na Damu ya Mwana-kondoo” (Ufunuo wa Yohana). Hii ni SIRI ya KUJAZA imani ya KUPOKELEA lakini pia kumshinda Adui azuiaye.

Mungu atusaidie kujenga IMANI zetu kwa KUJIFUNZA kwa bidii maandiko na kuomba. Hatimaye tuweze kutenda KILA jambo kwa imani kwa kusudi la kumpendeza Mungu na kuweza KUOMBA na KUPOKEA majibu ya maombi yetu kwa hiyo IMANI.

Roho Mtakatifu atufundishe NENO la Mungu na kutuwezesha kupata UFUNUO katika hilo Neno ili kujenga IMANI zetu. AMEN.

Frank Philip.

VITA KATIKA KUSAMEHE!!!


Kusamehe mtu aliyekukosea ni moja ya mambo magumu ya KIIMANI ambayo LAZIMA uweze kama unataka KUMUONA Mungu katika maisha yako.

Sababu na faida za kusamehe ni nyingi lakini nitataja chache. 1. Tunasamehe watu waliotukosea ili na sisi tusamehewe DHAMBI (madeni yetu) na Mungu. Katika sala ya Bwana kuna sehemu tunamwambia Mungu “utusamehe dhambi (deni) zetu kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea (wanaotudai). [nitarudi kueleza habari ya deni hapo baadae]. 2. Dhambi zina NGUVU ya kuficha uso wa Mungu usiuone, KUZIBA sikio lake ASIKUSIKIE na kuzuia Mkono wake USIKUOKOE. Nabii Isaya anasema hivi “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.” (Isaya 59:1,2).

Kumbuka KIPIMO ya KUSAMEHEWA dhambi na madeni yako kwa Mungu UNAJIPIMIA mwenyewe kwa JINSI unavyowasamehe wengine. Na hii unamwambia/unamwomba Mungu katika sala ya Bwana kila unaposali. Kwa lugha nyingina UNAMSIHI Mungu “USINISAMEHE kama jinsi ambavyo SIWASAMEHI watu walionikosea!”. Sasa, kwanini tunasema kwamba KUSAMEHE ni VITA? Kwa sababu anayetaka USISAMEHE sio wewe ila ni IBILISI! Mtu ataniuliza nimejuaje? Angalia hapo juu Isaya anasemaje: kwanza, “ili Ibilisi afanikiwe KUKUZUIA wewe kuuona USO wa Mungu anahakikisha una DHAMBI!”, pili, “ili Mkono wa Mungu USIKUFIKILIE na kukuokoa katika SHIDA, KILIO, na MAUMIVU yako, anakufarakanisha na Mungu kwa kuweka WINGU la uovu kati yako na Mungu na KUZUIA SIKIO lake kukusikiliza”! Mungu anasema “SITAKI kusikia” maombi yako. Ibilisi anachunga sana hii SIRI ili usije ukaondoa UOVU na DHAMBI zako maana ukifanikiwa kuondoa UOVU katikati yako MKONO wa Mungu utadhihirika katika maisha yako katika mambo YOTE na utakua UMEMSHINDA Ibilisi. Sikiliza, Mungu “hulitizama Neno lake na kulitimiza”. Usije ukasema Ibilisi kamdhibiti Mungu! Haiwezekani, ila Mungu ndio kasema HUTANIONA, SITAKUSIKIA na MKONO WANGU HAUTAKUAOKOA, kama kuna UOVU katikati yako! Na Ibilisi analikamata hilo Neno na kulitumia kukutesa. [kama ulikua hujui Ibilisi ni mtendaji wa Neno kuliko watu wengi sana japo huwa analitumia kinyumenyume, na kupambana naye ni LAZIMA ujue Neno na kulitumia kama silaha yako ya VITA. Bila Neno, wewe ni mawindo rahisi ya Ibilisi]

(Yeremia 29: 11-13) “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” Madhara ya kukaa na DHAMBI ni MENGI kuliko unavyoweza kufikiri. 1. Unajikuta unapoteza MATUMAINI (future hope). Huko mbele kwenye maisha yako unaanza kuona giza na kukata tama maana bila sababu, matumaini yanapotea ndani yako! Hii ni kazi ya Ibilisi. Kama unaona unaanza kupoteza matumaini na huko mbele ya maisha yako unaona hakuvutii usihangaike, saka WATU wa kusamehe maishani mwako! Ondoa UOVU katikati yako! Ukiwasamahe “wote” hii hali inakwisha kwa maana MATUMAINI ya mambo MAZURI ni ahadi ya MUNGU wa watu wake na Ibilisi anataka kuinyakua kutoka kwako kwa KUTOSAMEHE. Kama kuna kitu unahitaji ni MATUMAINI, hii ni nguvu ya ajabu sana inayokupa nguvu ya kusonga mbele hata kama uko katika majaribu mazito. “Abrahamu alipoiona ile ahadi…”, “Yesu alipoona huko mbele ya msalaba kuna nini….alishinda msalaba na maumivu yake yote”. Lazima uone MBELE/future na huwezi kuona kama huna MATUMAINI na Ibilisi anakuondolea MATUMAINI ili uzidi kushindwa katika VITA naye. Kitu anachotumia kukuwekea WINGU hili la kutokuona mbele ni nini? Jibu ni UOVU katikati yako! 2. Katika shida na mahitaji yetu mbali mbali huwa tunamwita Mungu. Naye anasema “mtakwenda KUNIITA na KUNIOMBA nami NITAWASIKILIZA, MTANITAFUTA na KUNIONA ila kwa BIDII”. Bidii inatakiwa kwa sababu gani? Ni VITA, Ibilisi hataki UITE na Mungu asikie, wala hataki UKIOMBA na KUMTAFUTA Mungu umuone. Sasa kwa kuwa hawezi KUMZUIA Mungu, anakuja kukudhibiti wewe kwa kuhakikisha UNASHINDWA kusamehe watu waliokukosea! Matokeo yake ni KUZUIA majibu ya maombi yako!

Mtu atauliza kwani Ibilisi anaweza kuzuia majibu ya maombi kutoka kwa Mungu? Sikiliza, Wakati Danieli anaomba, Mungu anamtuma malaika Gabriel kumpasha habari kwamba hizi siku 21 alizokua busy anaomba ajue kwamba ALIJIBU “tangu” ulipoweka NIA ya KUOMBA, (sio wakati alipoanza kuomba) ila kuna VITA hapo juu na MAJIBU ya maombi yako yamezuiliwa, hivyo nimemtuma MIKAELI ashuke kupambana ili huyu MKUU wa giza hapo anayekamata majibu ya maombi yako aachilie! Sasa, ukifuatilia sehemu nyingine utaona Danieli aliomba na alianza kwa “toba” kwanini? Ili kusafisha NJIA ya kupokea Majibu. Ndio maana tunafundishwa kwamba “kila tusimamapo kusali sameheni”! Ayubu alijua SIRI hii pia, sio kwamba alitubu kwa ajili yake tu, alitubu hata kwa ajili ya watoto wake, “isije ikawa wamemkosea Mungu mahali”, (isije ikawa…maana yake anatubu hata kama hajui dhambi iliyofanyika! Kama ipo au haipo, yeye anatubu tu na KUACHILIA). Sasa watu wengi sana wamekwama na wameteseka na kila namna ya SHIDA na MAUMIVU mengi kwa sababu WAMESHINDWA kusamehe. Sasa, hebu chukua MUDA kidogo wa kutafakari ile LIST ya mambo uliyoomba na unayotarajia Mungu kukujibu na mengine unakiri umepokea. Kisha kumbuka WATU uliogoma kuwasamehe na ulinganishe FAIDA ya kumsamehe “huyu mtu” na HASARA utakayopata kama ile LIST yako ya maombi HAIJIBWI na Mungu. Pima mwenyewe na chukua hatua. Ukiamua kusikiliza uongo wa shetani ni juu yako, Mungu analeta hili Neno AKUOKOE na KUKUHUDUMIA.

Ngoja nikwambie kitu shetani anafanya hadi unashindwa kusamehe halafu ntakwambia cha kufanya. 1. Ibilisi anajua DHAMBI zako kwa maana yeye ndio amekusababisha UFANYE au amesamabisha watu WAKUKOSEE. Kwahiyo anajua ni wapi ameweka KUFULI ya kukutesa. Ili kuimarisha ile kufuli ikamate sawasawa, unapomwaza “yule mtu” aliye kukosea ghafla unasikia HASIRA au UCHUNGU, halafu analeta VIDEO na PICHA hata na SAUTI ya “yale mambo” ili KUHUISHA ule UCHUNGU na HASIRA ndani yako. Na hii inatokea mara nyingi na UNASHINDWA kumsamehe “huyu mtu” aliyekukosea. 2. Ibilisi anakupa SABABU na VISINGIZIO vya kutokusamehe. Utasikia mtu anasema ndani ya moyo wake au kwa kinywa, “kama kweli uliamua kunisaliti wakati nipo mimi nimekukosea nini?”, “yaani pamoja na kujitahidi kufanya haya yote umeamua kunifanyia hivi?”, nk. Ukisikia SAUTI hizi ndani yako jua ni IBILISI anakuhubiria injili MFU ili ushindwe kusamehe na afanikiwe kukutenga na USO, SIKIO na MKONO wa Mungu na ukose MSAADA wa Mungu. 3. Dhambi inasema! Kila ukisimama kuomba au ukijitahidi kusimama katika BWANA unasikia “sauti ya dhambi” ikipiga kelele moyoni mwako kukuvunja UJASIRI. Kwa lugha nyingine naiita “deni ya dhambi” (guilty)! Kama umewahi kua na deni mtu anakudai na anakusumbua utaelewa nasema nini. Kila ukikumbuka lile deni ni kama “linasema” na wewe huko ndani ya moyo wako kwa sauti! Hii ni vita ya Ibilisi na HUWEZI kuzima hiyo sauti bila MSAADA wa Mungu na Damu ya Yesu. Ndio maana utasikia “kikaribieni kiti cha Rehema kwa UJASIRI kwa Damu ya Yesu”, huu ujasiri unapatikana kwa DAMU ya Yesu.

Kwa sababu MAMBO yako MAZURI na Majibu ya maombi yako kwa WATOTO, KAZI, BIASHARA, nk, yamedhibitiwa na KUTOKUSAMEHE kwako, jua IMEKUPASA kusamehe kwa FAIDA yako KWANZA na sio ya aliyekukosea. Tena, kama unataka uwepo wa Mungu ukutembelee na kukufunika kila wakati na MKONO wake kua pamoja na wewe na USIPUNGUE katika maisha yako ni LAZIMA uondoe UOVU katikati yako. Kumuona Mungu maana yake ni “kumuona akikupigania na adui zako wakishindwa huku na huku na wewe ukiwa mshindi BILA sababu”! Hii lugha ni ngumu lakini sikiliza, Mungu anasema kwa kinywa cha DAUDI kwamba “hii nchi hamkumiliki kwa sababu ya upanga wenu wala mkuki, (sio nguvu zenu, au hamkufanya chochote) ila ni nuru ya uso wangu umewaangazia” sasa kumbuka DHAMBI zako zinaficha USO wa Mungu usiuone! Kwa lugha nyingine pamoja na KUPAMBANA sana na UPANGA wako bado ni NGUMU, ila Yule aliyeondoa UOVU katikati yake nakwambia HATASHINDA kwa upanga, Mungu anatangulia mbele zake na kumpa ushindi bure! Mungu anasema “kabla ya kuomba mimi Bwana nitajibu, na mkiwa katika kunena Nitasikia”. Mungu anamwambia Danieli, “ulipotia tu nia mimi nilijibu” Sasa iweje leo watu wanafunga na kuomba na INAKWAMA? Ondoa UOVU na DHAMBI katikati yako! Sio tu kwa KUTUBU dhambi zako ILA na KUWASAMEHE walio kukosea hata kama ni NGUMU. Kumbuka kwa NJIA mbili zote kwa pamoja 1. Tubu (na geuka) na acha dhambi 2. Samehe dhambi zote watu walizokutendea. HAKIKA utamwona Mungu maishani mwako kwa namna hujawahi kutarajia.

Kwanini unapata ujasiri wa kutenda dhambi? Hii ni SIRI nyingine nataka nikupe kabla ya kumalizia kukupa DAWA ya kupona. Kufanya dhambi inahitaji ujasiri wa aina yake. Umewahi kufikiri mtu anachukua KISU anamchoma mwenzake? Bila ujasiri huwezi. Au umewahi kufikiri mtu mzima anavua NGUO zake mbele za mtu mwingine wa JINSIA tofauti na anazini? Kwa kweli inahitaji ujasiri na huu unaupata kwa Ibilisi. Sasa kabla ya kufanya “hii dhmbi” lazima akupe ujasiri. Utasikia ndani yako “kama huyu jamaa hanijali basi na mimi nafanya ngono na huyu mwingine kwa sababu angalau yeye ananijali”, “kama kila mtu anakula rushwa kwani nini na mimi nisichukue hiki kidogo tu?”, “kama amenirusha hela yangu na mimi simpi msaada”, “kama Fulani alianguka katika uzinzi na yuko kanisani mi naona hii ni ngumu kwa hiyo watu wataelewa”, “watasema mchana na usiku watalala”, “hii ni ZAWADI sio rushwa”, nk., ghafla! unapata UJASIRI kwa kufanya KITU ambacho ni KIOVU ndani yako UKISHUHUDIWA kwamba UNAMKOSEA Mungu ila Ibilisi kashakujaza UJASIRI kwa hiyo unajikaza na KUFANYA. Sasa kumbuka ukifanya dhambi “moja”, madhara huwa yanakua zaidi ya moja! 1. Unauzuia Mkono wa Mungu kukuokoa, Uso wake usikuone, na Sikio lake lisikusikie 2. Unatengwa na Mungu, 3. Unazuia majibu ya mombia yako. Haya mambo matatu yanatokea kwa pamoja! Sasa kumbuka nimetaja matatu ila ni mlolongo wa mambo mengi sana uko hapo. Kwa sababu kuzuiliwa “majibu ya maombi” yako itawaathiri na wale waliokua wanapona kwa WEWE kuwaombea! Kwa maana ni majibu ya maombi YOTE yamedhibitiwa. Unaanza kushangaa watoto wako wanateseka na uko busy kuwaombea na hakuna kinatokea! kumbe kisa HUTAKI kumsamehe baba yao, nk!

Kumbuka siku zote, Ibilisi AKIKUSUKUMA kutenda dhambi sio ili UFAIDI, NO! ni ili akutenge na Mungu na apate nafasi ya KUKUANGAMIZA! Sasa, Neema ya Mungu hututetea (hasa tunapokua wajinga). LAKINI ukilijua Neno hili na ukaufanya moyo wako MGUMU, utaangamia! Kwa maana Mungu hulituma Neno kuwaponya mataifa lakini wasipolipokea Maangamizi hufuata, ila kabla ya HUKUMU lazima Neno litangulie. Unaweza kushangaa nasema nini, lakini ukisoma maandiko utaona Nuhu alihubiri kwa miaka takriban 100 akiwaambia watu watubu, na hawataki NDIPO gharika ikaja. Sememu nyingine tunasoma “aonywaye MARA NYINGI akishupaza shingo itavunjika na dawa hapati”. Hii ina maana KABLA ya shingo kuvunjika Mungu anakuletea Neno MARA NYINGI kukuonya na ukikataa KUTII basi Ibilisi anakumaliza. Sehemu nyingine tunaambiwa kwamba Yesu atakuja kuhukumu Ulimwengu, lakini ni baada ya INJILI kuhubiriwa kwa KILA kiumbe! Ili aije sema mtu sikusikia. Hii ndio tunaita Neema! Ndani ya Neema kuna muda wa Mungu kukusubiri UTUBU, ukichezea huu muda na “kikombe kikijaa” Unaangamia! SIKIA SAUTI yake LEO na UFANYE maamuzi na KUGEUKA.

DAWA ya kupona ni KUZIUNGAMA (kutaja dhambi kwa majina yake) kwa Mungu DHAMBI zako na KUWATANGAZIA wale watu waliokukosea kwamba UMEWASAMEHE BURE! Sasa, sikiliza. Kuwatangazia watu MSAMAHA pia ni VITA, tena NGUMU sana kutokana na MAJERAHA uliyopata “ulipokosewa” na hawa watu. Ndio maana utakuta mtu ANALIA tu kila akikumbika MTESI wake, Jipe moyo, Mungu anaona MAUMIVU yako. Anza na KUMTANGAZIA huyo mtu msamahawa wake kwenye MAOMBI, kisha chukua hatua ya IMANI na kumtangazia masikioni kwamba “NIMEKUSAMEHE bure”! Na ukiona ile hali inarudi huku ndani, kimbilia magotini tena na MTANGAZIE na IBILISI kwamba hii dhambi haipo nimesamehe na Yesu kafuta kwa Damu yake. Sisitiza hili katika Maombi hadi usikie UHURU wa ndani. Ukivuka hapo ndio sasa kile kipengele ya KUSAMEHE na KUSAHAU kitaanza kuwa dhahiri kwako, la sivyo ni NGUMU kibinabadu asikudanganye mtu. Bila Mungu huwezi KUSAMEHE na KUSAHAU, tafuta msaada wa Mungu kushinda VITA ya KUSAMEHE.

Uwezo wa kusamehe mtu (tolerance) Kimungu ni ndefu hakuna awezaye kufikia. Yesu alisema 7x70 kwa siku. Tena ni mtu huyo huyo anarudia kukukosea na kuomba msamaha kwa SIKU! Unatakiwa kumsamehe, hata kama ANARUDIA makosa yale yale. Nakubaliana na wewe kwamba unaweza kukosewa mara “moja” ikawa kubwa kuliko “Elfu”! Sawa, ndio maana nasema ni VITA na unahitaji msaada ya YESU kushinda na UWEZE kusamehe maana madhara ya KUTOKUSAMEHE ni MAKUBWA kuliko unavyofikiri. Kumbuka, kama WEWE unatakiwa uwe na UWEZO wa kusamehe mara 490 kwa siku, Je! Yesu ANAWEZA kukusamehe wewe mara ngapi ukimkosea? Jifunze KUJISAMEHE na KUJIACHILIA mwenyewe maana kila dhambi ULIYOITUBU Yesu alifuta ghafla! Pale ulipoanza tu kutubu.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wake Mungu Baba Ukae nanyi tangu sasa na hata milele.

Frank Philip.

Sunday, December 29, 2013

"UPENDO"


(Jua uhusiano kati ya UASI kwenye MAHUSIANO ya kijamii na UPENDO wako kwa Mungu)

Ukifuatilia nyakati katika maandiko utagundua kwamba tunaishi nyakati za mwisho. Tumekaribia mahali ambapo Yesu anarudi kulichukua Kanisa lake. Hakuna ajuaye ni karibu kiasi gani ila ni KARIBU. Yesu anasema yuko malangoni, anakuja.

Yesu alisema dalili ya nyakati za mwisho (Mathayo 24:3-13) na zinaonekana. Ila nataka niongelee MAASI. Huku mwisho wa nyakati tuliko tunaambiwa KUTAONGEZEKA MAASI na UPENDO wa wengi utapoa. Upendo ni kitu cha ajabu sana ambacho Mungu amewaumbia wanadamu. Mtu AKIPENDA ghafla! anakua mtu wa hatari maana huo UPENDO utamsukuma kufanya vitu bila kujali “sana” GHARAMA wala MUDA. Kwa mfano UPENDO wa mtu kwa Mungu utamsukuma huyo mtu kusimama kwa UAMINIFU mbele za Mungu hata kama anateseka na ataridhika na kila kitu kigumu na cha MAUMIVU alimradi asimtende Mungu dhambi. Sasa, UPENDO wa mtu huyu UKIPOA hutaamini vitu ataanza kufanya. Ghafla! visingizio vingi sana vinaibuka na sababu nyingi sana za MSINGI za kumkosea Mungu zinaibuka, ila ukifuatilia kinachotokea kwa huyu ndugu ni kitu kimoja tu UPENDO WAKE KWA MUNGU UMEPOA!

Sasa tunajua kabisa kwamba Mungu wetu ana NGUVU kuliko Ibilisi. Na hakuna siku ibilisi atakinga MSULI kwa Yesu akafanikiwa maana Yesu yuko juu sana katika UWEZA, sana sana ikiibuka vita atamtuma tu MIKAELI akamshughulikie huko na yeye akaendelea kumtizama BIBI ARUSI wake anayempenda sana ambaye ni KANISA. Ibilisi anachofanya hapa kwa wana wa Mungu ni KUONGEZA MAASI kati yao! USALITI katika mahusiano, biashara, familia, ndugu, huduma, nk. Huu usaliti unasababisha watu KUJERUHIWA ndani yao na UPENDO wao UNAPOA bila wao kujua! Wengi sana wamefika mahali pa gumu sana na wameweka SILAHA zao chini kwa sababu wamejeruhuwa na ADUI wakiwa KAZINI. Madhara yake yanapelekea KAZI yao kusimama shambani mwa Bwana, wamebaki KULAUMIANA na SHUHUDA MFU za watu waliowatendea mambo “mabaya” badala ya kushuhudia MATENDO makuu ya Mungu!

Watumishi wengi sana na wana wa Mungu wameacha zile SHUHUDA za “kuokoa” watu na Ibilisi ameanza kuwatumia kusambaza shuhuda KANDAMIZI za kurudisha watu nyuma! Ushuhuda ni habari NJEMA! Hili ndilo jina jingine la INJILI, habari njema kwa watu wote! Sasa, watu wengi sana wamewekeza kwenye habari MBAYA za watu na zimewavunja wengi sana moyo (hasa wachanga katika imani) na kuwajeruhi badala ya kuwajenga! Hayo MAASI ambayo yametokea, na WEWE mwana wa Mungu umejeruhiwa na umepata UCHUNGU na kwasababu hujashughulikia uchungu wako UMENAJISI wengi kanisani na madhara ya ule UASI “mmoja” umekua JANGA kubwa maana umesambaa na KUZIMISHA upendo wa WENGI kwa mara moja bila wewe kujua. Tunaonywa tuangalie “shina la UCHUNGU lisichipuke ndani yetu” maana UCHUNGU ndani ya mtu mmoja una uwezo wa kunajisi watu WENGI ambao hawakuhusika katika TUKIO lililosababisha huo uchungu. Chunga sana hili ENEO maana unaweza kujikuta umegeuka kuwa mtumishi wa Ibilisi kusambaza UCHUNGU bila kujua na ukamfanikishia Ibilisi kazi yake ya KUNAJISI watu!

Nitatoa mfano wa huduma ya Yesu. Wakati huduma ya INJILI inaendelea kwa kasi kubwa, Petro na wenzake “wako tayari kupigana kwa upanga kumtetea Yesu hadi kufa”, na ikafika mahali Petro anatoa upanga ALANI mwake kwa ajili ya kumlinda Yesu, na alijikuta anakata mtu sikio ghafla, aliona huyu jamaa anamsogelea Yesu. UPENDO kwa Bwana wake ukamsukuma “kupiga mtu”. Kabla Petro hajakaa sawa anaona YUDA, ambaye ni MTUMISHI mwenzake hapo pembeni anachukua RUSHWA, kabla hajakaa sawa anaona ANAMBUSU Yesu hadharani, kabla hajakaa sawa anaona Bwana wake AMESALITIWA LIVE na sasa ANASULUBIWA! Na aliyemsaliti ni MTUMISHI mwenzake ambaye wamefanya HUDUMA pamoja kwa takriban mika 3! Yesu alimwamini YUDA kiasi cha kumfanya MWEKA HAZINA wa HUDUMA yao. Leo machoni pa kila mmoja wao katika HUDUMA na wakiwa KAZINI anamsaliti Bwana wao! Hili jambo liliwasambaratisha wote wakatawanyika, sio kwa hofu tu ya wale waliokua wanamsulubu Yesu lakini pia ile hali ya UASI iliyojitokeza imeathiri UPENDO wao na WAKARUDI nyuma!

Kabla Petro hajakaa sawa anaulizwa “wewe si ulikua na huyu jamaa”, Petro anasema SIMJUI mtu huyu! Hataki hata kutaja jina la Yesu, safari hii anamwita “mtu huyu”! Mara tatu anamkana YESU hadharani! ila kilichotokea kabla ya hapo ni UASI mkuu na USALITI wa waziwazi! Wanafunzi walitawanyika kwa sababu “mchungaji wao amepigwa”. Petro akarudi zake KUVUA samaki ziwani, akaachana na BIASHARA ya Yesu maana UPENDO umepoa! Huyu ni Yule Petro ambaye alisema “hata wakikuacha wote mimi sitakuacha, niko tayari kufa kwa ajili yako, nk”. Sasa kimetokea nini? Upendo umepoa. Yesu alipofufuka akamtafuta tena Petro, akamuuliza “Petro UNANIPENDA?”, akarudia mara ya pili “Petro UNANIPENDA?” na mara ya tatu kurudia Petro AKALIA! Na akamwambia “Bwana unajua nakupenda…”. Ninachotaka uone hapa ni ile hali ya KUKATA TAMAA na KURUDI nyuma ya Petro baada ya VURUGU nyingi kutokea katika HUDUMA yao. Na YESU alikua ANAHUISHA ule UPENDO kati yao ambao ULIATHIRIKA. Hapo wakati Yesu anampa Petro kazi unaweza kujiuliza kwanini amuulize kwanza “unanipenda” ndio asema “LISHA KONDOO”, “CHUNGA KONDOO”, nk.? Sababu ya msingi hapa ni HUWEZI kufanya kazi ya MUNGU kama HUMPENDI! Jaribu uone halafu mbwa mwitu aje kama hujakimbia na kuacha KONDOO wanaliwa huko! Nakwambia mchungaji ANAYEPENDA kondoo zake “itamgharimu” maisha kwa kondoo hao. Sio mimi, ni maandiko yamesema.

Sasa katika maisha ya leo wengi wetu tumejeruhiwa sana na “watu” katika michakato mbalimbali ya maisha na kwa sababu UASI umeongezeka UPENDO wetu kwa Mungu na kwa “hao watu” umeathirika kwa viwango tofauti. Wengine WAMEACHA wokovu na wengine WAMERUDI nyuma. Sasa Ibilisi akifanikiwa kukurudisha nyuma, ukampa nafasi ya kurudi pale alikofukuzwa wakati unampokea Yesu, huwa anaongeza “idadi ya MAPEPO mara 7, tena wale waovu zaidi, na hali ya mtu huyu inakua mbaya kuliko ya mwanzo”! ili akifanikiwa “akuchinje” kabisa usije ukatubu!

Ukifahamu SIRI hii utagundua ni kwanini MTU akisalitiwa katika MAHUSIANO ni rahisi sana kurudi nyuma katika WOKOVU pia! Ule UASI una NGUVU ya KUPOOZA upendo wako kwa Mungu na kukumaliza kiroho USIPOANGALIA. Katika NDOA, HUDUMA, MAKANISANI, nk. kumekua na hiki kitu cha KUSALITIANA na kimeathiri kazi ya Mungu kwa kiwango kikubwa sana kwa sababu kimegusa eneo nyeti la UPENDO. Ni jambo la kusikitisha sana “mmoja” katika HUDUMA au NDOA anakua AGENT wa shetani “kwa muda” (bila kujua) kama ilivyokua kwa YUDA. Na kwa kipindi kifupi anatumika kufanya KITU ambacho kitasambaratisha HUDUMA au NDOA moja kwa moja. Ibilisi akimwachia huyu mtu (kwa maana ilikua kwa kitambo tu) akizinduka, anajuta! Ndio maana YUDA alikimbilia KITANZI na wala ile RUSHWA hakuila! Alisikia vibaya sana baada ya KUFANYA ule UASI na USALITI na akachukua ile HELA na kuirudisha kwa wenyewe! Too LATE! Yesu yuko msalabani saa hizo na huku huduma ishasambaratika WATUMISHI wenzake akina Petro nao “washaharibu” na akina Yohana na wenzake washatokomea kusikojulikana. Yesu alipofufuka alifanya kazi ya KUWAKUSANYA hawa wanafunzi wake kwa UPYA baada ya kusambaratika vibaya.

Angalia mambo ya kwanza uyape umuhimu wa kwanza. Watu wengi sana wako busy na HUDUMA na kusahau kwamba UPENDO ni msingi wa YOTE. Mungu havutiwi sana na hayo mambo kama HUMPENDI, na utakosa Ufalme wa Mungu usipojipanga pamoja na huduma yako kubwa nchi nzima au hata dunia nzima. Kumbuka (1 Wakorintho 13:1,2) “Tena nijapokuwa na UNABII, na kujua SIRI zote na MAARIFA yote, nijapokuwa na IMANI TIMILIFU kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina UPENDO, si kitu mimi. 2 Tena NIKITOA MALI ZANGU ZOTE kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.” Shughulikia eneo lako la UPENDO wa KWANZA na Yesu. Fanya “toba” ya dhati ukikiri (kutaja kwa jina) pale “ulipoa anguka” maana unatakiwa UPAKUMBUKE na kumwambia Yesu, na kisha omba “maombi” yako ya dhati ili KUHUISHA ule UPENDO wa kwanza, na utaona mabadiliko na BARAKA zikimiminika kwako kwa namna ya tofauti.

Lengo la somo hili ni kukutahadharisha kuwa tuko nyakati za hatari. UASI ni mwingi na usipoangalia unaweza KUPOOZA UPENDO wako wa KWANZA! Na Yesu anasema na wewe akijua “umeuacha ule UPENDO wako wa kwanza”, ule ambao ulikuweka chini ukasoma Neno na kuomba na KUSHUHUDIA au kumtumikia Mungu katika ngazi mbali mbali. Naye anasema “kumbuka ni wapi ulipoanguka ukatubu”. Fanya HARAKA kwa sababu hizo njia za YUDA kweli zitakupa HELA, ila ni vipande 30 tu! Kumbuka thamani ya DAMU ya Yesu iliyokununua, FANYA uamuzi LEO kama UNAZIDI kumsaliti MWANA wa MUNGU au unamrudia. Mungu atusaidie kufanya maamuzi sahihi. NEEMA ya BWANA na iwe JUU yako tangu SASA na hata milele. AMEN.

Frank Philip.

Thursday, December 26, 2013

NDOA YA YUSUFU NA MARIA!!!


Nimetamani sana tujifuze jambo katika ndoa ya Yusufu na Maria. Nimechukua mfano huu kama ndoa/uhusiano wowote wa mwanaume na mwanamke ambao lengo lake ni kuishi kama mke na mume.

Kuna mambo kadhaa najifunza kwa maisha ya binafsi ya Yusufu na Maria. Yusufu alikuwa mtu wa haki, mtu mwenye heshima yake na jina jema katika jamii iliyomzunguka. Aliukuwa na kazi yake ya useremala ambayo yamkini ilimwingizia kipato. Kwa upande mwingine hatuambiwi Maria alikuwa anajishughulisha na nini ila alikuwa BIKIRA, ikimaanisha alikuwa msichana aliyejitunza na kuishi maisha masafi. Hawa wawili walikuwa wachumba na walidumu katika UHUSIANO huo katika USAFI wote. Kuna mambo manne (4) nataka tuone hapa. (Luka 1)

i. Kipindi cha Giza

Wakati maisha yanaendelea, ghafla! Malaika analeta habari kwa Maria kwamba atapata mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu na atazaa mtoto wa kiume. Kwa Maria ilikuwa ni habari ngumu ila alikubali kama MTUMWA kwa Bwana wake kwa sababu alijua ni mapenzi ya Mungu. Sasa nisikilize vizuri, wakati Malaika Gabriel analeta habari kwa Maria kwamba AMEBARIKIWA, tena amebarikiwa kuliko wanawake wote, na kwamba mtoto atakayezaliwa atarithi kwenye kiti cha mfalme “Daudi”, Maria anasikai raha hadi anaenda kwa ndugu yake Elizabeth [mama yake Yohana mbatizaji], anamshangilia Mungu kwa wimbo na wanajazwa Roho Mtakatifu pale na Yohana naye anashangilia kwa kucheza akiwa huko tumboni kwa mama yake. Sasa nataka uone kitu ambacho mimi nakiona. Wakati Maria anaitwa AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote, kwa Yusufu ilikuwa sio Baraka ila ni balaa tupu. Kwa maana binti aliyemwamini kabisa sasa ni mjamzito katika mazingira ambayo hayaelewi, wala hajawahi kusikia kitu cha sampuli hii kimetokea wapi (all was new experience), hakuna mahali pa kurejea (reference) na wala hakuna mtu anaweza kumshauri kwa maana katika ELIMU ya dunia wakati huo hakuna mahali kitu kama hicho kimeandikwa/kimetokea. Watu hawajui nini kinaendelea. [Angalizo: Sio kila jambo kwenye ndoa/uhusiano wako utapata mjuzi wa kukusaidia, jifunze kujipanga na Mungu kwa mambo ya ndoa yako]

Katika hali hii ya GIZA, Yusufu akaamua KUMWACHA Maria kwa siri! Hii ni hali ya kuchanganyikiwa ambayo wengi wanafika katika mazingira magumu katika mahusiano yao. Ghafla tu unaona hiki “kitu” ni kigumu na unaona hakuna njia tena na unajiambia “basi bwana kama ndio hivi basi mimi naacha” au “mimi nimefanya sehemu yangu ila mwenzangu amenisaliti, naachia ngazi”, au “kwani mimi ndio wa kwanza kuachika”, “kwa vile ameenda kupata mimba huko basi na mimi sioni tena haja ya kujitunza”, “kwanza nina kazi yangu na simtegemei, potelea mbali maisha yataendelea”, nk. Ni hali ya kukata tamaa. Hiki ni kipindi cha giza. Na mwili unataka kuleta majibu ya haraka (instant solutions), kukimbia na kupotelea mbali. Lakini Malaika anakuja kusema na Yusufu na kuugeuza Moyo wake. Sijui kama Yusufu alikuwa mwombaji ila tunaambiwa Mungu alisema naye, akasikia na KURUDISHA moyo nyuma. Usipo jifunza kukaa katika MAOMBI ni vigumu kuvuka hii ngazi. Hapa ni kipindi cha KUNGOJA maana unajisikia huku ndani kwamba BADO hujapata/hujafika mahali unataka. Kumbuka “wamngojao Bwana watapata NGUVU mpya”. Unahitaji Nguvu mpya kila siku kuvuka hapa. Utagundua ule “upendo wa zamani umepoa”, sasa unahitaji NGUVU mpya. Muombe Mungu akupe nguvu mpya.

ii. Kutembea katika Baraka

Mara nyingi watu wamefikiria Baraka za Mungu kwa upande mmoja tu wa kuwa na hela, majumba, magari au kufanikiwa katika mambo ya mwilini na kusahau upande mwingine. Utasikia watu wanasema “count your blessings” (“hesabu Baraka zako”). Sasa unajua huwezi kuhesabu KITU ambacho hukijui na wala hukioni. Nakwambia Leo kuna Baraka nyingi sana Mungu anatubariki na hatuwezi kuziona wala kuzihesabu kwa maana ziko kwa jinsi ya ROHONI na kwa sababu huzioni hujui kwamba UMEBARIKIWA na unabaki ukilalamika na kunung’unika kwa sababu ulishamwekea Mungu vigezo na vitu fulani kwamba “hiki kisipotokea basi sijabarikiwa bado”. Kama mambo yako “hivi” basi bado hakijaeleweka, nk. Maria alichukuwa tu kama Malaika alivyosema na “akayatia moyoni mwake” huku akijua kwamba AMEBARIKIWA kuliko wanawake wote. Kwanini aliweka moyoni mwake? Kwa maana hakuna mtu wa kawaida anaweza kuelewa hii lugha ya kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Akajua ni Mungu na hakuna haja ya kutoa maelezo ya ziada au kuuliza watu au kupeleka umbea. Akakaa mimya.

Hebu mfikirie Yusufu. Wakati anajua kabisa hii mimba sio yangu ila anamhudumia Maria. Wanaenda huko mbali mji mwingine kuhesabiwa na mama hajiwezi mimba ni kubwa. Yamkini huko njiani Yusufu alitembea kwa mguu wakati mkewe mjamzito yuko juu ya punda na yeye anakokota huku mbele, ila mimba sio yake! Yule mama anajifungua hapo, Yusufu anamsaidia, ila mimba sio yake! Ni mambo magumu kuelewa ila Yusufu alikaza USO kufanya MAPENZI ya Mungu kama Malaika alivyosema. Hapo hampendezi Maria, ila Mungu, kwa maana yeye alichagua kitu cha kumfanyia Maria tayari, yaani KUMWACHA kwa SIRI! Sasa huu mpango wa kubaki ni mpango mpya ambao anaambiwa na Malaika na anaamua kuutimiza mpango huu japo haelewi vizuri. Mimba sio yake! Na sio hivyo tu, hajawahi kumgusa kabisa huyu mama! Analea mimba miezi 9, akijua kabisa sio yeye!

Kumbuka sio kila kitu Mungu atafanya juu ya maisha yako UTAELEWA. Baraka nyingi sana tunapata sio BINAFSI. Mungu amelenga KUWABARIKI wengi kupitia BARAKA alizokupa. Katika kubariki wengi LAZIMA kuna UDHIA. Ndio maana Yesu alisema “hakuna mtu aliyeacha ndugu, wazazi, shamba, nk. na kumfuata asipate hivyo “vitu” mara 100 hapa duniani ila na UDHIA pia”. Watu wengi sana wanapenda BARAKA ila BINAFSI, wanasahau kwamba Mungu akishusha Baraka mara nyingi sana hulenga wengi sana kwa Baraka hiyo hiyo, na imekuwa udhia. Kwa maana sio UPENDAVYO wewe ila sasa ni kama WAPENDAVYO wengine pia kupitia Baraka hiyo hiyo. Hebu fikiri wewe ni Maria (mama wa Yesu), unaitwa MBARIKIWA kuliko wanawake wote, ila kijana hakai nyumbani, anapita mitaani KUHUBIRI vitu hata huelewi, ukimuuliza anasema anafanya MAPENZI ya Baba yake! Huku Yusufu naye haelewi pia. Ghafla! Watu wanajaa kila mahali hata hakuna muda wa kula na kuongea kama familia! Huwezi tena kusema huyu ni MWANANGU kwa maana hata yeye anasema “hawa wa hekaluni ndio mama na ndugu zangu”. Kijana anasema lugha ngumu-ngumu tu kila saa! Huku mtaani wanasema kachanganyikiwa (karukwa na akili) na wengine wanasema kijana ana pepo! Hebu fikiri hii ndio ile kitu Mungu anasema ni BARAKA!

iii. Machozi kwenye Baraka Yako

Bila shaka Maria na Yusufu walikuwa na vipindi vigumu na Yesu, japo waliitwa WABARIKIWA. Ghafla wanaambiwa wahame nchi kwa maana Herode anataka kumuua mtoto! Wanakimbilia Misri, sijui walikuwa na usafiri gani ila najua haikuwa rahisi. Hebu fikiri ghafla! unajikuta unaanza kupiga mahesabu ya kuacha kazi yako kama Yusufu kwa sababu ya hii BARAKA iliyokuja kwenye familia. Hebu fikiri wale wateja wake ambao alikuwa anawatengenezea furniture, anawaagaje? Hebu fikiri wale ndugu zake sasa hapo mtaani anawaagaje? Eti, anahama nchi! Maana sio tu hawamwelewi, ila wanamwona kachanganyikiwa pia. Hii ni BARAKA imeingia katika familia na watu wanaanza kuhangaika. Sasa ukifika mahali pa kukata tamaa jua UNAHARIBU ile Baraka ya Mungu kwa maana sasa inakuja kwa MTINDO ambao haujautarajia. Nakwambia kila mtu atakuelewa ukiamua kuitupilia mbali hiyo BARAKA isipokuwa Mungu. Lakini nakwambia ni aheri KILA mtu asikuelewe ila Mungu akuelewe inapofika kufanya MAPENZI yake.

Ndoa nyingi sana ni BARAKA katika maisha ya watu na pia Mungu amelenga hizi ndoa ziweze kuwa BARAKA kwa watu wengine. Utakuta hapo katikati kumetokea MAMBO magumu na watu wamesamabaratika na KUTOKA nje ya kusudi la Mungu. Sawa watu watakuelewe kwa maana kwa kweli “huyu jamaa” amekuwa kama kichaa kabisa, ila kusudi la Mungu ni nini? Nakwambia kuna BARAKA ambayo Mungu alitarajia watu wengine waipate kupitia NDOA yako ila sasa Ibilisi ameisambaratisha na amefuta BARAKA kubwa ambayo wengi wangeipata kupitia NDOA yako! Sio kila KUACHANA ni suluhisho hata kama mazingira yote ya KISHERIA na KIJAMII yamekaa sawasawa na kila mtu anakuunga mkono. Kumbuka Yusufu angeweza kumwacha Maria mapema tu akiwa kama mtu wa HAKI, ila alikaza uso kutimiza Mapenzi ya Mungu. Je! Unajua mapenzi ya Mungu kwa NDOA yako? Je! Kila mmoja anajua WITO wake na mlichoitiwa kufanya shambani mwa Bwana? LAZIMA kipo. Hebu fikiri hii MISUKOSUKO yote ya NDOA ya Yusufu na Maria halafu hawajui WITO wao ingekuaje? Mkijua kila mmoja alichoitiwa mtapona kwa urahisi zaidi katika VITA vya adui.

iv. Mahali pa Ushindi

Wakati Maria na Yusufu wanapita nyakati mbalimbali ngumu na BARAKA ya mtoto Yesu, inafika takriban miaka 30 ambapo sasa KIJANA anakomaa kuwa mtu mzima. Mara kijana anakuja na agenda za KUFA kwa ajili ya ULIMWENGU! Maria haelewi wakati kijana anasema “mkila mwili wangu na kunywa damu yangu mnauzima wa milele”! Pamoja na kupita hivi vipindi vizito sasa kijana anataka KUFA! Eti yeye ni kondoo wa SADAKA. Matarajio ya Maria alijua siku moja yeye atakuwa mama wa MFALME, mtu tajiri mtaani na watu wote, wakubwa kwa wadogo wanamwamkia na kumheshimu. Maria anapiga picha ya KIONGOZI mkubwa kwa jinsi ya mwili lakini KIJANA anakuja na AGENDA za kusulubiwa sasa. Yamkini nguvu ya kushinda mambo yote magumu ilikuwa kwenye matumaini kwamba SIKU MOJA huyu kijana atakuwa mfalme kwenye kiti cha Mfalme Daudi na hapa nitapumzika. Mambo yanakuja kinyume na matarajio yake japo anajua kuwa AMEBARIKIWA. Huyu mama anafuata kila hatua, anaona kijana anakamatwa, anapelekwa Golgotha kusulubiwa kama MHALIFU. Hebu fikiri hapo. Mama anamjua mwanae vizuri sana. Anajua ni mcha Mungu leo ghafla tu anasingiziwa vitu VIGUMU na sasa wamempiga vibaya damu inatiririka kila mahali na wanampeleka kumgongomelea MASALABANI. Mama analia Yesu anasema “USINILILIE mama, jililieni wenyewe!” Yesu alijua ili hii BARAKA ikamilike ni LAZIMA asulubiwe kwa maana yeye ni “Mwana-kondoo wa Mungu achukuaye dhambi za ulimwengu”. Hii ni Baraka kubwa ila haijakaa kwa namna watu wengi wataiona kama Baraka! Wengi wangelalamika na kuona ni BALAA kubwa kwenye familia! Kama unatarajia UZIMA wa Milele jifunze kusoma LUGHA za rohoni katika Baraka zako kwa maana nyingine zinakuja kwa mtindo ambao unaweza kukemea ukidhani ni Ibilisi au jaribu. (Luka 23)

Lengo la somo hili ni kutaka kukufungua macho juu ya mambo ambayo Mungu anafanya katika maisha yetu na tukumbuke kumshukuru hata kama hatuelewi kila kitu kwa maana “Mungu amekusudia mambo mema kwa ajili ya watoto wake kila siku”. Angalia usibebe roho ya KISASI kwa mambo yatakayokukuta katika MAHUSIANO kwa maana KILA uhusiano/ndoa itapita katika VIPINDI vigumu na vyepesi, vipindi vya huzuni na furaha, vicheko na vilio, nk. Angalia sana katika VIPINDI hivi usimkosee Mungu kwa sababu tu HUELEWEI mwenzako anafanya nini. Yamkini ameamua kukusaliti na wanawake/wanaume wengine na umejua. Kwa maana kama wewe ni mtu wa Mungu “hutakosa kuzijua HILA za Ibilisi na Mungu hatawaficha watu wake jambo”, na umefika mahali UMEJUA. Chunga USIMKOSEE Mungu kwa sababu mwenzako amemkosea Mungu. Uhusiano/NDOA ina mwisho ila uhusiano wako na Mungu hauna mwisho. Ukijua kwamba MATESO yako ni ya KITAMBO tu, usikubali KUPOTEZA hatma yako (mambo ya milele) kwa sababu ya mambo ya kitambo tu. Kaza uso wako kwa Mungu na kaa katika KUSUDI lake na WITO ulioitiwa ili ile BARAKA Mungu aliyoweka katika maisha yako ISIPOTELEE njiani. Tafakari yaliyo juu aliko Kristo kwa maana huku Duniani kuna ufisadi mwingi. Angalia MWISHO wa safari yako na ujitie moyo katika Bwana. Mambo yanayotokea kwenye uhusiano wako yasiujaze moyo wako hata ukakosa shukrani kwa Mungu wako.

Neema na Rehema zitokazo juu ziwahifadhi NIA zetu tangu sasa na hata milele. Bwana yu karibu.

Frank Philip.

Monday, December 23, 2013

KIBARAKA wa MWENYE NGUVU!!!


Kibaraka ni mtu anayefanya kazi kwa kutaka kumpendeza BWANA wake au mtu mwingine MWENYE NGUVU. Kibaraka haishi kwa matakwa yake ila ya MWENYE NGUVU.

Kibaraka anasifa nyingi za kuvutia. Nataja chache: Kibaraka hua na nguvu nyingi bila kuhesabu gharama ya kile afanyacho alimradi bwana wake ameridhika. Mara nyingi kibaraka halalamiki anapotumikishwa, na hata akilalamika bado huendelea kumtumikia bwana wake tu. Kibaraka haangalii muda, mahali wala kuwaza sana juu ya matokeo ya matendo yake japo mara nyingine hapendi afanyacho. Kwa sababu hii ya “ku-take risk” vibaraka hufanikiwa saana katika wayatendayo japo ni kwa ajili ya kumpendeza MWENYE NGUVU na sio Mungu!

Kuna sifa mbaya kadhaa za kibaraka. Nitazitaja chache. Kibaraka hua katika hali ya UHITAJI na KUPUNGUKIWA kila siku. Siku zote ni dhaifu kwa MWENYE NGUVU! Sifa nyingine mbaya zaidi inayomfanya kibaraka azidi kua kibaraka ni ile hali ya ‘kutojua kua yeye ni kibaraka’ na akiambiwa hukasirika na kubisha kwa nguvu!

Katika organizational structure ya Mungu, MUNGU yuko pale juu, punde kidogo akamweka mwanadamu na kisha malaika watakatifu. Kumbuka Shetani na mapepo yote yalikua katika ngazi ya malaika kabla ya kuasi. Hii inamaana Mwanadamu yuko juu ya shetani na mapepeo yote na juu ya malaika pia! Shetani na mapepo yote yatazidi kua CHINI yako daima kama unaishi maisha MATAKATIFU na kumtii Mungu.

Nitatoa mfano. Kila mtu, mvulana au msichana, anakua na nguvu kubwa ya kupambana na ‘uzinzi’ na kuupinga hata kama “hajaokoka”. Asili ya hiyo nguvu sio jina la Yesu, kwa maana hata hajui kuomba na wala sio Mkristo, ila asili ya nguvu hiyo ni ile ngazi ya juu Mungu aliyomweka katika ulimwengu wa roho kuliko mapepo. Siku anajaribiwa na “tamaa zake” na kufungulia ‘uzinzi’, kuna package ya mapepo yanahusika hapo na yanamfanya sasa kua KIBARAKA wa ngono! Anakua dhaifu wa ngono na anaanza sasa kutenda kwa mfano wa KIBARAKA na mapepo ya ngono yakiwa kama MWENYE NGUVU! Ushindi wa mtu huyu dhidi ya ngono sio natural na automatic tena, sasa atatumia jina la Yesu, tena kwa nguvu na kupambana na MWENYE NGUVU kwa maana mwenye nguvu ameshaingia ndani, sharti “umfunge kwanza ndio uweze kuchukua/kutawala vilivyo vyako” la sivyo utabaki kua kibaraka na utatumikishwa kweli hadi mauti. (Warumi 7)

Umewahi kufikiri gharama ambayo KIBARAKA anaweka katika salon, mavazi, viatu, vipodozi, simu na mawasiliano, gym, nk. Kwa lengo tu la kukaa katika “mkao fulani” ili kumpendezesha MWENYE NGUVU wake? Nakwambia kwenda fellowship na bible study ni bure ila KIBARAKA hataenda huko maana ‘anaswagwa’ kama ng’ombe na mwenye nguvu [“asije akasikia Neno akapona/akaokoka”], atapata muda na hela ya kulipa gym, eti ana-keep shape na tumbo lake liwe dogo! Au anajenga kifua na mkono kwa maana wadada wanapenda hiyo! [Sasa biblia inasema “mazoezi ya mwili yafaa, ila utaua wafaa zaidi”] Shida sio mazoezi, vipodozi wala jitihada zingine, shida iko katika chanzo na sababu na makusudi ya kufanya “hivyo vitu” ndio inayopima kwamba ufanyacho ni dhambi au la!, the motive behind! Je! Kuna mwenye NGUVU anakusukuma katika jitihada zako ziwazo zote? Je! Wewe ni kibaraka wa mwenye nguvu katika maeneo mbalimbali? Tafuta UKOMBOZI WA DAMU YA YESU nawe utakua huru..
Warumi 7: 14 “Tunafahamu kwamba sheria ni ya kiroho. Lakini mimi si wa kiroho; mimi nimeuzwa utumwani, ni mtumwa wa dhambi. 15. Sielewi nitendalo: kwa maana lile ninalotaka kulifanya, sifanyi; badala yake, ninafanya lile ambalo nachukia kulifanya. 16 Kwa hiyo kama ninafanya lile nisilopenda kufanya, hii ina maana kwamba nakubali kuwa sheria ni njema. 17 Basi, kwa kweli si mimi hasa nitendaye lile nisilolipenda bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.18 Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna wema wo wote ndani yangu mimi, yaani katika mwili wangu wa asili. Ingawa nina nia ya kutenda lililo jema, lakini ninashindwa kulitenda. 19 Sitendi lile jema nipendalo bali lile ovu nisilopenda, ndilo nitendalo. 20 Basi kama ninafanya lile nisilopenda kufanya, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. 21 Kwa hiyo imekuwa kama ni sheria: kila ninapotaka kufanya jambo jema, jambo ovu hujitokeza. 22 Kwa maana ndani yangu ninaifurahia sheria ya Mungu. 23 Lakini ninaona kuna sheria nyin gine mwilini mwangu inayopingana na ile sheria ninayoikubali akilini mwangu. Sheria hii inanifanya kuwa mateka wa sheria ya dhambi ambayo inafanya kazi mwilini mwangu. 24 Ole wangu, mimi mnyonge! Ni nani atakayeniokoa na huu mwili wa kifo? 25 Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa hiyo basi, mimi kwa moyo wangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu wa asili ninaitumikia sheria ya dhambi.”

Frank Philip.

KILIO CHA MWENYE HAKI!!!



Leo nataka niseme juu ya KILIO. Kuna tofauti ya kulia kwa machozi ya nje na kulia kwa machozi ya ndani. Mtu anapotendewa kitu na ndani yake akasikia KUNYANYASIKA na akasikia uchungu sana, mara nyingi anatoa machozi ya nje (atalia). Lakini sio kila mara mtu atalia kwa machozi, ila kuna ule UCHUNGU wa ndani ambao watu mbalimbali wamekua nao na wameenda mbele za Mungu kwa maombi au hata wametamka tu maneno na Mungu AMESIKIA (“nipo pamoja nanyi katika mipango yenu, kabla ya kuomba mimi Bwana nitasikia na mkiwa katika kunena mimi Bwana nitajibu”). Chunga hii kitu, Mungu anasikia KILIO kuliko unavyodhani. Na mara nyingi sana hiki KILIO hata kama mtu sio mlokole nakwambia UKIMDHULUMU, UKIMNYANYASA, UKIMTENDA JEURI mtu na akalia kwa UCHUNGU mbele za Mungu hata kama hakumwambia mtu au hata kama hajui kama Mungu anasika, nakwambia Mungu husikia VILIO.

Wakati Mungu anamtokea Musa na anamtuma Misri kuwakomboa wana wa Israel kutoka UTUMWANI, Mungu alisema “nimesikia kilio chao nami nimeshuka kuwakomboa”. Mungu hakusikia maombi bali KILIO! Sasa ninataka uone huu mfumo vizuri. Pale Misri wana wa Israel walikua watumwa, na juu yao kulikua na VIONGOZI na WASIMAMIZI na kule juu kabisa alikuwepo Mfalme Farao. Kiutawala hawa watumwa walikua chini kabisa, ila walikua WANA wa MUNGU aliye hai. Kumbuka “hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu na ile iliyopo imeamriwa na Mungu”. Kwa lugha ya kawaida BOSS mkubwa sana katika “utawala wowote” hapa duniani ni Mungu. Sasa kama mtu mwenye HAKI, amefika mahali pa gumu sana na amelia kwa MATESO mbalimbali, akiwa hajui huu mfumo bado BOSS mkubwa hushuka hapo na kurekebisha mambo, haleluya! Kwa wale wanajua hii SIRI na kusimama katika nafasi na zamu zao vizuri, HAWATAMSUJUDU boss wao wa duniani na kufanya NGONO, nk., na kumkosea Mungu kwa sababu ya kulinda MASLAHI yao ya kikazi. Watapambana kwa “NIA ya kushinda UOVU na KUTII kwao kutakapotimia MAMLAKA yao katika ulimwengu wa roho dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wa baya ITAONGEZEKA sana”. Na KILIO chao Mungu atasikia na ATASHUKA kuwaokoa. Kumbuka, Mungu ndio boss mkubwa pale juu ila maandiko yanatuonya TUTII mamlaka iliyo kuu. Na usithubutu kumwambia kiongozi wako kuwa wewe sio boss ila boss ni Mungu. Jua hilo moyoni na mtizame Mungu kama Mkuu wako wa kazi na chapa kazi kwa moyo, acha uvivu.

Nebkadneza mfalme wa Babeli alikwenda kula majani miaka/misimu 7 kwa kosa la kujisifia kwamba “huu mji ni mkono wangu umejenga?” Akatizama mafanikio ya Ufalme (kampuni yake) akajiinua ndani ya moyo wake! Mungu akasema sasa utajua kwamba mimi natawala pamoja na wanadamu, sio wewe Nebkadneza, ni Mimi! Hii siri watu “wachache” wanaijua na wamehusika kuwapiga “transfer” (uhamisho) mabosi wao kwa sabababu wameleta shida kwenye KAMPUNI na jina la Mungu linatukanwa au watu wamenyanyaswa. Transfer inaweza kuwa kulala, kushushwa cheo (kula majani), kuhama kituo cha kazi, nk. Ila vita vyetu sio juu ya DAMU na NYAMA. Ni katika roho, na tunapata NGUVU tukiwa na NIA thabiti ya kupinga UOVU wote na KUTII kwetu kutakapotimilika (2Kor. 10:4-6). CHUNGA sana usije ukafanya mambo kwa HUSUDA, WIVU au MASHINDANO, utashindwa. Mamlaka ya Mungu haifanyi kazi hapo. LAZIMA usimame katika KWELI na HAKI na sio maslahi binafsi. Usikubali kumkosea Mungu kwa kisingizio eti “sasa huyu ni MHESHIMIWA na mimi ningefanya je?”, mwite Yesu hapo akuokoe na KILA (hata kama sio mlokole) atakayeliitia jina la BWANA ataokoka katika hali anayopitia. NEEMA ya BWANA izidi KWENU. AMEN

Frank Philip.

Sunday, December 22, 2013

KAMA UNATAKA MUNGU AONEKANE NA WATU JIFUNZE HII SIRI



Kipimo cha UDHIHIRISHO (MANIFESTATION) wa Mungu kwenye HADHIRA (PUBLIC) ni MUDA, BIDII na HALI ya MOYO wako UKIJIHUDHURISHA mbele Zake mkiwa wenyewe wewe na Mungu pekeyenu (SIRINI).

Kama UKIJIHUDHURISHA mbele za Mungu wako kwa BIDII na kwa UELEKEVU mahali pa SIRI, basi Mungu ATAJIDHIHIRISHA mbele ya WATU hadharani.

Ukitaka Mungu aji-present kwa watu basi jifunze kuji-present kwa Mungu.

Ni aheri ukose MUDA wa kuandaa PRESENTATION kwa watu na sio MUDA wa kuji-present kwa Mungu, kwa maana unaweza ku-present kitu chochote mbele za watu ILA HUWEZI kum-present Mungu! Ndio maana kazi ya Mitume ilikua KUHUBIRI na KAZI ya Mungu likua KULITHIBITISHA hilo Neno kwa ISHARA na MAAJABU.

Kazi ya Musa ilikua kuji-present kwa Mungu na kupata maelekezo na KAZI ya Mungu ilikua KUTENDA miujiza (kuji-present) mbele za Farao!

Frank Philip.

Wednesday, December 18, 2013

(MAOMBI YENYE NGUVU).....SEHEMU ya II


Katika maisha yetu ya kila siku tumetamani MAMBO mengi mbalimbali yatokee. Mengi ya haya MAMBO yako nje ya uwezo wetu na IMETUPASA kuhitaji msaada wa Mungu au watu wengine. Mara nyingi utagundua ni vigumu sana KUTEGEMEA misaada ya watu KUTIMIZA mahitaji yetu ya kila siku. Njia rahisi ni kujua jinsi ya kujipanga vizuri na Baba yako wa Mbinguni na kwa kupitia Yeye, anaweza kuinua watu mbalimbali kuja kuingilia kati hali unazopitia na kukusaidia. Ikishindikana kabisa, Mungu anaweza kuinua kunguru, mawe au Malaika kuja kukupigania, na hii imetokea kwa wengi hata kwako pia inawezekana.

Kusudi la somo hili fupi ni kutaka kuhusianisha USHINDI wako na (i) NAFASI yako katika Kristo na KUZAA kwako MATUNDA, na (ii). KIWANGO chako cha MAOMBI na pia ujue (iii). VIKWAZO vya Majibu ya maombi yako, (iv). Kutofautisha imani ya KUOMBA na KUPOKEA, na (v). Ujue jinsi ya KUJITEGEMEA kimaombi.

i. NAFASI yako katika Kristo
Mambo kadhaa ni ya LAZIMA: (a) kukaa ndani ya Yesu, (b). Neno kukaa ndani yako, na (c). Omba lolote utapewa. Yesu alitufananisha na yeye akiwa mzabibu, akasema“ sisi ni matawi ya mzabibu na yeye ni Mzabibu. pasipo yeye sisi hatuwezi jambo lolote”. Pamoja na kwamba Yesu alikuwa anazungumzia KUZAA matunda, utagundua pia mistari iliyofuata alisema juu ya MAOMBI. Kwa upande mwingine kuna uhusianao kati ya KUZAA matunda na KUJIBIWA maombi yako. (Yohana 15:1-6).

ii. KIWANGO cha maombi
Yesu alipowatuma wanafunzi wake kwenye HUDUMA mambo mengine yalikuwa magumu, japo wametumwa na Bwana! Walipomuuliza kwanini mambo mengine yanagoma? Yesu alijibu “mambo mengine hayawezekani bila KUFUNGA na KUOMBA”. Hapa tunapata picha kwamba kuna kiwango fulani cha maombi kinaweza kukuvusha hadi hatua fulani. Ukifikia hiyo hatua inahitaji GIA nyingine ya maombi ya kiwango cha juu zaidi ili uvuke kwenda kwenye hatua ya juu zaidi.

Pamoja na BIDII (diligence) na KUDUMU (persistance), haya mambo mawili ni ya muhimu sana KUPIMA kiwango cha USHINDI wako katika yale unayoyaombea. Kuna wakati itakupasa kuongeza NGUVU/KIASI cha kuomba ili kuvuka mahali ulipo. Hata kama wewe ni TAWI na UKO ndani ya Yesu vizuri na Neno (imani) limejaa ndani. (Luka 18)

iii. VIKWAZO vya MAJIBU ya Maombi yako
Kuna uhusiano mkubwa sana wa KUPOKEA majibu ya MAOMBI na HALI ya MUOMBAJI mwenyewe pamoja na KUTIMIZA viwango vingine kama (i) na (ii) hapo juu. Kila mtu anajua kwamba tukiomba sio mara zote mambo hutokea wakati huo-huo. Kuna kipindi cha KUSUBIRI na wakati mwingine kinakuwa kirefu. Ili uweze KUPOKEA majibu yako angalia usikate tamaa kwa maana “Mtavuna kwa wakati msipozimia roho.” Huhitaji IMANI kubwa kupokea MAJIBU ya Maombi yako. “Imani kidogo sana kama chembe ya haradali tu, inaweza kuhamisha milima na kufanya mambo makubwa sana maishani mwako ila usipokuwa na SHAKA juu ya yale mambo uombayo”. MASHAKA ni KIKWAZO kikubwa cha kupokea uombayo hata kama una IMANI. Kwa lugha nyepesi, mashaka ni sumu ya IMANI yako. Adui anajua ukiomba kwa imani utapokea, sasa akishindwa kukuzuia usiombe, basi ataleta MASHAKA katika yale uyaombayo ili USIPOKEE. Ukiwa makini utamsikia katika “mawazo yako” akikukukatisha tamaa na saa nyingine akikuzomea kabisa. Pambana na hayo mawazo maana ni vita inayoweza kuathiri IMANI yako na majibu ya maombi yako. (2 Wakorinto 10:1-6)

iv. JUA kutofautisha IMANI ya KUOMBA na IMANI ya KUPOKEA
Watu wengi sana wana IMANI ya KUOMBA ila wachache wana IMANI ya KUPOKEA. Ukiwauliza watu juu ya maombi kwa kweli watakuambia Mungu anajibu ila ukichunguza WANACHOONA ndani ya MIOYO yao ni KUSHINDWA zaidi kuliko KUSHINDA. Matokeo yake hawawezi KUPOKEA majibu kwa maana hawana IMANI ya KUPOKELEA.

Nitakupa mfano. Pamoja na kwamba Yesu ni mponyaji na Muumbaji wa Ulimwengu, utasikia mahali anasema “imani yako imekuponya”. Ina maana imani ya KUPOKEA ni ya MPOKEAJI na sio imani ya Yesu japo kuna mahali ALIWAHURUMIA tu watu akafanya mambo kabla hata hajaombwa na mtu (Luka 7:12,13). Kati ya maeneo ambayo Yesu hakufanya miujiza ni kule mitaa ya nyumbani kwao, SABABU sio uhaba wa IMANI ya Yesu ila IMANI ya WAPOKEAJI haikwepo. Yesu hakufanya kitu japo wengi walikuwa na shida zao nyingi na aliwahurumia! Ndipo akasema “nabii hakubaliki kwa watu wake.”

v. EPUKA MAOMBI TEGEMEZI
Kuna kundi la watu wamefanya baadhi ya watumishi kama TIKETI ya kupokelea majibu ya MAOMBI yao. Sawa, kuna kiwango cha NEEMA juu ya watumishi wa Mungu kinachoweza kukuvusha mahali, lakini nakwambia kuna wakati hata YESU “alipoitizama imani ya watu, ndipo alipotenda jambo” pengine aliacha kwa sababu ya KUTOKUAMINI kwao! UELEKEVU wa MOYO wako kwa Yesu utakusaidia sana katika KUPOKEA majibu ya maombi yako.


Sasa tunakumbushwa siku zote kuomba kwa imani na kuambiwa kwamba “kuomba kwake mwenye HAKI kwa faa sana akiomba kwa bidii”. Jifunze na uchukue MAZOEZI ya kutumia IMANI yako kwa maana imani ina tabia ya KUKUA au KUPUNGUA. Kumbuka KUKUZA imani ya KUPOKEA majibu ya maombi yako kwa maana hiyo ndiyo inayokwamisha wengi. Kumbuka adui mkubwa wa imani ya KUPOKEA anaitwa MASHAKA.

Dawa ya kupambana na MASHAKA ni kufanya MAZOEZI ya KUOMBA wewe mwenyewe na KUPUNGUZA utegemezi wa WATUMSHI wa Mungu. Sisemi ni vibaya kuombewa, ninachotaka kusisitiza ni wewe kujijengea UWEZO wa kusimama kwa MIGUU yako MIWILI kumwamini Mungu kwamba UNAWEZA kuomba na KUOPOKEA mwenyewe. Kumbuka wewe ni TAWI la Mzabibu na mtumishi pia ni tawi tu, anayejibu maombi ni MZABIBU (Yesu). Ukiweza kuepuka utegemezi kwa MATAWI mengine utagundua UMEVUKA hatua nyingine ya IMANI na KUMPENDEZA Mungu pia kwa sababu “haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani”. Wengi sana tunaweza kumshangaa Petro jinsi alivyoweza kutembea kidogo juu ya maji na ALIPOONA upepo, akazama! Hiyo ndio kazi ya MASHAKA. Nadhani kama Petro angefanya tena mazoezi kwa mara nyingine, angekuwa hahitaji tena Mtumbwi kwenda ng’ambo! Kwanini? Alikuwa na IMANI ya kutosha KUTEMBEA juu ya maji ila MASHAKA yalikuwa kikwazo.

Nitakupa mfano. Nguvu ya DAUDI na UJASIRI aliokuwa nao wakati anamkabili Goliath, haikuwa kwa sababu tu alijuwa uweza wa Jina la Bwana wa Majeshi, ila “kama alivyofanya MAZOEZI ya kupambana na DUBU na SIMBA”, alijuwa kwa jinsi ILE ILE, BWANA atampigania kwa Goliathi. Hakubakia tu KUAMINI moyoni, DAUDI alimtangazia Goliath (adui) kwa SAUTI ya juu, mambo aliyoamini. Mara nyingi sana wakati UNAOMBA, adui akileta SAUTI ndani yako za kukutia mashaka, kumbuka KUMTANGAZIA kwa SAUTI juu ya USHINDI wako. Kwa njia hii utaweza kushinda MASHAKA. Msomee adui Neno, mwambie “imeandikwa”, kisha taja Neno (imani) katika biblia unalosimamia katika hayo maombi.

Uzoefu wa kutumia IMANI yako unakupa nguvu ya kuvuka hatua nyingine ya KUPOKEA mambo uombayo katika kiwango cha juu zaidi. Ukiwa unamtegemea MTUMISHI fulani tu, MOYO wako unaanza kuwa dhaifu na unaona PASIPO kujua unahamisha UELEKEVU wako kutoka kwa Mungu na kuuweka kwa huyu MTUMISHI. Hali hii imekuwa mtego mkubwa kwa watu wengi sana, wamehamisha MACHO yao kwa YESU na wengine wamefikia mahali pa kuona MTU mwingine anahusika na matatizo yao ndio maana wakati ule dada zake Lazaro walimlaumu Yesu (mtumishi) kwa kusema “ungekuwepo hapa kaka yetu asingekufa”!

Mungu atusaidie kuongeza IMANI ya KUPOKEA majibu ya maombi yetu.

Frank Philip.

Saturday, December 14, 2013

SABABU za KUKESHA!!!


Bwana Yesu alizungumza kwa mifano mingi akisisitiza UMUHIMU wa watu wake KUKESHA. Maana halisi ya KUKESHA ni kuwa macho hasa wakati wa USIKU ambapo watu kwa kwaida hulala. Katika maisha yetu kuna VIPINDI vya mchana ambapo kuna mwanga na tunaona. Pia kuna vipindi vya USIKU, kuna GIZA na hatuoni kitu kwa sababu ya giza. Mara nyingi watu wanakuwa SALAMA katika VIPINDI vya giza kuliko vipindi vya MCHANA kwa sababu wanachukuwa TAHADHARI na kujilinda. Lakini pia MAANDALIZI na MAFANIKIO ya ULINZI wako yanafanyika wakati wa MCHANA.

Vipindi vya MCHANA vina sifa nyingi. Mojawapo ni MWANGA. Kwa sababu UNAONA vyema, basi unakuwa na AMANI na UHAKIKA kwa sababu unaona VITU kwa jinsi ya MWILINI. Sasa tukumbuke tumeumbwa ili KUISHI katika ULIMWENGU wa MWILI na ULIMWENGU wa ROHO. Katika vipindi hivi tunaambiwa “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.” (1 Thesalonike 5:1-7). Ukifuatilia mistari hii utagundua watu wa Mungu wameitwa ni wana wa MCHANA au wana wa NURU! Kwa lugha nyingine kundi la pili linaitwa WANA wa USIKU! Sasa, pamoja na kwamba mistari hii ilikuwa inakumbusha KURUDI kwa Yesu kulichukuwa Kanisa, nataka tujifunze hii TABIA ya Mungu ya KUKESHA.

Sehemu nyingine Mungu anajiita MLINZI wa Israel, Daudi alijuwa tabia ya Mungu ya KUKESHA na akasema “Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli.” (Zab. 121:1-4). Hii tabia ya KUKESHA ni ya MUHIMU pia kwa WANA wa NURU ndio maana Yesu amesisitiza sana “kukesha katika kuomba” na pia akasema “atarudi kama MWIVI ajavyo usiku” akitutaka tuwe MACHO wakati WOTE. Pamoja na GIZA la dunia hii, Bwana anasema “tusiwe kama wale wanawali wapumbavu, waliochukua taa zao bila MAFUTA”, huko usiku wakati watu wamelala, ghafla! Bwana Harusi anakuja!

Kuna sababu nyingi za KUKESHA. (i) Tuweze kushinda/kutokuanguka majaribuni. (ii) Tuwe salama adui anapokuja kushambulia. (iii) Kujua wakati wa KUJILIWA na Bwana. (iv) Tusibaki Yesu akija kuchukua Kanisa lake. Sifa za WAKESHAJI utaziona hapa, “Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; Mishale yao ni mikali, na pinde zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli;” (Isaya 5:27,28). Nitazungumzia zaidi KUJILIWA. Yesu alipoutizama Yerusalemu alilia. Akasema “laiti ungejua yakupasayo amani”, Wakati Yesu (Baraka za Mungu) zinakuja, Israel hawakujua na kupokea kwa shukurani, na pia wakati ADUI anakuja kuharibu, hawakuwa na HABARI! Akalia. Maisha yetu tumejisahau sana na kuona tu mambo yataenda kama JANA! Tumepoa au kupunguza ile kasi ya kumtafuta Mungu na tunaishi kama MUNGU hayupo! Taratibu tunapoteza NURU na kuanza kutembea GIZANI. Usipoangalia Ghafla! Uharibifu unakuja, kwa maana ADUI anakuwinda na anasubiri GIZA akushambulie! “Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.” (1 Thesalonike 5).

Sio kila mara ukiona MWANGA (NURU) kwenye ulimwengu wa MWILI pia unaona MWANGA kwenye Ulimwengu wa roho. Ngoja tujifunze kwa Ayubu. “Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. (Ayubu 1:9,10). Huu uliku wa ni wakati wa MCHANA (NURU) kwa Ayubu. Wakati Baraka ziko kila upande, mali, watoto, na mafanikio ya kila namna. Huku unaouna mkono wa Bwana (ukingo) unakupigania, nk. Ghafla! Giza nene linatanda! Sasa sio watu wengi sana wanapona hapa. ILA wale ambao WANAKESHA “watayaona mabaya yakija” (1 Thesalonike 5), na Mungu wao atawapa DAWA ya KUSHINDA. Kwa sababu wako NURUNI, MLANGO wa KUTOKA wakati wa KUJARIBIWA kwao watauona.

Mara nyingi sana watu katika maisha ya kawaida hawajali sana kwa sababu BANK kumenona, wanajua hata wakifukuzwa kazi LEO hawafi njaa. VITEGA uchumi vimesimama sawia. Karibia kila kitu kimekatiwa BIMA. Wanaweza kupata MATIBABU mahali popote duniani. Mambo ni SAFI, hata wakitafuta kwamba SHIDA inaweza kutokezea wapi hawaoni. Huwezi kuona UMUHIMU wa kukesha na KUDUMU kumtegemea Mungu kama huna macho ya rohoni na UELEKEVU kwa Bwana kama Ayubu. Lakini kwa wale ambao wamepitia majanga wanajua nasema nini. Kuna habari MBAYA hata sipendi kusikia licha ya kusimulia. Utakuta watu wameokoka tu vizuri, wamebarikiwa kuingia kwenye NDOA. Wanakuwa na mipango mingi ya maisha na KAZI/BIASHARA zao nzuri ziko sawa. Ghafla! Wasipotarajia, wameenda wote kazini na kabla ya jioni mmoja ametwaliwa! Ghafla tu! Status inabadilika, mmoja anaitwa mjane. Adui kashambulia. Wengine katika hali isiyotarajiwa, watoto wameenda shule, ghafla jioni hawarudi! Wanapata taarifa waende chumba cha kuhifadhia maiti kukagua! Hizi ni habari mbaya sana. Lakini haya ndio yalikuwa yanamtokea Ayubu wakati wa GIZA ulipoanza. Anajigundua hana WATOTO hata mmoja, wamekufa wote! Hana MALI halafu ni mgonjwa hajiwezi hapo chini. Mke wake naye analeta mambo magumu ya kumchanganya zaidi. Huu ni wakati wa GIZA.

Kusudi la somo hili ni kukumbusha habari ya KUKESHA. Katika kukesha kuna kujaa NGUVU na kujiandaa kupambana (Isaya 5). Nguvu za kukuwezesha kuvuka kwenye GIZA hupatikana wakati wa MCHANA. Maisha ya Ayubu kabla ya JARIBU ndio yalimwezesha KUSHINDA wakati wa jaribu. Watu wengi sana wanasubiri MAJANGA (GIZA) ndio wanaanza KUFUNGA na KUOMBA kwa BIDII na KUKEMEA kwa NGUVU. Sasa kweli wanakemea, ila nguvu iko wapi? “Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache.” (Mithali 24:10). “Wamtumainio Bwana ni kama MLIMA Sayuni, hawatatikisika kamwe” lakini pia Isaya anasema “bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.” (Isaya 40:31). KUSUBIRI kunahusianishwa na tabia ya KUKESHA.

Yesu anaposema “ni rahisi ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuingia Ufamle wa Mungu” aliona hii shida KUFANYA mapenzi ya Mungu wakati watu wamezungukwa na kila kitu. Ndio maana alipomuuliza yule kijana tajiri habari za AMRI za Mungu, na kijana anasema ameshika ZOTE, maandiko yanasema “Yesu akampenda”. Kwanini? Sio rahisi kukaa katika Amri za Mungu wakati HELA inapiga kelele. Ukifanikiwa kumpendeza Mungu wakati una KILA kitu lazima uwe KIVUTIO kwa Yesu. Sasa, Angalia maisha yako vizuri. Pale mahali ulikuwa una SHIDA, huna hela na hujui unavukaje, ULIMTAFUTA Mungu kwa BIDII na kukaa mbali na DHAMBI. Leo Mungu amekuvusha, umemaliza shule salama, umepata kazi, nafasi na pesa, Ghafla! Unaanza kuwaza KUTENDA dhambi! Ukiwa kwenye SHIDA kwako ilikuwa MCHANA, sasa Mungu amekubariki na baraka za Mungu badala ya kuongeza NURU, zimekuwa GIZA! Na chukizo kwa Mungu. Je! Unataka Mungu akurudishe kule kwenye DHIKI ili taa yako iwake? Wakati unadhani ni “amani amani” angalia uharibifu uko njiani. Neno hili linakukumbusha UAMKE na KUCHANGAMKA, rudi kwenye MKESHA na kuishi kwa KIASI, huku ukimsubiri Bwana. Kuna faida gani “kuupata ulimwengu wote na kupoteza nafsi yako?” Jijibu mwenyewe na uchukue HATUA. Mungu akusaidie.

Basi Mungu atuwezeshe kukaa katika KIASI na KUKESHA kwa Jina la Yesu. AMEN

Frank Philip.

Friday, December 13, 2013

KAZI YA UVUVI [UPDATED] !!!


Kazi ya UVUVI ni moja ya kazi ambazo zinahitaji uzoefu lakini pia Imani. Umewahi kujiuliza mvuvi anaposhusha nyavu zake huko chini kwenye maji ambapo haoni kitu ila anasubiri kwa IMANI akijua samaki wataingia?

Petro alipoambiwa anabadilishiwa kazi kutoka kuvua SAMAKI kwenda kuvua WATU ilikau inahitaji shule zaidi kidogo ili aelewe somo. Siku moja Petro akaenda kwa UZOEFU, kumbuka sio ZIWA/BAHARI au maeneo asiyoyajua, anajua sana na ana uzoefu nayo. Si akakesha sasa usiku kucha na hakupata kitu! Yesu akaja, akamwambia “Petro shusha nyavu” na akampa maelekezo ya ziada. Petro akajiuliza, “nimehangaika usiku kucha ila sikukamata kitu na sasa unasema nishushe nyavu?”, akapiga moyo konde na kusema, “kwa Neno lako nitashusha”. Hao samaki aliokamata hakuweza kuvuta nyavu maana ni wengi hadi nyavu kuchanika! Akasema “ondoka kwangu mimi mwenye dhambi”! Kwanini? [kufanya kazi ya Mungu bila mapenzi yake ni kosa na itakugharmu].


Sikiliza. Watumishi wengi sana wa Mungu wanahangaikal na KINA na UZOEFU wa nondo (mafundisho, nyenzo, nk.) wanazotumia na USTADI wa kupiga MAKASIA. Bila KUSUDI la Mungu utakesha hapo nakutahadharisha. Sio katika HUDUMA tu ila hata katika michakato ya maisha, biashara, nk. Hakikisha unashusha NYAVU mahali ambapo unajua YESU amekuongoza. Huwezi kosa SAMAKI asilani. Uzoefu wako na UJUAJI vitakuponza tafuta KUSUDI la Mungu katika maisha yako na utaona MATUNDA yakimimnika maishani mwako kama MVUA. Mafanikio ya Petro hayakutegemea KINA cha maji, AINA ya nyavu, MTUMBI, UREFU wa MUDA, wala UZOEFU wake! Ila NENO la Yesu! Ukipata Neno la wakati huo katika MUKTADHA (context) na MAUDHUI (content) na MUDA (timely), mafaniko yako katika HUDUMA, BIASHARA, KAZI, SHULE, nk., yatakua makubwa kuliko kujitahidi kwa NGUVU zako mwenyewe na AKILI zako. Jifunze kumshirikisha Yesu nawe utaona HATUA atakazokufikisha.

Kumbuka. Mungu hulituma Neno lake “kama mvua ishukavyo kutoka juu kuangukia ardhi”, na LITATIMIZA makusudi yake, halitarudi bure. Ukijua Yesu anasema nini juu ya UVUVI wako, sema kama Petro “kwa Neno lako nitashusha nyavu” halafu tukikutana utanipa ushuhuda. Barikiwa.

Frank Philip

Thursday, December 12, 2013

JUA NGUVU YA NIA YAKO!!!


Katika mambo ya muhimu sana kwa maisha ya IMANI, moja wapo ni kujua NIA yako katika mambo fulani ya kimwili na kiroho. Kwa lugha nyepesi ni muhimu kujua MOYO wako “unasema nini juu ya jambo fulani” (nimetumia KUSEMA kwa maana Moyo unatoa sauti ya yale uwazayo mbele za Mungu). Au kwa lugha nyingine ni vizuri kujua “MTIZAMO wako juu ya mambo fulani” (Kuna picha/kitu halisi kinajengwa ndani yako na mawazo yako na ndicho Mungu anachokiona).

Sababu ya msingi ya kujua NIA (makusudi ya Moyo) yako ni kupima kiwango cha MUNGU kuhusika na hayo mambo UWAZAYO/UNAYOHITAJI ambayo mengi yanapita MOYONI mwako kama MAWAZO tu. Majibu ya maombi yako hayaji kwa yale mambo ambayo ULIMI wako ulitamka wakati wa maombi, bali yale mambo ambayo NIA (makusudi ya moyo) yako imetamka wakati wa kuomba. Sasa unaweza ukafikiri nataka kusema nini hapa ila ukitafakari kwa makini utagundua kwamba “unaweza kuomba au kunena jambo tofauti na unavyo NIA ndani yako (unavyo sikia/ona hilo jambo NDANI yako)”. Sikia, “Kwa MOYO mtu huamini hata akapata HAKI”, ticket ya kupokea inaitwa IMANI, na hukaa moyoni. Moyo wako ukinena (NIA) kwa imani UNAPOKEA majibu ya maombi yako! “Kinywa kinapitisha tu yaujazayo moyo wako”!

NIA yako ikisema KITU tofauti na ULIMI wako unachokisema, katika kuchagua kati ya haya MAWILI, Mungu anasikiliza NIA (makusudi ya moyo) yako na sio ULIMI (mambo yatokeayo akilini mwako) wako! Ndio maana Suleiman alisema “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.” (Mithali 16:1). Haijalishi ULIMI wako umekiri sana mangapi, je! Nia yako imejipanga sawasawa na KUSUDI la Bwana? Ukitaka MAJIBU mazuri, maandalio ya MOY O ni wewe unafanya sio Mungu, JAWABU la ULIMI kwa uombapo ni kazi ya Mungu kujibu.

Kutokana na UMUHIMU wa NIA (makusudi ya moyo) ndani ya mtu ndio maana “Mungu anachunguza moyo na kujaribu viuno”. Na katika vitu 6, naam 7 achukiavyo Mungu mojawapo ni “moyo uwazao mabaya” (Mithali 6:18). Sasa sisi tunapambana na watu kwa MATENDO au MANENO yao lakini kwa MUNGU hata ULIMI usiposema, MOYO unasema na Mungu anasikia na KUONA. Yesu akasisitiza, “sio alacho mtu hunajisi ila kimtokacho”, kwa maana kinatoka ndani ya MOYO na NIA yako inasema moyo ULICHOKUSUDIA kufanya. Kabla dhambi haijafanyika kwa jinsi ya mwili, ilianza kufanyika ndani ya moyo wako kisha UNAITIMIZA kwa MAKUSUDI ya MOYO wako (NIA).

Jifunze kudhibiti NIA yako kwa sababu hapo ndipo penye NGUVU ya kushinda au kushindwa kwako. Kama unataka kufanikwa zingatia “kulinda sana moyo wako kuliko vyote ulindavyo”. Watu wengi sana wanasahau kwamba MAWAZO ya mioyo yao yanapiga KELELE kwa SAUTI japo ULIMI haujasema kitu! Kwa Mungu hayo mawazo yanapita kama PICHA/SANAMU ndio maana Mungu anasema “umechukua vinyago na kuvitia moyoni”, yaani kule ndani yako Mungu anaweza kuona OBJECTS au PICHA japo wewe UNAWAZA tu. Yesu akasema “amwangaliaye mwanamke kwa kumtamni MOYONI mwake amezini”, sasa kila mtu anajua tamaa ni kama WAZO tu ndani ya mtu ila Mungu akiangalia kama umefuga hayo mawazo, Yeye anaona KITENDO/SAUTI/PICHA/SANAMU! Ndio maana Mungu anasema “anachukia MOYO uwazayo mabaya” kwa sabubu kwake ni VITU HALISI kuliko sisi tunavyofikiri na mara nyingi tunapuuzia tu.

Mungu alipomtokea Sulemain na kumwambia aombe kitu chochote, NDANI ya Sulemani kulikuwa na MENGI ila aliomba KUSUDI la Mungu juu ya KAZI aliyoitwa kufanya ili AMPENDEZE Mungu. Jambo hili LIKAMPENDEZA Mungu. Nataka uone kitu cha tofauti hapa. Usije ukafikiri Sulemani alikuwa na AKILI sana ndio maana ALISEMA hivyo. KUMBUKA, ilikuwa ni NDOTO tu! (1 Wafalme 3:8). Kila mtu anajua kwamba tukilala hatutumii AKILI kama tukiwa macho, sasa Sulemani aliwezaje KUOMBA kitu sahihi kwenye NDOTO? Inamaana MOYO wa Suleiman ulikuwa UKITAMANI kumpendeza Mungu (alikuwa na NIA) ambayo Mungu alipomtembelea japo ULIMI wake haukunena, NIA iliyoko ndani yake ILINENA na Mungu akajibu.

Ukisoma sehemu nyingine Bwana anasema “niko pamoja nanyi katika mipango yenu, KABLA ya kuomba mimi Bwana nitajibu, na mkiwa katika KUNENA nitasikia”! Sasa watu watakubaliana na mimi kwamba kila mmoja wetu huwa ana mipango ndani ya MOYO. Ukiwa na NIA (makusudi ya moyo) safi mbele za Mungu, hiyo MIPANGO yako katika MAWAZO yako, Mungu anasema NINASIKIA! Kabla HUJAOMBA, Mungu anajibu! Ukisoma kitabu cha Ayubu utaelewa vizuri NGUVU ya mawazo yako. Tunaambiwa Ayubu “hakumwazia Mungu kwa upumbavu”. Hili ni jambo KUBWA na Ibilisi amelificha kwa watu wengi ukiangalia ndani yao ni MAWAZO machafu tu na kuwaza vitu vya AIBU na wao hawajui kwamba mambo mawili yanatokea: i. Moyo wako unakua chukizo kwa Bwana ii. Unadhoofisha kiwango cha kupokea majibu ya maombi yako kwa maana MOYO wako unanena tofauti na ULIMI wako. Umepoteza UELEKEVU! “Na macho ya Mungu yanakimbia-kimbia diniani kote, anatafuta huo uelekevu ndani yako ili ajionyeshe mwenye NGUVU”

Petro akasema “kwa hiyo VIFUNGENI VIUNO VYA NIA ZENU, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu” (1Petro1:12,13). Hapa napata picha kwamba tunaweza KUAMUA kushughulika na NIA zetu na kizidhibiti, ndio maana tunaambiwa TUZIFUNGE NIA zotu viuno na kua na kiasi!

Kuna maswali mengi huwa najiluza. Hivi Mungu akiniangalia huku ndani ANAONA nini? Watu wengi sana utawakuta wamepiga MAGOTI kwenye IBADA kanisani/sehemu mbalimbali, lakini ndani ya MIOYO yao kwa kweli WAMESIMAMA. Jiulize tu, kwamba kweli kuna UWIANO (synchronization) kati ya USEMAYO, UTENDAYO na UWAZAYO? Watu hawatuoni lakini nakwambia kuna watu MIOYO yao inavurumisha matusi kwa nguvu kama wafanyavyo wavuta bangi. Sawa, watu hawasikii lakini nakuhakikishia leo Mungu wako anasikia SAUTI! Basi AMUA leo, katika dunia hii iliyojaa UOVU na HARUFU ya UVUNDO inayopanda kwa Mungu kila siku, wewe uwe MANUKATO na KITU cha kupendeza Mungu anapo CHUNGUZA moyo wako. Jifunze KUMBARIKI MUNGU kwa MAWAZO ya MOYO wako. Ukifanikiwa hili Mungu atajibu HAJA ya MOYO wako kabla hujaomba kwa sababu NIA yako husema kwa SAUTI mbele za Mungu.

Ukitaka kujua UMEFANANAJE mbele za Mungu, angalia NAFSINI mwako, kile kitu unachokiona ndani yako NDIVYO ULIVYO mbele za Mungu, kwa maana imeandikwa "mtu aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo".

Roho Mtakatifu tusaidie. AMEN.

Frank Philip.

Monday, December 9, 2013

MAOMBI YENYE NGUVU!!!


Kama kuna kitu unahitaji kujua kama Mkiristo ni kuomba VIZURI. Wanafunzi wa Yesu walimwomba Bwana awafundishe kuomba kwa maana waliona wanafunzi wa Yohana wanavyoomba wakajua lazima kuna namna ya kuomba na sio kufurumuka tu na maneno bila utaratibu (Luka 11).

Kama kuna swali gumu nilikuwa najiuliza ni hili la kuomba kwa muda mrefu. Yesu anasema “KESHENI mkiomba msiingie majaribuni”, sehemu nyingine anauliza “hamkuweza kukesha nami hata saa moja tu?”. Katika Agano la Kale utaona neno “WALINZI” limetumika. Bwana anasema “Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha Bwana, msiwe na kimya” (Isaya 62:6). Sasa kwa WAOMBAJI watajua hii lugha ya “KUMKUMBUSHA” Bwana maana yake ni nini. Unapoomba sio kwamba Bwana hajui, unamkumbusha tu, ndio maana “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama itupasavyo”. Sio tu kwamba hatujui kuomba ila hata cha kuomba mara nyingi hatujui hadi Roho atusaidie. Kumbuka, unapoomba hutakiwi kukaa kimya hadi utakapoona majibu ya maombi yako. Hii TABIA ya KUDUMU/KUKESHA katika maombi imejirudia tena wakati Yesu anafundisha wanafunzi wake FAIDA za kuomba BILA KUKOMA. Yesu “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” (Luka 18:1-8). Nilinachotaka uone hapa ni aina ya UOMBAJI unaotakiwa na jinsi unapaswa kujipanga na kuwa na nguvu za kuomba kwa muda mrefu. Nitakupa moja ya SIRI muhimu za kukusadia kuwa na nguvu za kukusukuma angalau muda zaidi kidogo katika maombi.

Kuna mambo mawili nataka uone. La kwanza ni BIDII na la pili ni MUDA. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa BIDII. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa BIDII mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.”(Yakobo 5:15,16). Ukiona mtu “anajifanya” eti anatamka neno “moja tu” na mambo yanatokea, anataka kuonyesha kwamba yeye yuko juu sana na karibu sana na Mungu na miujiza ni kama tu switch ya umeme, ON/OFF matatizo kwisha! Huwa najiuliza swali hili, je! Huyu jamaa huwa anakesha na kuomba sana na sasa anamalizia tu kile alichokuwa ameomba/anomba kwa muda mrefu? Na kama sio mwombaji, je! Hii nguvu ya ON/OFF na huku ameshika kiuno imetoka wapi? Naishia hapo. Usifike mahali ukaona watumishi wa Mungu wanatumika kwa mtindo ambao hujawahi kuona ukakimbilia kusema ni PEPO. Utaingia kwenye matata MAKUBWA kama ni Mungu kweli anawatumia. Lakini pia UJUE sio kila atendaye MIUJIZA anatoka kwa Mungu.


Biblia inasema Eliya aliomba kwa BIDII! Sasa wewe unasema hapa ni kuamuru tu mambo kama ON/OFF na huna TABIA ya kukesha kwenye maombi! Kumbuka Yesu aliamuru mambo kwa mtindo huu, just ON/OFF mambo yanatokea, wanafunzi wake wakajitahidi kuiga, “IKAGOMA”! Wakamwendea wakamuuliza “mbona sisi inagoma?” Yesu akasema “mambo mengine hayawezekani ila kwa KUFUNGA na KUOMBA”. Tunasoma kwenye maandiko kwamba Yesu alikesha milimani akiomba na asubuhi anaingia hekaluni kuhudumu. Anasema “sifanyi kitu ambacho sikumwona Baba yangu akifanya!” Swali je! Aliona saa ngapi? Kama Yesu ALIFUNGA na KUOMBA, halafu wewe HUTAKI kujifunza tabia hii na unataka tu usimame kama “AFANDE” na kutoa tu ishara kwa mkono mambo yanatokea, watu wanarushwa huku na kule. Jua unakaribia MAHALI pa GUMU.

Hatua SABA za maombi zitakusaidia kuomba kwa MUDA mrefu. Kumbuka siku zote MAOMBI hayaendi bila NENO. Ukitaka kufanikiwa kuomba ni LAZIMA uwe msomaji wa NENO pia. Jipe angalau milango (chapters) 2 kwa siku. Asubuhi na jioni au muda wa kusubiri (ukiwa kwenye gari, bank, nk.) Hizi hatua SABA sio ubunifu wangu ila ni SALA ya BWANA.

Hatua ya kwanza: Liitie Jina la Bwana wa Majeshi.
Yesu alisema “mkiomba neno LOLOTE kwa Jina langu nitafanya”. Pamoja na kwamba Daudi alimkabili Goliath kwa kombeo, fimbo na jiwe, alitumia “Jina la Bwana”. Hiyo ndio siri ya ushindi wake. Sehemu nyingine Daudi akasema “hawa wanataja magari na farasi lakini mimi nitalitaja jina la Bwana Mungu wangu”. NGUVU zako za kuomba na MAFANIKIO ya uombayo yapo katika Jina la Yesu.

Sasa, unaposimama na kuanza “Baba yetu/yangu uliye Mbinguni. JINA lako LITUKUZWE”. Jiulize, litukuzwe na nani? Kama ni wewe basi anza kulitukuza jina la Bwana. Usikurupuke na kuanza tu kukemea pepo bila utaratibu hapo, No! Mtukuze Mungu kwanza. Kukemea ni hatua ya 6 huko mwisho wakati umeshajaa NGUVU. Yesu akasema “huwezi kuchukua vitu vya mwenye nguvu mpaka umemfunga kwanza”. Sasa unamfungaje mwenye nguvu wakati huna NGUVU?

Watu wanajiuliza sasa nitamtukuzaje Mungu? Sikiliza. Wana wa Israel walipovuka mto Yordani na maji yakatindika mbele yao, waliambiwa waokote mawe 12 hapo mtoni wayaweke iwe ukumbusho huko mbele kwamba “Mungu alifanya matendo makuu”. Mungu anapenda hiki kitu. Taja “matendo makuu ya Mungu” yoyote unayoyajua huko kwenye Biblia, mshangilie na kumshukuru kwa sababu ya UWEZA na NGUVU zake. Unavyozidi KUZAMA katika kutafakari na KUTAJA matendo makuu ya Mungu, taratibu utagundua kuna kitu kinatokea, unaanza kujaa CHARGE! Unavyozidi kutaja na kumtukuza Mungu, NGUVU inaongezeka na unaanza kuwa mwepesi ghafla. Hii hatua ukipita vizuri, inakupa NGUVU ya kusogea hatua ya 2.

Hatua ya pili: Ita Ufalme wa Mungu.
Hakuna ufalme usio na mfalme! Ndani ya MFALME kuna MAMLAKA na NGUVU. Sasa unapoita Ufalme wa Mungu uje, kimsingi umeagiza MAMLAKA za Mbinguni zishuke kukuhudumia wewe na mambo unayoyaombea. Ndani ya ufalme wa Mungu kuna KILA kitu unachokitaka. Mahitaji yako yote yanapatikana humo. Lakini jipange na MOYO wako vizuri maana ukiomba vitu kwa tamaa yako hupati kitu (fuatilia somo kwenye “Mafundisho ya Neno la Mungu LIKE page” lenye kichwa “Jinsi ya kumwona Mungu akijidhihirisha kwako”). Jifunze kwamba NENO la Mfalme ndio NENO la MWISHO. Huwezi kumfundisha Mfalme chakufanya kama hataki. Wewe UNAMSIHI kwamba MAPENZI yake yatimizwe . Ukifika hapo unaingia hatua ya 3.

Hatua ya 3: Jua Mapenzi ya Mungu kwa unachokiombea.
Mapenzi ya Mungu yapo katika NENO la Mungu. Huwezi kupokea kama unaomba pasipo IMANI. Na tunajua kwamba “imani huja kwa kusikia, na kusikia huja kwa NENO la Kristo”. Sasa ukiwa na Neno la Mungu juu ya “hicho” unachoombea, jua una mtaji wa IMANI. Sasa kumbuka. Unapoenda mbele za Mungu uwe kama yule mama mjane ambaye alienda BILA KUCHOKA, “akirudi-rudi kudai haki yake” (Luka 18). Ukijua AHADI zako na NENO juu ya kitu unachoomba, kaa hapo usiondoke, omba na dai ahadi yako kwa UPOLE na UNYEYEKEVU mbele za Bwana, tena bila kuchoka (usipayuke kama mtu asiye na imani). Ukirudi-rudi hadi upokee kumbuka siku zote, “Mungu huliangalia Neno lake akalitimize, na Yeye hulituma Neno kama mvua ishukavyo juu ya Nchi, Litaenda (halikosi shabaha) kwa YALE mambo aliyoliagiza na halitamrudia bure”. Hakuna faida kama unajua KITU unachoomba kipo kwenye MAANDIKO. Hapo ndio nguvu na mafanikio yako yalipo. Kama una jambo “nyeti” unataka Mungu akutendee, hakikisha unachukua kalamu na karatasi na unatafuta mistari ya KUSIMAMIA. Imani ya KUPOKEA uombacho imejikita katika UFUNUO wa hilo Neno.

Hatua ya nne: Omba mahitaji yako.
Maombi ya unachokihitaji yamejengwa kwenye hatua ya 3 hapo juu. Unapoomba RIZIKI au mahitaji mbalimbali ya mwilini na rohoni, kwako au kwa mtu mwingine, yote yamejikita katika MAPENZI ya Mungu ambayo unayapata katika Neno. Neno hilo hilo linakupa imani ya kupokea majibu ya maombi yako. Sasa kumbuka siku zote kwamba majibu ya maombi yetu yako ya aina mbili tu. NDIO au HAPANA! Jifunze kwamba hata HAPANA imo katika mapenzi ya Mungu pia. Mungu anakuwazia mema siku zote, hakunyimi kitu bila SABABU. Na imetupasa kumshukuru Mungu katika Mambo yote. Kama tumepokea au hatujapokea yote ni mapenzi ya Mungu kwetu. Ukisikia mtu anakuhakikishia kwamba “LAZIMA” jambo fulani litatokea kwa MUDA anaotaka yeye, jiulize swali hili, Je! Mungu alimhakikishia hilo jambo kwa namna hiyo? Na kama hajahakikishiwa na Mungu, jiulize tena swali hili, je! Ukiri tu ushindi NJE ya MAPENZI ya Mungu ili “kumpinda” Mungu afuate matakwa yako? Ukijua majibu, jifunze UMUHIMU wa kujipanga kwenye mapenzi ya Mungu na KUMSHUKURU kwa KILA jambo.

Hatua ya tano: Toba.
Hii hatua huwa inakuwa ya tano kama tu wewe unadumu katika maombi muda wote, ila mara nyingi sana inakuwa ya kwanza pia. Mungu ni mtakatifu, “ujasiri wa kukariba Kiti cha rehema tunaupata katika Damu ya Yesu tu” mara nyingi sana ukianza kuomba unaweza KUSUKUMWA kujitakasa. Sizungumzii hii hatua ya kujitakasa ambayo inaweza kutokea mwanzo wa maombi. Nazungumzia hii hata ya 5 ambayo sasa unazama kwenye TOBA kwa UPANA wake. Hii hatua ukiifaya vizuri itakuwa ni UFUNGUO wa matatizo mengi sana na KIPOKELEO cha maombi yako. Yesu anaagiza “kila tusimamapo kusali tusamehe ili na sisi tusamehewe”. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]” (Marko11:24-26). Ili uweze KUPOKEA jifunze KUACHILIA watu waliokukosea/wadeni wako! Nakwambia jitahidi KUSAKA “huko” ndani yako KILA mtu ambaye ukimuwaza moyoni unasikia UCHUNGU na ukimpata, MSAMEHE na KUOMBA kwa ajili yake hadi upate UHURU. Kama bado una FUNDO ukimuwaza huyo mtu jua BADO hujavuka hapo hatua ya tano. Watu wengi sana wameshindwa “kupokea wanayoamini” (Marko 11) kwa sababu wameshindwa kuvuka hatua ya tano! Omba NEEMA ya KUSAMEHE kama inakuwa Ngumu na Yesu atakusaidia kumsamehe Mtu. Kama Yesu aliweza kuwasamehe WALIOMSULUBISHA katikati ya mijeledi, misumari, taji ya miba na kuangikwa msalabani huku anatukanwa na kutemewa mate, wakati yote yanaendelea ANAWASAMEHE na kumwomba Baba awasamehe! Yaani anapigwa, ila yeye yuko kwenye maombi! Huyu Yesu anaweza kukupa NEEMA hii ya KUSAMEHE mwenzako kwa faida yako WEWE mwenyewe KUVUKA hatua nyingine.

Hatua ya sita: Shughulika na ADUI.
Watu wengi sana wamejifunza njia moja tu ya kushughulika na Ibilisi. Kila mmoja yuko busy KUKEMEA kwa Jina la Yesu! Sawa, ni muhimu lakini nataka ujifunze Neno hili. Yesu alimwona Petro jinsi anakavyo mkana kabla hajamkana! Hakikumsumbua Yesu kwa sababu “huko” katika MAOMBI yake alikwisha omba kwamba “imani ya Petro isitindike wakati Ibilisi anampepeta kama ngano”. Yesu hakumkemea Ibilisi “asimpepete Petro ila aliomba Petro ASIANGUKE kwenye hilo JARIBU na akisimama awasaidie wenzake”. Majaribu ni package (kivunge/kifurushi) sio kitu kimoja. Sasa ukiwa na utaalamu wa kukemea kuna kitu kwenye hicho kifurushi kitakuwia kigumu. Kifurushi cha jaribu kina mambo makubwa matatu. Kwanza, jambo/kitu utakachojaribiwa nacho. Pili, kitakachotokea wakati unakutana na hicho “kitu” (kupepetwa kama ngano) na tatu, kusudi la jaribu. Ufanye nini baada ya jaribu (simama na imarisha wenzako). Hakuna mwanadamu atakemea MAJARIBU yasije maana majaribu yamo katika mapenzi ya Mungu. Unapaswa kutambua mambo haya matatu kwa makini sana: jaribu (kitu kinachokujaribu), namna ya kujaribiwa, na kusudi la jaribu. Sasa ukikazana tu na kukema huwezi kufanikiwa kila kitu kwa maana katika hilo jaribu, japo ni Ibilisi anakujaribu lakini ni Roho Mtakatifu katoa kibali kwa KIPIMO! Na huwezi kumkemea Roho Mtakatifu kwa maana ndani ya hilo JARIBU kuna KUSUDI la Mungu!

Kumbuka aliyempeleka Yesu Nyikani kujaribiwa hakuwa Ibilisi. Alipelekwa na Roho Mtakatifu! Sasa nataka ujifunze KUOMBA na sio KUKEMEA tu! Omba Mungu kwamba “usianguke majaribuni na uokolewe na yule Mwovu”. Jifunze kumshinda Ibilisi kwa Maombi sio kumkemea tu. Mara nyingi sana ukikuta mambo magumu na unawekwa kwenye “kona” badala ya kukemea pia unamwambia Ibilisi “imeandikwa”, halafu unamsomea msitari wa Biblia na Ibilisi anaachilia mara moja! Kumbuka “nao wakamshinda kwa Damu ya Mwana-kondoo na NENO la ushuhuda wao”, Neno lina nguvu ya kumshinda Ibilisi. Kwanini? Yesu ni Neno! Na tumehakikishiwa kwamba ni “aheri dunia iondoshwe kuliko yodi moja ya andiko kuondoshwa”. Sasa unaweza kuona kwamba hakuna UJANJA ibilisi anaweza kufanya kushindana na Neno la Mungu. Kwa mfano ni rahisi Ibilisi kuangamiza dunia ila sio Neno la Mungu! [japo dunia inalindwa na hakuna uharibifu wa kuangamiza dunia yote ambao utatokea kama Mungu hajaruhusu. Kumbuka agano la upinde wa mvua, nk. hii dunia imewekwa akiba..]

Hatua ya saba: Rudisha Utukufu kwa Mungu.
Hii hatua ni ya muhimu sana kama hatua nyingine zilizotangulia. “kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!”. Ulianza na “Jina lako Litukuzwe” na kuita “Ufalme wa Mungu uje”, sasa ukishahudumiwa na Mfalme na kuamini kwamba KILA ulichoomba kimesikika kwa Mfalme sasa lazima utoe HESHIMA kwa Mfalme! Unamalizia kwa kusema “kwa kuwa wako ni Ufalme, na nguvu, na Utukufu hata milele Amen!” Kumbuka kumshukuru Mungu kabla ya kupokea uliyoomba kwa sababu “imani ni hakika ya mambo YATARAJIWAYO na ni BAYANA ya mambo yasiyoonekana”. Mambo yatarajiwayo maana yake hujayapata ila UNAJUA yanakuja. Haya mambo yakiwa BAYANA unapata ujasiri wa KUKIRI kwa maana una UDHIHIRISHO wa NDANI kwamba umepokea ulichoomba. Usiiishie hapo, rudi-rudi kama yule mama mjane, kukumbusha hadi uhitimishe maombi yako kwa kuona sasa kwa jinsi ya mwilini jambo limetokea.

HITIMISHO

Kama utakuwa umefuata hizi hatua saba, na kujimimina utagundua kumbe saa nzima imeisha na unataka kuendelea kuomba. Fanya mazoezi halafu unipe ushuhuda. Najua hutaanza kupiga masaa tu kwa mara moja, ila angalau utavuka hatua kwa hatua.

Jambo la muhimu sana la kujifunza katika maombi ni juu ya MAHALI na MUDA. Watu wengi sana wamesindwa kuomba kwa sababu ya kufungwa na MAHALI na/au MUDA. Ukijifunza kuomba kila mahali, ukitembea, ukipika, ukifua, ukiwa darasani, ukiwa safarini, nk., utagundua unaweza kuombea mambo mengi sana kwa siku na kurudi-rudi kwa Mungu mara kadhaa “kumkumbusha jambo” kwa sababu huhitaji kujifungia mahali. Kama unaweza kuomba kwa “kunena” ni nzuri sana hasa unapokuwa katika michakato ambayo inachukua attention yako. Mtume Paulo anatufundisha kwamba tutumie mbinu zote mbili. Kuomba kwa lugha na kwa akili pia. “usikae kimya usiku wala mchana” (Isaya 62) usifungwe na muda.

Ukisikia unasukumwa KUFUNGA, fanya hivyo kwa kipimo cha mambo unayojihusisha nayo kama umetingwa na KAZI au aina ya MAJUKUMU yanahitaji sana nguvu za mwili. Ikiwezekana jipe siku malumu katikati ya wiki na kama kazi yako inahitaji nguvu nyingi za mwili jaribu kufanya maombi ya namna hii wakati wa mapumziko ya wiki, nk. Kila mtu afanye kama Roho Mtakatifu atakavyomongoza.

Neema ya Bwana wetu Yesu na izidi kwenu mnapojifunza na KUYATENDA haya. AMEN.

Frank Philip.